Wednesday, February 22, 2012

KITABU-MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU




MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU
Kimeandikwa na:
Jopo la Maulamaa (Misri)
Kimetarjumiwa na:
Ustadh Abdallah Mohamed

YALIYOMO

Mwanzo.............................................................................................2
Sehemu ya Kwanza:
Hali na haki za mtoto katika Uislam.....................................5
Mapenzi ya Mtume kwa mtoto..............................................7
Umuhimu wa mtoto katika Uislamu kabla ya kuzaliwa........8
Familia katika Uislamu..........................................................9
Pendo la wazazi...................................................................10
Usawa baina ya mtoto katika Uislamu na maoni yake juu ya
watoto wa kike.....................................................................12
Sehemu ya Pili:
Maisha na makazi ya mtoto.................................................14
Kuishi kwa mtoto.................................................................16
Jukumu la wazazi huko akhera, na mtunzo ya mtoto ........18
Jukumu la wazazi na makazi ya mtoto.............................. 20
Kuwalinda watoto ni huruma na huruma ni kinga............. 28
Uislamu na uzazi wa mpango............................................. 24
Uislamu na karantini za afya...............................................25
Sehemu ya Tatu:
Chakula bora na manufaa yake katika afya ya kimwili kiakili..........................................................................................
27
Umuhimu wa kinyonyesha kwa matiti katika Uislamu.......30
Lishe kwa akina mama waja wazito wanaonyonyesha.......33
Mchango wa chakula bora katika kukuza akili timamu..... 34
Sehemu ya Nne:
Maoni ya Uislamu juu ya malezi ya mtoto..........................38
Mtoto baina ya silika na athari na mazoea ya mazingira, na
jukumu la wazazi.................................................................39
Mwalimu aliye mfano bora, na kufundisha mtoto nidhamu..................................................................................
41
Uislamu na malezi ya kujitegemea kwa mtoto................... 42
Uislamu na kumuelimisha mtoto........................................ 44
Umuhimu wa vidude vya kuchezea watoto (toys) katika
Uislamu............................................................................... 46
Sehemu ya Tano:
Elimu ya afya, kimwili na kimazingira...............................47
Usafi wa swala.................................................................... 48
Usafi wa mikono................................................................. 49
Usafi wa kichwa..................................................................50
Usafi wa macho...................................................................50
Usafi wa Pua........................................................................50
Usafi wa mdomo (kinywa)..................................................51
Usafi wa nguo......................................................................51
Usafi wa nyumba.................................................................52
Kufanya Iktisadi katika matumizi ya maji...........................52
Usafi wa chakula na maji.....................................................53
Makatazo ya kwenda haja ndogo kwenye maji yaliyotulia.........................................................................................
53
Makatazo ya kukojoa majabalini na maweni.......................53
Mambo matatu yaliyolaaniwa........................................ .....54
Usafi wa barabara............................................................... 54

SEHEMU YAKWANZA
Hali na haki za mtoto katika Uislamu Hawa ni watoto wetu kwetu sisi wenye hadhi Ni kama maini yetu yaendayo kwenye ardhi Na tulivyo kati yetu hatuwezi kuwa radhi Tuwaonapo wanetu wanaugua maradhi (Tafsiri ya shairi la kale la kiarabu) Umoja wa mataifa umeanza kuonyesha kuvutiwa na suala la watoto kwa kufanya maadhimisho ya ‘Siku ya Watoto’ katika mwezi wa Novemba kila mwaka, ambayo inalingana na maadhimisho ya kutangazwa kwa haki za mtoto.

Kwa hali yoyote ile, ipo haja ya kutaja hapa kwamba, mazingatio ya Uislamu kwa watoto yameanza zamani na yanarejea nyuma zaidi ya miaka elfu moja na mia nne. Uislamu kwa mfululizo unaadhimisha na kuonyesha huruma yake kwa mtoto, si baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla ya kuzaliwa, na umeelezewa kwa makini haki zake. Wakati wa utoto katika Uislamu umepewa picha ya ulimwengu mzuri wa furaha, uzuri, ndoto, mapenzi na ruya njema. Na aya za Qur’ani zinaonyesha mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa watoto, na ndipo akaapa Mwenyezi Mungu: “Naapa kwa mji huu, (wa Makkah). Na wewe utahalalishwa katika mji huu. Na (kwa) mzazi na alichokizaa.” (90:1-3). 

Watoto wameelezwa katika Qur’ani kuwa ni bishara njema. Amesema Mwenyezi Mungu: “Ewe Zakaria tunakupa habari njema ya (kupata) mtoto jina lake ni Yahya….” (19:7). Pia watoto ni kiburudisho cha macho yetu. Amesema Mwenyezi Mungu: “Ewe Mola wetu, tupe katika wake zetu na watoto wetu watakaoyaburudisha macho yetu….”(25:74). Na watoto ni pambo la maisha katika ulimwengu huu. “Mali na watoto ni pambo la maisha ya duniani….” (18:16). Mtume (s.a.w.) anatudhihirishia ya kuwa ulimwengu wa utoto ni kama pepo, pale aliposema: “Watoto ni vipepeo vya Peponi.”

Kuwatunza watoto ni jambo la lazima, na kuwapenda humleta mtu karibu na Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.) amesema: “Lau kama si watoto wanyonyeshwao, na wazee wanaorukuu (kwa kuswali) na wanyama walishwao mashambani, basi mngelipatwa na adhabu kali.” Inaonyesha wazi kwamba huruma na uangalifu wa Mwenyezi Mungu kwa watoto ndiyo uliofanya Mwenyezi Mungu kuzuia adhabu juu ya watu wake. 

Mapenzi ya Mtume kwa watoto Mapenzi ya Mtume (s.a.w.) kwa watoto yalijaa ndani ya moyo wake mwema, imeelezwa katika Hadith: “Siku moja Mtume (s.a.w.) alipanda juu ya mimbari akiwahutubia watu, (mara) akawaona Hasan na Husein (a.s.) wanakimbia na huku wakijikwaa, akakatiza hotuba yake, akashuka kutoka juu ya mimbari kwenda kuwapokea watoto hao wawili. Akawabeba mikononi mwake, kisha akapanda tena juu ya mimbari akasema: “Enyi watu, hakika mali zenu na watoto wenu ni fitina, Wallahi nimewaona wajukuu zangu wawili wakikimbia na kujikwaa, basi sikuweza kujizuia mpaka nimeshuka nikawabeba.” Siku moja Mtume (s.a.w.) alikuwa anaswali, mara Hasan na Husein (a.s.) wakaingia ndani na kumpanda mgongoni kwake wakati alipokuwa amesujudu, Mtume (s.a.w.) akaendelea kusujudu tu. Alichukia kuwaharakisha washuke, mpaka waliposhuka wao wenyewe. Kisha alipotoa salaam na kumaliza Swala, akaulizwa na maswahaba zake sababu zilizomfanya asujudu kwa kitambo kirefu hivyo; akawajibu: “Wajukuu zangu wawili walikuwa wamepanda juu ya mgongo wangu nami nilichukia kuwahimiza washuke kwa haraka.”

Mtume (s.a.w.) alizoea kuharakisha Swala yake pindi asikiapo mtoto analia, na husema: “Mimi huchukia kumchosha mama yake.” Siku moja alikuwa anapita nyumbani kwa Fatima (a.s.) (binti yake), akamsikia mjukuu wake Husein (a.s.) akilia, aliingia ndani na baada ya kumkemea Fatima akasema: “Je hujui kwamba nimsikiapo Husein akilia huwa nakereka?” Siku moja Mtume (s.a.w.) alitembelewa na Al-Akraa Ibn Habis, ambaye alimwona Mtume (s.a.w.) akiwabusu wajukuu zake, Al-Akraa akasema: “Unawabusu watoto wa binti yako? Naapa kwa Mungu nina watoto kumi, 

Malezi ya Watoto katika Uislamu na sijawahi kumbusu hata mmoja.” Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Je ni kosa langu kama Mwenyezi Mungu ameing’oa rehma kutoka moyoni mwako.” 2. Umuhimu wa mtoto katika Uislamu kabla ya kuzaliwa Kutilia maanani kwa Uislamu kuhusu malezi ya mtoto hakuanzi baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla hajaanza kupata umbo (tumboni) kwani Uislamu unamuamuru mtu kuoa mke mcha Mungu na mtulivu. Mtume (s.a.w.) amesema: “Jitahidi umpate mwenye kushikamana na dini, basi furaha zote ni zako.” Uzuri, na utajiri si sifa pekee za kutosha kuchagua mke, sambamba na sifa hizo, pia mke ni lazima awe na sifa zingine, kwa mfano kumpata aliye na dini, na awe ametoka kwenye nyumba yenye mema. Kwa sababu watoto wake atakaowazaa mke huyo watarithi tabia, adabu na mwenendo wake. Mwenyezi Mungu amekataza kuoa mwanamke mzuri tu asiye na tabia nzuri na nidhamu. Mtume (s.a.w.) amekataza: “Jihadharini na wanawake wazuri wenye sifa mbaya.”

Mtume (s.a.w.) ameweka mwongozo kwa mwanamke ambaye yu tayari kuolewa: atafute mume mcha Mungu, mwenye tabia za kidini, atakayeangalia jamii yake kwa ukamilifu, kutekeleza haki za mke, na kusimamia malezi ya watoto. Mtume (s.a.w.) amesema: “Atakapowajia mtu mtakayeridhishwa na jinsi alivyoshika dini, na tabia yake, basi muozeni, ama msipofanya hivyo, mtaleta fitina na ufisadi mkubwa duniani.” Mtume (s.a.w.) ameonya pia kuhusu kuoana na ndugu wa karibu, ili watoto wasizaliwe wadhaifu, akasema: “Oeni walio nje ya jamii yenu, msiwadhoofishe watoto wenu.” 

Qur’ani imetaja ya kwamba, mwanadamu ameumbwa kutokana na tone la manii lililochanganyika: “Hakika tumemuumba mwanadamu kutokana na tone la manii lililochanganyika…” (76:2). Hii inaonyesha kwamba, mtoto azaliwaye na wazazi ambao si ndugu wa karibu atakuwa na uwerevu, utambuzi na mwenye nguvu za kimwili kuliko mtoto aliyezaliwa na wazazi wenye uhusiano wa karibu. Hii inaweza kuonekana kwamba Uislamu umezitangulia (kwa uvumbuzi) kanuni za kisayansi na elimu ya ‘tabia zinazorithishwa’ (Heredity) kwa kuonyesha umuhimu ulioko katika sehemu ya urithi wa tabia, na namna gani uteuzi mzuri wa watu wawili wanaooana utakavyopelekea kupata watoto ambao ni tuzo la Mwenyezi Mungu na furaha ya maisha.

Kwa kuwa mtoto atachukua mwenendo wa wajomba na shangazi zake, asili ya undani ya baba yake na mama yake, na akajifunza kupitia kwa urathi ambao umepitia kutokana kwa muungano wa baba yake na mama yake, na ndipo Uislamu ukazitengeneza asili hizi kwa njia hiyo ili kumhifadhi mtoto awe ni kiumbe mwenye heshima na nidhamu, na hivyo kuepukana na upungufu wowote. Mara tu mtu anapoanza kufikiria kuoa na kutunza familia, Uislamu unamuongoza kupitia katika njia hizo.

3. Familia katika Uislamu Familia katika Uislamu, ina utaratibu mzuri na wa hali ya juu sana, na ni utaratibu unaoheshimiwa sana hata ina mahali panapostahiwa. Ni kwa sababu hii na ndio maana Uislamu huipa nguvu (familia) kuanzia mwanzo wa nguvu yake. Ndoa ni sura mpya katika njia ya kuunda jamii, na uangalifu wa Uislamu katika nguzo hiyo muhimu, hatimaye unaongoza kuelekea katika maisha ya amani na furaha.

4. Pendo la wazazi Mtoto ni matokeo ya kimaumbile ya uhusiano imara wa wazazi, ubaba na umama ni matamko mawili ambayo Mwenyezi Mungu ameyazatiti kwa ihsani na mapenzi Yake, akayatajirisha na kuyapitia kwa maana ya kuungana watu wawili na kuendelea kuwa pamoja. Uhusiano wa karibu zaidi baina ya wazazi na watoto wao, ni miongoni mwa uhusiano ulio imara na wenye daraja ya juu zaidi kuliko uhusiano wowote ule wa kibinaadamu. Uhusiano huo umehifadhiwa na Mwenyezi Mungu, naye amehakikisha kuwa unaendelea na kustawi; kwa sababu kufanya hivyo ni kuendelea kwa jamii ya binaadamu na uhai. Upendo wa wazazi kwa watoto wao hauna nafasi yoyote ya kutia shaka, kwani ni alama ya Mwenyezi Mungu na ni neema Yake kubwa kwa walimwengu. Mwenyezi Mungu amesema: “Na katika alama zake, ni huku kuwaumbia wake zenu, kutoka miongoni mwenu ili mpate utulivu kwao, na akajaalia mapenzi na huruma baina yenu.” (30:21). Baadhi ya wafasiri wameeleza ‘penzi’ na ‘huruma’ hapa, kwa maana ya mtoto ambaye ameupa nguvu uhusiano baina ya wazazi na ameupa amani na usalama.

