Uislamu ni mfumo kamili na sahihi wa maisha unaozienea nyanja zote za maisha ya mwanadamu katika hali, mahala na zama zote. Mfumo uliofumwa na Allah Mola Muumba ulimwengu na walimwengu kwa ajili ya waja wake na akawaleta kupitia mitume wake. Tangu Nabii Adamu mwanadamu wa kwanza mpaka Nabii Muhamad Mtume wa mwisho. Ili uwe ni muongozo na katiba ya kukiendesha kila kipengele cha maisha yao katika maisha haya ya mpito ya ulimwengu huu yenye dhima ya kuwaandaa na maisha ya milele ya Akhera.
Mambo yote haya kwa ujumla wake ndio nguzo madhubuti na imara zinazolibeba jengo Uislamu. Akida hii ya UISLAMU ni ndugu baba moja mama mmoja na akida za mbinguni zilizotangulia kabla yake. Ambazo zote zina dhima ya kulingania kheri (wema) na kukemea mambo maovu na machafu. Uislamu umekuja kuikamilisha dhima hii. Hii ndio AKIDA ya Uislamu kupitia kitabu cha Uislamu (Qur-ani Tukufu).
“MTUME AMEAMINI YALIYOTEREMSHWA KWAKE KUTOKA KWA MOLA WAKE NA WAISLAMU (Pia wameamini hayo). WOTE WAMEMUAMINI ALLAH, NA MALAIKA WAKE, NA VITABU VYAKE, NA MITUME YAKE (nao husema) HATUBAGUI BAINA YA YOYOTE KATIKA MITUME YAKE (wote tunawaamini)………..” (2:285)
Na Uislamu haumlazimishi mtu kuifuata Akida yake hii kwa nguvu bali aingie Uislamu baada ya kukinaishwa na hoja zake. Hivi ndivyo tunavyosema katika kitabu cha Uislamu: “WAITE (watu) KATIKA NJIA YA MOLA KWAKO KWA HEKIMA NA MAUIDHA (nasaha) MEMA NA UJADILIANE NAO KWA NAMNA ILIYO BORA………..” (16:125)
“HAKUNA KULAZIMISHWA (mtu kuingia) KATIKA DINI. UONGOFU UMEKWISHA PAMBANUKA NA UPOTOFU………..” (2:256) Isitoshe Uislamu unawafundisha waislamu namna ya kujadiliana na watu wa dini nyingine.
“WALA MSIJADILIANE NA WATU WALIOPEWA KITABU (kabla yenu) ILA KWA YALE (majadiliano) YALIYO MAZURI……….” (29: 46)
b./ SHERIA
Sheria ya kiislamu ni mkusanyiko wa maneno ya Allah Mola Mwenyezi (sheria mama) na maneno ya Mtume wake kama sheria shereheshi/fafanuzi. Sheria hii imezienea nyanja zote za maisha ya mwanadamu kuanzia yale ya kibinafsi mpaka ya kijamii. Inagusa matendeano ya kila siku baina ya watu, mahusiano ya watu wenyewe kwa wenyewe, watu wa viumbe wengine, watu na ulimwenguu wao na watu na Mola Muumba wao. Kama inavyogusa mfumo wa familia,
mirathi, ndoa, mazishi na kadhalika.
02:03 – NIKITAKA KUWA MUISLAMU NIFANYE NINI?
Uislamu unaamini kwamba kila mtoto anazaliwa hali ya kuwa tayari ni muislamu tokea tumboni mwa mama yake. Anabakia na Uislamu wake huo wa kuzaliwa mpaka anapofikia umri wa utu uzima (baleghe) hali ya kuwa na akili timamu. Katika umri huu ndipo anapoweza kuitumia akili na khiyari aliyopewa na Mola wake:
“…………. BASI ANAYETAKA NA AAMINI (awe muislamu) NA ANAYETAKA NA AKUFURU (awe kafiri). HAKIKA TUMEWAANDALIA MADHALIMU (Makafiri) MOTO AMBAO KUTA ZAKE ZITAWAZUNGUKA …………” (18: 29).
Akaukana na kuuvua Uislamu ndio umbile aliloumbiwa: “BASI UELEKEZE USO WAKO KATIKA DINI ILIYO SAWA SAWA NDILO UMBILE ALLAH ALILOWAUMBIA WATU (yaani dini hii ya kiislamu inawafikiana barabara na umbo la binadamu). HAKUNA MABADILIKO KATIKA MAUMBILE YA VIUMBE VYA ALLAH. HIYO NDIYO DINI ILIYO YA HAKI, LAKINI WATU WENGI HAWAJUI” (30:30)
Kwa kufuata mfumo mwingine wa maisha (dini) ulio nje ya Uislamu ambapo atakuwa amejitia khasarani mwenyewe: “NA ANAYETAKA DINI ISIYOKUWA YA KIISLAMU BASI HAITAKUBALIWA KWAKE NAYE AKHERA ATAKUWA KATIKA WENYE KHASARA (kubwa kabisa)” (3:85).
Sasa muasi huyu anapotaka baada ya kuamua kwa khiyari yake kurudi katika umbile lake la asili (Uislamu) hahitaji kubatizwa. Kitu pekee anachotakwia kufanya ni kutamka hadharani shahada mbili na kuishi kwa mujibu wa shahada mbili hizo.
02:04 – SHAHADA MBILI NI NINI?
Shahada mbili ni mkusanyiko wa matamko mawili ya ahadi anayoichukua kiumbe (mwanadamu) mbele ya Muumba wake na viumbe wenzake. Ambapo mtamkaji hula kiapo cha utii kwa Allah Mola Mwenyezi na Mtume wake katika maisha yake yote kwa kufuata maamrisho na makatazo yake.
1. SHAHADA YA KWANZA – TAMKO LA UTII KWA ALLAH:
Ni mtu kutamka kwa moyo na ulimi:-
“ASH – HADU AN LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU”
Maana : “Ninakiri kwa moyo na kutamka kwa ulimi kwamba hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah (Mola asiye na mshirika wala mwana)”
2. SHAHADA YA PILI: TAMKO LA UTII KWA MTUME WA ALLAH.
Ni mtu kutamka kwa moyo na ulimi:-
“WA ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN ABDUHU WA RASUULUHU”
Maana: “Na ninakiri kwa moyo natamka kwa ulimi kwamba Muhammad ni mja na mjumbe wa Allah (kama alivyo Isa, Musa, Ibrahimu) Matamko mawili haya ya ahadi ndio tiketi ya kuingilia katika Uislamu baada ya mtu kujitoa mwenyewe. Mtu akiyatamka maneno haya tu tayari anakuwa muislamu tena na papo hapo anawajibika kuishi chini ya kivuli na mipaka ya shahada mbili hizo. Kwani kuishi kwa mujibu wa shahada mbili ndiko kutampa sifa ya kuwa muumini mbele ya Alah Mola Muumba wake na mbele ya viumbe (waumini) wenzake.
Huu kwa muhtasari ndio Uislamu, dini na mfumo sahihi na kamili wa maisha kwa wanadamu wote waliochaguliwa na Allah Mola Muumba wao: |………LEO NIMEKUKAMILISHENI DINI YENU NA KUKUTIMIZIENI NEEMA YANGU NA NIMEKUPENDELEENI UISLAMU UWE DINI YENU ………….” (5:3) elewa na ufahamu kwamba kuishi nje ya dini hii ni kulikana umbile lako kwani UISLAMU NI HAKI YAKO YA KUZALIWA uliyopewa hadiya (zawadi) na Mola Muumba wako.
No comments:
Post a Comment