Kwa Nini Waislamu Wamegawanyika Katika Makundi Tofauti Ya kuelewa Dini Yao?
Raashid Bin Husayn
Wakati Waislamu wote wanamfuata Mtume mmoja na Qur-aan moja lakini kuna makundi mengi na tofauti yaliyogawanyika miongoni mwa Waislamu?
1. WAISLAMU NI LAZIMA WAUNGANE
Ukweli ni kwamba Waislamu wa zama hizi, wamegawanyika mapote tofauti. Kugawanyika huko hakuungwi mkono na Uislamu kabisa. Uislamu unaamini ya kwamba wauumini ni lazima waungane.
Kwani Qur-aan Tukufu inasema:
"Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyokuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye Akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema Yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto, Naye Akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu Anakubainishia ishara Zake ili mpate kuongoka".
"Enyi mlioamini! mtiini Mwenyezi Mungu na mtíini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndio bora zaidi na ndio yenye mwisho mwema.”
Waislamu wote ni lazima kushikamana na Kitabu na Sunnah sahihi na sio kugawanyika makundi makundi.
2. IMEKATAZWA KUGAWANYIKA NA KUFANYA MAKUNDI
Mwenyezi Mungu Anasema ndani ya Qur-aan:
"Hakika walio igawa dini yao wakawa makundi makundi, huna uhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu; kisha atawaambia yale waliyokuwa wakiyatenda". [6:159]
Kwenye Aayah hii Mwenyezi Mungu Anasema ya kwamba yeyote yule asishirikiane na yule aliyeigawa dini yake katika makundi.
Lakini mtu akimuuliza Muislamu, ‘Wewe ni kundi gani?’, jibu litakuwa ‘Mimi ni Sunni’, au ‘Mie ni Ibadhi’. Na katika Masuni wengine hujiita Hanafi au Ash-Shaafi’iy au Maalik au Hanbaliy. Na humo tena utakuta mtu anajiita ‘Mimi Qadiriya’, ‘Mimi Naqshabandiya’ au ‘Mimi Shadhiliya’!
3. MTUME (SWALLA ALLAAHU ‘ALAYHI WA SALLAM) ALIKUA MUISLAMU
Anaweza kuulizwa Muislamu, "kipenzi chetu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa nani? Alikuwa Ibadhi, Hanafi, au Ash-Shaafi’iy, au Hanbali au Maaliki? Jibu litakuwa hapana alikuwa Muislamu kama vile Manabii na Mitume ya Allaah (Subhaanahu wa Taa'ala) kabla yake.
Imesemwa kwenye sura ya 3 Aayah ya 52 ya kwamba ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) alikuwa ni Muislamu.
Hata ukiangalia,kwenye sura ya 3 Aayah ya 67 ndani ya Qur-aan ya kwamba Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) hakuwa Myahudi wala Mnaswara lakini alikuwa Muislamu.
4. QUR-AAN INATUAMRISHA TUJIITE WAISLAMU
Asiyekuwa Muislamu akimuuliza Muislamu wewe ni nani, bila ya shaka atasema 'mimi ni MUISLAMU", sio Hanafi au Ash-Shaafi’iy...
Jawabu hili linapatikana ndani ya Qur-aan katika Surah Fusswilat 41 Aayah ya 33 ambayo inasema:"Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu"?
Qur-aan inasema:
"Hakika mimi ni katika Waislamu".Kwa maana nyengine inasema "mimi ni Muislamu".
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliandika barua kwa mfalme na mtawala ambaye alikuwa si Muislamu kumtaka awe Muislamu. Kwenye barua hiyo kulikuwemo na Aayah ya Qur-aan iliyoko katika Surah ya 3 Aal-‘Iimraan Aayah ya 64 isemayo:
"Shuhudieni ya kwamba mimi ni Muislamu"
5. NI WAJIBU KUWAHESHIMU WANAZUONI [MAULAMAA] WA KIISLAMU
Ni lazima kuwaheshimu wanazuoni wakubwa wa Kiislamu wakiwemo maImam wakubwa Imam Abu Haniyfah, Imam Ash-Shaafi’iy, Imam Ahmad bin Hanbali na Imam Maalik [Allaah Awarehemu].
Walikuwa ni wanazuoni wakubwa twamuomba Mwenyezi Mungu Awalipe ujira wao kwa utafiti wao na kazi ngumu waliyoifanya.
Hakuna kipingamizi kama kila mmoja wetu atakubaliana na utafiti wa Imam Abu Haniyfah au wa Imam Ash-Shafi’iy na wengineo. Lakini linapoulizwa swali "wewe ni madhehebu gani?" Jibu liwe "mimi ni Muislamu".
Zifuatazo ni kauli za Maimam juu ya msimamo wao wakufuata mwenendo sahihi yaani kitabu na Sunnah sahihi.
Imam Abu Haniyfah [Allaah Amrehemu] anasema:
"Itakaposihi Hadithi basi ndio madhehebu yangu". [Al-Haashiyah Juzuu ya 1 uk.63]
Imam Maalik [Allaah Amrehemu] anasema:
Imam Maalik [Allaah Amrehemu] anasema:
“Hakuna yeyote baada ya Mtume isipokua kauli yake huchukuliwa na kuachwa". [Irshaadus Saalik juzuu ya 1 uk. 227]
Imam Ash-Shaafi’iy [Allaah Amrehemu] amesema:
"Itakaposihi Hadithi basi ndio madhehebu yangu" [Al Majmuu Al Mussawwiy Juzuu ya 1 uk 63]
Baadhi wanaweza kujadili kwa kunukuu hadithi ya kipenzi chetu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kutoka kwenye Sunan Abu Daawuud hadithi nambari 4579, kwenye hadithi hii mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) iliripotiwa ya kwamba alisema:
"Umati wangu utagawanyika ktk makundi 73"
Hadithi hii inaripoti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliashiria ya kwamba umati wake utagawanyika makundi sabiini na tatu, hakusema Waislamu wawe katika harakati za kujigawanya katika makundi. Qur-aan Tukufu inatuamrisha tusiunde makundi. Wale wanaofuata muongozo wa Qur-aan na Sunnah Sahihi za Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na wasiounda makundi wao ndio walio katika mfumo sahihi.
Kulingana na At-Tirmidhiy hadithi nambari 171, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) iliripotiwa ya kwamba alisema:
“Ummah wangu utagawanyika katika mapote 73, na yote motoni isipokuwa kundi moja tu." Maswahaba waliuliza: ‘Ni lipi hilo, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?’ Akasema: (Ni lile nililokuwemo mimi na swahaba zangu).”
Aayah nyingi ndani ya Qur-aan zimeamrisha kwa kusema "Mtiini Allaah na mtiini Mtume".
Muumini wa kweli ni lazima afuate Qur-aan na Sunnah (Hadithi) Sahihi.
Anaweza mtu kukubaliana na ‘Aalim yeyote yule ilimuradi yuko kwenye mfumo wa mafundisho yatokanayo na Qur-aan na Sunnah Sahihi. Ikiwa mafundisho yatakwenda kinyume na maneno ya Allaah (Qur-aan) au na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), hivyo mafundisho hayo hayatakuwa na uzito wowote bila ya kuzingatia ya kwamba ‘Aalim (mwanachuoni) huyo alikuwa mwanachuoni mkubwa au la.
6. UMUHIMU WA KUHITAJI REHMA ZA ALLAAH (SUBHAANAHU WA TA’ALA)
Kuna baadhi ya watu wanajaribu kutoa hoja ya kwamba mbona Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) alishasema ndani ya Qur-aan ya kwamba:
“Na Mola wako Angelipenda Angewafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana” [Surat Huud 3:118]
Ni kweli aya hii ndio lakini walisahau Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye Aayah inayofuata aliwavua baadhi ya watu kwa kusema ila wale aliowarehemu.
Kama ilivyosema:
“Isipokuwa wale ambao Mola wako Amewarehemu; na kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu Amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako: Kweli kweli nitaijaza Jahannam kwa majini na watu pamoja.” [Surat Huud 3: 119]
a. Kuhitaji Rehma za Allaah ni Muhimu na hili limedhibitishwa na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwenye hadithi pale aliposema ya kwamba:
"Hataingia yeyote yule peponi ila kwa rahma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Maswahaba wakamuuliza, hata wewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akajibu hata mie ila kwa rahma za Allaah."
b. Hata Nabii Yuusuf (‘Alayhis Salaam) alipojaribiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa wanawake kumtaka na alipofaulu mtihani huo na kuulizwa ni kitu gani kilikufanya ukafaulu mtihani huu?
Alijibu ifuatavyo kama Qur-aani inavyosema:
“Nami sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu, isipokuwa ile ambayo Mola wangu Aliyoirehemu. Hakika Mola wangu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.” [Surat Yuusuf 12: 53]
Hivyo tunaona ya kwamba rehma za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) tunazihitaji kama walivyozihitaji Mitume na Manabii waliopita.
HITIMISHO
Iwapo Waislamu wote watasoma Qur-aan kwa kuielewa, kuzingatia yaliyomo ndani yake na kushikamana na Sunnah Sahihi na kutaraji rehma za Allaah (Subhanaahu wa Ta'ala) basi tofauti nyingi (au hayo makundi yalioko yatafutika) na kutapatikana ufumbuzi na tutakuwa ummah mmoja inshaAllaah.