Hakika katika mas-ala haya zipo Hadiyth tano kutoka kwa Mtume wa
Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – tatu sahihi na mbili
dhaifu. Moja ni kukataa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikojoa kwa kusimama, ya pili ni
kuonyesha kuwa alikojoa kwa kusimama na ya tatu akiwa ameketi. Na katika hizo
Hadiyth dhaifu ni kukataza kwake kukojoa kwa kusimama na ya pili ni kukemea
kwake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kukojoa kwa
kusimama ni katika kukengeuka. Hapa twazitaja zote kwa faida ya kila mmoja
wetu:
1. Hadiyth ya ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu
‘anha) aliyesema: Yeyote
anayekuhadithieni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
alikuwa akikojoa kwa kusimama msimsadiki. Alikuwa hakojoi ila kwa kuketi (Ahmad, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na
Ibn Maajah).
2. Hadiyth ya Hudhayfah (Radhiya Allaahu
‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda kwenye jaa la taka la watu,
akakojoa kwa kusimama. Mimi nikaondoka, akasema: “Njoo”. Nikarudi mpaka
nikasimama kwenye mabega yake, akatawadha na kupangusa juu ya viatu vyake (Ahmad, al-Bukhaariy, Muslim, Abu
Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah).
3. Hadiyth ya ‘Abdur-Rahman bin Hasnah
(Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Alitoka
kwetu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa
mkononi mwake ana ngao ya ngozi, akaiweka, kisha akaketi nyuma yake akakojoa
kuielekea… (Ahmad, Abu Daawuud,
an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).
Na hizi ni Hadiyth mbili zilizo
dhaifu:
4. Imepokewa na Ibn ‘Umar (Radhiya
Allaahu ‘anhuma) kuwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:Mtume wa Allaah
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniona nikikojoa kwa
kusimama. Akaniambia: Ewe ‘Umar! Usikojoe kwa kusimama. Akasema: Sikukojoa tena
kwa kusimama baada ya hapo (Ibn
Maajah, al-Bayhaqiy na al-Haakim lakini ni Hadiyth iliyo dhaifu).
5. Imepokewa na Buraydah (Radhiya Allaahu
‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Vitu vitatu ni katika kukengeuka: Mtu
kukojoa kwa kusimama, kupangusa mgongo wake kabla ya kuondoka katika Swalah na
kupuliza katika sijdah yake (Ameinukuu
al-Bukhaariy katika Taariykhyake,
al-Bazzaar, na akaikanusha al-Bukhaariy na at-Tirmidhiy. Na hii imethubutu kuwa
ni kauli ya Ibn Mas‘ud [Radhiya Allaahu ‘anhu]).
Kwa ajili ya Hadiyth hizi, wanachuoni
wametofautiana kuhusu kukojoa wima. Kwa ajili hiyo zikapatikana kauli tatu”
1. Inachukiza pasi na udhuru wowote:
Hii ni kauli ya ‘Aaishah, Ibn Mas‘ud, ‘Umar (katika riwaya yake moja) [Radhiya
Allaahu ‘anhum], Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhum), ash-Sha‘biy, Ibn ‘Uyaynah,
Abu Haniyfah na ash-Shaafi‘iy.
2. Inajuzu daima dawamu: Hii ni
kauli ya ‘Umar (katika riwaya yake ya pili), ‘Aliy, Zayd bin Thaabit, Ibn
‘Umar, Sahl bin Sa‘d, Anas, Abu Hurayrah, Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhum) na
ni kauli ya Ahmad bin Hanbal.
3. Ikiwa ni katika sehemu ambayo
hairudishi (hauruki) mkojo kwake inajuzu na ikiwa unarudi basi haifai: Hii
ni kauli ya Maalik, na Ibn al-Mundhir akaiona ni sahihi.
Baada ya hayo yaliyo juu,
twafupisha maneno kwa kusema kuwa hakuna uharamu wowote wa kukojoa kwa kusimama
ikiwa mkojo hautarudi au kumrukia mwenye kukojoa ila ni bora kukojoa kwa
kuketi. Imaam an-Nawawiy akizungumzia mas-ala haya amesema: “Kukojoa kwa kuketi
inapendeza zaidi kwa rai yangu, lakini kufanya hivyo kwa kusimama wima
kunaruhusiwa. Matendo yote mawili yamepatikana kwa Mtume wa Allaah (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.
No comments:
Post a Comment