Kutengeneza
Swafu ni kuinyoosha sawa sawa kabisa bila kupinda wengine kuwa mbele kidogo na
wengine kuwa nyuma. Kadhalika unyooshaji wa Swafu hunyooshwa kwa kulingana
visigino vya wenye kuswali na si kulingana vidole vya miguu kama wanavyodhania wengine.
Vilevile, kutengeza Swafu na kuinyoosha ni watu kugusana mabega
kama alivyoeleza Swahaba Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa walikuwa
wakikamatanisha mabega yao kamayaliyoshikamanishwa
kwa gundi. Na pia anaeleza kuwa walikuwa wakigusana mafundo ya miguu yaobila
kuwa na upenyo wala nafasi yoyote ile.
Tutazame Hadiyth zifuatazo tuone umuhimu wa Swafu na kuinyoosha
na kuitengeneza:
Imepokewa na mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika
Allaah na Malaika Wake wanawaombea wenye kuswali katika swafu, na mwenye kuziba
upenyo (nafasi) Allaah anamnyanyua daraja yake” (Ahmad, Ibn Maajah, Ibn
Khuzaymah na Ibn Hibbaan).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) aliusia: “… Wala
msiache upenyo kwa Shaytwaan, na mwenye kuunganisha swafu, Allaah Humuunganisha
na mwenye kuikata, naye Hukatwa na Allaah” (Ahmad na Abu Daawuud, na
kusahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy).
Imepokewa na Anas (Radhiya
Allaahu ‘anhu) aliyesema: Kulikimiwa Swalah, naye Mtume wa Allaah (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatukabili kwa uso wake, akasema: “Tengezeni
swafu zenu, kwani mimi nawaona nyuma ya mgongo wangu”
(al-Bukhaariy na Muslim).
Imepokewa na Jaabir bin Samurah
(Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa alitutokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) akasema: “Je, hamupangi swafu kama wanavyopanga Malaika mbele ya Mola wao
Mlezi?” Tukasema: “Ewe Mtume wa Allaah! Na Malaika wanapanga vipi swafu mbele
ya Mola wao Mlezi?” Akasema: “Wanatimiza swafu za kwanza na wanazipanga
sawasawa” (Muslim).
Imepokewa na Anas bin Maalik
(Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
amesema: “Tengezeni swafu zenu kwani katika kutengeza swafu ni katika
kusimamisha Swalah” (al-Bukhaariy na Muslim).
Na imepokewa na an-Nu‘man bin
Bashiyr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtaendelea kuweka swafu sawa au Allaah
Atazibadilisha nyuso zenu” (al-Bukhaariy na Muslim). Na katika riwaya ya Ahmad na Ibn
Hibbaan: “…au Allaah Atazibadilisha nyoyo zenu”.
Kinyume na leo tunavyoona kwenye Misikiti mingi hususan ya ndugu
zetu wa Ki-Hanafi ambao hawataki kugusana na wenzao miguu wala mabega na hivyo
kuachwa nafasi katika Swafu, nafasi ambazo wanaweza kuingia watu wengi katika
Swafu moja kama nafasi hizo zingezibwa na kama wangelifuata mafundisho ya Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake (Radhiya Allaahu
‘anhum) vizuri kama yalivyopokelewa na kuacha kasumba za kimadhehebu ambazo
zimeiletea madhara makubwa Diyn hii.
No comments:
Post a Comment