Saturday, February 11, 2012

ATHARI ZA SIGARA


Miongoni mwa kanuni jumla za uislamu katika vyakula na vinywaji ni Allah kuwahalalishia waja wake:-
1.        Vilivyo vizuri
2.        Vyenye kuwastarehesha wanapovila au huvinywa
3.        Vyenye manufaa
Na kuwaharamishia vilivyo vibaya kwa ladha, harufu au madhara. Msingi/kanuni hii inapatikana katika kauli tukufu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: “NA ANAWAHALALISHIA VIZURI NA KUWA HARAMISHIA VIBAYA”  (7:157)
Kwa kanuni hii haijuzu kisheria kwa mtu yeyote yule kula au kunywa kitu chochote kinachoidhuru afya yake na kuyatishia (kuyahatarisha) maisha yake. Hii ni kwa sababu muislamu haimiliki nafsi/roho yake mpaka akawa na uhuru wa kuitumia atakavyo ikiwa ni pamoja na kutumia yanayopelekea kuingamiza  nafsi/roho hiyo ambayo imo katika milki ya Allah. Uhai wa muislamu ni haki ya Allah aliyempa uhai huo bila ya maombi, makubaliano wala malipo yoyote kutoka kwake. Afya ya muislamu ni miongoni mwa neema za Allah alizomneemesha mja wake huyu, kwa hiyo si halali kwake kuichezea na kuihatarisha neema hii.
Hakuna tafauti baina ya mtu mwenye kujiua yeye mwenyewe kwa kitu chenye kuua mara moja (papo kwa papo) kama kisu, risasi na kadhalika, na yule mwenye kujiua kwa sumu inayoua taratibu (kidogo kidogo). Wote wawili hawa wanafanya kosa moja lile lile kwa njia tofauti, huyu anajiua haraka na yule anjiua taratibu ,wote wana hatiambele ya sheria kwa sababu wanalipinga agizo la Mola wao:
“…..WALA MSIJIUE(wala msiue wenzenu) HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUKUHURUMIENE”(4:29). Tuzidi kusoma :
“--- WALA MSIJITIE KWA MIKONO YENU KATIKA MAANGAMIZO---” (2:195)
Tujiulize ikiwa mtoa uhai anakuhurumia vipi wewe usiyeumiliki uhai huo hujuhurumii na unajiangamiza wewe mwenyewe, ni akili gani hiyo?!
Ni vema tukakumbuka pia kwamba mali ni neema ya Allah iliyo juu yetu, kwa hiyo ni wajibu wetu kuihifadhi na kuitumia vizuri neema hii. Muislamu hapaswi kuitumia mali ila katika njia/matumizi ya halali tu. Hii ni kwa sababu Allah ameifanya mali kuwa ndio zana ya maisha ya watu, kwa hivyo mtu kuifuja mali binafsi ni kuufuja utajiri wa rasilimali ya umma. Kanuni hii imethibiti katika tamko la Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie kwamba yeye “Amekataza ufujaji wa  mali” Muslim. Kulinda/kuhifadhi maisha (uhai) ya mtu, mali na akili ndio makusudio na dhima ya sheria ya Kiislamu. Hili linathibitishwa na adhabu kali zilzozowekwa na sheria dhidi ya mtu anayechezea au kuhatarisha vitu vitatu hivyo; maisha,mali na akili. Ni (kupitia katika) chini ya mwangaza wa kanuni na makusudi haya ndio tunaweza kuuhukumu uvutaji wa sigara na matumizi ya tumbaku kwa ujumla baada ya kujua madhara na athari yake mbaya. Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwamba tumbaku imeanza kutumiwa na wakazi asili wa Amerika, wahindi wekundu (Red Indian’s) tangu katika karne ya kumi na tano (15thcenturyA.D). Jamii hii ya wahindi wekundu ilitumia tumbaku kwa matumizi mbalimbali, walitumia kwa kuitafuna,kuitia puani (ugolo) na kwa kuisokota sigara au kuivuta ndani ya kiko kutoka hapo ndipo ada hii ya uvutaji wa sigara ikajipenyeza barani ulaya na kuenea pande mbalimbali za dunia. Baada ya tumbaku kuenea kwa kasi ya moto wa nyikani na kupata wateja wengi ndipo ilpozidishwa uzalishaji wake na kujengwa viwanda vikubwa. Dhima kuu ya viwanda hivi ni kuzalisha aina mbalimbali za sigara ili kukidhi mahitaji za wateja kuanzia hapo uvutaji wa sigara imekuwa ni janga kubwa kwa jamii ya wanadamu. Umekuwa ni gonjwa hatari la kuambukiza watu wanapokezana na kuambukizana gonjwa hili. Mdogo anamwiga mkubwa katika uvutaji, mtoto anamwiga baba yake, maskini anamwiga tajiri, watu wote wamekuwa ni watumwa wa janga hili wasiloweza kujikomboa nalo.
