Friday, February 24, 2012

Hukmu Ya Muislamu Kumuoa Mkiristo Au Myahudi


Imeandikwa na Tawakkal Juma Husayn

UTANGULIZI

Awali ya yote ifahamike kuwa ni haramu kwa kijana Mkiristo kumuoa binti wa Kiislamu, kwa kuwa mwanamke Muislamu yuko juu ya kijana Mkiristo kwa Tawhiyd, Imani, na Ucha Mungu wake, na inapotokea Mkiristo akamuoa Muislamu ndoa hiyo inakuwa haifai, ni haramu na inatakiwa ivunjwe kwani hakuna utawala (Al-Wilayaah) wa kafiri juu ya Muislamu wa kike au wa kiume. Kwa hiyo ndio maana utaona kuwa tunazungumzia Muislamu kumuoa Mkirsto na si Mkirsto kumuoa Muislamu.

Kwa kuwa familia ndio msingi na kiini cha Ummah, Uislamu umezingatia na kulipa umuhimu wa kipekee suala zima la familia na wigo wake mpana.

Miongoni mwa vipaumbele vya Uislamu juu ya familia ni pamoja na kuilinda na kuihifadhi familia kwa kuifanya iwe imejengwa katika msingi ulio imara na madhubuti wa Kiimani na iwe inaengwa engwa na Hukumu na Adabu za Kiislamu.

Katika kuandaa hali hii, Uislamu umeweka msingi wa kuwa hilo linawezekana tu kwa kupitia ndoa ya wema wawili, ambao wamechaguana katika msingi wa Dini, Uchaji Mungu na tabia njema. Ni kupitia kwa wawili kama hawa ndipo humea na kuchimbuka familia ya Kiislamu iliyo njema, na yenye kumridhisha Mola wake kwa kutimiza haki na nyajibu mbalimbali ilizoamrishwa.

Ilipoteremka Qur-aan katika awali ya kuteremka kwake iliwakuta watu; Waislamu na wasiokuwa Waislamu wakiwa na ada na mahusiano mbalimbali ya kijamii kati yao.

Waislamu wa mwanzo katika kipindi cha Makkahh kabla ya kuhama kwao kwenda Madiynah walikuwa na maingiliano na wasiokuwa Waislamu kifamilia, kijamii, kiuchumi, n.k. Hivyo ikawa ni vigumu kihalisia kuyang’amua mahusiano haya mara moja au kwa mkupuo mmoja. Miongoni mwa mahusiano yaliyokuwepo kati yao ni kama ndoa; ambapo ilikuwa Muislamu anamuoa kafiri au mshirikina na kafiri au mshirikina akimuoa binti wa Kiislamu, walikuwa pia wanakunywa pombe, na wakila vibudu, wakila riba, wakicheza kamari n.k. Na nyingi ya ada na mahusiano haya yalibaki kama yalivyokutwa hadi alipohamia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Swahaba zake Madiynah. Msingi wa ucheleweshaji huu ulikuwa ni kuwalea Waislamu kiimani kwanza. Walilelewa katika kuamini Ghaibu au yasiyoonekana, kumuamini Allaah na kumuabudu Yeye Peke Yake, kumuamini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumtii na kutokumtii yeyote mwenye kumpinga na kumkhalifu Mtume, na kuamini wahyi ulioteremshwa na Allaah kuwa ndio muongozo sahihi wa maisha ya wanaadamu, na kuamini Siku ya Mwisho ambayo ndani yake kuna ufufuo, hesabu na malipo, thawabu na adhabu, pepo na moto n.k. Aliendelea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kulingania mambo hayo takriban karibu kipindi chote cha miaka 13 cha yeye kuwa Makkahh. Na hakulingania katika kipindi cha Makkahh hukumu nyingine isipokuwa chache sana; kama zile ambazo zilizingatiwa kuwa misingi ya hukumu nyingine ambazo zitakuja kuamrishwa baadaye. Hukumu hizi ni kama tabia njema, adabu mbalimbali za kiujumla ambazo Ummah zote zimekubaliana, kama vile; ukweli, kuhifadhi amana na kuunganisha udugu. Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuhamia Madiynah, Waislamu walipata ardhi ya kuishi humo Madiynah, na wakapata nguvu za kidola. Hapo zikaanza kuamrishwa hukumu mbalimbali, lakini kidogo kidogo hadi pale Allaah alipoitimiza dini yake. Na miongoni mwa hukumu ambazo ziliteremka Madiynah ni Waislamu kuharamishiwa kuwaoa makafiri na washirikina. Ikawa haifai kwa Muislamu kumuoa kafiri au mshirikina au kuendelea naye kama alikuwa amemuoa kabla ya amri na hukumu hii isipokuwa kama kasilimu.
(Rejea Qur-aan Suratul Baqarah, Aayah ya 221, na Suratul Mumtahinah, Aayah ya 10).
Uharamu huu ulikuja ili kuhakiki mambo makuu mawili;

Jambo la kwanza: ni kutenganisha kati ya waja wa Allaah Waumini na maadui zao makafiri katika kuunda mbegu ya Ummah ambayo ni familia kwani mbegu mbaya hutoa mimea mibaya.

Jambo la Pili: lilikuwa ni kukokoteza dhana nzima ya mapenzi na udugu kati ya Waislamu kuanzia katika msingi wa familia.

Baada ya utangulizi huo ningependa sasa niingie katika maudhui hii ambayo ni hukumu ya kiislamu juu ya Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab au Kitaabiyah (Mkiristo au Myahudi).


Awali ya yote ifahamike kuwa Kitaabiyah au Ahlul Kitaab ni istlahi inayotumika kwa watu waliopewaTaurati na Injili ambao ni Mayahudi na Manaswara (Wakiristo). Qur-aan imetumia neno ‘Ahlul Kitaab’ mara nyingi sana.

Kwanza Wanachuoni wote wa Kiislamu wamekubaliana kuwa haifai kwa Muislamu kuoa mwanamke Kafiri, Majusi au Mshirikina. Lakini wametofautiana juu ya Muislamu kumuoa Mkiristo au Myahudi.

Msingi wa tofauti hizi ni kuwa imekuja aya katika Suratul Baqarah (Aayah ya 221) ikiwakataza Waislamu kuwaoa washirikina na nyingine ikaja katika Suratul Mumtahinah, Aayah ya 10 ikiwakataza Waislamu kuwaoa.

Kisha ikaja Aayah katika Suratul Maaidah (Aayah ya 5) ikiwaruhusu Waislamu kula kichinjwa cha Ahlul Kitaab na kuwaoa wanawake wema katika Ahlul Kitaab.

Kabla ya kuchambua kwa kina suala hili napenda niweke wazi jambo moja muhimu nalo ni kuwa zilipoteremka Aayah zenye kukataza kuwaoa washirikina na makafiri na zile zenye kuruhusu kuwaoa Ahlul Kitaab kama nilivyotanguliza hapo juu, ardhi ilikuwa inagawanyika makundi makuu mawili; moja ni ile iliyojulikana kama ‘Daarul Islaam’ na nyingine ni ile iliyokuwa  ikifahamika kama ‘Daarul Harb’. Hizi Istlahi mbili yafaa zifahamike vizuri katika maudhui hii muhimu kabisa.

Wanachuoni wanaposema ‘Daarul Islaam’ huwa wanakusudia sehemu ambayo husimamishwa bendera ya Uislamu, na Uislamu mzima husimamishwa hapo vilivyo pamoja na shari’ah zake. Kwa upande mwengine ‘Daarul Harb’ ni sehemu ambayo Waislamu walikuwa wanapigana au wanapigwa vita. Vita hiyo aidha iliwapelekea maadui wa Uislamu waingie katika Uislamu, au wabaki na dini zao lakini wakubali kuwa chini ya mfumo wa Kiislamu na walipe jizyah au kodi ya kichwa. Hawa wanajulikana kama ‘Ahlu Dhimmah’ na nchi yao inakuwa ‘Daarul Islaam’. Vinginevyo Waislamu hawakuwa wakikaa katika ‘Daarul Harb’ kwani Mwenyeezi Mungu  Kawaamrisha kuhamia ‘Daarul Islaam’ na kawakataza kukaa katika miji ya washirikina na makafiri wenye kuwapiga vita. Na jambo hili (Hijra) ni lenye kuendelea hadi siku ya Qiyaamah na kwa sehemu zote duniani ambazo patapatikana Waislamu kufanyiwa uadui wa dhahiri nao wakashindwa kupambana dhidi ya uadui huo hata kama sehemu hiyo ni Makkah au Madiynah!
                                                                                  
Sababu ya kuleta Tanbihi hii katika mas-ala haya ni ili kutanabaisha kuwa maneno ya Wanachuoni juu ya uhalali wa Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab au kutokufaa huwa inakusudiwa ndoa hiyo katika Daarul Islaam. Ama katika ‘Daarul Harb’ wao huweka wazi msimamo wao juu ya hukumu ya Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab katika sehemu hiyo. Pia ifahamike kuwa Waislamu hawakuwa wakiingia Daarul Harb isipokuwa kwa kutekwa mateka au wafanya biashara kama itakavyokuja katika maelezo.

Wanachuoni wamekhitalifiana kuhusiana na hukumu ya Muislamu kumuoa Ahlul kitaab katika ‘Daarul islaam’:

1.     Jopo la Wanachuoni (Jumhuurul ‘Ulamaa) wamejuzisha (wameruhusu) Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab katika ardhi ya kiislamu, Daarul Islaam, lakini wamelichukulia hilo kuwa linachukiza. Wamestadili kwa Aayah ya tano ya Suratul Maaidah ambayo inaruhusu kula vichinjwa vya Ahlul Kitaab na kuwaoa wanawake wao. Aayah hii ya Suratul Maaidah aidha; imevua ujumla wa ile Aayah ya Suratul Baqarah yenye kukataza kuwaoa washirikina hadi wawe wamesilimu. Au imefuta ile hukumu ya Aayah ya Suratul Baqarah kwa kuwa Suratul Maaidah imekuja baada ya Suratul Baqarah. Au lafdh ya ‘Mushrikina’ katika Aayah hii haiwahusu ‘Ahlul Kitaab’. Pia wamestadili kwa kile kilichothibiti kuwa baadhi ya Maswahaba walioa wanawake wa Kiyahudi na Kikiristo kama Twalha bin ‘Ubaydillaah, Hudhayfah bin Al-Yamaaniy na ‘Uthmaan bin ‘Afaan. Na mwisho wamestadili na hoja ya kiakili kuwa mwanamke wa ki-Ahlul Kitaab kiujumla kaamini Mwenyeezi Mungu na baadhi ya vitabu Vyake na siku ya Mwisho na baadhi ya Mitume, hivyo inatarajiwa kuwa ataupenda Uislamu atakapoujua. Kwa hiyo kusilimu kwake kunatarajiwa zaidi kuliko kusilimu kwa mwanamke mwenye kuabudu masanamu au mwanamke kafiri.


2.     Baadhi ya Wanachuoni wameona kuwa kumuoa Ahlul Kitaab ni haramu katika Daarul Islaam. Nao wamestadili kwa Aayah zile zile walizostadili kwazo wenye kujuzisha ndoa ya Ahlul Kitaab. Ama ile Aayah ya 221 ya Suratul Baqarah wao wameichukulia kuwa imekataza kumuoa kila mwanamke mshirikina, na kuwa sababu ya kukatazwa kwao ni Imani yao, na Imani inapotumika katika Qur-aan na Sunnah huwa inakusudiwa Imani ya Kishari’ah iliyoletwa na Qur-aan na Sunnah, na kila mshirikina anaingia katika ujumla huu. Kwa upande wao hawa wanaona kuwa Ahlul Kitaab ni washirikina kwa dalili ya kuwa Mwenyeezi Mungu Amewaelezea hivyo katika Aayah ya 30-31 ya Suratu Tawbah yenye kusema: “Na Mayahudi wanasema: “Uzeri ni mwana wa Mwenyeezi Mungu”; na wakiristo wanasema: “Masiyh ni mwana wa Mwenyeezi Mungu”; haya ndiyo wasemayokwa vinywa vyao (pasina kuyapima). Wanaiga maneno ya wale waliokufuru kabla yao, Mwenyeezi Mungu Awaangamize. Wanageuzwa namna gani hawa! Wamewafanya wanavyuoni wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyeezi Mungu, na (wamemfanya) Masiyh mwana wa Maryamu (pia mungu), hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Mungu mmoja, hakuna anayestahiki kuabudiwa ila Yeye. Ametakasika na yale wanayomshirikisha nayo”. Kwa mtazamo wao huu wanaona kuwa japo Suratul Maaidah ilishuka baada ya Suratul Baaqarah, hii haizuii kuwa baadhi ya Aayah zake ziliteremka kabla ya baadhi ya Aayah za Sura zilizoteremka kabla yake kama Suratul Baqarah. Ila hili limejibiwa na jopo la Wanachuoni kuwa hakuna dalili yeyote inayoonyesha kuja Aayah ya 221 ya Suratul Baqarah kabla ya Aayah ya 5 ya Suratul Maaidah, na hili linapata nguvu zaidi na kule kuthibiti baadhi ya Maswahaba kuwaoa Ahlul Kitaab, vinginevyo wasingefanya hivyo. Na kama ikichukuliwa kuwa Aayah ya Suratul Maaidah ilikuja baada ya ile ya Suratul Baqarah hapa kizuri zaidi ni kuzifanyia kazi Aayah zote zote mbili kwa mantiki ya kuifanya Aayah ya Suratul Baqarah kuwa ni ya kiujumla yenye kuwajumuisha washirikina wote pamoja na Ahlul Kitaab na hii ya Suratul Maaidah iwe ni khaswa ambayo imewavua Ahlul Kitaab kutoka katika makatazo hayo, hivyo itakuwa imebaki katika uhalali wa kuwaoa Ahlul Kitaab.

Upande huu umestadili pia kwa kile kilichothibiti kuwa baadhi ya Maswahaba walikataza Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab. Kwa mfano inasimuliwa kuwa ‘Umar aliwakataza Hudhayfah na Twalha wasiendelee na wake zao wa Ki-Ahlul Kitaab na akakasirika sana kwa sababu ya ndoa hizo, hadi akatamani awachape fimbo, na pindi walipomwambia kuwa sisi tunawapa Talaka usikasirike ewe ‘Umar, akasema ‘’Umar: kama zikiwa halali Talaka zao basi na ndoa zao zitakuwa halali lakini mimi nawavua kutoka kwenu…”

Kwa upande wao hii ni dalili kuwa kuoa Ahlul Kitaab kwa mtazamo wa Umar ni jambo lisilosihi kabisa. Hapa Wamejibiwa na Jopo la wanachuoni kuwa Umar alichukia tu kwa MUislamu kumuoa Ahlul Kitaab wala hakuharamisha hilo kwani yeye Umar mwenyewe aliweka wazi kutokuwa haramu hilo pale alipomwamrisha Hudhaifa atengane na Mke wake wa kiyahudi, Hudhaifa alimwandikia Umar akimuuliza: “huyo mwanamke wa kiyahudi ni haramu kumuoa?”. Umar alimwandikia akimjibu kwa kusema: hapana si haramu ila naogopa msije mkaingia kwa Machangudoa miongoni mwao”. (Angalia Ahkaamul Qur-aan ya Jaswaas 1/333 na Tafsir ya Twabari 2/376-378). Kwa ufupi ni kuwa Riwaya zote zinaonyesha kuwa Umar na wengine walioona kuwa Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab si haramu lakini hilo linachukiza. Na kuhusu kitendo cha Umar kumuamrisha Twal’ha na Hudhaifa waachane na wake zao kwa Kiahlul Kitaab ni kwa ajili ya kuchelea watu wasije wakawaiga juu ya hili ikawa ni sababu ya kuacha kuwaoa wanawake wa Kiislamu.

Kwa kifupi Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab ambaye hajatoka katika dini yake na kuingia katika dini ya kuabudu masanamu au ukafiri inajuzu japo wanachuoni wengi wanaonelea kuwa hilo halipendezi. Ila pia wamesema kwamba kujuzu huku ni ikiwa anamuoa katika Daarul Islaam hali ya kuwa Ahlul Kitaab huyu yuko katika dhima ya Waislamu. Na sababu ya wanachuoni kutokupendelea Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab ni kule kuogopea kwao kuwa Ahlul Kitaab huyo asije akamuathiri mume wake Muislamu, familia, na watoto wake kwa itikadi, ada na tabia zake ambazo zinaweza kuwa zinapingana na Uislamu.



HUKUMU YA KUMUOA MKIRISTO AU MYAHUDI KATIKA DAARUL HARB

Ama katika Daarul Harb wanachuoni wanaona kuwa kumuoa Ahlul Kitaab inakatazwa humo kutokana na mambo makuu matatu;

1.    Kukihofia kizazi kitakachozaliwa katika Daarul Harb kisije kikakua katika dini isiyokuwa ya baba yao.

Kwa kufanya hivyo watakuwa wamepanda na kuongeza idadi ya wasiokuwa Waislamu ambao wanaweza baadaye wakawa maadui watakaokuwa wakiupiga vita Uislamu. Hili linapingana na kusudio na lengo la msingi la Waislamu kupata watoto ambalo ni ili Waislamu waongezeke na waweze kuhakikisha lengo la kuumbwa kwao ambalo ni kufanya ibada na kuitawala ardhi utawala wenye kumridhisha Allaah ambao hautopatikana hadi vizazi viandaliwe kwa lengo hili maghususi. Hivyo kitendo cha Muislamu kuweka mbegu zake za uzazi katika tumbo ambalo dhana yake inampelekea kuwa watoto watakaozaliwa watakuwa katika kundi la makafiri ambao baadaye watakuwa wakiupiga vita Uislamu na kuwazuia watu na dini ya Allaah ni jambo lisilofaa kabisa katika Uislamu. Ni kwa mtazamo huu baadhi ya wanachuoni waliojuzisha kumuoa Ahlul Kitaab katika Daarul harbwameruhusu afanye hivyo pasina kukusudie kupata mtoto naye.


2.    Jambo la pili ni kuchelea Muislamu asije akachagua kuishi na makafiri wenye kuupiga vita Uislamu.

Na jambo hili lina madhara mengi, miongoni mwa madhara hayo ni;

·         Kukhalifu amri ya kufanya Hijra (Kuhama kwa ajili ya Allaah). Kwa kufanya hivyo Muislamu anakuwa anajiweka karibu na Adhabu ya Allaah na Makasiriko yake, na atakuwa akiidhalilisha nafsi yake kwa adui zake. Kwa ufupi ni kuwa Muislamu anayekaa katika Daarul Harb kisha asihame wakati uwezo wa kufanya hivyo anao kisheria anakuwa anakasirikiwa na Allâh.
·         Kuongeza idadi ya makafiri dhidi ya Waislamu. Jambo ambalo litapelekea kuwapa nguvu makafiri za kuwadhoofisha Waislamu.
·         Kukiweka kizazi chake katika hatari ya Ukafiri au Utumwa pindi inapotokea vita kati ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Hii ni kwa sababu mama yake anaweza akatekwa hali ya kuwa yeye ni mjamzito na hivyo mtoto wake kuzaliwa mtumwa.
·         Muislamu kukabiliwa na mambo yenye kumchukiza Allaah au Munkar kama kula haramu ambayo mara nyingine inawezekana akashindwa kuikimbia, au kuangalia mambo yenye kumchukiza Mwenyeezi Mungu , ambayo kidogo kidogo moyo wake waweza kuyazoea na hatimaye kuona ni ya kawaida na hata mara nyingine ikatokea akayapenda, jambo ambalo linaweza kuua imani katika moyo wa Muislamu.
·         Mwanamke anaweza kupenda Munkar au mambo yenye kumchukiza Allâh na mume wake akashindwa kumzuia juu ya hali hii. Hili linapelekea nione kauli yenye kukataza kuoa Ahlul Kitaab katika Daarul Harb ina nguvu zaidi kwa kuwa kitendo cha Muislamu kuoa Ahlul Kitaab katikaDaarul Islaam wamekiruhusu huku wakieleza kuwa kitendo hicho kinachukiza. Ijulikane kuwa matumizi ya jambo la halali ikiwa yanapelekea katika madhara yenye kuzidi manufaa, hali hii kisheria huzingatiwa kuwa kitu hicho chenye sifa hii hugeuka kuwa haramu. Ni dhahiri kama tulivyoona kuwa madhara ya kumuoa Ahlul Kitaab katika Daarul Harb ni makubwa kuliko manufaa yake. Na Allâh ni mjuzi zaidi. Namalizia maelezo yangu kwa kueleza hukumu ya kumuoa Ahlul Kitaab sasa au katika wakati wa sasa ambayo ndiyo sehemu muhimu maudhui hii.



HUKUMU YA MUISLAMU KUMUOA MUKIRISTO AU MYAHUDI KATIKA WAKATI WA SASA.

Hii ndiyo sehemu ngumu sana ya maudhui hii na ndiyo sehemu ambayo watu wengi huuliza sana.

Kama nilivyotanguliza kusema kuwa wakati zikiteremka aya mbili moja ikiharamisha kuwaoa washirikina na nyingine baadaye ikaruhusu Waislamu kuwaoa Ahlul Kitaab, miji wakati ule iligawanyika katika sehemu kuu mbili; Daarul Harb na Daarul Islaam. Nimekwisha kukueleza maana ya istilahi hizi mbili. Kwa kuwa msingi wa majadiliano na hoja mbalimbali za wanachuoni juu ya suala la Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab umejikita katika mafhuumu ya istilahi hizi. Wakati wa sasa suala hili pia litaangukia katika sehemu hizo mbili. Yaani hii ni kusema tujiulize swali la msingi kuwa sasa hivi kama wewe uko Tanzania au katika nchi nyingine yoyote duniani nchi hiyo kisheria ni Daarul Harb au Daarul Islaam?Ukweli ni kwamba nchi nyingi au niseme karibia nchi zote duniani hivi sasa ziko katika hukumu yaDaarul Harb hata kama Waislamu katika baadhi ya nchi hizo ni wengi kuliko Ahlul Kitaab. Alipoulizwa Raisi wa kikao cha juu cha mambo ya hukumu za kiislamu wa Saudi Arabia AbdAllaah Humaid kuhusiana na wakati wa sasa ni kigezo kipi kitumike kutenganisha Daarul Harb na Daarul Islaam,alisema kuwa: mazingatio ni kina nani wanatawala sehemu hizo, ikiwa wanaotawala ni Waislamu tena wanatawala kwa kutumia sheria ya kiislamu basi nchi hiyo ni Daarul Islaam vinginevyo sehemu hiyo itakuwa ni Daarul Harb hata kama Waislamu ni wengi kuliko wasiokuwa Waislamu na hata wao Waislamu ndio wanaotawala lakini ikiwa hawahukumu kwa Kitabu cha Allâh na Sunna za Nabii Muhammad.

Katika wakati wa Mtume na Maswahaba kama nilivyotanguliza kusema kuwa nchi ziligawanyika sehemu mbili; Daarul Harb na Daarul Islaam. Ama watu, wao waligawanyika katika makundi matatu;
1.    Waislamu,
2.     Wasiokuwa Waislamu lakini wako katika dhima na ulinzi wa Waislamu kwa sharti la kulipa kodi, na
3.     Maadui wenye kuwapiga vita Waislamu.

Ukiziangalia nchi za makafiri sasa hivi utakuta kuwa uhalisia wake zinagawanyika katika makundi mawili;

Kundi la kwanza ni zile nchi ambazo zimetangaza mikataba ya Amani na nchi za kiislamu. Hizi zina sifa mbili;

Moja ni ile sura inayodhihiri kuwa zenyewe haziwapigi vita Waislamu au nchi za Kiislamu. Hii inadhihirishwa na Mikataba wanayowekeana na Makubaliano ya kiinchi kama kubadilishana Mabalozi, Biashara, Uchumi, Sayansi na Teknologia, Maarifa, Elimu n.k. Hali hii inazifanya nchi hizi zifanane na nchi zile zilizokuwa zimewekeana mikataba ya amani na nchi za Kiislamu katika karne zilizotangulia isipokuwa makubaliano haya kwa sasa ni ya kudumu na hayako katika misingi ya kiislamu tofauti na wakati ule ambapo yalikuwa ni ya muda mfupi na yalikuwa katika misingi ya kiislamu. Kwa sasa mengi ya makubaliano haya maslahi yake makubwa yako kwa makafiri na wala si kwa Waislamu hasa hasa nchi za magharibi ambazo zina nguvu na zinatawala nchi nyingine za dunia. Mfano wa nchi hizi ni kama Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.

Sifa ya pili na hii imejificha ni sifa yenye kuonyesha kuwa nchi hizi ni Daarul Harb. Hii inaonyeshwa wazi na kule nchi hizi kuzisaidia nchi zinazowapiga Waislamu iwe ni kwa kuzipa silaha, mali, vyakula, wataalamu, habari n.k kama ifanyavyo Marekani kwa kuwasaidia Waisraeli dhidi ya Wapalestina. Jambo jingine ni kuwa kule kuzipeleka manuwari na meli za kivita karibu na nchi za kiislamu ni dalili kuwa nchi hizi zinatafuta fursa tu na mwanya wa kuzivamia nchi za kiislamu mfano pale Marekani ilipokivurumishia mabomu kiwanda cha madawa cha Sudani kutoka katika manuwari yake. Pia ifahamike kuwa uadui wa nchi hizi umezidi zaidi dhidi ya Waislamu baada ya tukio la Septemba kumi na moja.

Jingine ni kule nchi hizi kujitahidi kuweka viongozi mamluki katika nchi mbalimbali za kiislamu kwa ajili ya kuwapiga vita Waislamu, pamoja na kuwasaidia viongozi hawa kwa hali na mali na kudhamini shughuli za kuwapindua viongozi wenye mwelekeo wa kiislamu kama wanavyotaka kumfanyia Raisi Umar Bashir wa Sudani kwa kigezo cha Mgogoro wa Darfur. Haya yote na mithili ya haya yanatosha kabisa kwetu kuzihukumia nchi hizi kuwa ni Daarul Harb.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliwazingatia Makureishi walipokuwa wamewekeana mkataba wa amani naye kuwa ni watu wa vita au Ahlul harbi pale walipowasaidia Banii Bakr waliokuwa wakiwapiga vita kabila la Khuzaa ambalo liliwekeana mkataba wa amani na Mtume.  (Angalia Tafsiiri ya Bakhawi, 2/266.)

Kwa kuwa Waislamu kwa sasa (kwa sababu ya udhaifu wao, na kugawanyika kwao, na kwa sababu ya mikataba na makubaliano ya kiinchi), hawawezi kuamiliana na nchi za kikafiri muamala wa kivita au kufanya moja kati ya mambo mawili; kuwalingania kuingia katika Uislamu, au kulipa kodi na wakikataa kuwatangazia Jihadi kama ilivyokuwa wakati wa Mtume na Maswahaba. Cha kufanya ni kwa Waislamu kujiandaa kwa kuongeza imani na kujikurubisha kikweli kweli kwa Allaah, na kuwa na Ikhlasi ya kweli kwa Allaah, na kujiandaa kimazoezi, kislaha na kivita dhidi ya makafiri kwa ajili ya siku ya kupambana nayo ambayo bila shaka itakuja siku moja.

Kundi la pili ni zile  nchi ambazo kwa asli yake zilikuwa za kiislamu kisha zikageuka kuwa Daarul Harb kwa sababu ya kukaliwa kimabavu na Maadui wa Uislamu, Mayahudi, na sehemu hii ni  Palestina ambayo inakaliwa kimabavu na mayahudi kwa msaada wa nchi za kikiristo za kimagharibi hasa Marekani na Uingereza.

Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa hakuna tofauti kihukumu kati ya Daarul Harb za zamani na za sasa katika suala la kutofaa Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab katika sehemu hizi kutokana na ushahidi niliotanguliza kutoa.

Wengi wa Waislamu wanaohamia nchi za kikafiri na kuishi humo, wanafanya hivyo kwa ajili ya kupata maslahi tu ya kimaisha, wengine hutafuta hifadhi za kisiasa na wengine ambao ni wachache sana hubaki huko kwa ajili ya Da’awa. Ama hali za Waislamu katika miji hiyo bila shaka maslahi wanayopata makafiri kupitia kwa Waislamu hao ni makubwa zaidi kuliko yale wanayopata Waislamu. Kiasi cha faida wanachopata Waislamu humo ni kidogo zaidi kuliko waajiri wao ambao si Waislamu. Ni matunda ya nguvu hizo za Waislamu katika kuwafanyia kazi wasiokuwa Waislamu zimekuwa zikitumika katika kuwapiga Waislamu moja kwa moja au vinginevyo. Japo inaweza kudhaniwa kuwa Waislamu wanaokimbilia nchi hizo wanapata faida zaidi, hilo kidhana linaweza kuwa sahihi lakini kwa hakika wanapata hasara kubwa zaidi.

Ukweli ni kwamba Waislamu katika nchi za kikafiri ni kama tone la maji safi na matamu lililodondokea katika bahari chafu, waonaje tone hilo la maji litaathiri chochote katika maji ya bahari hiyo au litayeyuka lisiache athari yeyote?. Muislamu mmoja atafanya nini katikati ya maelfu ya wakiristo au mayahudi? Muislamu mmoja au familia moja itafanya nini katika sehemu yenye mamilioni ya makafiri? Kituo kidogo cha kiislamu ambacho hakina walinganiaji wa kidini wajuzi kitakabilianaje dhidi ya walinganiaje maelfu ya maadui wenye kuupinga na kuupiga vita Uislamu huku wakisaidiwa na nguvu za kidola? Jengo litatimia lini ikiwa wewe unalijenga na wengine wanalibomoa? Lau ingekuwa mjengaje mmoja ana mvunjaji mmoja nyuma yake ingetosha jengo hilo lisisimame vipi ikiwa mjengaji mmoja na wavunjaji mia moja?

Ni mara nyingi Waislamu waliohamia katika miji ya kikafiri wanapoteza imani yao na utambuzi sahihi katika dini yao, jambo ambalo limepelekea wawe Waislamu majina tu. La hatari zaidi ni kuwa uhuru huo unawapelekea watoto wao wanapofikia umri wa miaka 18 wazazi wao wasiwe na maamuzi yoyote juu yao, hapo binti anaweza akaamua aolewa na yeyote pasina kuingiliwa kwani hiyo ni sehemu ya uhuru wake.  Watoto wadogo wa kiislamu ambao wazazi wao hawaujui vizuri Uislamu, wakicheza wanacheza na watoto wasiokuwa Waislamu, kisha baada ya michezo hii ya kichekechea akiendelea na hatua nyingine za masomo anachanganyika na wenzake ambao si Waislamu, ambao wana ada, tabia, na itikadi zao na waalimu pia si Waislamu ambao wanamwelekeza katika kuzipenda ada, itikadi na tabia  zao, naye anaona haya yote katika mienendo yao atawezaje kuokoka na ukafiri na athari zake katika hatua zote za masomo yake kwanzia chekechea hadi chuo kikuu?. Binti naye atawezaje kusalimika kuchanganyika na marafiki zake wasiokuwa Waislamu, na atawezaje kusalimika na vijana katika mazingira kama haya? Atawezaje kuepuka vilevya, kitimoto na hata kuingia kanisani? Atasalimika vipi na shubha zinazoelekezwa dhidi ya Uislamu?. Kisha wazazi wake wanaweza kuwa wazuri kidini na wanajitahidi kumulea binti wao katika msimamo wa kiislamu lakini watoto wakishafikia umri wa miaka 18 wazazi wanakuwa hawana amri yoyote kwa watoto wao kwa msingi wa uhuru usio na mipaka katika nchi hizo. Hii ndiyo hali ya Waislamu katika nchi za kikiristo za kimagharibi.





MADHARA YANAYOPATIKANA KWA MUISLAMU KUMUOA MKIRISTO AU MYAHUDI KATIKA WAKATI WA SASA.

1.    Kuridhia Muislamu kukaa katika mji wa kikafiri au Daarul Harb jambo ambalo linabatilisha hukumu ya Jihadi.
2.    Kunapelekea Muislamu anayekaa katika miji hiyo kuwasaidia makafiri kuwapiga vita Waislamu. Hili ni kutokana na mchango wa juhudi zake za kufanya kazi humo.
3.    Muislamu kujiweka karibu na ada, tabia na mwenendo wa makafiri. Vingi vya vitu hivi vinakhalifu dini ya kiislamu. Na inawezekana mara nyingine akashindwa kabisa kuviacha vitu hivi kutokana na kulazimika kwake kuchanganyika nao katika majumba yao na sehemu za kazi na safari zake mbalimbali. Jambo ambalo linaogopewa ikiwa atakuwa mdhaifu wa imani anaweza kuiacha dini yake na kuingia katika dini ya ukafiri. Na mithili ya haya yametokea.
4.    Kukosa Muislamu maana nzima ya kupendana kwa ajili ya Allaah na kuchukiana kwa ajili ya Allaah (Al’walaa wal’baraa) jambo ambalo limeamrishwa sana na Allaah katika aya nyingi za Qur-aankama katika Suratul Maaidah aya 51, 55-55 na Suratul Mumtahina, aya ya 4. Ilivyo kawaida ni kuwa Muislamu ambaye anachanganyika na makafiri, anakula nao, anakunywa nao na kisha ameoa kwao, haya humpelekea kuondoka katika moyo wake chuki dhidi yao, na mapenzi yake kwa Allaah na Mtume na Waislamu yanapungua.
5.    Kuridhia Muislamu munkar anaouona mara kwa mara mbele yake kila wakati kama ulaji wa nguruwe, unywaji wa pombe, ukafiri dhidi ya Uislamu, zinaa na vichecheo vyake. Anaweza yeye mwenyewe uzalendo ukamshinda na kujikuta akiingia katika maasia hayo na kubobea jambo ambalo litampelekea kupungua hisia za kuona kuwa hayo ni mambo yenye kumchukiza Allaah kutokana na kuyafanya mara kwa mara au mambo hayo kumzunguka usiku na mchana. Ni kwa mantiki hii nawausia ndugu zangu wanaosoma sehemu zinazofanana na haya niliyosema wajitahidi kumuomba sana Allaah awalinde na kuwafanyia wepesi mambo yao ili wakipata kilichowapeleka huko warudi nyumbani haraka!
6.    Kumuathiri mwanamke wa KiAhlul Kitaab mumewe Muislamu kwa ada, tabia na mwenendo wake wa kiAhlul Kitaab.
7.    Mke wake wa Kiahlul Kitaab ambaye hafuati maamrisho ya Allaah anaweza kupata watoto na mtu mwingine kisha akawanasibisha kwa mumewe. Katika hali hii kuna hukumu nyingi zisizofaa zinapatina kama vile kurithi wakibaki katika dini ya baba kumbe kisheria hawatakiwi kurithi, jingine ni wao kuchanganyika na watoto wake wengine wa kike na kiume na wengineo kwa msingi wa kuwa wao ni mahaarimu kumbe sivyo.
8.    Kuwalea watoto katika misingi ya kikafiri, ada, tabia na mwenendo wa kikafiri. Mara nyingine anaweza kuwachukua na kuwapeleka kanisani, disko na sehemu nyingine zisizofaa na ambazo zinaweza kuharibu tabia za watoto. Si sharti kulazimishwa kwenda kwenye ukafiri kuwe kwa nguvu na mabavu kama kutishiwa kuuliwa au kupigwa bali kunaweza kuwa kiakili tu, kijamii, kielimu, kisiasa na kuuchafua Uislamu na yote haya yanapatikana katika nchi za kikafiri.
9.    Sheria zinamlinda na kumtetea mwanamke katika nchi za kikafiri kwa kila namna, mfano lau kamaatampa talaka sheria itamlazimu aondoke na kumwachia nyumba mwanamke na watoto. Hapo mwanamke anapewa uhuru wa kuwalea watoto atakavyo na mwanamume akiyaona haya lakini hawezi kufanya chochote. Bali mwanamke wa Kiahlul Kitaab ambaye anaolewa na Muislamu na akamchukua kwenda kwenye mji wake (Mji wa Kiislamu), mwanamke huyo anapomchukia anaweza akaenda katika ubalozi wa nchi yake hapo alipo na watoto wake akapewa hifadhi hapo. Akawa humo kama yuko katika nchi za kikafiri analindwa na sheria za nchi yake na hapo akachukuliwa na wanawe kurudi kwao wala yeyote asiweze kumzuia yeye wala watoto wake.
10.           Kuacha Muislamu kuwaoa mabinti wa kiislamu waliopo katika nchi hizo za kikafiri. Jambo ambalo linapelekea wanawake wa kiislamu waliopo sehemu hizo kufitiniwa na vijana wa kikafiri iwe ni kwa kuziniwa au kuolewa na makafiri ambao kisheria hawaruhusiwi kuwaoa Waislamu. Na jambo hili lipo katika nchi za kikafiri.

N.B; Kwa kuwa Allaah alitaja kuwa wanawake wa Kiahlul Kitaab wanaoweza kuolewa ni wale wacha Mungu, kuna umuhimu kugusia ucha mungu aliokusudia Allaah katika kuwaoa wanawake wa Ahlul Kitaab. Baadhi ya wanawachouni wanaona kuwa maana yake ni kuwa asiwe mzinifu na wengine wanaona kuwa makusudio yake ni kuwa awe huru na si mtumwa hata kama ilitokea akawa alifanya uchafu wa zinaa lakini ikiwa ametubia au kaacha kwa sharti asiwe katika sehemu ambayo muoaji hamuogopei mtoto wake asije akalazimishwa kuwa kafiri baadaye. Kuna Waislamu wengi  katika nchi za kikafiri wanatamani mabinti zao waolewe na vijana wa kiislamu katika miji hiyo ambao wanaoa mabinti wa kikafiri kwa ajili ya malengo ya kidunia kama kupata kibali cha kuishi humo, uraia au kazi.
Kwa kumalizia katika sheria ya kiislamu, jambo la halali linapopelekea katika haramu jambo hilonalo huwa haramu. Inajulikana pia kuwa mubaaha ni jambo ambalo kulifanya au kuliacha ni sawa, yaani si lazima kulifanya wala kuliacha kwa asili ya uhalali wake, lakini ikiwa jambo hilo linapelekea kwenda katika jambo lililohimizwa zaidi basi jambo hilo kulifanya kimsingi kunakuwa kunahimizwa zaidi, na ikiwa linapelekea katika makuruhu linakuwa jambo hilo ni makuruhu kisheria linatakiwa liachwe na ikiwa linapelekea katika haramu nalo linakuwa haramu na ikiwa linapelekea katika waajibu nalo linakuwa waajibu. Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab kwa asli inafaa lakini ikiwa kwa kufanya hivyo inapelekea katika madhara niliyotanguliza kusema ambayo kila dhara katika hayo ni haramu, hapo inakuwa kila dhara hilo linampelekea Muislamu asioe Ahlul Kitaab.

Hii ndiyo hukumu yenye kutuliza nafsi juu ya jambo hili la Muislamu kuoa Ahlul Kitaab katika Daarul Harb. Maadamu madhara kama hayo yanapatikana katika miji hiyo na ikiwa itadaiwa kuwa hayapatikani madhara kama hayo na akathibitisha hilo hukmu hapo itabadilika na hili halitokei isipokuwa katika hali chache tu binafsi. Mazingatio huchukuliwa kwa kwa aghlabu ya mambo na si kwa nadra yao.
Hadi hapa naweza kumalizia mjadala huu kwa kusema kuwa, lililo sahihi kwa wanachuoni walio wengi ni kuwa inafaa Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab katika Daarul Islaam au nchi za kiislamu ambapo hapo kimsingi mwanamke wa kiAhlul Kitaab huwa anakuwa dhimiya mwenye kutii sheria na hukumu za kiislamu, pamoja na ruksa katika hali hii iliyo bora zaidi ni kutokuwaoa.

Haifai kwa Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab katika Daarul Harb au nchi zenye kupiga vita Uislamu kama Amerika. Na kwa sera ya Amerika ya sasa ya kuwa aidha nchi ijiunge na Amerika vinginevyo nchi hiyo itachukuliwa kuwa ni ya kigaidi kwa mantiki hii nchi zote kasoro chache sana kama zipo ni Daarul Harb kwa sasa. Hivyo nchi karibia zote sasa hivi duniani ni Daarul Harb ambazo kuna madhara mengi na makubwa kwa Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab humo. Hivyo kwa sasa utaona kuwa ni wazi kuwa Muislamu haifai kwake kuoa Mkiristo au Myahudi.

Baadhi ya Wanachuoni wanaona kuwa ikiwa dharura itapelekea Muislamu kumuoa Ahlul Kitaab katika miji ya kikafiri na akawa na uhakika kuwa watoto wake watalelewa katika malezi ya kiislamu basi hapo si lazima kwake kutumia njia za kuzuia kuzaa watoto, kinyume cha hivyo ni haramu kwake kumuoa Ahlul Kitaab na kama atalazimika kuoa basi achukue njia za kuzuia kuzaa. Ila tunaweza pia kusema kama mazingira yanayopelekea Waislamu kuruhusiwa kuwaoa Wakiristo na Mayahudi yatajitokeza tena  Ruksa hiyo itakuwepo kwa kuwa aya ya Suratul Maaidah bado hukumu yake inaendelea wala haikunasikhiwa lakini katika hali tuliyoeleza katika sehemu iliyotangulia ya makala hii.

Hivi ndivyo Waislamu wanavyotakikana walitazame suala la Muislamu kumuoa Mkiristo au Myahudi.


WAllaahu A’alam

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget