Thursday, April 12, 2012

KITABU-MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA

KITABU—MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA—kimezungumzia mambo mengi kuanzia upotoshaji wa Krismasi, Desemba 25 na siku ya kuzaliwa Yesu Kristo. Hata useja wa ukasisi wa Kikatoliki umetiliwa mashaka makubwa kwa sababu unatokana na upagani na wala si Ukristo. Ukweli umewekwa bayana katika kitabu hiki. Kuna watu ambao hawatakipenda, lakini ni vyema wakakisoma chote na kisha kuamua kuitafakari changamoto hii. Ni katika mijadala ya aina hii ndipo mtu anapoitwa mwendawazimu kwa sababu ya kuandika mambo tofauti na mazoea.

Tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo haijulikani. Biblia hunyamaza kimya unapokuja wakati wa kuzungumzia tarehe ya kuzaliwa Yesu. Haitaji tarehe yoyote ya kuzaliwa kwake. Hoja yangu si katika ukweli wa kwamba tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo haitajwi popote katika Maandiko Matakatifu, bali ni katika ukweli kwamba chanzo cha tarehe hiyo ni Upagani.

Wataalam wa kupima ufasaha, ukweli na uhafifu wa vitabu wanaweza wasikubaliane na maelezo ya kitabu hiki, wakabaki wakitafuta-tafuta makosa katika hoja na vielelezo vilivyotumiwa. Lakini vyovyote itakavyokuwa, wanaotaka kupinga wanaweza kufanya hivyo kwa kuwa ni watu wanaoweza kubishania hoja yenye hali ya kuwa na maana nyingi. Ingawa wanaweza kujitahidi kupinga mengi, kamwe hawataweza kupinga yote. Watajikuta wakikubaliana na jambo moja la uhakika, kwamba Maandiko Matakatifu hayaonyeshi tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu, na Biblia haina msamiati unaoitwa ‘Krismasi’, wala Yesu Kristo hakuwahi kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Ingawa wao wanaweza kusema kuwa hakuna ushahidi wowote unaotosha kupinga kwamba Yesu hakuzaliwa Desemba 25, vivyo hivyo naweza kuwaambia kuwa hawana ushahidi wowote unaotosha kuthibitisha kwamba alizaliwa Desemba 25. Wakosoaji wanaweza kusema ni vigumu kukana kwamba Yesu alizaliwa Desemba 25, au siku ya Krismasi, lakini ikiwa ni vigumu kukana kuwa alizaliwa Desemba 25, ni vigumu hata zaidi kwa yeyote kuthibitisha kwamba alizaliwa Desemba 25. Kwa sababu tarehe ya kuzaliwa kwake haijulikani, inawezekana ikawa kweli kwamba alizaliwa Desemba 25, lakini ni nani anayeweza kuthibitisha? Ni rahisi zaidi kukanusha kuwa alizaliwa Desemba 25 kuliko ilivyo rahisi kuthibitisha kuwa alizaliwa Desemba 25. Msingi wa dini ya Kikristo, yaani Biblia, hauonyeshi uhusiano wowote wa Desemba 25 na Krismasi, au uhusiano wa tarehe nyingine yoyote na siku aliyozaliwa Yesu Kristo kwa kuwa siku ya kuzaliwa kwake “haiwezi kuthibitishwa na Agano Jipya, au, kwa kweli haiwezi kuthibitishwa na chanzo kingine chochote,” kinasema kitabu Cyclopedia of Biblical, Theological and Ecclesiastical Literature.

Kinachodokezwa na Biblia katika kitabu cha Yeremia 52:31, ambacho kinaweza kudaiwa kuwa ni Desemba 25, ni “...mwezi wa kumi na mbili, siku ya ishirini na tano ya mwezi...” Kwa kuiweka sentensi hiyo katika tarakimu, hiyo inaweza kusomeka kama Desemba 25 kwa mujibu wa kalenda inayotumika sasa. Lakini mstari huo hautaji kuzaliwa kwa Yesu, wala kwa yeyote anayehusiana na Yesu, wala tarehe ya kuzaliwa kwa mtu yeyote anayehusiana na masimulizi ya Biblia. Hata kama ingekuwa hivyo, hiyo ni kalenda ya Kiyahudi na wala siyo kalenda ya Kirumi (Gregorian Calendar) inayotumika hivi sasa duniani kote.

Mstari huo wa Biblia unasema hivi: “Hata ikawa, katika mwaka wa thelathini na saba wa kuhamishwa kwake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi na mbili, siku ya ishirini na tano ya mwezi, Evil-merodaki, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, akamwinua kichwa chake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani.”

Biblia inawaambia Wakristo hivi: “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini mambo hayo.” (Wafilipi 4:8). Mstari wa tisa unaofuata unasema hivi: “Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.”

Je, mafundisho yanayotolewa na makanisa ni mambo ya kweli? Yaliyo ya staha? Yaliyo ya haki? Yaliyo safi? Yenye kupendeza? Yenye sifa njema? Yana wema wo wote, sifa nzuri yo yote? Je, wameyatafakari mambo hayo? (Wafilipi 4:8). Je, mafundisho hayo ni “Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu...; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi”? (Wafilipi 4:9).

Ingawa kusudi la uchambuzi wa kitabu hiki si kuondoa wingu la kihistoria lililowekwa na makanisa—au baadhi ya makanisa—bali ni kujaribu kutazama kwa macho ya kawaida kupitia wingu hilo ili kuonyesha tu jinsi hali ilivyo, kwa watu wengi ni vigumu siku zote kuchukua msimamo tofauti na ule unaochukuliwa na halaiki ya watu duniani kote. Lakini wanaojaribu kuipinga mambo mengi yaliyopotoshwa wanatetewa na Biblia inapowaelekeza kutofuata ya wengi hata kama msongo unakuwa mkali kadiri gani, na hata kama jambo fulani laonekana kufuatwa na kila mtu duniani kote.

Ingawa ni wengi ambao hukubaliana, bila kuhoji, mafundisho mengi ya makanisa, na kuyaamini kwa moyo wote, wachache zaidi wanao msimamo tofauti, wakisema kuwa msingi wa imani ya Kikristo, Biblia, hupinga mambo mengi yanayofundishwa na makanisa makanisani. Ingawa wanaoamini hivyo ni wachache zaidi wakizidiwa na wale wengi zaidi, wao wanasadiki kuwa wana sababu ya kuwafanya wawe na msimamo huo.

Hufarijika wasomapo aya hii: “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao katika mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionayo ni wachache.” (Mathayo 7:13-14). Njia pana hupitisha watu wengi, tena kwa urahisi, lakini njia nyembamba hupitisha watu wachache sana, tena kwa shida. Kwa kuwa jambo linafuatwa na kuheshimiwa na kila mtu duniani halimaanishi kwamba ni jambo jema. Huenda likamaanisha njia pana iendayo upotevuni. Na nyakati nyingi mambo mabaya na yasiyo sawasawa hufuatwa na wengi, na mara nyingi wakifanya hivyo bila kutambua, wakidhani kwamba kwa kuwa kila mtu anacheka, basi kicheko ni chema, na kwa kuwa watu wachache sana wanalia, basi kilio chao ni kiovu. Lakini, kama ilivyokuwa mwanzo ndivyo itakavyokuwa mwisho.

Nakukaribisha usome kitabu hiki.

William Shao.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget