Monday, February 20, 2012

Hoja za Maulidi Na Majibu Yake


BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi waAswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:

Tunaandika makala hii kwa ikhlaasw na unyenyekevu kabisa mbele ya Allaah سبحانه وتعالى kisha mbele ya ndugu zetu wanaodhani kwamba kushereheka Mawlid ni jambo jema na si jambo la bid'ah.
Niya yetu ni kutaka kuwatanabahisha ndugu zetu Waislamu kuhusu mas-ala yaliyoingia shubuhaat na yanayoharibu 'Aqiydah ya Muislamu kwani kama wanavyosema Maulamaa kuwa ufisadi mkubwa wa dini ni uzushi (bid'ah) wa mambo katika dini. Kwa hiyo tunataka kuwaonyesha ndugu zetu yaliyo baatil na ya haki ili wabakie katika 'Aqiydah safi na mwendo wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na Maswahaba zake.
Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba mas-ala haya ya kuonyesha yaliyo sahihi na kukataza bid'ah yanaleta kufarikiana Ummah huu, hata kufikia kuzozana baina ya Waislamu. Tunachopenda kuwakumbusha ndugu zetu ni kwamba huu ni ujumbe tunaofikisha na hali tukiamini ni wa haki ingawa unakubali kukosolewa, na ni juu ya msomaji mwenyewe kuamua kuufuata au kuuacha lakini bila ya kufarikiana, bali ubakie undugu na ihsaan baina yetu bila ya kuingia chuki au kutengana.
Tufahamu kuwa Allaah   سبحانه وتعالىAmetuamrisha jambo la kuamrishana mema na kukatazana mabaya na ndio iwe kazi yetu kama Anavyosema:
((وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ))
((Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu)) [At-Tawbah:71]
Na vile vile ni kutimiza amri ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   aliyotuambia kwamba:
عن أَبي سعيدٍ الخُدْريِّ رضي اللَّه عنه قال : سمِعْتُ رسُولَ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ :   ((مَنْ رَأَى مِنْكُم مُنْكراً فَلْيغيِّرْهُ بِيَدهِ ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطعْ فبِلِسَانِهِ ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبقَلبهِ وَذَلَكَ أَضْعَفُ الإِيمانِ)) رواه مسلم .
Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudhriy رضي الله عنه  ambaye amesema: Nilimsikia Mtume صلى الله عليه وآله وسلمakisema: ((Yeyote yule atakayeona kitendo kiovu mwache akiondoe (abadilishe) kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake (alikemee au kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake (achukie) na huo (yaani kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Imani)) [Imesimuliwa na Muslim]
Hatuna budi kufuata uongozi katika ibada kwa njia aliyotufundisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kamaAnavyosema Allaah سبحانه وتعالى:
((لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ))
((Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho)) [Al-Ahzaab:21]
Na Anasema Allaah سبحانه وتعالى    
((وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا))
((Na anachokupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho)) [Al-Hashr: 7]
Naye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametuamrisha katika nasw nyingi tumfuate katika ibaada, mbili zifuatazo:
((صلوا كما رأيتموني أصلي))
 ((Swalini kama mlivyoniona naswali)) [Al-Bukhaariy]
((يا أيها الناس خذوا عني مناسككم))  صحيح الجامع  
((Enyi watu, chukueni kwangu manaasik zenu [utaratibu wa ibada ya Hajj])) [Muslim]
 Na Ametuonya kwamba tukifanya kitendo kilichokuwa si katika mwendo wake na Maswahaba zake basi hakina thamani, bali hakitapokelewa:
 (( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري
((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Muslim]
HOJA YA KWANZA YA WATETEZI WA MAWLID
Aayah katika Surat Yuunus:
((قُلْ بِفَضْلِ اللّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُواْ هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ))
((Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na Rehma yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya)) [Yuunus:58]
Jibu la kwanza la Hoja hiyo: 
Baadhi ya watetezi wa Mawlid wanatoa hoja ya Aayah hii kuwa kuambiwa na Allaah  سبحانه وتعالىwafurahi, basi ni kufurahia mazazi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم. Lakini tukitazama tafsiri ya Aayah hiyo kwa wafasiri wote wakubwa kama Ibnu Jariyr, Ibnu Kathiyr, Qurtubiy, Al-Baghaawiy, Ibnul-Arabiy na wengineo, hatukuti maana hiyo kabisa. Maana iliyotajwa na wafasiri ni wafurahi kwa yale yaliyowajia kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى  ya uongofu na dini ya haki. Na pia imefasiriwa kuwa, wafurahi kwa Qur-aan na Uislam. Ushahidi ni kutokana na Aayah ya kabla yake inayosema:
((يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ))
((Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uongofu, na Rehma kwa Waumini)) [Yuunus:57]
Nayo ni Qur-aan. Na kama pia Aayah ya 170 ya Suratul 'Imraan isemayo, ((Na ni wenye kufurahia fadhila Zake)). Vilevile imefasiriwa kuwa fadhila Zake ni Uislam, na Rahma Zake ni Qur-aan. wa Allaahu A'alam
Amesema Ibnu Kathiyr katika tafsiyr yake kuhusu: ((uongofu na Rahma kwa Waumini)), ni kupata uongofu na Rahma kwa waumini waliosadiki na kukinaika. Kama zinavyoonyesha kauli Zake Allaahسبحانه وتعالى nyingine:
((وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِلْمُؤْمِنِينَ وَلا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَاراً))  
((Na Tunateremsha katika Qur-aan yaliyo ni matibabu na Rehma kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara)) [Al-Israa:82]
Na kauli Yake Allaah  :سبحانه وتعالى    
((قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدىً وَشِفَاء))
((Sema: Hii Qur-aan ni uongofu na poza kwa wenye kuamini)) [Fuswilat:44]
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Rahma kwa watu haiwi kwa mazazi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   bali ni kwa kupewa kwake Utume na kutumwa kufikisha ujumbe kwa watu. Na dalili ni kutoka katika Qur-aan na Sunnah.
Nasw kutoka katika Qur-aan ni kwamba yeye ni Rahma kwa viumbe wote kutokana na kutumwa kwake na wala haikutaja kuzaliwa kwake. Anasema Allaah  سبحانه وتعالى
((وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ))
((Nasi Hatukukutuma ila uwe ni Rehma kwa walimwengu wote)) [Al-Anibyaa:107]
Ama katika Sunnah ni Hadiyth:
عن أبي هريرة رضي الله عنه   قال: قيل : يا رسول الله ! ادع على المشركين . قال صلى الله عليه وسلم  (( إني لم أبعث لعانا  وإنما بعثت رحمة)) مسلم     
Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه ambaye amesema: Aliambiwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   "Waombee (walaaniwe) Washirikina". Akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ((Mimi sikupewa utume (sikutumwa kuja kuwa) ni mlaaniji (mwenye kuwaombea laana watu) bali nimepewa utume kuwa ni Rahma)) [Muslim]
HOJA YA PILI YA WATETEZI WA MAWLID
 Aayah katika Suratul-Ahzaab
 ((إِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيماً))
((Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu)) [Al-Ahzaab:56]
 Kwamba Mawlid yanahusu kumswalia kama ilivyo Aayah hiyo. 
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Imaam Al-Bukhaariy anatueleza tafsiri ya Aayah hiyo ni kuwa Maswahaba رضي الله عنهم walimuuliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuwa washajua namna ya kumtakia amani juu yake, lakini hawakujua namna gani wamswalie. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akawaambia waseme, 'Allahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'ala aali Muhammad...' hadi mwisho kama ilivyo kwenye tashahud.
Na maana au tafsiri ya Aayah hiyo imeelezwa na wafasiri na wana Hadiyth taqriban wote kwa maana hiyo au karibu na hiyo ya Imaam Al-Bukhaariy. Kwa maana hiyo tunakutana na ulinganisho usiolingana unaofanywa na watetezi wa jambo hilo
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Inatupasa tumsawalie Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   kwa wingi kila mara kama ilivyothibiti fadhila zake katika Hadiyth ifuatayo:
عنْ عبد اللَّه بن عمرو بن العاص ، رضي اللَّه عنْهُمَا أنَّهُ سمِع رسُول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ : (( من صلَّى عليَّ صلاَةً ، صلَّى اللَّه علَيّهِ بِهَا عشْراً))   رواهُ مسلم
Imetoka kwa 'Abdullah ibn 'Amru ibn Al-'Aasw  رضي اللَّه عنْهُمَاkwamba kamsikia Mtume صلى الله عليه وآله وسلمanasema, ((Atakayeniswalia (kuniombea Rahma) mara moja, Allaah Atamswalia (Atampa Rahma) mara kumi)) [Muslim]
Kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametufundishia nyakati za kumswalia kama siku ya Ijumaa, baada ya adhaan, anapotajwa n.k. Lakini hakutufundisha kuwa tumswalie siku ya kuzaliwa kwake

HOJA YA TATU YA WATETEZI WA MAWLID
Kufurahikia kuzaliwa kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   ni jambo lililoamrishwa katika Qur-aan wakitaja Aayah mbili zifuatazo zinazohusiana na Nabii Yahya  عليه السلام   na Nabii 'Iysa  :عليه السلام    
 ((وَسَلَامٌ عَلَيْهِ يَوْمَ وُلِدَ وَيَوْمَ يَمُوتُ وَيَوْمَ يُبْعَثُ حَيًّا))
((Na amani iwe juu yake siku ya kuzaliwa, na siku ya kufa, na siku ya kufufuliwa)) [Maryam: 15] Akimaanishwa Yahya عليه السلام  
((وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا))
((Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai))[Maryam: 33] Akimaanishwa 'Iysa عليه السلام  
Jibu la kwanza la Hoja hiyo: 
Aayah inasema ((amani...)). Je, ina maana kwamba, neno 'amani' ni sawa na kufurahikia? Vile vile Aayah hizo hazikutaja kuzaliwa peke yake bali zimetaja; kuzaliwa, kufa na kufufuliwa. Sasa vipi ichukuliwe utajo mmoja tu na nyingine ziachwe? Vile vile Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amefariki mwezi huu wa Rabiy'ul Awwal na kama walivyokubaliana Maulamaa kwamba ni tarehe hiyo ambayo inayodaiwa kuwa kazaliwa, nayo ni 12 Rabiy'ul Awwal, ingawa uhakika wa kuzaliwa kwake haujulikani kama ni siku hiyo. Na je, wanaosherehekea kuzaliwa kwake vile vile wanasherehekea kufa kwake na kufufuliwa kwake? Ikiwa ni hivyo, vipi watasherehekea siku ya kufufuliwa kwake?
HOJA YA NNE YA WATETEZI WA MAULID:
Kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akifunga siku ya Jumatatu ambayo ilikuwa siku ya kuzaliwa kwake kama ilivyokuja nasw katika Hadiyth ifuatayo, kwa hiyo aliiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake:
عن أبي قتادة رضي الله عنه : أن النبي صلى الله عليه وسلم سئل عن صوم يوم الاثنين فقال: ((ذلك يوم ولدت فيه وأنزل علي فيه))  رواه الإمام مسلم
Imetoka kwa Abu Qataadah  رضي الله عنهkwamba aliulizwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kuhusu kufunga Jumatatu akasema: ((Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku ulioteremshwa kwangu [Utume])) [Imaam Muslim]
Kwa hiyo alikuwa akimshukuru Allaah سبحانه وتعالى kwa neema hiyo.
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Kuiadhimisha siku yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   ya kuzaliwa na kumshukuru kulikuwa ni kwa kufanya ibada kama hiyo ya kufunga na sio kwa kusherehekea kusoma Mawlid. 
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Mtume  صلى الله عليه وآله وسلم hakufunga siku maalum katika mwezi huu wa Rabiy'ul Awwal ikiwa ni tarehe 12 au nyingine yoyote, bali alikuwa akifunga kila Jumatatu mwaka mzima. 
Jibu la tatu la Hoja hiyo:
Kufunga kwake Jumatatu kwa ajili ya kumshukuru Allaah سبحانه وتعالى  kupewa Utume awe 'mbashiriaji na muonyaji' kwa ulimwengu wote kulikuwa ni kwa kufunga pekee na si kwa kukusanya watu kwa kufunga au kusherehekea kama inavyosherehekewa na wasomaji Mawlid.  
HOJA YA TANO YA WATETEZI WA MAULID
Kwamba Maswahaba walimpokea Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    alipoingia Madiynah kwa qaswiydah na wengine walikuwa wakimsomea mashairi na qaswiydah Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   za kumsifu na yeye alikuwa akikubali kusomewa hayo mashairi.
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Kwanza kuna shaka na usemi huo wa kusomewa qaswiydah ya 'Twala'al-Badru 'Alayna, Min Thaniyaatil Wada'a' wakati wa kupokelewa alipofika Madiynah. Historia za kuaminika za tukio hilozinaonyesha hakuna ushahidi kuwa Mtume alipita njia hiyo ya 'Thaniyat al Wada'a' wakati wa kuelekea Madiynah, na hali qaswiydah hiyo inaelezea mapitio yake ya sehemu hiyo! 
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Haikuthibitika kwamba Maswahaba walikuwa wakimsomea mashairi na qaswyidah siku ya kuzaliwa kwake, bali ilikuwa zaidi kunapotokea ushindi wa vita kuwashinda maadui.
HOJA YA SITA YA WATETEZI WA MAWLID
Kwamba kusherehekea Mawlid ni kumpenda, kumuadhimisha, kumtukuza na ni kumbukumbu ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa watu, na hili ni jambo linalotupasa tufanye ili vizazi vyetu pia vipate kumtambua Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Kumkumbuka na kumuadhimisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    kunatupasa kila siku katika maisha yetu kwa kumpenda na kufuata Sunnah zake. Na si kwa njia ya kusherehekea kama inavyosherehekewa kwa kusoma Mawlid mara moja tu katika mwaka.
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Kumbukumbu ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kwa watu na vizazi vyetu vimeshabainishiwa na Allaah سبحانه وتعالى katika Qur-aan na Sunnah. Nayo ni kwa kila siku vile vile na si kwa mwaka mara moja tu. Katika Qur-aan Anasema Allaah سبحانه وتعالى    
 ((وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ))
 ((Na Tukakutukuza utajo wako)) [Ash-Sharh:4]
Na kutukuzwa huko ni katika kila Swalah zetu tunapomswalia katika tashahhud, katika kutimiza fardhi zetu kama Hajj na Swawm, inapoadhiniwa na iqaamah ya Swalah, kwenye khutba, kumswalia anapotajwa jina lake, tunaposoma au kusikia Hadiyth zake, katika kufuata Sunnah zake, katika vikao vya darsa za dini yetu na kadhalika, kwa hiyo ni kumbukumbu ya kila siku, kila wakati katika maisha yetu na sio siku moja tu katika mwaka. 
 HOJA YA SABA YA WATETEZI WA MAULID
Kwamba kuna Bid'atun-hasanah (bid'ah njema).
Jibu la hoja hiyo:
Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  alipotaja kuhusu bid'ah amesema:
((....وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ ))  رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح
((…na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila  bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth hasan sahiyh]   
Hapa ametaja kuwa 'Kullu bid'atin Dhwalaalah' (KILA bid'ah ni upotofu). Na ikiwa kauli hii wanaipinga kuwa si KILA bid'ah, basi wanasemaje kuhusu kauli za Allaah سبحانه وتعالىAnaposema:
 ((كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ))
((Kila nafsi itaonja mauti)) [Al-'Imraan: 185]
 ((وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَآئِرَهُ فِي عُنُقِهِ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا ))
((Na kila mtu Tumemfungia amali yake shingoni mwake. Na Siku ya Qiyaamah Tutamtolea kitabu atakachokikuta kiwazi kimekunjuliwa)) [Al-Israa:13]
((كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ))
 ((Kila nafsi imo rahanini kwa mabaya iliyoyachuma))  [Al-Mudathhir:38]
((وَكُلُّ شَيْءٍ فَعَلُوهُ فِي الزُّبُرِ))   ((وَكُلُّ صَغِيرٍ وَكَبِيرٍ مُسْتَطَرٌ))
((Na kila jambo walilolifanya limo vitabuni))
((Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa))  [Al-Qamar:52-53]
Je, tutakanusha kwamba sio kila nafsi itaonja mauti, au si kila mtu amefungiwa amali zake shingoni, au si kila nafsi iko rahanini, au si kila jambo tunalolifanya dogo na kubwa liko vitabuni? Bila shaka kauli ya Allaah سبحانه وتعالى Inathibitisha kuwa kila binaadamu atakufa na kila mmoja ana hesabu yake atakayoikuta siku ya Qiyaamah. Kwa hiyo na kauli ya 'kullu bid'atin dhwalaalah' (kila bid'ah ni upotofu) pia ina maana kwamba hiyo hiyo bila ya kuigawa ikawa ni baadhi tu ya bid'ah. 
HOJA NA NANE YA WATETEZI WA MAWLID
Kwamba kuna baadhi ya mambo yamefanyika baada ya kufa kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  na yanaendelea kutendeka kwa hiyo ni bid'ah. Mifano wa hayo yanayotolewa kama hoja ni; kukusanywa Qur-aan na kuwekwa katika mus-haf na Abu Bakar  رضي الله عنه kuhamishwa Maqaam Ibrahiym na 'Umar ibnul Khatwaab  رضي الله عنه au kuongezwa adhaan ya pili na ya tatu siku ya Ijumaa na 'Uthmaan bin'Affaan رضي الله عنه 
Jibu la Hoja hiyo:
Kwamba jambo lolote walilolifanya hao Makhalifa ni Sunnah za kuzifuata pia kama Alivyosema Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم :
 ((... أُوصِيكُمْ بِتَقْوى اللَّه، وَالسَّمْعِ وَالطَّاعَةِ وإِنْ تَأَمَّر عَلَيْكُمْ عَبْدٌ حبشيٌ، وَأَنَّهُ مَنْ يَعِشْ مِنْكُمْ فَسَيرى اخْتِلافاً كثِيرا . فَعَلَيْكُمْ بسُنَّتي وَسُنَّةِ الْخُلُفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ ، عضُّوا عَلَيْهَا بالنَّواجِذِ، وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ)    رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح
((Nakuusieni kumcha Allah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrisheni) ni Mtumwa  wa Kihabashi. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu.  Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth hasan sahiyh] 
 HOJA YA TISA YA WATETEZI WA MAWLID
Kwamba msahafu ulikuwa hauna irabu/harakaat (vokali), au Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  na Maswahaba hawakutumia kipaza sauti (speakers) katika adhaan, au kufanya twawaaf juu badala ya chini, au hawakupanda magari bali walipanda ngamia, au hakukuweko na zana za utamaduni za kujifunza dinikama radio, televisheni, mtandao, tovuti, CD's na kadhalika. Kwa hiyo kutumia vitu hivyo pia ni bid'ah.
Jibu la Hoja hiyo:
Kuhusu Mus-haf na irabu – Qur-aan ilikuwa imehifadhiwa katika vifua vya Maswahaba ambao walikuwa ni wenye lugha ya Kiarabu fasaha, kwa hiyo hawakuhitaji irabu. Ilipotokea haja ya kukusanya Qur-aan katika mus-haf kwa vile Maswahaba wengi waliohifadhi Qur-aan waliuliwa katika vita vya Yamaamah, Maswahaba wakaingiwa na khofu ya kupotea Qur-aan kabisa hata isiweze kutufikia sisi na vizazi vyote hadi siku ya Qiyaamah. Ndipo ilipokusanywa baada ya ushauri mzito baina ya Makhalifa na Maswahaba na wakakubaliana kuikusanya katika Mus-haf.
Hata hivyo kukawa vile vile hakuna haja ya kuweka irabu kutokana na ufasaha wa lugha ya Kiarabu. Ilipofikia zama za Yusuf bin Hajjaaj, khofu iliingia ya kutowezekana kuisoma Qur-aan inavyopasa kwa vile lugha ya Kiarabu ilianza kupotea ufasaha wake. Kwa hiyo jambo kama hili lilikuwa ni jambo lililohitajika kufanyika ili kuendeleza ibada ya kuisoma Qur-aan na kupata mafunzo yake, na khaswa kwamba Qur-aan ni uongofu wa ulimwengu mzima, hivyo hata ambao si Waarabu waweze kuisoma baada ya kuweka irabu/harakaat, la sivyo ingelikuwa vigumu kusomeka kwa wasiojua lugha ya Kiarabu sawa sawa.
Hali kadhalika kufanya twawaaf juu kumehitajika na kumekuwa hakuna budi, kwa umuhimu wa kutimiza ibada hiyo ya fardhi, na kutokana na zahma kubwa ya Mahujaji haiwezekani wote kutimiza twawaaf chini. Kwa hiyo panapotokea umuhimu wa jambo la lazima kufanyika kwa manufaa ya Ummah wa Kiislamu ili tuweze kutimiza ibada zetu  basi hakuna budi kutendeka na hata hivyo haiingii katika kuzidisha ibada yenyewe khaswa.   
Ama kuhusu nyenzo kama vipaza sauti, njia za usafirishaji, vifaa vya utamaduni vya kujifunzia na kadhalika vyote hivyo ni nyenzo tu za kutuwepesishia kutekeleza ibada zetu na yote yanayotupasa katika amri za dini. Kuchanganya nyenzo na ibada ni jambo lilisilokuwa la mantiki (logic). Na Allaah سبحانه وتعالى Mjuzi wa mambo yasiyoonekana Amejua yote hayo kuwa yatatokea. Mfano kuhusu usafiri Allaah سبحانه وتعالى    Amejua kwamba watu watatoka kila pembe ya dunia kufika Makkah kutimiza Hajj, sasa vipi mtu ategemee kuwa usafiri wa nchi ya kutoka Kaskazini kufika Kusini asafiri na mnyama? Bila shaka haingii akilini jambo hili.
Hivyo Allaah سبحانه وتعالى Ametambua shida ya usafiri zitakazotokea kutokana na umbali wa nchi na nchi ndio Akasema:  
((وَالأَنْعَامَ خَلَقَهَا لَكُمْ فِيهَا دِفْءٌ وَمَنَافِعُ وَمِنْهَا تَأْكُلُون))
((وَلَكُمْ فِيهَا جَمَالٌ حِينَ تُرِيحُونَ وَحِينَ تَسْرَحُونَ))
 ((وَتَحْمِلُ أَثْقَالَكُمْ إِلَى بَلَدٍ لَّمْ تَكُونُواْ بَالِغِيهِ إِلاَّ بِشِقِّ الأَنفُسِ إِنَّ رَبَّكُمْ لَرَؤُوفٌ رَّحِيمٌ)) 
  ((وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَةً وَيَخْلُقُ مَا لاَ تَعْلَمُونَ))
((Na wanyama hao Amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala))
((Na wanakupeni furaha pale mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka malishoni asubuhi))
((Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyoweza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole na Mwenye kurehemu))
((Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na kuwa ni pambo. Na Ataumba msivyovijua)) [An-Nahl:5-8]
Tusivyovijua ndio kama njia za usafiri za kisasa kama magari, ndege, matreni na kadhalika [Aysarut-Tafaasiyr Shaykh Abu Bakr Al-Jazaairy: 3:102]
Kwa hiyo kila inapopatikana njia au kifaa bora cha kutusahilishia maisha yetu kinafaa kutumika na haiwi ni jambo la bid'ah katika dini, bali unaweza kuita bid'ah kilugha kwani hivyo sio ibada iliyokusudiwa kuwa ni bid'ah.
Tukimalizia, tunaona kwamba hoja zote hizo zitolewazwo na wanaounga mkono Mawlid si sahihi, bali ni za kujaribu kulipa jambo hilo sheria na hali halimo katika sheria katu. Na wengi wengine watakwambia, "Kwani kuna ubaya gani?" Au watakutuhumu wewe unayewauliza ushahidi wa kufanya jambo hilo, kuwa humpendi Mtume صلى الله عليه وآله وسلم.  
Lau kama kusherehekea mazazi yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   ingelikuwa ni amali njema, basi Maswahaba na Salaf Swaalih (wema waliopita) wangelitutangulia katika jambo hilo. Wao walikuwa wakizielewa mno Sunnah za Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   kuliko sisi, walimpenda mno kuliko sisi, na walikuwa tayari kupoteza  nafsi zao au mali zao kwa mapenzi yao kwake, na walifuata sheria kuwashinda wale waliokuja baada yao.

Sisi tumeamrishwa 'kufuata' na tumekatazwa 'kuzua'. Hii ni kwa sababu ukamilifu wa dini ya Kiislamu na utoshelezaji wa yale tuliyopewa na Allaah سبحانه وتعالى  na Mtume Wake, na hayo yamefuatwa na Waislam wote wa mwanzo kuanzia Maswahaba  na wafuasi wao wema.
 اللَّهُمَّ  اَرِنا الْحَقَّ حَقاً وَارْزُقْنا اتِباعَه وَارِنا الباطِلَ باطلاً وَارْزُقْنا اجْتِنابه .
Allaahumma Arinal-Haqqa Haqqaw-War-Zuqnat-tibaa'ah, Wa Arinal-Baatwila Baatwilaw-War-Zuqnaj-tinaabah.
Ee Allaah, Tuonyeshe haki kuwa ni haki Na Uturuzuku kuifuata. Na utuonyeshe batili kuwa ni batili na Uturuzuku kuiepuka.


No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget