Uislamu, Dini ya rehma, hauruhusu ugaidi. Katika Qur-aan, Mwenyezi Mungu Amesema: “Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu Huwapenda wafanyao uadilifu.” (Qur-aan, 60:8)
Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwakataza askari dhidi ya kuwaua wanawake na watoto,[Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 1744, na Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 3015]na alikuwa akiwashauri: ((...Msisaliti, msizidishe sana, msimwue mtoto mchanga.))”[Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 1731, na At-Tirmidhiy, Na, 1408 ]
Alisema pia: ((Mwenye kumuua mtu aliye katika mkataba na Waislamu, hataipata harufu ya Peponi, ingawa harufu yake hupatikana mpaka katika umbali wa mwendo wa miaka arubaini.))[
Imeandikwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy, Na. 3166, na Ibn Majah, Na. 2686]
Kadhalika, Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kutoa adhabu ya moto.[Iko ndani ya Abu Daawuud, Na. 2675]
Kuna wakati aliorodhesha dhambi ya kuua kuwa ya pili miongoni mwa madhambi makubwa,[
Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 6871, na Swahiyh Muslim Na. 88]
hata akatahadharisha hilo juu ya Siku ya Hukumu, ((Kesi za mwanzo kuhukumiwa baina ya watu ka tika Siku ya Hukumu zitakuwa ni zile za umwagaji damu.
Hii inamaanisha kuua na kujeruhi))[Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 1678, na Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 6533]
Waislamu huhimizwa hata kuwa wakarimu kwa wanyama na wamekatazwa kuwadhuru. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema siku moja: ((Mwanamke aliadhibiwa kwa sababu alimweka paka kifungoni mpaka akafa. Kwa minajili hii, aliangamiziwa Motoni. Wakati alipomweka kifungoni, hakumpatia paka chakula wala kinywaji, wala hakumwacha huru ale wadudu wa ardhini.)) [
Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 2422, na Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 2365]
Pia alisema kuwa kuna mtu alimpatia kinywaji mbwa aliyekuwa na kiu kikali, hivyo Mwenyezi Mungu Alimsamehe madhambi yake, kwa kitendo hiki. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Je, sisi hulipwa kutokana na ukarimu wetu kwa wanyama?” Alijibu: ((Kuna malipo kwa ukarimu kwa kila mnyama hai au mwanaadamu.)) [
Hadiyth hii ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) imeelezwa kwa kirefu hapo nyuma. Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 2244, na Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 2466]
Zaidi ya hayo, wakati wa kuchinja mnyama kwa ajili ya chakula, Waislamu wameamrishwa kufanya hivyo katika namna inayopelekea hofu ndogo na mateso madogo sana kwa mnyama, kadiri itakavyowezekana. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mnapomchinja mnyama, fanyeni katika njia iliyo bora zaidi. Mchinjaji akinoe kisu chake kwa ajili ya kupunguza mateso ya mnyama.))[Imeandikwa katika Swahiyh Muslim, Na. 1955 na At-Tirmidhiy, Na. 1409]
Kutokana na mwangaza wa haya na mafundisho mengine ya Kiislamu, kitendo cha kuchochea khofu katika nyoyo za raia wasio na ulinzi, uharibifu wa majengo na mali, ulipuaji mabomu na kuwalemaza wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia, yote haya yamekatazwa, tena ni matendo ya kuchukiza kwa mujibu wa Uislamu na Waislamu. Waislamu wanaifuata Dini ya amani, huruma na msamaha, na wengi hawahusiani na matukio ya vurugu ambayo baadhi yamehusishwa na Waislamu. Ikiwa Muislamu mmojawapo atajihusisha na kitendo cha kigaidi, mtu huyo atakuwa katika hatia ya kukiuka sheria za Uislamu.
No comments:
Post a Comment