Isbaal ni urefushaji wa kitu na makusudio hapa katika makala hii
ambayo itazungumzia vazi la mwanamme, makusudio yake kishari’ah ni kuvaa kivazi
chochote chenye kuvuka chini ya mafundo ya miguu kwa mwanamme; iwe ni kikoi,
shuka, kanzu, joho au suruali. Nalo ni
jambo lenye kukatazwa na limeharamishwa kwa nuswuus (maandiko) mbalimbali ya
kishari’ah kutoka katika Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam).
Lengo la makala haya, ni
kuwatanabahisha Waislam wanaume kuhusiana na ubaya na madhara ya jambo hilo na
pia kuweka sawa ufahamu wa makatazo hayo kuwa hayawahusu tu wenyye kuvaa kwa
kiburi au kwa fakhari, bali ni kwa wanaume wote wa hali zote.
Kwa kumkumbusha aliyesahau,
kumjuza asiyejua, na kumweka sawa mwenye ufahamu wa kinyume wa Hadiyth hizo za
Mtume wetu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tutakuwa
tumesaidiana katika kuyaepuka makatazo ambayo yanaweza yakawa sababu ya kutupwa
motoni kwa jambo ambalo si zito kabisa kuliepuka. Na pia kwa kukumbushana huku,
kutatusaidia kufuata mafunzo ya kipenzi chetu na kufanana naye pamoja na
Maswahaba zake wema kama tutakavyoona
katika makala haya inshaAllaah.
Na kwa kuwa wengi wetu wanaliona
jambo hili la Isbaal ni jambo dogo sana na halina
maana hata ya kulizungumzia au kukumbushana, tunapenda kumkumbusha mwenye fikra
finyu kama hiyo kuwa
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitujulisha kuhusu watu wa
makaburi mawili ambayo alipita katikati yake, akasema:
“Hakika hawa wanaadhibiwa na
hawaadhibiwi kwa mambo makubwa; ama mmoja wao alikuwa hajilindi na chembe
chembe za mkojo, na mwengine alikuwa akipita na kuhamisha maneno (umbea)”Al-Bukhaariy
na Muslim.
Makusudio hapo ya kuwa walikuwa
hawaadhibiwi kwa mambo makubwa, ni kuwa kwa mtazamo wao au dhana zao, hayo
waliyokuwa wakiyafanya yalikuwa si makubwa kwao. Lakini kiuhakika hayo ni
makubwa na ndio maana wakawa wanaadhibiwa.
Hivyo, ndugu Waislam, wale wenye
mawazo ya kuwa suruali yake ikiwa ndefu na kuvuka mafundo yake ya miguu,
kuwa ni jambo dogo sana , basi ni
bora ajihadhari tena ajihadhari na amche Mola wake mapema. Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) singeweza kutoa makemeo makali kama
tutakyosoma huko chini ikiwa jambo hilo si zito
na kubwa. Suruali zetu, kanzu zetu, majoho tunayovaa ya kuolea au kutolea
khutbah za Ijumaa na siku ya ‘Iyd au suti za ofisini na za harusini, zisije
kuwa ni sababu ya kututumbukiza kwenye moto na kufanya tusitazamwe na Allaah,
au kusemeshwa Naye au kutakaswa Naye na mwisho kupata adhabu iumizayo.
Hadiyth zifuatazo zinatoa kwa
uwazi makatazo ya mtu kufanya Isbaal (kuburuza/kuburuta nguo yake):
1- Amesema Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Chenye kuvuka chini ya mafundo ya
miguu katika vazi hupelekea motoni” Al-Bukhaariy
2- Kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya
Allaahu ‘anhu) amesema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Watu watatu Hatowasemesha
Mwenyeezi Mungu siku ya Qiyaamah, na Hatowatazama,
na Hatowatakasa, na watakuwa na adhabu iumizayo. Akarudia mara tatu. Abu Dharr
akasema: Wameangamia na wamekhasirika hao ni nani ee Mjumbe wa Allaah? Akasema
(Mtume): (Hao ni) Al-Musbil – Mwenye kuburuza nguo yake, Mwenye kutoa na kukizungumzia
(kusimbulia) alichokitoa, Na mwenye kuuza bidhaa zake kwa kutumia kiapo cha
uongo” Muslim
3- Kutoka kwa ‘Abdullaah bin
‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) anasema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) amesema:
“Mtu mmoja alipokuwa anatembea, huku
anaburuza nguo yake kwa kibri, alifanywa amezwe na ardhi na ataendelea
kudidimia ndani yake mpaka siku
ya Qiyaamah” Al-Bukhaariy
Pamoja na makatazo yote hayo
yaliyotangulia yaliyoambatana na makemeo, makaripio, na maonyo ya mwisho mbaya
wa jambo hilo, na pamoja
na kuwa Isbaal – kuburuza nguo ni katika madhambi makubwa, lakini utakuta watu
wengi wanatumbukia katika madhambi hayo ima kwa wengi kutokujua ubaya wake,
wengine kwa kughafilika, na wengine wanaojua hayo bado wanaendelea kubaki
katika hali hiyo wakidai kuwa makatazo hayo yanahusu wenye kuvaa nguo ndefu
(wanaoburuza au kuburuta) kwa kiburi wakitegemea baadhi ya Hadiyth zinazoonyesha
hivyo.
Hata hivyo, mtu huyo huyo
anayetoa hoja hiyo; awe ni Mwanachuoni, mtafutaji elimu au mtu wa kawaida,
anajua wazi kabisa kuwa, ikiwa mwenyewe ameamua kuvaa kwa kuburuza vazi lake
hilo pamoja na kufahamu maelezo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam), au utamkuta amekwenda mwenyewe dukani na kuchagua vazi refu lenye
kuburuza, au aende kwa fundi na kumtaka amshonee suruali au kanzu yenye urefu
huo unaovuka mafundoni na labda wakati fundi akiteremsha utepe wake wa kupimia
kwenye mafundo yake, atamwambia teremsha kidogo chini ya mafundo…je, hapo
ataweza kudai kuwa hicho si kiburi na hali ameshasikia au kuziona au kujulishwa
Ahaadiyth zote za Mtume zenye kukemea, kukaripia, na kukataza jambo hilo? Na kama hicho si
kiburi basi kiburi kitakuwa kipi?
Kuwa Isbaal Inawahusu Wenye Kuvaa Kwa Kiburi Au Kwa Fakhari Tu
Baadhi ya watu wanarukhusu Isbaal
kwa kudai kuwa makatazo yaliyokuja katika Hadiyth mbalimbali ni kwa wale tu
wanaovaa kwa kiburi au kujifakharisha. Ima kwa wale wanaovaa tu bila kukusudia kiburi
basi inafaa na hakuna ubaya wowote. Wakitoa hoja kwa kutumia baadhi ya Hadiyth,
mojawapo ya Hadiyth hizo ni Hadiyth maarufu ya kumhusu Abu Bakr (Radhiya
Allaahu kuwa nguo yake ilikuwa ikiburuza, ambayo Mtume ‘anhu) anasema:
“Mwenye kuburuza nguo yake kwa
kiburi, Allaah Hatomtazama siku ya Qiyaamah” Abu Bakr akasema: Ee Mjumbe wa
Allaah! Upande mmoja wa kikoi changu unashuka hadi niuvute na kuuzuia, Mtume
akamjibu: Wewe si mwenye kufanya kwa kiburi”Imesimuliwa na al-Bukhaariy
Majibu Ya Hoja Hiyo:
Kwa kujibu hoja yao ya
kutegemea Hadiyth hiyo kuonyesha kuwa Abu Bakr alikuwa akiburuza nguo yake,
tunajibu kwa maneno ya Wanachuoni ambao wameunganisha Hadiyth za pande zote
kuhusiana na suala hilo na kuweka
ufahamu ulio sahihi:
1- Ametaja Mwanachuoni Ibn Hajar
kuwa, katika masimulizi ya Imaam At-Tirmidhiy kuna ziada baada ya maneno ya
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Atakayeburuza nguo yake kwa
fakhari (kiburi), Hatomtazama Allaah mtu huyo siku ya Qiyaamah), akasema Ummu
Salamah: Je, watafanyaje wanawake na mikia yao (nguo zao zenye kuburuza)? Akasema
(Mtume): Waongeze shibri (kiasi cha kiganja kimoja), Akasema (Ummu Salamah):
Hata hivyo bado miguu yao itakuwa wazi. Akajibu (Mtume): Basi
wazidishe dhiraa na si zaidi ya hapo.”
Ibn Hajar akasema: Alivyofahamu –
yaani Ummu Salamah – ni kuwa makatazo ya kuburuzwa kwa nguo makusudio yake ni
kwa hali zote; iwe kwa kiburi au bila kiburi. Ndipo alipomuuliza Mtume hukumu
ya wanawake kuhusiana na hilo kwa kuhitajia kwao kuburuza ili waweze kujistiri
vizuri miguu yao ili isiwe uchi… kisha akaendelea kusema Ibn Hajar katika
uchambuzi wake: Na Qaadhi ‘Iyaadhw amenukuu ‘Ijmaa’ (makubaliano) ya kuwa
makatazo ya Isbaal ni kwa wanaume na si wanawake, na makusudio yake ni kuwa kukatazwa
kwa Isbaal ni kwa kukariri kwake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) kwa Ummu Salamah ili kumfahamisha. Fat-hul Baariy Mj. 10, uk . 259.
2- Na akasema Ibn Hajar (Allaah
Amrehemu): Ama Isbaal bila ya kiburi, ni wazi kutokana na Hadiyth mbalimbali
kuwa ni Haraam. Kisha akasema: Na ikiwa nguo ni ndefu kuliko urefu wa mtu
mwenyewe basi hiyo huenda ikapelekea kwenye makatazo kwa ajili ya israfu na
kufikia kwenye uharamu. Na vilevile inapelekea makatazo kwa kufanana nako na
mavazi ya wanawake, na hii inawezekana zaidi kuliko sababu ya mwanzo. Na
kadhalika ameeleza Al-Haakim usahihi wa Hadiyth iliyopokelewa na Abu Hurayrah
kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwanamme
anayevaa mavazi ya mwanamke. Vilevile yanapelekea makatazo ya Isbaal kwa mwenye
kuvaa kutosalimika na kupatwa vazi lake na najisi
kwa upande mwengine. Fat-hul Baariy Mj. 10, uk . 263.
3- Ibn Al-‘Arabiy (Abu Bakr) naye
kasema: Haijuzu kwa mwanamme kuachia nguo yake kuvuka mafundo ya miguu, na
akasema: Siburuzi kwa kiburi, kwa kuwa makatazo yanaweza kuhusu hali hiyo
kimatamshi, na wala haijuzu kwa mwenye kuchukulia matamshi hayo ya makatazo kwa
kiburi kuwa ndio hukumu akasema: Mimi hukumu hiyo hainihusu kwa kuwa ‘ilah(sababu)
yake hainihusu. Hakika anayesema hivyo, ajue kuwa madai hayo hayajasalimika,
bali ni kuwa kurefusha nguo na kuvuka mafundo kunaonyesha kiburi chake (huyo
mwenye kurefusha). Fat-hul Baariy Mj.10, uk . 264.
4- Isbaal ni mwelekeo wa kiburi.
Anasema Ibn Hajar (Allaah Amrehemu): Isbaal inalazimu kuburuzika kwa nguo, na
kuburuzika kwa nguo kunalazimu kiburi japo ikiwa mwenye kuvaa hajakusudia
kiburi. Na yanaungwa mkono maneno yake hayo na aliyosimulia Ahmad bin Muniy’i
kwa upande mwengine kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kutoka
katika Hadiyth ambayo inasema,
“Ole wako na kuburuza nguo (kuvuka
mafundo ya miguu), kwani kuburuza nguo ni alama ya kiburi”. Fat-hul
Baariy Mj.10, uk . 264.
5- Amesema Mwanachuoni Shaykh
Muhammad bin Swaalih bin Al-‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) kuhusu Hadiyth hii,
“Mwenye kuburuza nguo yake kwa
kiburi, Allaah Hatomtazama siku ya Qiyaamah” na
Hadiyth hii, “Chenye
kuwa chini ya mafundo ya miguu katika mavazi, basi ni motoni”: Kwa
kuwa kumekhitilafiana adhabu hizo mbili, basi kunakatazika kuifanya hukumu hiyo
(ya Isbaal) kuwa ‘Mutwlaq’ (iliyo wazi ya moja kwa moja) ni yenye kuwa juu ya
‘Muqayyad’ (iliyofungamanishwa na kitu), kwani kanuni ya kubeba ‘Mutwlaq’ juu
ya ‘Muqayyad’ ni sharti kukubaliana ‘Nasw’ (maandiko) mbili katika hukumu. Ama
ikitofautiana hukumu (kama ilivyo
kwenye hizo Hadiyth mbili juu) basi haibebeshwi mojawapo juu ya mwenzake. Na
hivyo ndivyo hata Aayah ya kutayamamu ambayo Amesema Allah:
“Na mpanguse nyuso zenu na
mikono yenu kwayo” haikufunganishwa
na Aayah ya Wudhuu ambayo Allaah Amesema:
“Na muoshe nyuso zenu na mikono
yenu hadi kwenye viwiko” maana
haiwi Tayammum hadi kwenye viwiko.
6- Naye Mwanachuoni mwengine,
Shaykh Mash-huur Aal-Salmaan (Allaah Amhifadhi) anasema: Na ametupa faida
Shaykh wetu Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) katika baadhi ya vikao vyake kwamba
haijuzu Muislam kukusudia kurefusha vazi lake miguuni kwa madai kuwa hafanyi
hivyo kwa kiburi, na anaunganisha hayo kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyomwambia Abu Bakr, “Wewe si mwenye kufanya kwa
kiburi”, kwa sababu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuwa akivaa nguo ndefu,
na Mtume akamwambia, “Wewe si mwenye kufanya kwa kiburi”, ila hayo majibu ya
Mtume kwa Abu Bakr yalikuwa ni kwa sababu Abu Bakr vazi lake lilikuwa lamshuka
lenyewe, na akawa akionekana ni kama mwenye kurefusha nguo. Na Mtume akamjibu
kumwambia kuwa hilo ni jambo
ambalo huchukuliwi kwalo, kwani hujakusudia na wala hukulifanya kwa kiburi.
Hivyo, ni makosa kabisa watu kuuunganisha tukio la Abu Bakr na kuburuza kwao
nguo kwa makusudi kisha wakadai kuwa: ‘Sisi hatufanyi kwa kiburi’! Tukio la Abu
Bakr haliwezi katu kuwa hoja ya wanayoyafanya.
7- Amesema Mwanachuoni Faqiyh
Shaykh Muhammad bin Swaalih bin Al-‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu): “Hakika Abu
Bakr katakaswa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatoa
Mtume ushahidi kuwa Abu Bakr si katika wale wanaofanya hivyo (kuvaa nguo
ikaburuza) kwa fakhari. Sasa je, hao wanaovaa nguo zikavuka mafundo
(zikaburuza) wamepata utakaso au ushuhuda kama huo wa
Abu Bakr?!
Lakini Shaytwaan anawafungulia
baadhi ya watu milango ya kufuata yale maandiko yenye utata kwenye Qur-aan na
Sunnah ili yaendane na matashi yao na yale
wayafanyayo, na Allaah Ndiye Humuongoza Amtakaye katika njia nyoofu, tunamuomba
Allaah Atupe sisi na wao hidaaya”
No comments:
Post a Comment