Friday, February 24, 2012

Tofauti za Sheria za Allah na za Mwanadamu


Tofauti Kuu Baina Ya Shari'ah Za Allah سبحانه وتعالى Na Sheria Azitungazo Mwanaadamu

Imeandaliwa na ‘Abdun-Naaswir Hikmaniy
"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha 
(humpa elimu) kwenye diniHadith Tukufu.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma na Mwenye Kurehemu, Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na Mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo. Sala na salamu ziwe juu ya kipenzi wa viumbe vyote duniani, mbora wa viumbe, Mtume wetu (Swalla Allahu Alayhi Wasalam). Shukrani ni zake Allah (Subhanahu Wataala) na Kwake tunajitakasa na Kwake tunaomba msaada, muongozo sahihi na msamaha wa makosa yetu. Tunaomba hifadhi Kwake Yeye Allah (Subhanahu Wataala) kutokana na vitimbi vya sheytan na hifadhi ya makosa ambayo tumeyatenda.
 UTANGULIZI.
Hamna shaka yoyote kuwa kuna tofauti kubwa baina ya Sheria za Kiislamu na zile atungazo mwanaadamu. Sababu hii ndiyo inayowafanya maadui wa Uislamu kuzitaka Sheria za Kiislamu ziwe ni kama za kwao. Masikio na macho yetu hayajaacha kushuhudia ni namna gani Sheria za Kiislamu zinavyopingwa mbele ya wale Makafiri na hata Waislamu poa. Kwa Muislamu wa kweli anaelewa fika kuwa ni sheria za Allah (Subhanahu Wataala) ndizo zitampa mafanikio hapa duniani na Akhera. Nimejitahidi kutoa maneno yalokuwa magumu na kutumia zaidi maneno ya Kiswahili ili makala hii iweze kusomeka na Waislamu wote. Yapo baadhi ya maneno ambayo nimeyawekea kwenye mabano kwa ueleo mzuri. Hali kadhalika nimeonelea kuonesha mifano michache kwa kutumia sheria za nchi ili kuweka wazi hoja.

Makala hii nimeigawa na kuelezea kwenye vipengele vifuatavyo:
  1. Asili ya Sheria za Kiislamu.
  2. Sheria za Kiislamu hazina tofauti ya mwanaadamu.
  3. Sheria za Kiislamu zinaenda na wakati.
  4. Sheria za Kiislamu na Muumba.
  5. Sheria na mahusiano ya wanaadamu.
  6. Usimamizi na muundo wa sheria.
  7. Adhabu (Punishment)
  8. Malipo mema kwa anayejiepusha kuvunja sheria.

Baada ya kusoma makala hii, utakuwa na nafasi nzuri ya kuelewa ni namna gani sheria za Kiislamu zinamfaa binaadamu. Tofauti kuu baina ya Sheria za Kiislamu na zile zitungwazo na binaadamu utapata kuzielewa na kujiweka katika ufahamu mzuri wa dini ya Kiislamu. Mwisho utakuwa na uwezo mzuri wa kuzitetea sheria hizi mbele ya wale wasiozifahamu au wale wanaozikejeli.

I  - ASILI YA SHERIA ZA KIISLAMU
 Kwa dunia ya sasa na maisha yaliyotuzunguka, hapana shaka kuwa Sheria nyingi zinazotugusa ni kutoka kwa binaadamu ambazo zinaamrisha mwenendo wa binaadamu na mahusiano yake na Serikali ilokuwa madarakani. Qur-aan na mafundisho ya Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam) ndio chanzo na msingi wa Sheria za Kiislamu.
 Tunaposema sheria za Uingereza, Marekani n.k ni mifano ya sheria za binaadamu. Takriban mataifa mengi, yakiwemo Tanzania, Uganda na Kenya. Ukiachilia nchi za Kiislamu, nchi nyingi zina sheria za Muingereza (Common Law). Tofauti na sheria za Kiislamu ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja kwa Allah (Subhanahu Wataala). Sheria za duniani zinatoka kwa binaadamu ambaye ameumbwa na Allah (Subhanahu Wataala). Hivyo, sheria za binaadamu ni zenye kubadilika, wakati Sheria za Kiislamu hazibadiliki kwa sababu zimewekwa na Allah(Subhanahu Wataala). Tokea mwanzo wa kuumbwa mwanaadamu, ni jambo lisilopingika kuwa mwanaadamu hana ukamilifu kwenye maisha yake, ni mnyonge, asiyejitosheleza kwa nafsi yake moja. Matokeo yake ni sawa sawa na sheria zake, hazina ukamilifu wowote. Dunia inazunguka na kuendelea ndivyo sheria zake zinavyobadilika na kuhitaji mabadiliko ili ziendane na wakati. Kwa maneno mengine sheria za mwanaadamu hazina ukamilifu kwenye sehemu yoyote wala haziwezi kuwa kamili mpaka binaadamu aondokane na kasoro zote. Sheria za Kiislamu zinagusa sehemu zote za maisha ikiwa ni katika uchumi, jamii, siasa au imani.

II - SHERIA ZA KIISLAMU HAZINA TOFAUTI YA MWANAADAMU.