Ni baada ya muda mchache tu tangu kuenea kwa matumizi ya tumbaku, madaktari waligundua matumizi makubwa yanayoipata jamii ya wanadamu kutokana na utumiaji wa tumbaku katika mwaka 1598 A.D ilitoka kwa mara ya kwanza nchini Uingereza makala ielezayo madhari na hatari ya utumiaji wa tumbaku. Kisha zikafuatia tafiti mbalimbali zilizoendelea kugundua na kuelezea madhara yatokanayo na matumizi ya tumbaku na namna inavyoathiri na kuhatarisha afya ya binadamu. Matokeo ya tafiti hizi za wanasayansi ya tiba zilipelekea baadhi ya nchi kama vile Denmark,Uholanzi na Sweden kuweka (kutunga) sheria  zinazozuia uvataji wa sigara. Lakini baadae serikali hizo zikaona zinapata upungufu katika bajeti zao kutokana na kukosa kodi kubwa itokanayo na uzalishaji wa tumbaku na uuzaji wa sigara. Makampuni na mashirika yanayojishughulisha na uzalishaji na uuzaji wa sigara  hutenga fungu kubwa la fedha katika kuitangaza biashara yao hii hatari.
Madhara na athari mbaya itokanayo na matumizi ya tumbaku iko wazi sasa kwa kila mmoja wetu. Sio siri tena kwamba tumbaku ina madhara kwa afya ya binadamu na ndio maana Shirika la Afya Duniani (WHO)  likayaagiza mashiriki yote yanayozalisha sigara kutangaza kwa kuandika katika bidhaa zake kuwa "Uvutaji sigara una madhara kwa afya yako”. Uvutaji sigara unasababisha maradhi mbalimbali kama vile saratani ya mapafu, wazimu, kupooza matatizo ya mfumo wa hewa (kupumua), kutoboka kwa utumbo, kunyonyoka nywele, upungufu wa nguvu za kiume, maradhi ya ngozi na kadhalika. Madhara yatokanayo na matumizi ya tumbaku hayajitokezi mara moja bali kuchukua miaka kadhaa hata miaka thelathini, ni jambo ambalo huwafanya watu wengi kufumbia macho madhara hayo ya pole pole na hivyo kuendelea na tabia ya uvutaji wa sigara. Mvutaji sigara mbali ya kujidhuru mwenyewe huwadhuru wengine pia kwa kuwalazimisha kuvuta hewa iliyochafuliwa na moshi wenye sumu ya tumbaku. Mvutaji huwaathiri watu waliomzunguka, humuathiri mkewe/mumewe, huwaathiri wanawe kama anavyoyaathiri mazingira aishimo.
UVUTAJI HUATHIRI AKILI YAKO:
Mwenyezi Mungu ametuzawadia akili ili itusaidie kufikiri, kutatua na kupanga mambo yetu mbalimbali. Ni vipi basi mtu mwenyewe akili timamu anathubutu kufikia uamuzi wa kujidhuru yeye mwenyewe kwa hiyari yake bila kuladhimishwa na mtu mwingine?! Uvutaji unaiathiri akili yako, kwa sababu ndani ya uvutaji kuna kiasi fulani cha ulevi unaosababisha ulegevu wa mwili. Hili aneweza kuliona mvutaji anapovuta sigara kwa mara ya kwanza kabisa. Hawa wanaotumia mali zao kununua kinachowadhuru  wakati ambapo familia zao zinakosa mahitaji muhimu, nao hawajali. Hebu tuwe wakweli, watu hawa wana akili kweli?!
UVUTAJI UNAIDHURU DINI
Kamaambavyo uvutaji unavyoidhuru akili, na ya maisha mvutaji na watu wengine, pia huiathiri na kuidhuru dini. Tunawajua baadhi ya watu wasiofunga mwezi wa Ramadhani. Ukiwauliza kwa nini, hujibu: siwezi kuacha kuvuta sigara, kwa sababu ndio uhai wangu! Kwa mtu huyu sumu ya sigara inayomuua kidogo kidogo ni bora zaidi kuliko swaumu inayompa ucha-Mungu na siha njema watu. Wengi hufunga, muadhini anapoadhini  tu Magharibi futari yao ya mwanzo huwa ni sigara yenye kuwadhuru. Huku ni kuyapinga na kwenda kinyume na maelekezo na amri ya Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie-alipotuambia tufuturu kwa tende, maziwa  au hata maji vitu vyenye faida mwilini. Isitoshe uvutaji sigara humsukuma mvutaji kufanya ubadhirifu israfu na kuwaudhi wengine, mambo yote haya yamekatazwa na Allah. Pia ni kweli kuwa mvutaji hawezi kuwa askari shujaa na mwenye nguvu katika kuipigania dini ya Allah,kuilinda nchi yake na heshima ya waislamu na uislamu. Kwa nini, hii ni kwa sababu tayari sumu nya sigara itakuwa imeshamdhoofisha na kuzimaliza nguvu zake. Je, huku si kuidhuru dini?!
UVUTAJI WAKO UNAIATHIRI FAMILIA YAKO
Mvutaji sigara huilazimisha familia yake kuvuta hewa iliyochafuliwa na kutiwa sumu itokanayo na moshi wa sigara aivutayo na hivyo kumdhuru mkewe, wanawe hata yule masikini mtoto mchanga anadhuriwa ! Utafiti wa kitaalamu umedhibitisha kwamba watoto wanaolelewa katika mazingira ya baba/mama mvutaji huathirika mishipa yao inayosafirisha damu kuipeleka katika moyo. Hali hii husababisha kuharibika kwa mfumo mzima wa usafirishaji damu mwilini na kuwafanya watoto hawa wasio na hatia kuwa ni wahanga wa maradhi mbalimbali. Zaidi ya hayo ni ukweli kuwa mtoto ni kiumbe wa kuiga kizuri au kibaya, yeye anachojua  ni kuiga tu. Kwa mantiki hii, watoto watamuiga baba yao mvutaji, nao wataanza kuvuta kwa kudhani kuwa huo ndio uanamume na ndio ustarabu. Janga hili umelileta wewe baba/mama mvutaji, je, huko si kuidhuru familia yako?! Wewe mama mjamzito mvutaji, elewa kuwa uvutaji unakudhuru na kumdhuru na kumdhuru mwanao aliye tumboni. Uvutaji wakati kumdhuru mwanao aliye tumboni. Uvutaji wakati wa ujauzito husababisha:-
1.        Kuathirika kwa suala zima la ukuaji wa mimba kutokana na sumu ya tumbaku.
2.        Kondo la nyuma {placenta} kushindwa kusafirisha vizuri chakula kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
3.        Mtoto kuzaliwa akiwa na uzito pungufu jambo ambalo litaathiri ukuaji wake.
4.        Kupungua hamu ya chakula kwa mama mjamzito ambako huchangia kwa kiasi kikubwa kuathirika kwa afya ya mama na mtoto
Ewe mama wee! Mbona unamdhulumu na kumdhuru malaika huyu, amekosa nini masikini huyu?
UVUTAJI UNAIDHURU MALI (UCHUMI):
Mvutaji huitumia mali (pesa) yake katika kitu  kisicho na manufaa, si duniani  wala kule akhera. Wanawazuoni wamekongamana kwamba utumiaji wa mali katika yasiyo na manufaa ni HARAMU haijuzu kabisa kisheria. Ufujaji mali hauna nafasi kabisa katika Uislamu, Bwana Mtume –Rehema na Amani- amelikemea na kulikataza hilo. Elewa ewe mvutaji na kila mbadhirifu wa mali, uliyonayo  mali ni mali ya Allah  na wewe ni mchungaji/mtunzaji wa mali hiyo. Kwa msingi huu huna haki ya kutumia mali yako katika mambo/vitu visivyo na manufaa kwako. Haviinufaishi roho yako, mwili wako, akili yako, famalia wala jamii yako. Mvutaji huitumia mali yake kununua madhara, anajidhuru kwa gharama! Afadhali angekuwa anajidhuru bure bila ya kutoa gharama hivi hii ndio akili?! Au hii ndio dini?! Au haya ndio maendeleo na ustaraabu?! Kwa kweli lau si mazoea ya watu kuizoea tumbaku, mtu asingeliionja, angeliichukia na kuitupilia mbali. Lakina mtu akizoea kitu hata kama ni kula udongo au mkaa au pilipili kali, basi nguvu ya mazoea humfanya akione kizuri na kitamu kitu hicho na hili ni janga jingine! Ewe mvutaji ihurumie nafsi yako, acha leo kuvuta, amua! Ukiwa unaweza kujizuia kuvuta, masaa kumi na tano (15 hours) ndani ya mwezi wa Ramadhani unapofunga, kwa nini ushindwe sasa?! Allah anatuambia:-“--- NA UFUNGAPO NIA  MTEGEMEE  ALLAH (tu ili ufanye hili uliloazimia) HAKIKA ALLAH ANAWAPENDA WAMTEGEMEAO.” (3:159)
Kumbuka huu ni ushauri nasaha, kunasihika au kutonasihika au kutonasihika hilo ni shauri lako
 

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget