Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola
Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume
Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya
Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani sana kwa muulizaji lake hili kuhusu
haya mas-ala ya kumuita Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au
Swahaba au mtu mwingine yeyote kwa jina la SAYYID.
Kabla ya kuja kuhitimisha kauli yetu inafaa sisi tufahamu maana ya neno hilo .
Neno hilo lina maana ya
Mtukufu au Bwana katika lugha. Hata katika matumizi inatumika Sayyid al-Bayt
(yaani bwana au mkubwa wa nyumba).
Hakika Allaah Aliyetukuka Amelitumia neno hili kwa Nabii Wake Yahyaa
(‘Alayhis Salaam), pale Aliposema: “Alipokuwa kasimama
chumbani akiswali, Malaika kamnadia: Hakika Allaah Anakubashiria Yahyaa,
atayekuwa mwenye kusadikisha neno litokalo kwa Allaah, na ni Sayyid (bwana) na
mtawa na Nabii kwa watu wema” (3:
39 ).
Pia kuhusu waziri wa Misri, “Na wote wawili
wakakimbilia mlangoni, na mwanamke akairarua kanzu yake Yuusuf kwa nyuma. Na
wakamkuta Sayyid (bwana) wake mlangoni. Mwanamke akasema: Hapana malipo ya
mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo isipokuwa kufungwa au kupewa adhabu iumizayo” (12: 25 ).
Hii Hadiyth inaonyesha kila mmoja wetu ana mas-uliya
(majukumu) yake na ataulizwa kuhusu alichokichunga. Ibara tuliyoipiga msitari
ina maana: “Na mtumwa wa mtu ni mchunga wa mali ya
bwanake, naye ana jukumu kwayo” (al-Bukhaariy).
Hadiyth nyingine inasema: “Alikuja mtu
anayeitwa Thumaamah bin Athal naye alikuwa ni Sayyid wa watu wa Yamaamah” (al-Bukhaariy).
Na nyingine: “Akasimama Sa‘d bin
‘Ubadah, naye alikuwa Sayyid (Chifu) wa Khazraj”
(al-Bukhaariy).
Hadiyth kuhusu neno hili ni nyingi sana
lakini kufupisha katika Hadiyth iliyo sahihi, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) alisema: “Mimi ni Sayyid (bwana
na mtukufu) katika watoto wa Aadam Siku ya Qiyaama”
(Muslim).
Pia, “Mimi Sayyid wa watu Siku ya Qiyaama, na
mnajua ni nini hiyo” (al-Bukhaariy).
Pia, “Alikuja Hasan kwake, naye (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, ‘Mtoto wangu huyu ni Sayyid, huenda
Allaah kwake akasuluhisha baina makundi mawili ya Waislamu” (al-Bukhaariy). Na ndivyo ilivyokuwa, maana Hasan aliweka suluhu na
Mu’aawiyah na hivyo kuokoa umwagikaji mkubwa wa damu ambao ungesababishwa na
vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) wakati wa ukhalifa wake alisema: “Abu Bakar ni Sayyid wetu na alimuacha huru Sayyid wetu (yaani Bilaal bin
Rabaah)”. (al-Bukhaariy kutoka kwa Jaabir bin
‘Abdillahi [Radhiya Allaahu ‘anhuma]).
Hivyo, kumuita Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au
Swahaba kwa jina hili kama cheo
chake cha daraja halina neno katika sharia, ila haifai kumuita hivyo ndani ya
Swalah kwenye Tashahhud au kwenye Adhaan au Iqaamah.
No comments:
Post a Comment