Hapana shaka kuwa binaadamu mmoja anatofautiana na mwengine, ni sababu hii imesababisha kuwepo mipaka ya nchi, tofauti ya lugha, kutofautiana kwa makabila na rangi. Ndivyo sheria za mwanaadamu zinavyotafautiana baina ya sheria moja na nyengine. Pia sheria hizi za leo ni tofauti na zile za miaka hamsini tu iliyopita.

Sheria za Kiislamu zinajulikana na zitaendelea kuwa hazina mpaka (boundary) wowote wa tofauti ya wakati, taifa au sehemu anayoishi. Tuelewe kuwa mwananchi yeyote aliyekuwa chini ya Taifa la Kiislamu awe mweupe au mweusi, wa nchi yoyote, basi sheria ya mwizi (pindi ushahidi wa kweli ukithibitishwa) ni kukatwa kiganja cha mkono wa kulia, mlevi bakora 80 na mengineyo. Tofauti na sheria za binaadamu ambapo akibadili taifa na sheria zake zitabadilika.

Kwa mfano, twaelewa sote namna ya gonjwa hatari la ukimwi linavyoangamiza dunia nzima. Lakini Tanzania ipo kimya kuhusu muathirika anayetambuwa kuwa ameathirika kujamiiana na asokuwa muathirika kwa lengo la kumuambukiza gonjwa la ukimwi kwa makusudi. Hali sio hiyo kwa Afrika ya Kusini kwani sheria zao zinaruhusu muathirika wa namna hiyo kufikishwa Mahakamani. Kwa upande wa silaha za nyuklia, Marekani na Israel zimejipa ruhusa ya kutengeneza na kuhifadhi silaha hizo ilhali nchi nyengine zote yawa ni haramu kwao sio tu kutengeneza, hata kuhifadhi mali asili zinazotumika kutengenezea nyuklia kama zebaki “mercury”. Pia vitendo vya liwaati vimezuiwa Zanzibar (kifungu namba 150 cha Sheria ya Jinai namba 6 ya mwaka 2004). Wakati sheria za Magharibi sio tu zinaruhusu maingiliano haya machafu, hata ndoa zafungwa baina ya watu wa jinsia moja.

Hivyo, ni kusema Tanzania inaruhusu kuambukizana ukimwi wakati Afrika Kusini inazuia.Israel na Marekani wanaruhusa ya kutengeneza nyuklia ilhali nchi nyengine ni kosa. Liwaati ni kosa ndani ya Zanzibar wakati nchi za Magharibi zinaruhusu.

Tofauti na Uislamu, Sheria ipo wazi kuhusu muathirika kumuambukiza mwengine kwa lengo la kupata maradhi ateseke na mwisho kufariki kifo kibaya. Uislamu unasema anayeua nafsi moja ni sawa na kuua nafsi zote. Pia ipo Hadithi ya Mtume (SwallaAllahu Alayhi Wasalam)inayosema “Aliye na maradhi asimuambukize asiyekuwa nayo.” Kwa upande wa nyuklia, ni sawa tunasema mtu ajihami na kumruhusu kukaa nazo lakini nyuklia zina hatma mbaya.Sadd adh-dharai ni sheria inayozuia halali ambayo inaweza kuleta athari ya haramu. Sheria inayofafanua  mwenendo wa maisha ya Muislamu (Majallah al-ahkaam adaliyah) Kifungu 30 pia chaeleza Sadd al-dharai. Haramu hii ni mfano wa ile tuipatayo juu ya ulevi, kwani ina manufaa lakini ni finyu ukilinganisha na athari zake. Allah (Subhanahu Wataala) anasema na tutajaribu kutafsiri kama ifuatavyo:

{Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: “Katika hivyo mna madhara makuu na (baadhi ya) manufaa kwa (baadhi ya) watu. Lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake.”} [Suratul Al-Baqarah: 2)

Hivyo nyuklia inafanana na kesi ya ulevi na hivyo kuwa ni haramu. Ama kuhusu liwati, hamna mjadala kuwa ni haraam na itafika Qiyama, liwaat itabaki kuwa ni haraam. Liwaat ni katika dhambi kubwa ndani ya Uislamu na katu haikubaliki kwa jamii. Sheria zote hizi hazitakuwa na mabadiliko ndani ya Uislamu kwa sababu Mungu ni Mmoja na Sheria Zake ni hizo hizo. Allah Anasema na tutajaribu kutafsiri kama ifuatavyo:

{“Je mnawaendea wanaume, na mnawakatia njia (watu kwa kuwaua na kuwanyan’ganya njiani) na mnafanya maovu katika mikusanyiko yenu?” Basi halikuwa jawabu ya watu wake ila kusema: “Tuletee adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa miongoni mwa wasemao kweli!”} [Suratul Al-Ankabuut: 29]

Je, hamna mtu asiyejua nini kiliwafika watu wa Nabii Luut (Alayhi Salaatu Wasalaam)?.

Sheria kuu za Kiislamu ambazo zinapatikana ndani ya Qur-aan imechukua sifa Yake Muumba, imehifadhiwa tokea mwanzo wa kushushwa hadi leo na mpaka siku ya Qiyama. Allah(Subhanahu Wataala) Anasema na tutajaribu kutafsiri kama ifuatavyo:

{Hakika Sisi ndio Tulioiteremsha mawaidha haya (hii Qur-aan), na hakika Sisi ndio Tutakayoilinda} [Suratu Al-Hijr: 9]

Hapana shaka kuwa Qur-aan tuliyonayo leo ni kitabu hichi hichi alichoshushiwa Nabii wetu(Swalla Allahu Alayhi Wasalam) kwa Ummah wake wote. Sheria hizi zilizowekwa kutoka Kwake Allah (Subhanahu Wataala) zinadhihirisha sifa Zake Mola ambazo hazina doa, Mwenye kuishi daima, Hakimu wa Mahakimu, Mfalme wa Wafalme na sifa zengine nzuri nzuri. Sifa hizi Allah (Subhanahu Wataala) anazo kabla, leo na mpaka Qiyama. Ni sifa hizi tuzipatazo kwa Qur-aan isobadilika na kwa sheria za Kiislamu zisotaka mabadiliko yoyote!

Kwa hiyo sheria za binaadamu ni kanuni zinazotungwa kwa ajili ya kuitengeneza vizuri jamii ili kutimiza matakwa ya hiyo jamii husika. Sheria za binaadamu zinatungwa kutokana na matatizo yanayojitokeza ndani ya jamii. Mahitaji ya jamii yenye kubadilika kutokana na yeye binaadamu kuwa na mabadiliko ndio sababu ya sheria za binaadamu. Jamii inaendelea, ndivyo sheria zinavyobadilika. Hivyo, sheria za binaadamu haziishi maisha ya milele, bali zinazaliwa na kufa. Kutokana na sababu ya wakati, sheria za mwanaadamu zinakwisha muda (expire). Hapa tunaona kuwa sheria za mwanaadamu zinatengenezwa kutokana na mahitaji ya jamii na kwa ajili ya muda fulani na baada ya muda huo kupita na jamii kubadilika kutokana na sheria hizo basi sheria hizo huwa sawa na takataka zitakiwazo kutupwa jalalani.

Kwa mfano sheria ya makosa ya Jinai ya Zanzibar namba 13 ya mwaka 1934 inaruhusu adhabu ya viboko. Adhabu hii imefutwa mwaka 2004 (Kifungu namba 26 ya sheria namba 6 ya mwaka 2004 – Sheria ya Makosa ya Jinai ya Zanzibar) Hivyo ni kusema sheria hii imezaliwa 1934, imeishi na kufa mwaka 2004. Adhabu zinazokubaliwa kwa sasa ni kama faini, kifungo cha jela na nyenginezo.

Tofauti na Uislamu, kwa mfano sheria ya mzinifu asoowa/kuolewa atatumikia mijeledi mia moja. Haitobadilika sheria hii mpaka Qiyama kisimame hata ikiwa Waislamu poa hawaitaki hata kuisikia. Ile dhana za zinaa kamwe hazijabadilika ila huongezeka. Uislamu umeliona hilondiyo maana sheria hiyo inadumu. Mwanadamu ana kasoro zake na huona yale madhara ndiyo faida. Mwanaadamu anaivamia zinaa akidhani ina manufaa ila haina hiyo zinaa ila madhara matupu tena ya kuangamiza. Matokeo ya kukataa kufuata Sheria za Kiislamu ni kujiangamiza. Sheria za Kiislamu zinamzuia mwanaadamu asijiangamize. Ni dhambi kubwa mtu kujiingiza katika hilaki yeye mwenyewe kwa mwenyewe.

III  - SHERIA ZA KIISLAMU ZINAENDA NA WAKATI

Dalili zinaonesha kuwa sheria za Kiislamu ni za milele na hazihitaji marekebisho na wala marekebisho hayahitajiki kwa sheria za kiislamu. Sheria za Kiislamu zimewekwa kurekebisha tabia na matatizo ya jamii ya binaadamu kwa muda wote ambao atajaaliwa kuishi ndani ya dunia hii. Ingawa Sheria za Kiislamu msingi wake ni Qur-aan na isiyohitaji mabadiliko, lakini sheria hizi za Kiislamu zinaweza kuendelezwa na kupatiwa ufumbuzi wa mambo ambayo yana khitilafu ndogo ndogo. Hii ni kwa kutumia vipengele vya Fiqhi kama Qiyaas (ufumbuzi), kauli za Maswahabah, Sadd al-dharai (kuharamisha halali inayopelekea kwenye haramu) na nyenginezo.

Kwa mfano asili ya kuharamishwa ulevi ni kuwa na athari mbaya kwa jamii, lakini Qur-aan imezungumzia kinywaji cha ulevi na sio kuhusu madawa ya kulevya kama kokeni na bangi. Hapa tunatumia Qiyaas ili kupata hukmu yake na kuona kuwa nayo pia yana athari mbaya kwa jamii, hivyo kila chenye madhara ni haramu. Na kupata hukmu ya madawa ya kulevya kuwa ni haramu pia.

Itambulike kuwa vipengele hivi (mfano QiyaasSadd al-dharai, kauli za Maswahabah na kadhalika) vyote vya Fiqhi vinapitia msingi wa sheria ya Qur-aan ama Sunnah. Ikiwa Qur-aan au Sunnah imetoa hukmu, hamna sheria nyengine itakayotolewa ufafanuzi. Na wala isiwe sheria itokanayo na fiqhi haramu inayohalalisha au halali inayoharamishwa. Kwa mfano kuhalalisha kutovaa Hijabu kwa mwanamke au kuharamisha Zakaah.

Mfano mzuri ni kuhusu mjadala wa Hijaab. Kwani Hijaab ina nafasi kubwa katika hukmu za Kiislamu. Lakini Dkt. Zaki Badawi (mwanazuoni wa Kiislamu kutoka Uingereza) ameruhusu wanawake kutovaa hijaabu kwa kuwa hijabu inamfanya adhuriwe kama vile kutukanwa, kusumbuliwa na hata kuvamiwa. Dr. Badawi ameghafilika na kusahau Quran (Suratu An-Nur:31 na Suratul Ahzab:59) kuwa hijabu ni lazima na wala sio Sunnah. Kisingizio cha kukejeliwa wanaovaa hijab sio sahihi kwani Waislamu waliopita walikashifiwa zaidi ya haya lakini sheria zilibaki kama zilivyo.

Hivyo, sheria za Kiislamu ni zenye kwenda na wakati, kwani sheria kuu za Kiislamu zipo kamili na mawazo ya kisheria (Fiqhi) yapo wazi kutumika.

Sheria za Kiislamu zinatofautiana baina ya mwanazuoni mmoja na mwengine tu. Tunaposema Qur-aan na Sunnah ni vyanzo vya sheria, tunakusudia kusema kuwa hivi ndivyo vyanzo na dalili kuu zinazofuatwa na kupatiwa ufumbuzi ikizingatiwa kufuata kanuni zinazohusika katika kutoa ufumbuzi kwa suala la Kiislamu.

Kanuni hizi za Kiislamu hazipatikani isipokuwa kwenye vyanzo vikuu. Hii ndio tofauti kubwa na sheria zenginezo. Kwani sheria za mwanaadamu zinatokana na akili yake mwenyewe, akija mmoja ataweka sheria hii na akiingia mwengine madarakani atazibadilisha. Anavyoamka ndivyo anavyotunga sheria. Sheria za Kiislamu zimeshushwa zaidi ya miaka 1400 iliyopita. Tokea muda huo, binaadamu anajulikana kubadilika kiakili, muundo na maendeleo. Watu wa kale hawakuweza hata kuota uvumbuzi usioingia akilini kutoka katika sheria za Kiislamu. Adabu za binaadamu zimeelezwa humo na matawi mengi tu ya elimu yametokana na hiyo Sheria kuu ya dunia.

Ama kwa binaadamu, huweka sheria kwa ajili ya kutawala muda mchache unaomzunguka akiangalia matakwa yake na jamii kuwa ujumla. Juu ya kubadilishwa na kutiwa viraka sheria hii, haijawa mfano hata chembe, mbele ya sheria za Kiislamu ilhali sheria hizi zinatungwa mpya. Lakini ile kongwe (Sheria ya Kiislamu) ipo imara na katu haihitaji viraka na wala haitohitaji viraka. Ukiangalia na kuisoma Sheria ya Kiislamu utakutia bado binaadamu hajafikia mambo yote yaliyotajwa, hivyo kuifanya kwenda na wakati. Kwa mfano ujio wa Nabii Issa (Alayhis Salaatu wa Salaam) kabla ya Qiyama, ni nani ajuaye lini atafika duniani? Ni Qurani tu iliyoeleza haya! Bado wakati wake tu kufika. Ni hivi karibuni tu imegundulika kuwa ni dunia inayozunguka jua na sio jua kulizunguka dunia. Qur-aan imetaja hili miaka 1400 iliyopita. Mfano mwengine ni kugundulika upulizwaji wa roho kwa kiumbe kilicho ndani ya tumbo la mama kabla ya kuzaliwa, wanasayansi wasiokuwa na ujuzi wa Qur-aan bado wanashikilia kusema kuwa kiumbe kinakuwa hai tokea pale yanapotoka manii. Hii sivyo kwa elimu sahihi ya Uislamu kwani tunafundishwa kuwa linakuwa ni pande la nyama tu (sio kiumbe hai), na hupuliziwa roho baada ya miezi minne tokea mimba inapotungwa.

Imepokewa kutoka kwa Bukhari na Muslim, kutoka kwa Abdillahi bin Masuud (Radhiya Allahu Anhu), kutokana na Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam) amesema: ((Hakika mmoja wenu linakusanywa umbile lake ndani ya tumbo la mama yake kwa siku arobaini kuwa ni tone (nutfaa), kisha linageuzwa kuwa pande la nyama (‘alaqatah) mfano wa hizo (siku), kisha linakuwa mifupa mfano wa hizo (siku), kisha anateremshwa juu yake malaika, anampulizia ndani yake roho…)) [Amesema kweli Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam)]

Sheria za Kiislamu sio zenye kubadilika ukilinganisha na za binaadamu ambazo zinabadilishwa kuanzia sheria ndogo mpaka Katiba. Kwa mfano ili kuingiza siasa za sasa (demokrasia) inabidi Katiba ibadilishwe kuruhusu vyama vingi. Historia ya Uislamu umeruhusu changamoto inayoanza kutoka Kwake Allah (Subhanahu Wataala) dhidi ya Ibilisi. Kisha kumuachia ibilisi akawa na sifa ya kuishi, kutembea ndani ya mishipa ya damu ya mwanaadamu. Akimuachia mwanaadamu aamue mwenyewe pa kufuata (ama Allah (Subhanahu Wataala) au Ibilisi). Siasa ya Uislamu iliendelea hata kwa Maswahaba baada ya kufa Nabii Muhammad (Swalla Allahu Alayhi Wasalam).

Historia ya Kiislamu inaonesha kuwa baada ya kufa Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam)Waislamu walichagua Khalifa (kiongozi) wa mwanzo msikitini, walitumia haki yao kwa kwenda kumpa mkono (kura) Sayyidna Abubakar (Radhiya Allahu Anhu) na kuonesha kuridhika naye kuwa ni Khalifa wao. Hakuingia madarakani Sayyidna Abubakar (Radhiya Allahu Anhu) kwa nguvu au kujipigia kampeni na propaganda. Hataaa! Njia ya Baya’h (kupiga kura) ilitumika.

IV - SHERIA ZA KIISLAMU NA MUUMBA.

Mazingatio makuu ya Sheria ya Kiislamu ni kuweka uhusiano imara baina ya Muumba na kiumbe. Kwa mfano Swalah, Zakaah, kufunga Ramadhan ni kwa ajili ya Allah (Subhanahu Wataala) peke Yake tu na kumuabudu Yeye Allah (Subhanahu Wataala.) Yeye ndie Mtoa Sheria, Anaamrisha binaadamu kufanya au kujizuia kufanya kitu kwa minajili ya kuwa karibu na Muumba na wakati huo huo kulinda haki yake mwanaadamu na viumbe wengine. Kwa mfano tunazuiwa kuzini, kuiba, kuua, kuharibu mazingira n.k ili kulinda cheo cha binaadamu pamoja na kulinda haki za binaadamu na viumbe wengine. Tofauti na sheria za binaadamu ambapo mazingatio yake makuu ni kutofautisha dini na sheria. Ni kusema kuwa sheria za mwanaadamu haiweki kanuni na mahusiano baina ya watu au watu na Serikali yao. Lakini sheria ni sehemu ya dini ndani ya Uislamu. Uislamu unaweka kanuni baina ya binaadamu na Muumba wake na wakati huo huo ukiwekwa uhusiano mzuri baina yake na watu wengine, tofauti na sheria za binaadamu ambazo zinaweka mahusiano baina ya watu tu.

Hapa lazima tukumbushe kuwa mwanaadamu ametunga sheria za kulinda wanyama na mazingira. Sio kwa ajili ya hao wanyama au mazingira, bali kuharibiwa kwake kunaathiri maisha ya mwanaadamu na uhai wa dunia kwa ujumla. Uislamu umeenda mbali na kusema kila kiumbe (hata jua ni kiumbe) kina haki ya kuishi na kutumiwa kulingana na mafundisho sahihi ya dini.

V - SHERIA NA MAHUSIANO YA WANAADAMU.

Wamejiwekea wanaadamu sheria zinazoeleza mahusiano baina ya watu “tort.” Sheria hizi hazina uhusiano wa maadili, msingi mkuu wa sheria hizi (tort) ni kutoka kwa aliyevunjiwa hizo sheria na wala sio Serikali.

Kwa upande wa Uislamu, kiini kikuu cha mahusiano ya wanaadamu ni kutoka kwenye Qur-aan ambayo inakataza dhana mbaya, kupeleleza na kusengenya. Allah (Subhanahu Wataala)anasema na tutajaribu kutafsiri kama ifuatavyo:

{Enyi mlioamini! Jiepusheni sana na (kuwadhani watu) dhana (mbaya) kwani (kuwadhani watu) dhana (mbaya) ni dhambi. Wala msipeleleze (habari za watu). Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine. Je! Mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliyekufa? La, Hampendi; (Basi na haya msiyapende). Na Mcheni Mwenyezi Mungu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba (na) Mwingi wa kurehemu.} [Suratul Al-Hujurat: 149]

Hivyo, sio tu sheria ya Kiislamu inakataza mahusiano mabaya baina ya wanaadamu bali inaeleza kwanini asifanye hivyo na kutolea mfano ni namna gani lilivyo hilo kosa kuwa ni kubwa. Hapa tumeoneshwa kusengenya ni mfano wa kula nyama ya ndugu yako tena aliye maiti. Subhanallah!

Baadhi tu ya kasoro juu ya sheria hizi ni kama ifuatavyo:

Hazielezi (tort) ni kwa nini mwananchi asikiuke hizo sheria. Bali zinamzuia na kumlazimisha tu kufuata hiyo sheria. Kwa mfano asiwashe redio sauti kubwa hadi kumuudhi jirani. Akiwa hayupo jirani? Ni ruhusa kuwasha? Je wapita njia? Ndege warukao? Haki za majini na malaika zipo hapa? Majibu yote utayapata kuwa sheria za mwanaadamu hazina mazingatio kwa viumbe vyote. Zinagusa sehemu chache tu ya vitu.

Kasoro nyengine ni kuwa hazifikishwi Mahakamani kuvunjwa kwake ila mpaka aliyekosewa afunguwe kesi kwa gharama zake mwenyewe. Serikali haina mkono wake kwenye kesi hizi. Hii ni kwa sababu sheria za mwanaadamu hazitaki kujiingiza kwenye mahusiano haya wala hazigusi maadili. Tofauti na Uislamu, umegusa kila nyanja ya maisha ya mwanaadamu. Katu Taifa la Kiislamu haliruhusiwi kukimbia majukumu kwani sheria zote zinatoka kwa Mkuu wa Serikali zote duniani, naye ni Allah (Subhanahu Wataala).

VI - USIMAMIZI NA MUUNDO WA SHERIA.

Tofauti nyengine inahusiana na usimamizi na namna zinavyoundwa hizo sheria.

Kawaida, jamii fulani inaunda sheria zake kwa ajili ya kutawala jamii husika na kuilinda. Mfano Hitler alipoingia madarakani alipitisha sheria ya kuuawa kwa Mayahudi wote ilimradi tu kulinda maslahi ya wajerumani walio wengi ndani ya Ujerumani. Alipoondoka madarakani sheria hii ikafa. Ama kwa Sheria ya Kiislamu, sio ya jamii fulani pekee. Inagusa ulimwengu mzima hata kwa wasio Waislamu. Kwa mfano kuna sheria baina ya taifa la Kiislamu linavyoishi na wasio Waislamu (Dhimmi). Muislamu hatakiwi kuimwaga damu ya binaadamu hata awe Dhimmi bila ya sababu. Ni dhambi kubwa kuimwaga damu ya Muislamu bila ya sababu yoyote. Maingiliano baina ya Waislamu na wasio Waislamu, uchumi wa Kiislamu na siasa za Kiislamu ni vipengele vilivyokuwa huru kutumiwa na walimwengu wote kwani kuna faida kubwa. Ikiwa ni Muislamu au sio Muislamu. Sheria ya Kiislamu ni ya ulimwengu mzima na watu wake wote. Tofauti na sheria za binaadamu ambazo haziwezi kwenda pamoja na maendeleo anayofanya mwanaadamu duniani. Ni lazima zitabadilika tu.

Dhumuni kuu ya Sheria ya Kiislamu haikufungwa kuzunguka jamii pekee. Bali kumpa haki kila mmoja, kuunda jamii yenye tabia nzuri, taifa imara na mwisho kuifanya dunia sehemu inayofaa kuishi kwa mazingira yake mwenyewe binaadamu.

VII - ADHABU (PUNISHMENT).

Adhabu za Sheria ya Kiislamu pia ni tofauti na sheria za mwanaadamu. Hakika haitakuwa sheria ikikosa adhabu, na kama sheria itakosa adhabu ni sawa na msumeno usokuwa na meno (makali) au kisu butu. Ingawa zote zinawaadhibu wanaokiuka hiyo sheria, lakini bado tofauti ipo.

Kabla ya kuendelea mbele, lazima tuelewe kuwa Uislamu umeletwa kwa wanaadamu wote. Hivyo kukataa kufuata Uislamu hapa duniani na kuabudia asiyekuwa Allah (Subhanahu Wataala) basi hilo pia ni kosa.

Sheria ambazo atakiuka Muislamu ataadhibiwa Qiyama na mara nyengine sheria inaruhusu kuadhibiwa duniani na Qiyama pia. Kwa mfano shirk, khadaa ya kujifanya umefunga, kibri, riyaa na dhambi nyenginezo ambazo haziwezi kuonekana ila kwa Allah (Subhanahu Wataala)zitaenda kuadhibiwa Qiyama, hii ni kwa sababu zinafanywa kupitia ndani ya nafsi ya mwanaadamu. Ni Yeye Allah (Subhanahu Wataala) pekee mwenye uwezo wa kuona kinachopita ndani ya nafsi. Kwa nini tuseme hivi?

Chukua mfano wa Marekani akirusha roketi kwenye mwezi, hakika haitoachiwa kwenda tu yenyewe, bali itakuwa inarikodi na kuangaliwa huku duniani kila hatua inayokwenda na namna mashine yake inavyofanya kazi. Pia “black box” kwa upande wa ndege “aeroplane” inarikodi hata mazungumzo ya pilot, na ndio maana ndege inapopata ajali kwanza hutafutwa hiyo “black box”. Hivyo kila mtengenezaji hukijua vizuri mwenendo wa anachotengeneza, na hamna mwengine wa kujuwa nafsi ya mwanaadamu ila Muumba Subhaana.

Na kwa mfano wa adhabu zinazoweza kuthibitika duniani ni zina, wizi, ulevi na mengineo ambayo mkosaji anaweza kutiwa hatiani tofauti na yale makosa yalokuwa yanapita ndani ya nafsi.

Pia Uislamu utamuadhibu mtenda dhambi aliyekuwa hajatiwa hatiani hapa duniani. Mfano wanaokiuka kutoa Zakaah, ingawa anaweza kufoji karatasi na kusema uongo ili tu kukwepa kutoa Zakaah hapa duniani lakini ataenda kuilipa huko Qiyama. Hamna kukimbia kosa ndani ya Uislamu, limetendwa basi litahesabiwa tu mbele ya Muumba. Mfano mwengine ni makafiri walokataa kufuata Uislamu. Pia nao wana hukmu zao siku ya Haki.

Tofauti na sheria za mwanaadamu ambazo zinamuadhibu mkosaji duniani pekee. Na ikiwa mwanaadamu atakwepa mkono wa sheria hadi kufa hatahisabiwa katu kuwa ni mkosaji. Uislamu unamkamata mkosaji duniani na kama hatakamatwa basi adhabu ipo siku ya Qiyama. Sheria ya Kiislamu inawafanya Waislamu kuwa makini muda wote kutokiuka sheria za dini.

VIII - MALIPO MEMA KWA ANAYEJIEPUSHA KUVUNJA SHERIA.

Juu ya hayo, Uislamu unatoa malipo kwa mtiifu na adhabu kwa mtenda dhambi. Hivyo, Sheria za Kiislamu zinawakamata wote ikiwa ni mtiifu au ni mtenda makosa. Sheria za Kiislamu zinalinda kanuni zake na zinawalazimisha binaadamu kujisalimisha nazo sio kwa kuweka adhabu tu bali hata kwa kutoa malipo mazuri kwa mwenye kuzifuata. Ambapo sheria za mwanaadamu zinamuadhibu mkosaji na wala hazitoi zawadi kwa anayezifata. Jee tumepata kusikia Raisi/Hakimu akitoa zawadi kwa mwananchi aliyejiepusha kuiba hadi uzee umemfikia? Hapa sio mzee aliyeiba lakini hakukamatwa, tunazungumzia mzee aliyekuwa mswaafi wa matendo tokea kuzaliwa kwake.

Kwa mfano dhambi ya kuua mtoto, Allah (Subhanahu Wataala) anasema na tutajaribu kuitafsiri kama ifuatavyo:

{“Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi ndio Tunaowaruzuku wao na nyinyi (pia). Kwa yakini kuwaua ni khatia kubwa.”} [Suratu Bani Israil:31]

Hivyo binaadamu anayeacha kumuuwa mtoto wake anaahidiwa kuruzukiwa yeye na mtoto wake.

Ni Rehma Zake Allah (Subhanahu Wataala) kuweka malipo hata kwa jambo la kutosheleza shahawa za binaadamu kwa njia ya halali. Hili sio tendo jengine ila ni tendo la ndoa baina ya mume na mke nalo pia lina ajira ndani yake.

Imepokewa na Muslim kutoka kwa Abi Dharr Al-Ghaffarriy (Radhiya Allahu Anhu) kutokana na Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam) amesema ((Hakika ya tasbiha ni sadaka, na kila takbira ni sadaka, na kila shukrani ni sadaka, na kila tahliyl ni sadaka, na kuamrisha mema ni sadaka, na kukatazana maovu ni sadaka, na kumuingilia mmoja wenu ni sadaka)) Wakasema Maswahaba (Radhiya Allahu Anhum), Je kumuendea mmoja wetu kwa kuondoa shahawa, pia ndani yake kuna malipo? Akasema Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam): ((Je, anaonaje kama ataendea tendo hilo katika haramu, halitakuwa dhambi?….Na hivyo basi, likiendewa kwa uhalali, lina malipo))

Allah (Subhanahu Wataala) pia Anatoa malipo kwa wacha Mungu. Allah (Subhanahu Wataala)Anasema na tutajaribu kuitafsiri kama ifuatavyo: [Suratun Nabaa:31-36]

{“31-Bila shaka wanaomcha Mwenyezi Mungu wamewekewa (mambo ya kuonyesha) kwao.
32 - Mabustani na mizabibu
33 – Na wanawake vijana walio hirimu (na waume zao)
34 – Na gilasi zilizojaa (vinywaji vizuri vizuri).
35 – Hawatasikia humo (maneno ya) upuuzi wala ya kukadhibishana.
36 – Watalipwa kutoka kwa Mola wako atia yenye kutosha.”}

Sheria za Kiislamu zinagusa nyanja zote muhimu za maisha, roho, usalama, amani na heshima. Kwa vile kuna malipo mazuri kwa mwenye kushikamana nazo, basi hakika ni kivutio kwa mwenye kushikamana nazo. Vitu hivi vyote vinakosekana kutoka sheria za mwanaadamu. Kwa sababu kushikamana kwa Sheria za Kiislamu ni kitendo cha utiifu na kujitoa mhanga kwa ajili ya Muumba, utiifu ambao unamweka karibu na Muumba wake.

Ikiwa kanuni zimeegemea kwa dini na kujilinda nazo, mwanaadamu yoyote atahofia adhabu zake hata kama sheria za mwanaadamu hazitamtia hatiani. Mfano, Uislamu unaamrisha kuwa msafi na kuweka mazingira safi. Hivyo kiimani tunajuwa kuwa Allah (Subhanahu Wataala) anatuona, hivyo hata ukiwa pwani hutokaa ukatupa uchafu ndani ya bahari (kwani kutaathiri viumbe baharini) seuze kwa kutupa uchafu duniani. Hii ni kwa sababu ya “mkono wa sheria” chini ya Utakaso Wake Allah (Subhanahu Wataala) ambao hautegemei kukamatwa mtuhumiwa wala kushitakiwa kabla ya Mahkama za sheria. Hakuna njia ya kukimbia mtenda dhambi asotubia ila atahukumiwa tu.

Kwa kumalizia makala hii, majumuisho yafuatayo yanatolewa kwa tofauti kuu mbili baina ya sheria hizi:

KWANZA, kiini cha Sheria ya Kiislamu ni kutoka kwa Allah (Subhanahu Wataala). Kwa upande wa sheria za mwanaadamu zinatokana na akili za binaadamu. Sheria na adhabu zake ndani ya Uislamu zinapatikana kwenye viini vikuu: Qur-aan na Sunnah. Fiqhi hutumika kutoa ufumbuzi wa jambo kutoka Qur-aan na Sunnah. Utawala wa Taifa la Kiislamu hauruhusiki kuharamisha halali iliyobainishwa chini ya Muumba wala kinyume chake. Halali, haraam na adhabu zake ni vitu vinavyozuiwa kwa hali zote.

PILI, maadili ndani ya sheria za Kiislamu yana nafasi muhimu. Wakati sheria za mwanaadamu inakataa kabisa maadili na haijishughulishi nayo. Uislamu unachukua maadili ni asili ya dini, hakuna mtengano wowote.

Kwa mfano, muislamu anawajibu wa kuwatumikia vizuri wazee wake bila ya hata kusema “AH!” na wazazi wakifika uzee basi ukae nao kwa wema. Sheria ya mwanaadamu haina kanuni kama hiyo. Au kwa mfano mwengine ni mwanamke anayevaa hijaabu vizuri, sio kwamba ndio amemaliza sheria zote za dini. Na haimlazimu mwanamke huyu kuswali, hataaa. Hapa Uislamu unagusa maadili (kuvaa hijabu) na kuswali, (sheria) zote zafuatwa bila ya kuacha nyengine.

Fikra ya kuwa sheria ni upande mmoja na maadili upande mwengine ni kosa. Mtengano huu hauna nafasi ndani ya Uislamu kwani unaweza kusababisha kutokea kwa watu wa aina mbili ambao wote hawataweza kukubalika. Kwa mfano:

Wa mwanzo ni mtu mwenye maadili mabaya lakini ni mzuri wa kufuata sheria. Mfano kutowatumikia vizuri wazee lakini hana chembe ya uzinifu.

Wa pili ni mfuataji mbaya wa sheria lakini anajionesha kwa watu kutenda mema.  Mtu huyu hana tofauti na Mnafiki. Hivyo huwa anachanganya mambo tu, huku yupo na kule yule. Allah (Subhanahu wa Taala) amemwita mtu kama huyu kwa jina la Mudhabdhabiyna. Mfano anatoa hukumu ya waliodhulumiana hali ya kuwa yeye mwenyewe ni mdhulumu mkuu.

Mifano hii inadhihirisha ya kuwa upande wa sheria za mwanaadamu huangukia baina ya pande hizo mbili. Binaadamu anajizuia kuiba kwa sababu tu ni kosa mbele ya sheria lakini hatoi kipato chake kuwasaidia masikini kwa sababu sheria haijashurutisha hivyo. Na kwa upande wa pili unamkuta mtu ameamua kuvunja sheria na kuanza kuiba lakini anatoa mali yake kuwasaidia masikini.

Pia tunaona sheria za mwanaadamu zinazuia wari/wajane kupata mimba lakini haiwazuii kufanya tendo la ndoa (Sheria ya Kuwalinda Wari na Wajane Namba 4 ya mwaka 1985 kifungu cha 3 – Zanzibar). Kwa sababu kujamiiana ni tendo linalogusa maadili na sheria za mwanaadamu hazijishughulishi na vitu vya maadili kama kujamiiana wasokuwa wanandoa, kutembea utupu wanawake, kuchanganya mavazi baina ya mwanaume na mwanamke na mengineyo.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhanahau wa Taala Atuhifadhi na makosa, Atupe malipo kwa amali zetu njema. Atuepushe na elimu isiyokuwa na manufaa. Tunamuomba Atuthibitishe katika itikadi hii na Atuonjeshe matunda Yake na Atuongezee katika fadhila Zake na Asizipoteze nyoyo zetu baada ya kuziongoza, na Atumiminie Rehma kutoka Kwake kwani Yeye ndiye Mpaji.
Shukrani zote ni Zake Yeye Mola wa ulimwengu, na viumbe vyote vya dhahir na siri. Mola wetu Msalie na Mpe Amani Mtume wako Muhammad (SwallaAllahu Alayhi wa Salam) pamoja na Masahaba wake na Aali zake wema, na kila atakayewafuata kwa wema na uongofu mpaka Siku ya Kiama. Kwake Yeye Allah twajitakasa na Kwake twaomba Atutakabalie dua zetu.
AMIYN

Imeandikwa na:
Abdul-Nasser H. R. Hikmany,
Madrasat Al-Tanwir,
Kilimani, Zanzibar,
Shaaban, 1427 H
September, 2006 AD

MAREJEO:

Ø      Britanic Encyclopaedia VOL XXII
Ø      Dr. H. H. Hussain, AN INTRODUCTION TO ISLAMIC LAW.
Ø      H. P. Thomas, DICTIONARY OF ISLAM, Adam Publishers and Distributors, India (1998)
Ø      J. J. Mohammed, INTRODUCTION TO ISLAMIC LAW, International Islamic Publishers (1989
Ø      Nyanzi, ISLAMIC JURISPRUDENCE.
Ø      Q. Abdul-Qadir, CRIMINAL LAW OF ISLAM, VOL. I
Ø      Q. Abdul-Rahman, CRIMINAL LAW OF ISLAM, VOL. I
Ø      Sh. Muhammad Ahmad Kan’ani, USUL AL-MAASHARATU ZAWJIYAH (Misingi ya Maisha ya Ndoa).
Ø      Sheria ya Kuwalinda Wari na Wajane ya Zanzibar ya mwaka 1985.
Ø      Tafsiri ya Qur-aan kwa lugha ya Kiswahili, Sheikh Abdullah Saleh Farsy.
Ø      Zanzibar Penal Act No. 6 of 2004


No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget