Wednesday, April 4, 2012

Mwanaadamu anahitaji mwongozo


"Tuongoze njia iliyonyooka". (1:5)


PENGINE moja ya vitabu bora vilivyomzungumzia mwanaadamu katika karne iliyopita ni kile kilichoandikwa na Alexis Carl kiitwacho Man: The Unknown Beingambacho moja ya kurasa zake umeandika, haiwezekani kumueleza mwanaadamu kwa vigezo au kanuni za kisayansi. Hata katika zama hizi zenye majaribio makubwa ya kifizikia, biokemia na biolojia kutokuwezekana huko kunaendelea kubaki katika nafasi yake..
Bwana Carl ameandika kuwa taratibu za kisayansi zaidi zimezama kulichunguza au kulitibu umbile la nje la mwanadamu, huku zikipuuzia roho yake. Ni mageuzi ya kitabia pekee yanayoweza kufungua njia ya kumuelewa kiumbe huyu mwenye fahamu na anayejifahamu nafsi yake, mwanadamu.
Hata hivyo, Dkt. Carl anasema haiwezekani na wala hatapakuwa na uhakika wa kufuata njia ya salama na uokovu isiyoingiliwa kwa jitihada za kibinadamu.
Hapa ndipo tunapoweza kuifahamu vyema maana ya ya "tuongoze njia iliyonyooka". (1:5).
Mwanaadamu anahitaji mwongozo kutoka kwa Muumba wake, kwa sababu maisha ya mwanaadamu hayakutuama wala hayafuati bila ya hiari kanuni maalum ya kimaumbile kama vile mashine fulani, Kompyuta au sayari angani. Mwanaadamu ameumbwa katika umbile lenye kuhitajia mabadiliko likiongozwa na neema ya hiyari na uchaguzi. Kwa sababu hiyo mwanaadamu katika maisha yake yote ni mtafutaji, mdadisi na mvumbuzi mwenye tamaa na haja ya mwongozo.
Bwana Carl akionesha haja na tamaa aliyonayo ya mwongozo wa kimaadili ameandika:
"Kwa kutoa mwangaza juu ya ukweli wa maumbile yetu, vipawa vyetu, na namna ya kuvitumia, sayansi hii itatupatia maelezo juu ya udhaifu wetu wa kimwili na kiroho, ya kupambanua haramu na halali, ya kutambua kuwa hatuna uhuru wa kubadili mazingira yetu na sisi wenyewe kufuata matashi yetu. Kwa kuwa mazingira asilia ya uhai wetu yameharibiwa na utamaduni wa kisasa, sayansi ya binaadamu imekuwa muhimu kuliko sayansi zote".
Qur'an katika aya mbalimbali imesisitiza kuwa Mitume walitumwa kuwaongoza na kuwatoa watu kwenye batili, ujinga na kujisahau ili kuwaweka katika uongofu na kumkumbuka Allah (s.w.). Qur'an imewaonya watu waachane na njia zenye hatari na majanga wanazozibuni wao wenyewe. 

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget