Monday, February 20, 2012

MAANDIKO MATAKATIFU YA KIKRISTO

Dini iliyofunuliwa kutoka kwa Mungu ina nguvu na inakubalika sawa sawa na vile ufunuo ulivyo na nguvu na unavyokubalika. Kwa upande wa ukristo, msingi huu ambao ni mkubwa na mkuu kuliko yote ni dhaifu kabisa kutokana na kuingizwa mikono na akili za watu ndani ya Biblia. Ufunuo hauna mushkeli, tatizo ni juu ya nini kilitokea baina ya muda ufunuo ulipoteremka mpaka kipindi ufunuo huu ulipoandikwa.


Uchunguzi Makini Juu ya Agano La Kale
Wayahudi walishuhudia nyumba yao ya ibada ya Jerusalem ikiharibiwa kabisa mnamo mwaka 581 B.K. Pamoja na tukio hili pia, Torati yenyewe halisi pia iliharibiwa na baadaye walifanikiwa kurejesha hasara iliyotokea, lakini walizifanyia mabadiliko makubwa nakala chache zilizopata bahati ya kutoharibiwa kabla ya kuandika nakala nyingi zaidi kwa ajili ya matumizi ya kila mtu. Ukweli kwamba nakala chache za Agano la Kale zilizonusurika kuharibiwa zilizifanyiwa mabadiliko makubwa unakubalika na wasomi na wanazuoni wakubwa isipokuwa wachache. Mabadiliko yalifanywa katika fani (style) muundo wa lugha na sarufi (grammer), ili kuzipamba habari na visa mbalimbali vilivyomo katika Biblia, na pia walithubutu hata kuviondoa kabisa vitu ambavyo wao waandishi hawakuvifurahia. Kwa kifupi, kazi za waandishi hawa ziliathiriwa sana na wakati walioshi pamoja na hisia, maoni, na imani zao binafsi.

Mifano kadhaa ya maongezo na mapunguzo yaliyopelekea kuchafuliwa kwa agano la kale ni kama ifuatavyo:
1) Kuna aya mbili zinazotofautiana juu ya uumbaji zinazopatikana katika kitabu cha mwanzo: Katika sura ya kwanza imeandikwa kwamba uumbaji ulichukua siku sita. Ajabu ni kwamba katika sura ya pili, imeandikwa kwamba Mungu aliifanya kazi hii kwa siku moja (2:4). Tukiendelea na mikorogano hii iliyofanywa na waandishi ni juu ya ukweli kwamba Adam alikuwa ni kiumbe wa mwisho kuumbwa (1:27) wakati katika aya ya pili imeandikwa kwamba alikuwa ni kiumbe wa kwanza kuumbwa kabla ya kiumbe kingine chochote (2:4-9).
Tukiacha aya hizi mbili zinazotofautiana juu ya uumbaji, katika kifungu cha kwanza na cha pili pia kuna aya nyingine mbili zinazotofautiana juu ya gharika (mafuriko) katika kitabu cha mwanzo 6,7 na 8. Katika vifungu hivi, aya mbili zinatofautiana juu ya idadi ya wanyama ambao Nuhu aliwaingiza katika safina. Aya nyingine mbili zinatofautiana juu ya sababu ya gharika, na aya nyingine mbili zinatofautiana juu ya muda ambao mafuriko yalidumu.
2) Katika kitabu cha Mwanzo 22:2, Mungu anatoa amri ifuatayo kwa Nabii Ibrahimu:
"Mchukue sasa mwanao, Is-haq mwanao wa pekee".Hapa maneno "mwanao wa pekee" yeyote anaweza kukubali kwamba maneno haya yaliongezwa makusudi kwa lengo la kupotosha ukweli fulani kwa sababu wakati ule Ibrahimu alikuwa na watoto wawili Is-haq NA ndugu yake mkubwa Ismail, hakuwa Is-haq peke yake.
3) Na kama ni kweli kwamba Nabii Musa ndiye mwandishi wa kitabu cha kumbukumbu la Torati kama inavyodaiwa, inawezekanaje akaandika habari juu ya yaliyotokea wakati wa kifo chake kama inavyoonekana katika kumbukumbu la Torati kifungu cha 34?
Pia kuna suala juu ya jinsi Mungu anavyoonyeshwa katika Agano la kale kuwa ni katili na asiyekuwa na huruma hata kidogo:
1) Katika kitabu cha Hesabu 21:5-6, inaonyesha kwamba Mungu alipeleka nyoka wenye sumu kali kwa Wayahudi ambapo wetu wengi waliumwa na kufa kwa sababu tu walilalamika juu ya chakula chao.
2) Katika kumbukumbu la Torati 7:2, inaonyesha kwamba Mungu aliwaamuru Wayahudi wawaue watu wote watakaowakamata kama mateka katika vita - wasionyeshe huruma na rehema hata kidogo.
3) Katika Samuel wa Pili 24:1-7, inaonyesha kwamba Wayahudi 70,000 walikufa kutokana na maradhi hatari ya kuambukiza yaliyoletwa na Mungu kwa sababu ya kutoridhishwa kwake na sensa (kuhesabu watu) iliyofanywa na Daud.
Mbali na kuonyeshwa sifa hizi za kutisha alizonazo Mwenyezi Mungu, kuna mifano mingi; inayowa dhalilisha mitume mbalimbali wa Mwenyezi Mungu:
1) Mabinti wa Luti walimnywesha pombe baba yao ili waweze kufanya naye mapenzi katika kitabu cha Mwanzo 19:30-38.
2) Inasemekana kwamba Daud alikuwa mzinifu katika Samwel wa pili 11:4-5.
3) Inasemekana Suleimani alikuwa muabudu masanamu katika Wafalme wa Pili 11:9-10.
Ndiyo, ni muhimu kujua kuwa Mitume hawa wa mwanzo walikuwa ni wanadamu katika nyanja zote, lakini kusema kuwa walifanya hayo yaliyotajwa hapo juu ni kuvuka mpaka MNO.
Haya sio yote. Katika vitabu vya Samueli, Wafalme na Mambo ya Nyakati kuna matukio mengi kama haya yaliyotokea katika historia ya mwanzo ya kiyahudi na pia ndani yake kuna idadi kubwa ya migongano na kupingana katika uelezeaji wa matukio haya. Kitabu cha Isaya, ambacho ni kitabu kinachopendwa sana cha "utabiri" kwa Wakristo kinatofautiana na vingine kwa kuwa na mifano inayonga'a ya maovu katika Agano la kale. Kwa mfano nukuu ya neno kwa neno, tazama Isaya 37, ambapo takribani ni nukuu ya neno kwa neno ya jitihada za mtunzi (mwandishi) wa Biblia inayopatikana katika Wafalme wa Pili 19.
Hii ni mifano michache tu inayoweza kupatikana katika Agano la Kale katika kuthibitisha tuhuma kwamba Biblia imebadilishwa mara kadhaa na kupotolewa na mikono ya watu. Ni vigumu kuzitetea tuhuma hizi hasa kwa sababu kuna mifano mingi mno inayothibitisha tuhuma hizi katika Biblia tukiachilia ukweli kwamba hakuna maandiko ya asili (original) ya Agano la Kale yaliyopo leo hii.

Uchunguzi Makini Juu Ya Agano Jipya
Ambapo Agano la kale lina umuhimu mkubwa sana kwa Wayahudi, kwa Wakristo halina nafasi muhimu kiasi hicho ambapo wao wanaliona kuwa kwa sehemu kubwa ni mkusanyiko wa utabiri wa manabii juu ya kuja kwa Yesu. Amri na mafundisho yake hayana uthabiti wala umuhimu wowote kwao.
Mapenzi ya Wakristo yapo kwenye Agano Jipya. Katika vitabu hivi 27 vya Agano Jipya kimsingi kuna maandiko ya Paulo; vitabu ambavyo vinajumuisha vitabu vinne vya Injili - ambavyo ilivyo hakuviandika kwa mkono wake japokuwa alianzisha wazo la kuviandika. Kwa asili, maelekezo yote ya kuandika vitabu hivi yalitolewa na Paulo.
Baada ya kufanya uchunguzi makini katika vitabu vyote viwili, Biblia na Quran, Dr. Maurice Bucaille anasema kwamba: "---- kuzisoma injili kikamilifu (vitabu vinne vya Injili) ni kama kuwayumbisha na kuwavuruga Wakristo kabisa".[16]
Ametoa maelezo haya kwa sababu kwa mujibu wa utafiti wake, migongano, mikorogano, umyakinifu, uwingi wa makosa na upotoshaji wa maandiko: "--- vinaongezea juu ya ukweli kwamba vitabu vya Injili vina sura na vifungu ambavyo bila chembe ya shaka ni zao la fikra na ubunifu wa wanadamu".[17]
Mifano mbalimbali juu ya migongano katika vitabu vya Injili ni:
1) Injili ya Mathayo ina mtiririko wa kizazi cha Yesu (Mathayo 1:7) ambapo unamuonyesha kutoka kwa Ibrahimu hadi kwa Suleiman, mtoto wa Daud, ambapo mtiririko wa kizazi hiki katika Injili ya Luka (3:31) unamuonyesha Yesu kutoka kwa Adam kupitia kwa Nathan ambaye ni mtoto mwingine wa Ibrahim asiyekuwa Suleiman kama ilivyo katika Mathayo. Na hata mtu akijaribu kulinganisha majina yaliyopo katika orodha ya Mathayo na ile ya Luka hayawiani kabisa.
Nukta muhimu ya kuzingatia hapa ni kwamba aina YOYOTE ya mtiririko wa kizazi Yesu kwa Ukoo wa ubabani kupitia kwa Yosefu ni jambo la kichekesho kwa sababu Yesu hakuwa na baba wa kibailojia. Ukoo sahihi wa Yesu unaweza kuwa ni ule unaopitia kwa mama yake, Mariam - sio kwa Yosefu (Yusuf).
2) Injili ya Yohana inakhitilafiana sana na Injili nyingine tatu katika KILA upande na sura ya maisha ya Yesu na kazi yake kama vile sehemu alipozaliwa na kukua, ubatizo wake, na hata maeneo aliyofanya kazi na ukubwa wa kazi yake. Inasemekana kwamba 92% ya maelezo na habari zilizomo katika injili ya Yohana hayamo kabisa katika zile injili nyingine tatu.[18]
Moja ya tofauti kubwa kati ya injili ya Yohana na zile nyingine tatu ni kwamba Yohana hasemi lolote juu ya Komunio Takatifu (chakula cha Bwana yaani mkate na divai). Katika maelezo ya Yohana juu ya Karamu (chakula) ya Mwisho, inayopatikana katika vifungu vya 13-17, Yesu anawaosha wanafunzi wake miguu na kisha anatoa hotuba ndefu ambapo sasa inaonyesha kutatanisha kidogo juu ya Mfariji atakaye kuja baada yake, hapakugusiwa hata kidogo juu ya komunio takatifu - yaani mkate (mwili wa Bwana) na divai (damu ya Bwana) ambayo ni jambo muhimu mno kwa Ukristo leo hii.
3) Mathayo na Yohana hawajazungumza lolote juu ya kupaa kwa Yesu. Luka ameandika juu ya hili katika Injili yake na pia katika kitabu chake kingine kiitwacho Matendo ya Mitume wakati na mahali vinatofautiana kuhusiana na mada hii katika vitabu hivi viwili.
Marko pia anazungumzia juu ya kupaa kwa Yesu, lakini sasa hivi wanazuoni na wasomi wa Biblia wanakubali kwamba taarifa yote juu ya tukio la kupaa mbinguni kama ilivyoandikwa katika injili ya Marko "Sio sahihi" (angalia sehemu ya mbele kuhusiana na aya zinazothibitisha hili).
Kuhusiana na "mafundisho tusiyokubaliana nayo" hebu tuichunguze imani ya kafara, (yaani kwamba Yesu aliteswa na kuuawa ili awe kafara ya dhambi za wanadamu) ambayo imejengwa juu ya msingi kwamba Yesu alikuwa kiumbe mkamilifu katika kila hali. Mtu anaweza kushangaa, kutokana na dai hili, vipi Wakristo wanazithibitisha nukuu (aya) mbalimbali katika vitabu vya injili zinazoonyesha kuwa Yesu hakuwa mkamilifu baadhi yake ni hizi zifuatazo:
1) Katika Mathayo 16:23, Yesu anamwita Petro "Shetani" na "mtego wa hatari". Petro anapojaribu kumkinga.
2) Katika marko 11, Yesu anaulaani mti kwa sababu tu haukuwa na matunda msimu ambao haukuwa wa matunda ilipotokea kwamba alikuwa na njaa na kupitia kuangalia kama kulikuwa tunda lolote na akawa hakupata.
3) Katika Yohana 2:1- 4, Yesu anaonyesha kukosa adabu kwa mama yake.
Katika Mathayo 28:19 Yesu anawaambia wanafunzi wake waende wakawabatize watu kwa jina la Baba na Mwana na Roho matakatifu. Ukweli kwamba maneno haya yaliongezwa baadaye katika Biblia inaweza kuthibitika kwa kusoma barua ya Paulo ambapo anasemahapo awali ubatizo ulifanyika kwa jina la Yesu peke yake.
Tunaona kwamba katika Marko, 16:15 Yesu anasema:
"Enendeni ulimwenguni kote, mkahubiri injili kwa watu wote (viumbe wote)".Marko anazungumzia katika 16:15 tukio lile lile linalozungumziwa na Mathayo katika 28:19, sasa maneno ya ziada tunayoyaona katika Mathayo (ambayo hayapo katika Marko) yametoka wapi?

Yesu Katika Injili
Kama ilivyodokezwa hapo awali, Agano Jipya, na hususan vitabu vitatu vya injili - lina nafasi maalumu kwa Wakristo. Wanavichukulia vitabu hivi vinne kama mwongozo, kwa sababu moja muhimu. Vitabu hivi vinne vya injili viliandikwa KWA AJILI YA Wakristo na viliandikwa NA Wakristo. Katika injili nne Yesu wa kihistoria amewekwa pembeni kwa manufaa ya Yesu aliyefanywa Mkristo (Paulo).
Waandishi wa injili wenyewe bado wana maswali mengi. Ingawa hakuna uhakika ni nani aliyeziandika injili hizi nne, wanazuoni wengi wa Biblia wamekubaliana kwamba Mathayo na Marko hawakuwa waandishi wa injili zinazobeba majina yao. Injili ya Luka inadhaniwa kuandikwa na rafiki wa Paulo ambaye alikuwa mtu wa mataifa (Hakuwa myahudi) ambaye hakuwahi hata kumuona Yesu; ni sehemu ya kwanza ya maandiko yake juu Ukristo wa Mwanzo ambayo inajumuisha kitabu cha Matendo ya Mitume. Ingawa wakristo wengi wanasema kwamba injili ya Yohana iliandikwa na mwanafunzi wa Yesu aliyekuwa na jina kama hili (yaani Yohana). Sasa hivi wanazuoni wa Biblia wanatia mashaka juu ya hili kutokana na ukweli kwamba kitabu hiki kiliandikwa mwaka 100 Baada ya kristo, na Yohana, mwanafunzi wa Yesu alikufa shahidi mwaka 70 Baada ya kristo, miaka 30 baada ya kifo chake.
Katika kuikubali nadharia kwamba watu wengine tofauti na wanafunzi wa Yesu waliandika vitabu vinne vya injili lazima pia ikubalike kwamba waandishi hawa inawezekana kwamba hawakuona kwa macho yao au kusikia kwa masikio yao mengi - kama si yote - ya matukio waliyoyaandika. Hata tukiamua kusema kwamba wanafunzi wa Yesu waliziandika injili kwa mikono yao, tunaelewa kwamba hawakushuhudia matukio yaliyotokea pindi Yesu alipochukuliwa na maaskari kutoka katika Bustani ya Gethsemane kwa sababu imeandikwa: "- - kisha wanafunzi wote walimuacha wakakimbia --", katika injili zote mbili katika Mathayo 26:56 na katika Marko 14:50. Kwa kifupi, mengi tunayoyaona katika injili ni fununu na tetesi tu - si maandiko ya watu, walioshuhudia matukio yenyewe.
Nukta nyingine tunayoweza kuiangalia katika uchunguzi wetu juu ya injili ni kwamba katika injili zote nne hakuna hata moja iliyoandikwa wakati wa Yesu, ikizingatiwa kuwa hakuna taarifa iliyohifadhiwa juu ya kazi zake (Yesu) katika wakati wa uhai wake. Kwa kweli, karibu miaka arobaini ilipita kuanzia kipindi Yesu alipoondoka duniani mpaka kitabu cha kwanza cha injili kilipoandikwa. Mwishoni wakati injili ya Marko inakuwa tayari, Paulo alikuwa ameshaanza kuhubiri kwa takriban miaka ishirini; na alikuwa tayari ameshaandika barua (waraka) yake kwa Warumi, ambapo alielezea imani na mafundisho yake yote aliyoyaandaa na kuyaingiza katika Ukristo. Kutokana na ukweli huu tunaweza kuona kwamba mafundisho ya Paulo, bila chembe yoyote ya shaka, yaliwaathiri na kuwavuta waandishi wa injili kwa kiasi kikubwa katika maandiko waliyoyaandika.
Vitabu vinne vya injili viliandikwa kati ya miaka 70 B.K. na 100 B.K. ya Marko ilikuwa ya kwanza, ikafuatiwa na ya Mathayo, kisha Luka na mwisho Yohana. Injili tatu za mwanzo zinafanana sana katika uandishi wake, uchunguzi wa haraka utaonyesha kwamba waandishi wa injili ya Mathayo na Luka walichukua (waliibia) habari nyingi sana kutoka kwa Marko walipokuwa wanaandika injili zao. Hii ndio sababu injili hizi tatu zinaonekana kuelezea kitu kimoja.
Injili ya Yohana inatofautiana sana na injili nyingine, hata hivyo hii ndio yenye mashaka zaidi juu ya ukweli na usahihi wake hasa kwa sababu mwandishi alijishughulisha zaidi na umuhimu wa Yesu katika imani ya ukristo kuliko yale yaliyosemwa na kufanywa naYesu.
Tunaweza kuhitimisha, kwa sababu ya uchache wa muda, kwamba kuandika kutokana na tetesi au fununu, na mvuto wa Paulo aliowaathiri waandishi, sura ya Yesu iliyoletwa kwetu katika injili si ya yule Yesu wa kihistoria (Yesu halisi). Badala yake, waandishi hawa waliandika juu ya Yesu aliyetokana na masimulizi ya kale, kwa kutumia hoja ya kithiolojia kwamba waandishi hawa waliukristisha ukweli (yaani waliufanya ukweli uwe wa Kikristo). Waandishi walikuwa na imani kali za kikristo, na waliandika wakiwa na mtazamo huu akilini.
Matokeo yake ni kwamba injili hizi nne zina visa na masimulizi ya kale badala ya ukweli. Ujumbe wa Yesu aliokuja nao kutoka kwa Mungu wote umepotea kwa sababu ya shinikizo la yale ambayo watu walitaraji na kutaka Yesu aseme na kufanya badala ya lile lililofanyika kiukweli.

Nakala za Nakala za Biblia
Nakala zote za mwanzo za Biblia zilikuwa ni nakala tu. Nakala hizi ziliandikwa kwa mkono. Nakala ya kwanza kuchapwa kwa mashine ilitoka katika karne ya kumi na tatu ambayo iliitwa Biblia ya "Gutenburg". Maandiko ya asili (original manuscripts) yalitupiliwa mbali na badala yake zikaanza kutumika nakala mpya kwa sababu zile zilikuwa zimechoka na kuchanika chanika kutokana na kutumiwa kwa muda mrefu. Nakala hizi mpya baadaye, zilitumika kutengenezea nakala nyingi zaidi.
Hata hivyo, kila nakala iliyotengezwa, ilimaanisha kuwepo kwa nafasi zaidi ya kufanya mabadiliko - aidha ya bahati mbaya au ya makusudi ambayo yote haya yaliingizwa katika Biblia. Kama ilivyokuwa kwa Agano la Kale, Agano Jipya pia lilipatwa na balaa la kuongezewa na kupunguziwa baadhi ya maneno, aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya kutoka kwa waandishi wake.
Ni lazima ionyeshwe kwamba hakukuwa na namna yoyote ya kurudi nyuma na kuangalia usahihi wa kazi za waandishi hasa kwa vile hakuna maandiko ya asili (original manuscripts) ya Agano la Kale wala Jipya. Nakala zilizopo ambazo tunaweza kusema ni za zamani kabisa ni za karne ya saba au ya nane baada ya kristo ambapo zilichambuliwa na kuchaguliwa ambazo ni bora zaidi kutokana na nakala nyingi na za aina mbalimbali zilizokuwepo wakati ule. Kwa upande wa Agano Jipya hakuna nakala ya asili iliyopo. Tuna nakala tu, ambazo tunaweza kusema ni za zamani zaidi ambazo ziliandikwa katika karne ya nne, kipindi ambacho maandiko "rasmi au maandiko ya kiofisi" yaliwekwa na kanisa. Ukosefu huu wa nakala za asili (original manuscripts) uliondoa kabisa uwezekano kwa yeyote kujaribu kukagua usahili; na mabadiliko mbalimbali yaliyopenyezwa katika Biblia.

Suala la Kutokamilika
Makanisa ya mwanzo ya kikristo hayakuwa na seti maalum (ya kiofisi - rasmi) ya maandiko Matakatifu. Baadhi ya Makanisa yalikuwa na seti fulani ya vitabu wakati Makanisa mengine yalikuwa na seti tofauti ya vitabu. Kuna baadhi ya watu waliridhika hata kuwa na kitabu kimoja cha Injili katika vinne, wakiamini kwamba vyote vilikuwa sawa na vilikuwa na habari moja.
Kulikuwa hata vitabu ambavyo katika Biblia za leo havimo - kwa mfano kulikuwa vitabu kumi na tano vilivyozidi katika Agano la kale na vitabu kumi na sita katika Agano Jipya.
Kutokana na ukosefu wa mpangilio maalum katika kanisa kuhusiana na maandiko yake Matakatifu, Maaskofu walikutana pamoja ili kuweka sera ya kiofisi ya kanisa kuhusiana na suala la utatu Mtakatifu katika Mkutano wa Nicea mwaka 325 B.K. ambapo pia waliandaa na kujiwekea Maandiko Maalum Rasmi yatakayotumika katika Kanisa.
Walikusanya nakala moja kwa kila aina (seti) ya maandiko aliyokuwa ikitumika wakati ule na wakafanya maamuzi juu ya ni vitabu vipi vitambulike kuwa ndio maalum na rasmi kwa Wakristo wote na nchi zote za Kikristo (kuwa ni Maandiko Matakatifu). Hatimaye vitabu sitini na sita vilichaguliwa, 39 kwa ajili ya Agano la Kale na 27 kwa ajili ya Agano Jipya.
Vitabu saba katika kumi na tano vilivyozidi katika vitabu vya Agano la Kale viliendelea kutumiwa na kanisa Katoliki, lakini hata hivi baadaye vilitupiliwa mbali na Waprotestanti wakati wa harakati za mageuzi katika karne ya kumi na sita. HAKUNA HATA KIMOJA katika vitabu kumi na sita "vilivyozidi" vya Agano Jipya kilichofanywa kuwa ni sehemu ya Maandiko Matakatifu maalum na rasmi yanayotumika.
Vitabu hivi vilivyozidi vilipewa jina la "Apocrypha" - - neno la kigiriki lenye maana ya "iliyofichika" - vitabu hivi vya ziada ambavyo hapo awali vilikuwa sehemu ya Biblia vilitupiliwa mbali kwa kile kilichodaiwa na viongozi wa kanisa kuwa "vilikhitilafiana" na imani zilizokuwa zikikubaliwa na kanisa. "Waandishi wa vitabu vya Aprocrypha (yaani vitabu vya ziada) bila shaka walikuwa wachamungu na waliofanya kazi kwa dhati na uhodari mkubwa - na tukisoma waliyoyaandika, mara moja tutagundua kwamba maneno yao -- yalikuwa yameepukana na udhaifu wa kutokuwa sifa za kuwa maandiko matakatifu --".[19]
La kushangaza zaidi ni kwamba rejea ya baadhi ya vitabu hivi vilivyofichikana (Apocrypha) zinaweza kupatikana katika Biblia ya leo inayotambulika kiofisi kama vile "kitabu cha vita vya Yehova" kilichotajwa katika Hesabu 21:14 "kitabu cha Jashar" kilichotajwa katika Joshua 10:13.
Hivyo, Biblia, tuliyonayo leo hii, si tu kwamba imekuwa (victim) muhanga wa kuingiliwa, kuongezwa na kupunguzwa bali pia haiwezi kuchukuliwa kuwa ni kamilifu. Inawezekanaje Maneno ya Mungu yakaondolewa na kutupiliwa mbali kwa sababu ya matakwa ya mwanaadamu?

Tatizo la Kutafsiri
Wataliano wana usemo usemao "Wafasiri ni waongo". Msemo huu una ukweli ndani yake na umetokana na uchunguzi makini. Kuchukua kitu fulani kilichoandikwa katika lugha fulani na kujaribu kukiingiza katika lugha nyingine huwa inaleta matatizo kwa sababu mara nyingi wafasiri hupambana na maneno katika lugha moja ambayo hayamo katika lugha nyingine. Neno jingine badala yake lazima litumike na matokeo yake ni kubadilika kwa maana.
Agano la kale mwanzo kabisa liliandikwa kwa Kiebrania, lakini lilitafsiriwa katika karne ya tatu kwenda katika lugha ya Kigiriki kwa ajili ya Wayahudi waliokuwa wanaishi nje ya Palestina (ambao walikuwa wanaongea Kigiriki - badala ya Kiebrania). Tafsiri hii iliitwa "septuagint" na ilitumika sana hata na wakristo wa mwanzo.
Agano Jipya liliandikwa katika lugha ya Kigiriki lakini maadamYesu mwenyewe alitumia lugha ya kiaramaiki, hii ina maana kwamba maneno yake yalilazimika kutafsiriwa na hivyo kusababisha uwezekano wa makosa
Tafsiri ya kigiriki iliyokuwa ikiitwa Septuagint iliunganishwa na maandiko ya Agano Jipya yaliyokuwa katika lugha ya kigiriki katika karne ya nne. Maandiko haya yaliyounda Biblia kamili sasa hivi yanaeleweka kama "Codexsinaiticus" na "Codex Vaticanus" na hizi ndio nakala za maandiko ya zamani kabisa zilizopo leo. Hakuna maandiko ya mwanzo kuliko haya yaliyonusurika kutupiliwa mbali.
Katika karne ya nne, Biblia ilitafsiriwa kwenda katika lugha ya Kilatini na Mt. Jerome. Na hii ilibakia kuwa lugha ya Biblia hadi karne ya kumi na sita ambapo watu wa Mageuzi kama John Wycliffe, William Tyndale na Martin Luther walipoifasiri Biblia katika lugha mbalimbali za watu - jambo ambalo lilikuwa haliruhusiwi kabisa na viongozi wa kanisa wa wakati ule na ili kufanikisha lilimgharimu Tyndale maisha yake. Walifanya hivi ili kuwazuia watu kuyasoma, kuyaelewa au kuyahisi maandiko yao Matakatifu - haya yalifanywa makusudi na viongozi wa kanisa.
Tafsiri nyingine zilifuatia ndani ya muda mfupi. Karibu na mwisho wa karne ya kumi na sita kulikuwa na tafsiri za lugha mbalimbali na tafsiri mbalimbali za lugha moja ambazo zilileta malumbano na mabishano makubwa jambo lililomfanya Mfalme James I wa Uingereza kuteua kamati ya wanazuoni hamsini na nne ili kuandaa toleo "rasmi" na litakalotambulika na mamlaka. Watu hawa (kamati) walizisoma tafsiri zote zilizokuwepo wakati ule na, mnamo mwaka 1611, walitoa toleo lililoitwa "King James Versions of the Bible" yaani toleo la Biblia la Mfalme James - ambalo lilikuwa ndio toleo rasmi miongoni mwa Wakristo kwa mamia ya miaka.

Tatizo Lililopo Leo: Matoleo Mapya
Tatizo la uharibifu na upotoshaji lililoambatana na kutafsiri liliisha mwaka 1611, kwa kupatikana toleo la King James Versions of the Bible, tatizo la marudio - - "kuiboresha" au kuifanya kuwa ya "kisasa" limeikabili Biblia leo hii.
Kiwango cha uharibifu na upotoshaji huu ni kama ifuatavyo: katika mwaka 1952, makala yenye kichwa cha habari "Ukweli kuhusu Biblia" yalionekana katika gazeti la "Look" (Tazama). Makala haya yalisema kwamba kulikuwa makosa zaidi ya 20,000 (elfu ishirini) katika Agano Jipya peke yake. Mashahidi wa Yehova walilizungumzia suala hili katika toleo la Septemba, 1957 la gazeti lao la "Awake" (Amka) ambapo walisema "- - - Wafasiri walifanya makosa katika kufasiri (Biblia) ambayo yamesahihishwa na wanazuoni wa zama hizi- -"[20]. Mtu anaweza kujiuliza ni jambo la ajabu wanazuoni hawa walilifanya!!
Katika karne ya kumi na tisa, Wakristo waliamua kuiboresha lugha ilivyotumika katika King James Version. Jitihada zao zilizaa toleo jipya la Biblia liitwalo "American Standard Version" lililotolewa mwaka 1901. Wakristo waliolifanyia kazi toleo hili sio tu kwamba waliikuza na kuiboresha lugha bali pia walifanya mabadiliko katika Biblia yenyewe:
1) Katika kuuthibitisha ukweli kwamba baadhi ya maneno yaliondolewa na mengine kuongezwa, tunaweza kuangalia katika maandiko ya mwanzo ya Biblia yaliyokuwa katika lugha ya kigiriki toleo la Biblia la King James Version Yohana 5:8 ambapo imeandikwa "Baba, Mwana na Roho Mtakatifu". Lakini toleo jipya la American Standard Version, wanazuoni walibadilisha na badala yake wakatumia maneno "Roho, Maji na Damu".
2) Aya nzima inayopatikana katika Mathayo 17:21 ambayo inazungumzia juu ya ukuaji wa usafi wa kiroho kwa sala na kufunga iliondolewa kwenye American Standard Version, na neno "Kufunga" liliondolewa katika aya kama hii inayopatikana katika Marko 9:29.
Maelezo juu ya hili yanayopatikana katika sherehe yake (chini ya ukurasa) yanasema: "Mamlaka nyingi, baadhi zikiwa ni za zamani, zinaiingiza pia aya 21" (ambapo katika Biblia za sasa aya hii ya 21 imeondelewa).
3) Katika kukubali ukweli mwingine juu ya uongezaji na upunguzaji wa baadhi ya maneno katika Maandiko Matakatifu (Biblia), vifungu vya Yohana 7:53 na Yohana 8:1-11 umefungiwa mabano na katika sherehe yake (maelezo ya ziada) wameeleza kwamba vifungu hivi "havipatikani katika Biblia (Maandiko matakatifu) nyingi za zamani".
Baada ya miaka kadhaa viongozi wa kanisa walikutana wakaamua kuliboresha toleo la Biblia la American Standard Version. Matokeo ya jitihada zao ilikuwa ni kupatikana toleo jingine la Biblia linalojulikana kama "The Revised Standard Version" - yaani toleo la Biblia la kiwango bora na lililofanyiwa marekebisho. Toleo hili lilitoka rasmi mwaka 1952.
Katika dibaji ya Toleo hili kuna maelezo haya: "- - - Toleo la King James (King James Version) lina makosa na mapungufu mengi mno na hatari sana kiasi kwamba kuna haja kubwa ya kulifanyia marudio na marekebisho toleo zima - -".
Katika toleo la Biblia la 'The Revised Standard Version' tunakuta kwamba aya katika injili ya Marko zinazozungumzia juu ya kupaa kwa Yesu (Marko 16 : 9-20) zimeondolewa kwa madai kwamba aya hizi hazipatikani katika Biblia (maandiko) za zamani kabisa.
Katika mwaka 1989, toleo la Biblia la 'The Revised Standard Version' la 1952 liliboreshwa tena na hivyo likapatikana toleo jipya "The New Revised Standard Version". Na katika toleo hili aya zinazozungumzia juu ya kupaa kwa Yesu katika Marko 16 zilirejeshwa. Kwa vile Wakristo wengi hawakufurahia "kumomonyolewa" kwa moja ya imani zao za msingi kulikofanywa na Wahariri wa "The Revised Standard Version", ilibidi aya hizi zirejeshwe ili kuwaridhisha.
Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema, kutokana na marudio ya mara kwa mara yaliyofanyika kwa miaka mingi wakati wa kufasiri na "Matoleo" mbalimbali mapya katika Biblia tuliyonayo leo maandiko ya wanadamu ndio mengi zaidi kuliko ufunuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Wakristo Wenyewe Wanasemaje
Juu ya Tatizo Hili
Huko nyuma katika karne ya nne, Mt. Augustino aligundua makosa mengi, ndani ya Biblia. Akizungumzia juu ya suala hili katika barua yake Na. 82. Alisema kwamba makosa katika uelewaji ndio sababu ya tatizo hili (la kuona aya zinapingana, na nyingine zipo katika toleo hili, lakini katika toleo jingine hazipo na utatanishi mwingine mwingi). Anasema yeye haamini kwamba watu kuongeza, kupunguza na kubadilisha baadhi ya mambo katika Biblia kuwa ni tatizo ila tatizo ni uelewaji mbaya katika usomaji. Kwa maneno mengine anasema kwamba baada ya msomaji kukumbana na mikorogano hii katika Biblia anatakiwa abuni maelezo fulani yatakayokuwa ni msamaha wa makosa haya.
Utafiti unaojaribu kuangalia na kuonyesha makosa katika Maandiko Matakatifu, tofauti na watu wengi wanavyofikiri, umeanza hivi karibuni. Kwa mamia ya miaka Biblia ilikubalika tu "kama ilivyo". Ilichukuliwa kuwa ni dhambi kubwa sana kujaribu kukosoa kosa, hata dogo lililomo ndani ya Biblia na viongozi wa kanisa walifanikiwa sana kuyazima majaribio yoyote ya kujaribu kuikosoa Biblia.
Kitabu cha kwanza kuonyesha na kukosoa makosa katika Biblia kilichoandikwa na Richard Simon kiitwacho Critical History of the Old Testament (Historia inayojaribu kuonyesha na kukosoa makosa yaliyomo katika Agano la kale), kilitoka mwaka 1678. Kitabu hiki kilileta tafrani na mtafaruku mkubwa lakini kilisaidia sana kufungua njia kwa wale waliokuja baadaye katika karne ya 18 na 19 kwa dhumuni la kufanya utafiti juu ya makosa yaliyomo katika Agano la Kale.
Kutokana na ukweli mwingi usiopingika uliotolewa na watu mbalimbali, Halmashauri ya awamu ya Pili ya Vatican (1962- 1965) ilitoa maelezo yanayoshangaza juu ya jambo hili "- - - Vitabu vya Agano la Kale vina (ndani yake) habari zisizo sahihi na zenye mapungufu mengi --."[21]
Agano Jipya pia lina kasoro na mapungufu mengi. Ingawa Halmashauri ya awamu ya pili ya Vatican inashikilia kwamba Injili "kihistoria ni ya kweli " na kwamba wao "kwa uaminifu kabisa wanaeneza yale ambayo Yesu alifanya na kufundisha watu wakati wa maisha yake".[22] Wanazuoni wengine wamekuwa na maelezo ambayo ni kinyume kabisa na msimamo wa Vatican.
Katika kitabu chake "The Call of the Minaret" (Wito kutoka katika mnara wa msikiti, Adhana), Dr. Kenneth Cragg anasema kwamba kuna "mambo yaliyoongezwa na kupunguzwa" katika Agano Jipya Injili na ni kazi ya akili ya viongozi wa kanisa ikiongozwa na waandishi, na kwamba katika kazi zao wanatumia uzoefu na historia."[23]
Padre Kannengiesser, Profesa katika taasisi ya kikatoliki katika mji wa Paris, alionya katika kitabu chake "Faith in Resurrection" (Imani juu ya ufunuo), kwamba watu wasijaribu "kuyatafsiri na kuyaelewa maneno kama yalivyo" juu taarifa za kweli kuhusiana na Yesu katika Injili - onyo ambalo pia lilitolewa na Padre Rognet wa Paris katika kitabu chake "Initiation to the Gospels".
Carl Andrey, profesa wa falsafa na masomo ya dini katika Chuo kikuu cha Ball State kilichopo Indiana anasema kwamba vitabu vinne vya Injili: "- - - viliandikwa na watu wenye shauku wa harakati za mwanzo za kikristo na kwamba wanatupatia nusu tu ya habari kamili na kwa kiasi kikubwa ni mazao ya fikra za waandishi wao"[24]
Mwisho tuna maelezo ya Dr. W. Graham Scroggie wa "Prestigious Moody Bible Institute" ambaye anasema: "Ndiyo, Biblia ni zao la kazi iliyofanywa na binadamu - - - vitabu hivyo vimetokana na akili za watu, vimeandikwa kwa mikono ya watu, na fani ya uandishi wake ni ya kibinadamu.[25]
Kama huu ndio msimamo wa wanazuoni wa Biblia, wakristo wa "kawaida" watakuwa na lipi la kusema juu ya jambo hili?
Wengi (wa wakristo wa kawaida) hata hawajui lolote juu ya kasoro nyingi zilizomo ndani ya Biblia kwa sababu waandishi wa utangulizi na washereheshaji (wanatoa maelezo ya ziada) wa Biblia. Wanatumia mbinu mbalimbali za kijanja ili kuwafanya Wakristo wasiyajali na wajisahaulishe na maswali ambayo wangejiuliza juu ya kasoro nyingi zilizomo ndani ya Biblia. Pamoja na mambo mengine, waandishi hawa:
1) Wanaandika mambo kama ukweli uliothibitika wakati ukweli na uthabiti wake una mashaka, na
2) Wanayafunika makosa na kasoro zilizomo ndani ya Biblia kwa kutoa nyudhuru na kuomba radhi mbinu ambayo inaondoa umakini wa msomaji kutoka kwenye dosari na kasoro zilizomo ndani ya Biblia na badala yake kuangalia mambo mengine.
Kina wanachokwenda washereheshaji (Commentators) katika kujaribu kutetea kasoro na dosari zilizomo ndani ya Biblia ni alama na ushahidi tosha juu kutojisikia kwao vizuri na ugumu wanaoupata katika jitihada zao za kujaribu kutetea makosa, dosari na kasoro zilizomo ndani ya Biblia.
Pamoja na ukweli huu juu ya kasoro na dosari zilizomo ndani ya Biblia, ajabu ni kwamba mtu anapojaribu kuzionyesha hataambulia chochote kutoka kwa wakristo isipokuwa uadui. Niliwahi kupeleka makaratasi yenye utafiti wangu juu ya kasoro na dosari mbalimbali zilizomo ndani ya Biblia katika mishenari ya kikristo ambapo walinijia muda mfupi baadaye wakinishutumu kwa kufanya "uvamizi dhidi ya Biblia. Muongeaji aliendelea kusema kwamba "Biblia imefanyiwa uvamizi (imevamiwa) kwa karne nyingi, lakini bado ipo. Imestahimili vishindo (vyote) vya nje na ndani".[26]
Nastaajabu vipi mtu awe na msimamo kama huu mbele ya mifano tele inayoweza kuthibitishwa, sielewi anamaanisha nini katika neno "vishindo". Labda linaendeleza lile linalopatikana katika "kazi bora " ya vitabu vinavyotetea dosari na kasoro zilizomo katika vitabu vya Kikristo iliyomo katika kitabu kiitwacho "Is Bible Reliable. (Je, Biblia inaaminika?).
Katika kitabu hiki, mwandishi Bjug Horstal anasema kwamba Mungu "aliwashawishi" waandishi wa Maandiko Matakatifu "- - - kuandika kasoro na dosari zilizoambatana (zinazotokana) na lugha , na kwamba tunatakiwa tuliache jambo hili kwa Mungu mwenyewe, awe huru kutumia idadi yoyote ile ya fani na hata udhaifu wa kibinadamu kama anavyotaka mwenyewe - - -".[27]
Mashahidi wa Yehova wameandika kitabu kizima kiitwacho: Bible: God's Word or Man's? (Biblia: Ni neno la Mungu au la Mwanaadamu?), ambacho kinazungumzia kasoro na dosari zilizomo ndani ya Biblia. Katika kitabu hiki, wamelizungumzia suala hili kwa namna tofauti na ya pekee kwa kusema kwamba: 'kuna baadhi ya "kasoro na dosari za wazi" katika Biblia ambazo "ni vigumu kuzitetea". Hata hivyo tusizichukulie dosari na kasoro hizi kuwa ni kugongana na kupingana kwa aya za Biblia; mara nyingi ni kwa sababu ya ukosefu wa taarifa na habari kamili'.[28]
Nilibahatika kupata nakala ya tafsiri ya Biblia ya Mashahidi wa Yehova "The New World Translation of the Holy Scriptures". Nilimuuliza mjumbe mmoja wa ngazi za juu wa jopo la Wafasiri wa mjini petu kuwa ana maelezo gani juu ya aya ya Mathayo 17:21, ambayo inasomeka: "Hakuna aya, kuna namba tu mstari mrefu ulio wazi". Mjumbe yule alibabaika sana alipoangalia sehemu hiyo. Akaahidi kuwa angekuja kuniona kwa mara nyingine tena ningependa kujua anasemaje kuhusiana na suala hili.
Kwa kifupi, Wakristo hawako tayari kuukubali ukweli kwamba Maandiko yao Matakatifu yamepotolewa kwa madai kwamba, ikiwa msingi utayumba na kutokuwa na uhakika, je tutasimama juu ya nini katika siku za masaibu na mashaka?"[29]
Sio hayo tu, bali kuna aya inayozungumzia juu ya kuyabadilisha maandiko matakatifu katika maandiko hayo hayo:
" - - - ikiwa mtu yeyote ataongeza (au kufuta) neno lolote katika kitabu hiki, Mungu atamuongezea balaa zilizoandikwa katika kitabu hiki". (Ufunuo 22:18,19)Ushahidi uko hapo, upo wazi na rahisi kwa kila mtu kuelewa. Ikiwa Mungu aliwaongoza kwa ufunuo kuandika vitabu vya Biblia, hakuna shaka kwamba wanadamu wameingilia na kubadilisha mambo mengi. Swali muhimu kabisa la kumuuliza Mkristo ni kwamba: Inawezekanaje kwa neno la Mungu kubadilishwa, kuondolewa na hata kutupiliwa mbali kwa matakwa ya mwanaadamu??

Msimamo wa Uislamu
Suala zima la wanadamu kubadilisha maneno (ufunuo) wa Mwenyezi Mungu ndio ilikuwa sababu ya Mtume Muhammad (SAWW) kuteremshi wa Quran: Ufunuo wa mwisho kwa Mjumbe wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu.
Quran katika aya zake kadhaa inazungumzia juu ya kubadilishwa, kupunguzwa na hata kuondolewa kwa baadhi ya mambo katika Maandiko Matakatifu yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu kabla ya Qur'an. Baadhi ya aya ni kama vile.
" - - Walioruka mipaka (ya Mwenyezi Mungu) walibadilisha maneno kutoka katika yale waliyoteremshiwa". (Qur'an 2:59)
"Kundi moja miongoni mwao lilisikia Maneno ya Mwenyezi Mungu kisha likayabadili baada ya kuwa limeyaelewa (maneno hayo)". (Quran 2:75)
"Kuna sehemu (kundi) miongoni mwao ambao wanapotosha (wanakibadilisha) Kitabu (cha Mwenyezi Mungu) kwa ndimi zao pindi wanaposoma ili ufikiri kuwa ni sehemu ya kitabu (cha Mwenyezi Mungu). Lakini sio sehemu ya kitabu; na wanasema Hayo yametoka kwa Mwenyezi Mungu lakini sio --". (Qur'an 3:78)
Aya hizi zinaonyesha ukweli mwingine kwamba, japokuwa Waislamu wametakiwa kuamini ufunuo ulioteremshwa kabla ya Quran, imani juu ya vitabu hivi - - Taurati, Zaburi na Injili - - inamaanisha imani juu ya ufunuo HALISI (ORIGINAL) ulioteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; na si yale tunayoyakuta katika Biblia zetu za leo, wala si ule uliopatikana katika zama za Nabii Muhammad (SAWW).
Imani ya Waislamu ni kwamba Qur'an ililetwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kuyasahihisha na kuondoa mambo yote yaliyoongezwa na kuyarejesha yale yaliyoondolewa kwa makusudi na wanadamu katika ufunuo wake wa awali. Mwenyezi Mungu aliweka wazi kwamba huu, Ufunuo wake Mwisho, hautapatwa na masaibu na balaa la kupotolewa (kubadilishwa) kama vitabu vilivyotangulia:
"Bila shaka, Tumeiteremsha Quran, na bila shaka sisi ndio tutakaoilinda kutokana na kupotolewa". (Quran 15:9)Juu ya hili, Quran ina msimamo thabiti. Imebakia katika hali yake ya asili kama ilivyokuwa wakati ilipoteremshwa kwa Mtume Muhammad (SAWW). Na pia makaratasi yaliyoandikwa Quran juu yake yaliyoandikwa kwa mkono (Original Manuscripts) wakati wa Mtume bado yapo mpaka leo katika mji wa Madina, Arabia. Nakala ya Quran iliyoandikwa katika karne ya saba hii ni miongoni mwa nakala za mwanzo kabisa zinazoeleweka tulizonazo leo hii, na iliandikwa kwa mkono juu ya ngozi ya mnyama jamii ya swala miaka michache baada ya kutawafu Mtume Muhammad (SAWW). Nakala nyingine iliyoandikwa katika karne ya saba iliyoandikwa katika zama za Khalifa wa tatu, Uthman, ipo katika jumba la makumbusho la Topkapi, Istanbul, Uturuki. Ikiwa mtu atachukua Quran iliyo katika lugha ya kiarabu kisha akajaribu kulinganisha na nakala hizi zilizoandikwa katika karne ya saba hatakuta tofauti (khitilafu) yoyote.
Quran iliyo katika lugha ya kiarabu haijabadilishwa, kupunguzwa wala kuongezwa lolote licha ya kupita miaka zaidi ya 1400. Kutokana na hili, hakuna uthibitisho bora kuliko huu juu ya kutimia kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwa atailinda Quran dhidi ya mikono ya watu (kupotolewa), ambayo ni ufunuo wake wa mwisho.
Kuhusiana na waanadamu kuyabadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu, Qur'an inasema:
"Na wasomee na uwafundishe yale yaliyoteremka kwako katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, hakuna atakayeweza kuyabadili Maneno yake na hamtapata msaidizi mwingine yeyote badala Yake (Mwenyezi Mungu)". (Quran 18:27)[16] The Bible The Qur'an and Science, p. 44. (Biblia, Qur'an na Sayansi, uk. 44.)
[17] Ibid, p. 109. (Kitabu hicho hapo juu).
[18] All Scripture Is Inspired of God and Beneficial, p. 195. (Maandiko yote yametoka kwa Mungu na ni yenye Manufaa, uk. 195).
[19] Is the Bible Reliable? p. 30. (Je Biblia inaaminika? uk. 30)
[20] Awake! p. 26 (Amka! uk. 26).
[21] The Bible, the Qur'an and Science, p. 41. (Biblia, Qur'an na Sayansi, uk. 41).
[22] Ibid, p. 57. (Kitabu hicho hapo juu).
[23] Is the Bible God's Word? pp. 1,2 (Je Biblia ni Neno la Mungu? Uk. 1,2).
[24] Jesus and the Four Gospels, pp. 6,7. (Yesu na Injili nne, vitabu vinne vya injili, uk. 6,7).
[25] Is the Bible God's Word?, p. 1. (Je Biblia ni Neno la Mungu, uk . 1)
[26] Personal Communication, Del Kingsriter of Centre for Ministry to Muslims, March 3, 1993. (Mawasiliano ya mtu binafsi).
[27] Is the Bible Reliable? pp. 86, 87. (Je biblia inaaminika? Uk. 86, 87).
[28] The Bible: God's Word or Man's? p. 97. (Biblia ni neno la Mungu au la Mwanadamu? uk. 97).
[29] Is the Bible Reliable? p. 84. (Je Biblia inaaminika, uk. 84).

Imechukuliwa kutoka Al-Islam

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget