Mwanzo tunatakiwa tufahamu kuwa du’aa ni jambo ambalo linahitajika
kwa Muislamu. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
anatufahamisha kuwa du’aa ni silaha ya Muumini. Kwa hiyo, baada ya kila
‘Ibaadah, Allaah Aliyetukuka Akatuwekea du’aa. Na ‘Ibaadah ya Swalah si
tofauti, kwani Aliyetukuka Ametuambia:
“Mkisha
swali basi mkumbukeni Allaah mkisimama, na mkikaa, na mnapo jinyoosha kwa
kulala. Na mtapotulia basi simamisheni Swalah kama dasturi.
Kwani hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu” (4:
103).
Na Akasema: “Na
itakapokwisha Swalah, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Allaah, na
mkumbukeni Allaah kwa wingi ili mpate kufanikiwa” (62: 10).
Hata hivyo, inatakiwa tuilete
hiyo du’aa kwa njia ambayo tumefundishwa na sheria sio tunavyotaka sisi.
Tukianza na Hadiyth ya Abu
Umaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu). Nadhani itakuwa bora mwanzo tuanze na
kuifasiri kwa ukamilifu wake ili ifahamike vizuri. Imepokewa kwa Abu Umaamah
(Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
Aliulizwa Mtume wa Allaah (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni du’aa gani yenye kusikilizwa
zaidi (inayokubaliwa)?” Akasema: “Sehemu ya mwisho ya usiku na baada ya kila
Swalah ya faradhi” (at-Tirmidhiy ambaye amesema ni Hasan).
Hivyo ndivyo ilivyonukuliwa na
Imaam an-Nawawiy. Labda tuitazame msimamo wa wanachuoni kuhusu Hadiyth hiyo.
Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn al-Albaaniy ameiweka Hadiyth kuwa ni ya 1508,
naye amesema Hadiyth hii ni Sahihi. Hata hivyo, Shaykh Shu‘ayb al-Arna’ut
amesema Hadiyth hii ni dhaifu kwa sababu ya Isnadi yake lakini inatiliwa nguvu
na Hadiyth nyingine, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
amesema: “Mja anakuwa karibu zaidi katika du’aa zake wakati wa usiku wa
mwisho” (at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy, na Isnadi yake ni Sahihi).
Hata hivyo, tukichukulia kuwa
Hadith hii ni sahihi kabisa kama alivyosema
Sh. Muhammad Naaswir ad-Diyn al-Albaaniy haimaanishi kuwa adhkaar na du’aa
zinazoletwa baada ya Swalah ni kwa pamoja. Zipo Hadiyth nyingi Sahihi
zinazotufundisha adhkaar na du’aa kwa mpangilo maalumu baada ya Swalah ya
Faradhi. Na kufanya hivyo kunampatia mwenye kutekeleza ujira na thawabu nyingi.
Kwa hiyo, ni muhimu kuhifadhi du’aa hizo na kuzileta kwa njia inayotakiwa na
sheria. Pia tunatakiwa tulete baada ya Swalah tu na kabla ya kuinuka latika
sehemu aliyoswali Muislamu. Utaratibu wenyewe ni kamaufuatao:
1. Kusema
AstaghfiruLlaah mara tatu baada ya salamu na kisha kusema: Allaahumma
Antas Salaam wa Minkas Salaam tabaarakta yaa dhal Jalaal wal Ikraam (Muslim).
2. Kisha ni
kusema: Laa
ilaaha illaa Allaahu wahdahu laa shariyka lahu, lahul
Mulku wa lahul Hamdu wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr. Allaahumma laa maani’a
limaa A‘twayta walaa Mu‘twiya limaa mana‘ta walaa yanfa‘u dhal jaddi Minkal
Jadd. (al-Bukhaariy
na Muslim).
3. Baada ya
hapo, Laa Hawla
walaa Quwwata illaa Billaahi. Laa ilaaha illaa Allaahu walaa na‘budu illa
Iyyaahu lahun Ni‘matu wa lahul Fadhwlu wa lahuth Thanaaul Hasan. Laa
ilaaha illa Allaahu mukhliswiyna lahud Diyna walaw Karihal kaafiruun (Muslim).
4. Kisha
utaleta: Tasbiyh mara 33, Takbiyr 33, Tahmiyd 33 na
kukamilisha mia utasema: Laa
ilaaha illaa Allaahu wahdahu laa shariyka lahu lahul Mulk wa lahul Hamd wa Huwa
‘alaa kulli shay’in Qadiyr. (Muslim).
5. Na baada
ya Swalah ya Maghrib na Alfajiri utaleta Tahliyl mara kumi
(Ahmad) na Rabbi
ajirniy minan Naar mara saba
(Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).
6. Kusoma
Ayaatul Kursiy (2: 255) {an-Nasaa’iy, atw-Twabaraaniy na Ibn Sunniy}
7. Kusoma
Suratul Ikhlasw, al-Falaq na an-Naas (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy).
Shaykh Dkt. Swaalih Fawzaan bin
‘Abdallaah al-Fawzaan katika kitabu chake al-Mulakhkhaswu
al-Fiqhiyy amesema:
“Na inapendeza kujihirisha Tahliyl,
Tasbiyh, Tahmiyd na Takbiyr baada ya
kila Swalah lakini isiwe kwa sauti ya pamoja. Kila mmoja ananyanyua sauti peke
yake. Baada ya kumaliza adhkaar hizi, kila mmoja anaomba kwa siri kwa
anachotaka. Hakika ni kuwa du’aa baada ya ‘Ibaadah na hizi adhkaar tukufu
inaleta uwezekano mkubwa zaidi wa kujibiwa. Haifai kujihirisha du’aa bali
anaifanya kwa sauti ndogo, kwani kufanya hivyo ni karibu zaidi na Ikhlaswi,
unyenyekevu na mbali zaidi na riyaa. Na ama kwa yale yanayofanywa na baadhi ya
watu katika baadhi ya nchi kwa kuleta du’aa ya pamoja baada ya Swalah kwa sauti
kubwa au Imaam aombe na maamuma waseme Aamiyn. Hii ni bid‘ah inayochukiza kwani
haijapokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa
alikuwa anaposwalisha watu na baada ya kumaliza Swalah akiomba kwa njia hii.
Hakufanya hivyo katika Swalah ya Alfajiri, wala Alasiri, wala Swalah nyinginezo,
wala hakupendeza hilo yeyote
miongoni mwa maimamu” (Mj. 1, uk. 154 – 160).
Ama tukija katika Fat-hul Baariy
nimeipitia Hadiythi hizo ulizozitaja katika Mj. 11, uk . 159,
chapa ya Daar as-Salaam, chapa ya tatu ya mwaka 1421 H/ 2001 M. Imaam al-Bukhaariy
ana mlango wa 18:Baab ad-Du’aa’i ba‘da asw-Swalaah (Mlango
wa Du’aa baada ya Swalah). Imaam al-Bukhaariy ameweka Hadiyth mbili
zilizoshereheshwa na Ibn Hajar, nazo ni kama zifuatazo:
1- Imepokewa
na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu): Wakasema: Ewe Mtume
wa Allaah! Hakika wametangulia wenye mali kwa daraja na neema za kuendelea.
Akasema: Itakuwaje hivyo? Akasema: Wanaswali kama tunavyoswali, wanapigana
Jihaad kama tunavyopigana, na wanatoa katika fadhila za mali zao, nasi hatuna cha kutoa. Akasema:
Je, niwajulishe jambo ambalo mkifanya mtawafikia waliokuwa kabla yenu na
kuwashinda wanaokuja baada yenu, wala hatofikia yeyote kwa mlioleta ila
atakayeleta mfano wake? Leteni Tasbiyh
baada ya kila Swalah mara kumi, Tahmiyd kumi na Takbiyr kumi.
2- Mughiyrah
bin Shu‘bah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuandikia Mu‘awiyah bin Abi Sufyaan
(Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) alikuwa akisema baada ya kila Swalah baada ya salaam: Laa ilaaha
illa Allaahu wahdahu laa shariyka lahu, lahul Mulku wa lahul Hamdu wa Huwa
‘alaa kulli shay-in Qadiyr. Allaahumma
laa maani’a limaa A‘twayta walaa Mu‘twiya limaa mana‘ta walaa yanfa‘u dhal
jaddi Minkal Jadd.
Kauli yake: “Mlango wa Du’aa
baada ya Swalah”, yaani baada ya Swalah za faradhi. Hadiyth hizo mbili zilizo
hapo juu zinatufahamisha kuwa ipo du’aa baada ya Swalah, du’aa ambazo ni
makhsusi kamaalizotufundisha
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata hivyo, hizo
Hadiyth hazionyeshi kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
alikuwa akiomba na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakiitikia Amiyn.
Ama tukija katika Hadiyth
ulizozitaja kwa muhtasari ambazo amezitaja Ibn Hajr al-Asqalaaniy, na pia kuna
nyingine umeziacha zote hazina dalili ya kuomba du’aa kwa pamoja baada ya
Swalah. Na hivyo akamuusia Mu‘aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ‘anhu) asiache kuomba
du’aa baada ya Swalah, du’aa maalumu ((Abu Daawuud, an-Nasaa’iy, al-Haakim na
Ibn Hibbaan). Pia Hadiyth ya Abu Bakrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kauli:
“Ewe Allaah! Najilinda Kwako
kutokana na ukafiri, ufakiri na adhabu ya kaburi”. Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba kwayo baada ya kila Swalah (Ahmad,
at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, na kusahihishwa na al-Haakim).
Na pia Hadiyth ya Sa‘d, Zayd bin
al-Arqam, Swuhayb na Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ‘anhum) zatuonyesha du’aa za
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya Swalah kwa njia ya
siri ila kwa wakati mwengine alikuwa akinyanyua sauti ili wafuasi wake wapate
kujifunza kwa njia sahali na rahisi.
Na maelezo yote hayo yanaweza
kufupishwa kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka Aliyesema:
“Na mkumbuke Mola Mlezi wako
nafsini kwako kwa unyenyekevu na khofu, na bila ya kupiga kelele kwa kauli,
asubuhi na jioni. Wala usiwe miongoni wa walioghafilika”
(al-A‘raaf [7]: 205).
Imaam ash-Shawkaaniy amesema
kuieleza Aayah hii katika tafsiri yake Fat-hul Qadiyr kuwa, “Hiyo ni
kuisikilizisha nafsi yake bila kutoa sauti, yaani kwa unyenyekevu na kwa khofu
na kuzungumza kwa mazungumzo chini ya kujihirisha”. Na Ibn Kathiyr naye amesema
katika tafsiri yake, Tafsiyr Qur-aanil ‘Adhwiym: “Mtaje Mola wako Mlezi kwa
matumaini na hofu na kwa kimoyomoyo, si kwa jahara. Na hivi ndivyo Dhikr
inavyopendekezwa iwe, si kwa sauti ya juu wala kwa jahara”.
Na Aayah hii inafafanuliwa na
Hadiyth iliyowazi kabisa kutoka kwa Abu Muusa al-Ash‘ariy (Radhiya Allaahu
‘anhu) alisema:
“Watu walinyanyua sauti zao
katika du’aa wakati wa baadhi ya safari, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) akawaambia: ‘Enyi watu! Jifanyieni wepesi katika nafsi zenu,
kwani mnayemwomba si kiziwi wala si wa kughibu. Kwa hakika mnayemwomba ni
Mwenye kusikia, wa karibu, yu karibu zaidi ya mmoja wenu kuliko shingo ya
mnyama wake” (al-Bukhaariy na Muslim).
No comments:
Post a Comment