Familia ndicho kitu cha kwanza ambacho Uislamu unakichukulia kuwa ni cha kwanza katika jamii ya watu. Familia huunda nyoyoni mwao penzi lisilo na kikomo kwa watoto wao, penzi hili ni nuru waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.) aliwaambia maswahaba zake na huku akiwaonyesha mwanamke akasema: “Je Mnaweza kufikiria kwamba siku moja mwanamke huyu anaweza kumtupa mwanawe motoni?” Wao wakasema: “La”, akasema: “Basi Mwenyezi Mungu ni mwenye huruma zaidi kwa waja wake kuliko mama huyu alivyo na huruma kwa mtoto wake.” Basi haya ni maumbile, na ni aina ya pendo la kiasili ambalo hapana yeyote awezaye kulizuia au kushindana nalo, na kwa sababu hii ndipo Mwenyezi Mungu akawausia wazazi kuwaangalia watoto wao. Amesema: “Na tumemuusia mwanaadamu (kuwafanyia wema) wazazi wake, mama ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumnyonyesha na kumwachisha kunyonya katika miaka miwili, nishukuru Mimi na wazazi wako na kwangu ndio marejeo.”(31:14). Amesema tena: 

“Na tumemuuusia mwanaadamu kuwatendea wema wazazi wake. Mama yake ameichukua mimba yake kwa taabu na akamzaa kwa taabu. Na kubeba mimba yake (mpaka) kumwachisha kunyonya ni miezi thelathini mpaka anapofikia kubaleghe kwake, na akafikia miaka arubaini. Akasema: ‘Ewe Mola wangu niwezeshe nizishukuru neema zako ambazo umenineemesha mimi na wazazi wangu. Na uniwezeshe nifanye amali njema uzipendazo, na unitengenezee watoto wangu. Kwa hakika natubu kwako, kwa hakika mimi ni miongoni mwa waislamu.’” (46:15). Mwenyezi Mungu amefanya kuwapenda watoto na kuwahurumia ni sehemu ya maumbile ya kiasili ya kibinaadamu yasioepukika. Pia ameziingiza hisia hizi thabiti ndani ya nyoyo za wazazi. Ni kwa ajili hii basi ndipo maelezo haya yote pamoja na wasia yameelekezwa moja kwa moja kwa watoto, kwa ajili ya kuwatendea wema na kuwapa heshima wazazi wao. Maelekezo haya amepewa mtoto ili kuzivutia hisia zake.


Ni maelekezo ya hali ya juu ambayo yanategemeza uhusiano wa karibu na hisia ya kibinaadamu ambazo ndio sababu kubwa ya kuwepo kwetu duniani.
5. Usawa baina ya watoto katika Uislamu na maoni yake juu ya watoto wa kike Kadri Uislamu unavyochukulia watoto kuwa ni kiburudisho cha macho yetu, ni lazima hii idhihiri kwa vitendo na kwa njia zake. Usawa baina ya watoto hauna budi kutekelezwa hata katika kuwabusu. Uislamu unataka usawa ufanywe kulingana na maagizo yake matukufu.

Siku moja Mtume (s.a.w.) alimwona baba ambaye alikuwa na watoto waw- ili, akambusu mmoja na kumwacha mwingine, kisha Mtume mtukufu akamuuliza: “Je huwezi kuwafanyia usawa?” Tukiangalia mvuto wa kumpendelea mtoto mmoja zaidi ya mwingine au jinsia moja (wa kike au wa kiume) zaidi ya nyingine, hii ni kinyume kabisa na maadili ya kiislamu, mila na fikra za usawa ambazo Uislamu umejengewa. Uislamu hautofautishi baina ya mwanamume na mwanamke, wala hautofautishi baina ya mvulana na msichana. Wote sawa, hapana yeyote ampitaye mwenzake ila kutokana na baadhi ya sifa alizonazo kitabia alizojipatia yeye mwenyewe, Mwenyezi Mungu amesema: “Mola akawakubalia (maombi yao), ya kwamba mimi sipotezi amali ya mwenye kutenda, awe ni mwanamume au mwanamke, baadhi yenu kwa baadhi nyingine….”(3:195).

Kwenda kinyume na misingi hii kunafuatia kwenda kinyume na fikra za usawa, maarifa, na haki. Kwa ajili hii, Uislamu unawaamuru Waislamu kuwafanyia usawa watoto wao ili kwamba kusiwe na yeyote yule atakayekuwa na kinyongo au kusononeka. Kwa njia kama hiyo, Uislamu unazuia kuzagaa kwa chuki badala ya mapenzi, na kusema maudhi badala ya amani. Mambo haya iwapo yataendelea, hatimaye yataleta matatizo ya kinafsi, majonzi, na utengano, na haya yote huvunja hisia za moyo. Mtume (s.a.w.) mara kwa mara alikataza kuwapendelea watoto wa kiume zaidi ya wa kike pasi na sababu yoyote, kwa maana hiyo, ndiyo akaipa daraja la juu heshima ya watoto wa kike na akaipa nguvu thamani na staha yao.

Amesema Mtume (s.a.w.): “Bora ya watoto wenu ni mabinti.” Mtume (s.a.w.) alipopewa habari ya kuzaliwa bintiye Fatima (a.s.), nyuso za maswahaba zilionekana kuparama, Mtume (s.a.w.) akawaambia: “Mna jambo gani linalowahuzunisha? (kumzaa Fatima) ni kama kupata ua la mrehani niunusao, na riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu.” Hapa Mtume (s.a.w.) kwa ubaba wake mtukufu alijaribu kubadilisha mawazo ya watu ya kuwapendelea watoto wa kiume zaidi ya watoto wa kike, tena hata aliwatanguliza watoto wa kike zaidi kwa kusema: “Mwenye kwenda sokoni, na kununua zawadi na kuwapelekea jamii yake, (familia yake) ni kama mtu aliyewapelekea sadaka wahitaji, basi aanze kuwapatia watoto wa kike kabla ya kiume.”

Mtume (s.a.w.) amejaribu kwa kadri awezavyo kuvutia penzi la watoto wa kike kama vile lilivyo penzi la asili kwa watoto wa kiume. Amesema: “Mwenye kuwalisha (kuwalea) watoto watatu wa kike ataingia Peponi.” Akaulizwa: “Je wakiwa ni wawili?”, akajibu: “Hata kama wawili”, Akaulizwa: “Je mmoja”, akajibu: “Hata kama ni moja.”



SEHEMU YA PILI
Maisha na makazi ya mtoto Mtume (s.a.w.) amesema: “Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kutowaangalia wanaomtegemea.” Kuna maagizo kadhaa na misingi ya kanuni iongozayo, ambapo Uislamu unaamuru kwa jinsi gani maisha na maendeleo ya mtoto yalivyo lazima, na kwamba uzembe wowote ama kufanya ajizi katika kutimiza misingi hii ya kanuni ni kosa kubwa. Misingi hii imetolewa mfano kama ifuatavyo: Amesema Mwenyezi Mungu: “Wala msijiue.” Amesema tena: “…..wala msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha kuuawa ila kwa njia ya haki….”(6:151). Amesema tena: “Mtu atakayemuua mtu bila ya yeye kuua, au bila ya kufanya ufisadi nchini, basi ni kama amewaua watu wote, na atakayeokoa maisha ya mtu, basi ni kama ameokoa maisha ya watu wote…”(5:32). Amesema tena: “Wala msiwaue watoto wenu….” (6:151). Amesema tena: “Mwenyezi Mungu anataka kukurahisishieni (mambo mazito) kwani mwanaadamu ameumbwa dhaifu.”(4:28). 

Amesema tena: “Na waogope (mawasii kuwadhulumu yatima, na wakumbuke) kama wao wangeacha nyuma yao watoto dhaifu wangekuwa na khofu juu yao.”(4:9). Amesema tena: “Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu kutokana na moto.” (66:6) Amesema tena Mwenyezi Mungu: “Wala msijitie wenyewe katika maangamivu.”(2:195). Amesema Mtume (s.a.w.): “Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kumtupa yule anayemtegemea.” 1. Kuishi kwa mtoto Uislamu unamchukulia mtu kuwa ni khalifa wa Mwenyezi Mungu duniani, imetajwa katika Qur’ani: “….Hakika nitaweka katika dunia hii khalifa…” (2:30).

Kwa hivyo, jambo lolote litakalomtia khalifa huyu kwenye aibu, fedheha, ama kudhoofisha uwezo wake, limekatazwa na sheria ya Kiislamu. Na hii ni kwa sababu ya kuhifadhi heshima na daraja ya mwanaadamu aliyopati- wa akiwa kama khalifa wake duniani. Mwenyezi Mungu amempa uwezo binaadamu kuwa na fahamu za kujua mambo bila ya kufundishwa, nguvu za ulinzi za kuweza kujihami, na kumwezesha kupata kudumu kwa ulimwengu. Pia Mwenyezi Mungu amempa mwanaadamu undani wa maarifa, na amemtukuza zaidi ya viumbe vyote vilivyosalia. Miongoni mwa uwezo aliopewa mwanaadamu ili kukabiliana na vitisho ni uwezo wa kujihami.

Uangalifu wa Uislamu kuhusiana na maisha ya mtoto na ulinzi wake, tayari wenyewe una mamlaka kwenye jamii ya kiislamu kimwili au kiroho, kwa sababu uangalifu huu unazalisha miili imara yenye siha. Kuwa na miili yenye afya katika Uislamu hakuleti natija ya nguvu ya kiakili tu, bali pia uhakika, mafanikio na matumaini katika kushughulika na maisha na watu. Ni kwa sababu hizi ndipo Uislamu umekusanya taratibu zifaazo za kujikinga, ili kuyahifadhi maisha ya waislamu na kuwaongoza katika njia yenye utaratibu na iliyopangwa katika maisha yao yote. Afya ndiyo neema bora kuliko zote alizotunikiwa mwanaadamu baada ya kuwa muislamu, kwani bila ya kuwa na afya huwezi kufanya kazi na kuweza kumtii Mungu sawasawa, kwa hivyo, hakuna chochote kinachoweza kulinganishwa nayo.

Imetajwa na Tirmidhy, kutokana na Abu Huraira ya kwamba Mtume (s.a.w) amesema: “Kitu cha kwanza atakachoulizwa mwanaadamu Siku ya Kiyama, kutokana na neema alizopewa ni: Je mwili wako, sikuupa afya? (uliifanyia nini?)” 

2. Jukumu la wazazi huko akhera, na matunzo ya watoto Inasadikiwa ya kwamba, kulingana na maumbile na hisia za binaadamu, anaweza kuepuka hali zinazotishia (maisha yake). Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu amemuumbia mwanaadamu nguvu ya kiasili inayomlinda kutokana na hatari hizo. Licha ya hivyo, Uislamu umeipa uwezo nguvu hiyo, na umemkumbusha mwanaadamu aitumie kwa kujihami na kwa kuongozea mikakati ya ulinzi kwa ajili ya maisha yake. Kwa hivyo inaonyesha wazi namna gani Uislamu ulivyoupa daraja ulinzi na kuuimarisha. Ulinzi kwa maana hiyo (ilivyotajwa hapa) ungeweza kuwa na maana ya ulinzi wa mwanaadamu hapo Akhera, ambao utamwokoa kutokana na moto na vitisho vya Siku ya Kiyama. Au ungeweza kuwa ni kujilinda kwa mtu kutokana na moto ambako kunamaanisha wakati huo huo, kuilinda familia yake.

Imetajwa katika Qur’ani: “Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu (jamii) yenu kutokana na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe….” (66:6). Aya hizo zilizotangulia zinawataka wacha Mungu waumini kujilinda na kujihami wao na jamii zao pia kutokana na Moto ambao kuni zake zitakuwa ni watu waovu. Kujilinda maana yake (hapa) inarejea kwenye kutenda amali njema, na kuwa na mwenendo mzuri, kumtii Mwenyezi Mungu na kujizuia na makatazo yake. Miongoni mwa matendo ya kujilinda kwa Akhera, ni kujizuia na maamrisho yote ya Mwenyezi Mungu, kuhusiana na chakula, kinywaji, mavazi, n.k. 

Imetajwa katika Qur’ani: “Enyi Mitume! Kuleni vyakula vilivyo vizuri (halali) na tendeni mambo mema, hakika Mimi najua yote myafanyayo.” (23:51). 3. Jukumu la wazazi maishani na matunzo ya mtoto Matunzo ya mtoto wakati wa maisha yake yanahusiana na kumkinga kutokana na magonjwa na maradhi yaambukizayo na yote yale yawezayo kumpata mtu kutokana na uzembe, na kutojihusisha. Imesema Qur’ani: “Wala msijitie wenyewe katika maangamivu ….” (2:195). Katika Aya iliyotangulia hapo juu, Mwenyezi Mungu amemkataza mwanaadamu kuchangia maangamivu yake mwenyewe kupitia kwenye vitendo ambavyo angevitenda kulingana na mwenyewe. Ijapokuwa mtu kujidhuru au kujiangamiza kunaonekana kwamba kunapingana na fikra zilizo timamu (yaani haiwezekani), lakini yaelekea kuwa kunaweza kutokea kutokana na uzembe ama kutojihusisha na kuchukua kinga zifaazo ili kuyachunga maisha yake mwenyewe.

‘Kujiangamiza’ hapa, haina maana tu ya maangamivu yanayosababishwa na kiu, njaa, au mtu mwenyewe kujitoa mhanga kwa njia moja au nyingine kutokana na madhambi ayatendayo. ‘Kuangamia’ kwa maana hiyo, kunamaanisha kwamba kufanya ajizi kidogo tu, au kuzembea katika kujikinga, ndiko kujiangamiza. Kwa hivyo hii ni pamoja na mtu kujihatarisha na magonjwa, maradhi yaambukizayo, ukosefu wa chanjo kutokana na maradhi yauwayo, na ukosefu wa uangalifu wakati wa shida na hatari. Vitendo hivyo vyote vilivyotangulia kutajwa vinachukuliwa kuwa ni kumchangia mtu katika maangamivu yake mwenyewe.

Kwa sababu hiyo ndipo Uislamu ukaamuru kuchukua kinga zifaazo, na kutafuta matibabu kwa ajili ya magonjwa yote. Mtume (s.a.w.) amesema: “Mwenyezi Mungu hakuweka maradhi ila ameleta na dawa ya kuyatibu.”

4. Jukumu la wazazi na makuzi ya mtoto Sheria ya Kiislamu imewaamuru wazazi kuwa ni dhamana kwa maisha ya mtoto na makuzi yake. Kwa msingi wa kwamba, mtoto huchukuliwa kuwa ni dhamana waliyopewa, ambayo inapaswa kutunzwa nao kwani watakujaeleza mbele ya Mwenyezi Mungu (jinsi walivyoitunza amana waliyopewa). Mtoto mwanzoni mwa maisha yake huwa hajui hatari hasa ambazo zingehatarisha maisha yake. Kwa kuongezea ni kwamba yeye hawezi kujilisha na kuchunga maisha yake, kwa hivyo basi, ndipo Mwenyezi Mungu akawafanya wazazi kuwa ni dhamana kwa ajili ya kuwalinda watoto wao kutokana na magonjwa mbalimbali na hatari ambazo zingetishia maisha na makuzi yao.

Imetajwa katika Hadith: “Kila mmoja wenu ni mchungaji na kila mmoja ataulizwa juu ya kile akichungacho. Baba ni mlezi wa jamii yake. Mke ni mchungaji wa mali ya mumewe na watoto wake, na ndiye atakayeulizwa kuhusu akitunzacho. Mtumishi ni mtunzaji wa mali ya tajiri yake na ndiye atakayeulizwa kuhusu mali aitunzayo. Ndiyo, kila mmoja wenu ni mchungaji na ndiye atakayeulizwa juu ya anachokiangalia.” Mbali na kuwa ni dhamana, ni wajibu wao pia kuwalisha watoto wao na kuwatosheleza mahitaji yao, hii inaweza kuwa kwa kuwachagulia kwa njia nzuri chakula chao, na kuwalinda kutokana na maradhi yote yatakayowad- huru.

Miongoni mwa hatari zinazoweza kutishia maisha ya mtoto katika miaka yake ya mwanzoni ni uwezekano wa kupatwa na mojawapo ya maradhi yauwayo watoto kama: Ugonjwa wa kupooza (Polio), Surua (Ukambi), dondakoo (DPT au Diphtheria) n.k. Au upungufu wa maji mwilini uletwao na magonjwa ya kuharisha n.k. Magonjwa hayo yote yanaweza kumshambulia mtoto, kumlemaza na kumhuzunisha maisha yake na ya wazazi wake. Uislamu unatuonya vikali sana tusipuuze matunzo na matibabu ya watoto wetu kutokana na maradhi yauwayo watoto au mengineo. Kwa ajili hiyo, Uislamu unaamrisha waumini wake kuwa wenye nguvu na afya. Mtume (s.a.w.) amesema: “Muislamu mwenye nguvu ni bora na ndiye apendezaye zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko Muislamu mnyonge.’’

Kwa kuwa upendo wa wazazi kwa watoto ni sehemu ya maumbile yao (wazazi) ya kiasili, ndipo ikawa hapana haja ya kuagizwa juu ya jambo hilo, kwa hivyo Uislamu umetilia mkazo zaidi umuhimu wa ‘matunzo’ ya watoto na ukaonya vikali wazazi wasizembee katika jambo hilo, ili familia na jamii ziweze kuishi kwa raha na furaha. Na hii hatimaye huleta muundo wa kizazi ambacho kitategemewa kuweza kubeba mzigo wake barabara na katika hali ya kujitegemea. Imetajwa katika Qur’ani: “Wala msijitie wenyewe katika maangamivu.” (2:145).

Na je ni maangamivu gani maovu zaidi ambayo mtu anaweza akajifanyia mwenyewe kuliko kuingiza kiwiliwili chake na damu (watoto) wake kwenye hatari ya kifo na adhabu? Imetajwa tena katika Qur’ani: “Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu (jamii) wenu kutokana na moto, ambao kuni zake ni watu na mawe….”(66:6) 

Kujilinda na maangamivu (ya ugonjwa n.k.) kuna maana sawa na kuna daraja moja na kuilinda jamii kutokana na maangamivu ya motoni. Ikiwa kujilinda kunahitajika kwa ajili ya maisha ya akhera, basi kujilinda huko kunahitajika zaidi wakati wa maisha ya duniani kwani kile ukipendacho katika maisha yako duniani ndicho utakachokivuna akhera. Kujilinda kwa maana hiyo, hakumaanishi kujizuia kutokana na kutenda maovu, madhambi na mambo ya fedheha tu, bali ina maana ya ndani zaidi kuhusiana na usawa baina ya mahitaji ya nafsi, kiwiliwili, roho, na kujilinda na maneno ya Mtume (s.a.w.) aliposema: “Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kutomjali yule anaemtegemea.” Pia: “Nyote ni wachungaji na kila mmoja wenu ataulizwa kutokana na kile anachokichunga.”

Tukizingatia, inatudhihirikia wazi kwamba kuwakinga watu wetu kutokana na maradhi ni amri ya kidini na ni wajibu wa jamii na pia ni wajibu wa taifa zima. Mtume (s.a.w.) amesema: “Mwenye kuitunza jamii na hakuipa nasaha (maonyo), basi mtu huyo atanyimwa pepo.” Kuwapatia watoto huduma za chanjo dhidi ya maradhi yauwayo na yalemazayo, humwokoa mtunzaji wa jamii kutokana na kosa la kupuuza jamii yake. Na mwishowe ataokoka Siku ya Kiyama kutokana na vitisho ambavyo vingempata wakati Mwenyezi Mungu atapomuuliza kuhusu hali ya wafuasi wake (wenye kumtegemea) na sababu ya kuwa mzembe katika jambo hilo. Kwa hivyo basi, iwapo wazazi hawatachukua hatua zifaazo ili kulinda maisha ya watoto wao kuwakinga kutokana na maradhi, kuna uwezekano mkubwa wa kunyimwa pepo akhera.

Chanjo na huduma za O.R.S. (Maji ya dawa ya kurudisha maji mwilini kutokana na maradhi ya kuharisha) hutolewa bure na serikali. Wazazi wanachotakiwa kufanya ni kuzitumia huduma hizi, ili kuwakinga watoto wao kutokana na madhara na hatari ziletwazo na magonjwa. Hata kama watalazimika kulipa ili watoto wao wachanjwe, Uislamu unawapa moyo kufanya hivyo, kwani Mtume (s.a.w.) amesema: “Bora ya matumizi, ni kutumia (japo) senti kwa ajili ya familia yako.”

5. Kuwalinda watoto ni huruma, na huruma ni kinga Mtume (s.a.w.) ametueleza mpango maalum wa kutuwezesha tuwe na huruma na upendo kwa watoto wetu. Ametaja Bukhari katika kitabu chake cha Al-Adab, katika mlango maalum kwamba “wahurumieni watoto” na pale Mtume (s.a.w.) aliposema: “Si katika sisi yule mtu asiyemhurumia mdogo, na asiyejua haki ya mkubwa (asiye mheshimu). Akasema tena: “Rehemuni (sikitikieni) wenzenu, nanyi mtarehemewa.” Ni dhahiri kutokana na Hadith zilizotajwa hapo juu kwamba Mtume (s.a.w.) ameeleza jinsi wale watu ambao hawana huruma kwa wadogo zao wanavyochukuliwa kuwa si waislamu wa kweli na hawako pamoja na Mtume (s.a.w.) na ujumbe wake Mtukufu. Inasemekana kuwa hapana yeyote awezaye kuwa na huruma kwa mtoto kama ilivyo wazazi wake (mtoto).

Ikiwa Mtume (s.a.w.) amewataka watu wote kwa pamoja kuwa na huruma kwa watoto, basi ni jambo lililo muhimu zaidi kwanza kwa wazazi kuwaonea huruma watoto wao kuliko watu wengine. Sehemu ya huruma yao kwa watoto wao ni kuwapeleka wakapatiwe chanjo na kinga kutokana na magonjwa na maradhi yote yenye kuenea yawezayo kuwashambulia.

Wazazi watakapokuwa na huruma kwa watoto wao, basi huruma hiyo hiyo huwarudia (wazazi) wakati wa uzeeni kwa sababu upendo ni kitu cha kulipana. Mtume (s.a.w.) ameeleza kwa ubainifu kuhusiana na suala hili la huruma na kinga, na akaeleza jinsi huruma ilivyokuwa sehemu ya kinga na kinga ni sehemu ya huruma. Amesema: “Harehemiwi (haonewi huruma) yule mtu asiyemrehemu mwingine, na hasemehewi yule asiyemsamehe mwingine, wala hapewi toba (na Mwenyezi Mungu) mtu asiyetubu, na wala halindwi yule asiyejilinda.”

Katika Hadith hii Mtume (s.a.w.) ametilia mkazo ya kuwa huruma ndilo jambo la msingi na akaeleza ya kwamba, yeyote asiyejilinda, basi Mwenyezi Mungu hatamlinda kutokana na maradhi. Ijapokuwa jambo hilo limeelezwa, lakini Mtume (s.a.w.) amelielezea kimantiki kwa njia ya maombi. Amesisitiza Mtume (s.a.w.) kwamba, yeyote asiyejilinda ama kulinda wengine kutokana na kitakachowadhuru au kuwaingiza hatarini au kwenye ugonjwa, basi Mwenyezi Mungu naye hawezi kumlinda kutokana na mambo hayo. Kwa hivyo basi Mtume (s.a.w.) katika maelezo yake hapa anakusudia kuifanya huruma isambae miongoni mwa watu, na anaazimia kuwapa moyo watu kujaribu kupata huduma za kinga zifaazo dhidi ya hii ikiwa ni kukamilisha sehemu ya huruma. 6. Uislamu na uzazi wa mpango

Qur’ani imefafanua waziwazi kuhusu muda maalum ufaao kwa kutenganisha baina ya kuzaliwa mtoto mmoja hadi kupata mwingine. Imetajwa ndani ya Qur’ani kuwa kubeba mimba ya mtoto hadi kumwachisha kunyonya ni kipindi cha miezi thelathini; Amesema Mwenyezi Mungu: “…Kubeba mimba ya mtoto hadi kumwachisha ni miezi thelathini…”(46:15) Pamoja na hayo, Uislamu unaunga mkono kunyonyesha kwa maziwa ya mama kunakodumu kwa miaka miwili kamili kwa wale wanaotaka kutimiza muda huo kamili. Kwa kufanya hivi, kunamwezesha mama (aliyezaa) kurekebisha afya yake, na kumrudisha nguvu zake za mwilini alizozipoteza katika kipindi cha uja uzito hadi kujifungua.

Muda huu maalum pia utamwezesha mtoto kupata muda wa kutosha wa kunyonya matiti ambapo utaalamu wa utabibu (wa kisasa) umekuja kuunga mkono baada ya kutofaulu kwa muda mrefu, kwa kutumia chupa ya kunyonyea. Kwa hivyo hapa ni dhahiri namna gani Uislamu unavyopigania uzazi wa mpango ili kuwapatia afya bora mama na mtoto.

Imetajwa katika Qur’ani: “Na tumemwusia mwanaadamu kuwatendea wema wazazi wake, mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu, kubeba mimba yake mpaka kumwachisha kunyonya ni (kipindi cha) miezi thelathini….”(46:15). Imetajwa pia katika Qur’ani: “Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia mema wazazi wake, mama yake amebeba mimba yake kwa unyonge juu ya unyonge, na (kumnyonyesha na) kumwachisha kunyonya katika miaka miwili.” 7. Uislamu na Karantini za afya:

Uislamu unaonya sana tuwe macho kutokana na maradhi yaambukizayo na unatusihi tujikinge na maradhi hayo. Imepokewa Hadith ya kwamba Mtume (s.a.w.) alibaiwa (kuungwa mkono wa uongozi) na mtu mwenye ugonjwa wa ukoma pasi na kupeana naye mkono1, ama kumruhusu kutangamana na watu. Imepokewa kutoka kwa Umar bin Shareed, kutoka kwa baba yake amesema:
1 Ilikuwa zamani kiongozi anapoungwa mkono uongozi wake, watu huja mmoja mmoja wakapeana naye mkono ikiwa ni ishara ya kumkubali - Mfasiri 

Katika ujumbe wa Thaqif uliokuja kum’bai (kumtambua kama kiongozi) kulikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa ukoma, basi Mtume (s.a.w.) alimrejesha (bila ya kumpa mkono) kwa kusema: “Hakika tumekutambua.” Na katika Sahih Bukhari, Mtume (s.a.w.) amesema: “Kaa mbali na mwenye ukoma kama unavyokaa mbali na simba.” Mtume (s.a.w.) ameeleza wazi wazi kwamba wakati yatapoingia maradhi ya tauni, watu ni lazima wawe macho sana, na wachukue hadhari zote za lazima ili kujikinga na kujiepusha na mtu aliyeambukizwa.

Imetajwa katika Hadith: “Tauni (ugonjwa ueneao) ni alama ya adhabu ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu huwajaribu nayo watu miongoni mwa waja wake. Mtakaposikia kuwa umeingia nchini, basi msiingie nchini humo na iwapo utatokea nanyi mko ndani ya nchi hiyo basi msitoke.” Hapa Mtume (s.a.w.) anaamuru ‘Karantini’ na anatukataza kuingia katika nchi iliyokumbwa na ugonjwa wa tauni, ili tujilinde kutokana na kifo, vile vile tumeonywa tusitoke nje ya nchi ambayo tayari imekumbwa na ugonjwa huo, ili tusisambaze maradhi. Na hii pia ni aina nyingine ya kujilinda. Aina hizi mbili za maonyo (zilizotangulia hapo juu) zinachukuliwa kuwa ni aina za hasi (Negative) za kujikinga. Wakati ambapo kuchanja kwa ajili ya kinga za magonjwa na maradhi ya kuambukiza ni aina ya chanya (Positive). Kwa hivyo Uislamu unapigania sana aina hii ya chanjo kwani ndiyo iliyo bora na ni yenye gharama ndogo zaidi kuliko matibabu.

SEHEMU YA TATU
Chakula bora na manufaa yake katika afya ya kimwili na kiakili i. Uislamu na kunyonyesha kwa matiti (maziwa ya mama) Mtoto anapozaliwa na kuja ulimwenguni, mtu anayemuhitajia na kufungamana naye zaidi ni mama yake, ni sawa kabisa na kusema kwamba nusu ya kitu imeungana na kamili. Mtoto anahitaji kulishwa chakula sawa na kile alichozoea kukila kupitia kwenye damu ya mama yake, wakati alipokuwa kilenge (kitoto tumboni). Chakula hicho alichozoea kukila ndicho huchezea kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, na kuwa maziwa ambayo yana chembechembe zilizo lazima kwa uhai wa mtoto huyo na vitu muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya kukua kwake.

Maziwa hayo hutoka kupitia kwenye matiti, na mtoto kwa uwezo wa Mola, huyahitajia na huyanyonya. Qur’ani imeeleza kanuni zinazosimamia uhusiano baina ya mtoto na mnyonyeshaji wa kuajiriwa (yaani wakati mama mzazi anaposhindwa kumnyonyesha mtoto wake kwa sababu mahsusi, kisha akakodisha mnyonyeshaji ili amnyonyeshee mtoto wake). Imetajwa katika Qur’ani: “Na wanawake waliozaa wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili, kwa anayetaka kukamilisha muda wa kunyonyesha….” (2:233). Kutokana na Aya hii, tunaweza kueleza mambo yafuatayo:
1. Ni wajibu wa mama kumnyonyesha mtoto wake, na si kumnyima haki ya kunufaika na maziwa ya matiti, lakini hii inategemea kama ataweza kumnyonyesha (yaani kutokuwa mgonjwa, n.k.).
2. Muda wa kunyonyesha kwa wale wanaotaka kutimiza muda ni miaka miwili kamili.

3. Kumwachisha mtoto kunyonya kunaruhusiwa kabla ya kutimiza muda (wa miaka miwili) kwa sharti uamuzi huu upitishwe kwa makubaliano ya wawili kati ya baba na mama, tena baada ya kujadiliana kwa pamoja uzuri na ubaya wa uamuzi huo, na jinsi ya kumpa matunzo ya kutosha mtoto wao. Imetajwa katika Qur’ani: “Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha kunyonya (kabla ya miaka miwili) kwa kuridhiana na kushauriana, basi hapana ubaya juu yao.” (2:233).

4. Ni juu ya baba kumsaidia mama anayenyonyesha, kumweka katika mazingira yafaayo anayohitaji ili kumyonyesha mtoto wake. Hii inadhihirisha kwamba Uislamu unachukulia kunyonyesha kuwa ni wajibu mkubwa kwa upande wa mama, ambapo haufai kufuatiliziwa na kazi nyingine za ziada. Hivyo basi hii inaonyesha waziwazi jinsi Qur’ani ilivyoeleza kwa ufafanuzi juu ya haki za mama anayenyonyesha.

5. Baba atakapokuwa hayuko, ama amefariki, mmoja kati ya watu wa familia atachukua jukumu la kumlisha mtoto na kumtoshelezea mahitaji yake yeye na mama yake, ili aendelee kunyonyesha. Hali mojawapo kati ya hizo zinapotokea huwa zinazingatiwa kwa makini sana na Uislamu, ndipo Uislamu ukaweka kanuni mahsusi kwa waislamu zinazoelezaea mambo haya.

6. Mama anayeweza kumnyonyesha mtoto wake, anakatazwa kuajiri mnyonyeshaji wa kumnyonyesha mtoto wake badala yake. Uislamu unamlazimisha baba wa mtoto kutoa posho ya pesa kumpatia mama aliyemtaliki (aliyemwacha wakati akinyonyesha), anyonyeshaye mtoto yule. Kwa hali hiyo, Uislamu unahakikisha kwamba mtoto anapata mahitaji yake yote anayopaswa kupewa katika kipindi hiki cha kunyonya. Ni vizuri kutaja hapa kwamba Mwenyezi Mungu ameyatosheleza mahitaji (yote ya lishe) ya mtoto kutokana na maziwa anayoyanyonya kutoka kwenye matiti ya mamake.

Katika siku tatu za mwanzo wa maisha ya mtoto, matiti hutowa majimaji ya kimanjano yajulikanayo kama ‘dang’aa’ (beestings) na ambayo hutoka kwa kiasi kidogo. Majimaji haya hutosheleza kumpatia mtoto chakula anachokihitaji mwanzo wa maisha, aidha hulisaidia tumbo lake kuanza kupokea na kuyeyusha chakula anachokila. Katika siku ya nne, matiti huanza kutoa maziwa ambayo ni ya muhimu kwa kumlisha mtoto mpaka atakapofikia kuacha.

Mama anayekataa kumnyonyesha mtoto wake bila ya sababu za maana, basi hujinyima yeye na humnyima mtoto wake faida muhimu sana. Kwani kunyonyesha kunamletea mama hisia za mapenzi na humwongezea (moy- oni mwake) hisia za huruma ya umama. Kwa kuongezea tu, kwa yale yaliyotajwa hapo awali ni kwamba, kunyonyesha kunafanya utaratibu wa kuyeyusha chakula kwa mama kuweza kutengeza chakula kinachohitajika, kilicho muhimu kwa mtoto wake na kustawisha hali yake ya kiafya kwa ujumla. Pamoja na hayo, kunyonyesha kunasaidia kurekebisha njia ya uzazi wa mwanamke na kuweza kuirudisha katika hali iliyo sawasawa na ya kawaida baada ya kumalizika kwa zoezi la kuzaa.

ii. Umuhimu wa kunyonyesha kwa matiti katika Uislamu Qur’ani imetilia mkazo umuhimu wa kunyonyesha kwa matiti katika Uislamu ikasema: “Tukampelekea mama yake nabii Musa ufunuo (ufahamu wa moyoni - wahyi) kuwa mnyonyeshe, na utakapomhofia, basi mtie mtoni, usiogope, wala usihuzunike kwani sisi tutamrejesha kwako. Na tutamfanya kuwa ni miongoni mwa Mitume.” (28:7).

Hapa Mwenyezi Mungu amemwamuru mama yake nabii Musa (a.s.) kumnyonyesha ili kuleta hisia maalum za kiroho, hisia ambazo zinafanya kunyonyesha kuwa ni mwenendo wenye kusisimua. Wakati mama anaponyonyesha, huwa katika hali ya msisimko mkubwa usiyomithilika, na hisia za umama na huruma zake pia huwa zimeamshwa (huwa na huruma sana). Kwa ajili hii ndipo mama yake nabii Musa (a.s.) alipoanza kuhofia kuhusu maisha ya mwanawe. Mwenyezi Mungu alimwamrisha amnyonyeshe, kwani katika muda huo wa kumnyonyesha ndipo njia ya uhusiano inapotokea baina yake na mama yake. Au kwa upande mwingine, mama pia huanza kuunda hisia za moyoni kwa mtoto wake ambaye anazungukwa na pendo na huruma ya hali ya juu. Kumnyonyesha kwa mama yake nabii Musa mtoto wake kulikuwa ni kwa pendo na huruma yake yote. Hii ndiyo ikawa sababu kubwa ya Mwenyezi Mungu kumharamishia (kumfanya akatae kunyonya) maziwa ya mnyonyeshaji wa kukodishwa aliyeletwa na Firauni, kwani nabii Musa alikuwa ameshaonja maziwa ya mama yake, na hivyo kukataa kuonja maziwa ya mwanamke mwingine yeyote.

Amesema Mwenyezi Mungu: “Na tukamharamishia wanyonyeshaji tangu mwanzo….”(28:12). Qur’ani imeeleza tena kuhusu umuhimu wa kunyonyesha na maana yake; na mfungamano imara wa kiakili wa kimoyo kati ya mtoto na mamaye unaotokana na kunyonyesha kwa matiti. Imeelezwa kwamba, hapana mama yeyote awezaye kumtupa mtoto wake mchanga anyonyaye ila awe amepatwa na hofu kuu na hatari itishayo kabisa! Amesema Mwenyezi Mungu:

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu, hakika mtetemeko wa Siku ya Kiyama, ni jambo kubwa (sana). Siku mtakapokiona (Kiyama), kila mwanamke anyonyeshaye atamsahau (mtoto) amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba yake. Na utawaona watu wamelewa na wala hawakulewa, lakini (hiyo) ni adhabu ya Mwenyezi Mungu iliyo kali.”(22:1-2) Maumbile haya ya dhahiri na ya ajabu, ya uhusiano (wa mtoto na mama) yatageuzwa Siku ya Kiyama kwa mama kumsahau mtoto wake anayemnyonyesha, ambalo hilo kwa hakika ni tukio la kutisha.

Kabla ya ukhalifa wa Umar Ibn al-Khattab, dola ya kiislamu ilikuwa ikitoa posho maalum kwa mtoto anayeachishwa kunyonya. Mpango huu ukawa unatumiwa vibaya na familia maskini, kwani walikuwa wakiwaachisha watoto wao kunyonya mapema sana ili wakajipatie posho hizo. Umar Ibn al-Khattab akalichunguza jambo hilo kwa kina kwa jinsi akina mama walivyowanyima watoto wao haki za kuwanyonyesha kwa muhula wa miaka miwiwli kamili, kama ilivyotajwa katika Qur’ani.

Hatimaye tabia hiyo ilidhuru afya na makuzi ya watoto. Kwa sababu hiyo, ndipo Umar (wakati wa ukhalifa wake) akaurekebisha utaratibu huo, akafanya malipo ya posho hiyo yatolewe mara tu mtoto anapozaliwa. Marekebisho haya yakawapa nguvu akina mama ya kuweza kukamilisha kuwanyonyesha watoto wao kwa kipindi cha miaka miwili pasi na kuwanyima haki hii muhimu. Vizazi vya kiislamu vilivyotangulia mara kwa mara vilikuwa vikihimiza kunyonyesha kwa kutambua umuhimu wake katika maisha ya mtoto na familia.

Kwa kuwa Uislamu ni dini ya kimaendeleo na yenye huruma ambayo inafaa kwa wakati wowote na mahali popote, unamtaka kila mtu mwenye busara kufuata na kudumisha vitendo vyema na vilivyo sawa. Ikiwa utaalamu wa kisayansi katika zama zetu hizi za kisasa umetilia mkazo umuhimu wa kunyonyesha, basi ni vizuri kutaja kwamba Uislamu umetilia mkazo jambo hili tangu miaka elfu moja mia nne (1400) iliyopi- ta.

Kwa hivyo Uislamu unampa taadhima baba na mama Muislamu, mtoto na jamii yote ya Kiislamu kwa ujumla, pale unapotuamrisha kufuata vitendo vizuri kama hivyo. Inaeleweka wazi kuhusu athari ya maziwa ya mama kwa afya ya mtoto, tabia yake na maisha yake ya baadaye. Kwa hivyo si ajabu kwa nini Mtume (s.a.w.) ametukataza tusimpatie kumnyonyesha mtoto mwanamke kahaba au asiye na akili timamu. Mtume (s.a.w.) ametuamuru tumlinde mtoto kutokana na jambo lolote litakaloharibu uzuri wa maumbile yake. Amesema: “Walindeni watoto wenu kutokana na maziwa ya kahaba na ya mwendawazimu, kwani maziwa yanaambukiza.” Ndani ya maelekezo haya, hapana shaka kwamba Uislamu unahakikisha kabisa kwamba watoto wanapata malezi na matunzo ya kutosha wanayostahili kuyapata. iii. Lishe kwa akina mama waja wazito na wanaonyonyesha Afya ya mtoto aliye tumboni mwa mama yake hutegemea sana utaratibu wa chakula kiletacho afya mwilini wakati mama anapokuwa mja mzito. Ukosefu wa chakula bora wakati wa uja uzito huwaathiri wote kwa pamoja, kitoto na mama yake.

Tumeshazungumza hapo awali kwamba Uislamu humlinda mtoto hata kabla hajazaliwa ili mtoto azaliwe akiwa na nguvu na afya. Ni kwa sababu hii ndipo mwanamke mja mzito lazima awe mwangalifu sana kwa kuchagua vizuri mchanganyiko wa vyakula wakati huo, kwani kwa kufanya hivyo tu ndipo mtoto wake atakapozaliwa katika hali ya afya njema. Mchanganyiko wa chakula bora wakati wa uja uzito utamwezesha mzazi kuwa na hali nzuri ya kiafya baada ya kujifungua ili kumnyonyesha mtoto wake vizuri. Kutokana na mazingatio ya Uislamu juu ya mambo haya, ndipo ukawaruhusu akina mama waja wazito na wanyonyeshao wasifunge katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, iwapo wanahofia pengine kufanya hivyo kungemdhuru mtoto aliye tumboni.

Ruhusa hii si ya kudumu, bali inategemea kitambo atakachokitumia mama mnyonyeshaji katika kumnyonyesha mwanawe; ikiwa ni kirefu au kifupi. Ni dhahiri kwamba shabaha ya Uislamu ni kutekeleza utoshelezaji wa mahitaji ya lazima ya mtoto, na kwa jinsi gani unavyoheshimu hisia za huruma za umama. Mtume (s.a.w.) amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu amemruhusu mwenye kusafiri asifunge, na apunguze Swala, pia amemruhusu mwanamke mja mzito na anayenyonyesha asifunge.” iv. Mchango wa chakula bora katika kukuza akili timamu Miongoni mwa mambo yanayozingatiwa sana na Uislamu ni ustawi wa akili na nafsi ya Muislamu. Kula chakula bora ndio ufunguo wa afya nzuri na ustawi wa kiakili na wa nafsi, na yapasa kuanza wakati mama anapokuwa mja mzito na kuendelea katika muda wa maisha ya kila mmoja. Sheria ya Kiislamu inashauri watu wale vyakula mbali mbali vyenye afya ambavyo ni vya lazima kwa mwili wa binaadamu na kuongezeka kwa afya. Mtume (s.a.w.) amesema: “Muislamu mwenye nguvu ni bora na yu karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko Muislamu dhaifu.”

Mwili wa binaadamu daima unahitaji chakula bora ili kuweza kurudisha nguvu zilizopotea wakati wa kufanya kazi na harakati nyinginezo, na kuuwezesha kuendelea na kazi zake za kawaida, kwa sababu hizi ndipo Uislamu ukasisitiza kuhusu kula chakula bora bila ya kufanya ubadhilifu. Mwenyezi Mungu amesema: “..…kuleni na kunyweni (vizuri) lakini msifanye ubadhilifu…..”(7:31). Amesema tena: “Naye ndiye aliyeumba mabustani yanayoegemezwa (yanayokingamana) na yasiyoegemezwa, na (akaumba) mitende na mimea ya aina mbali mbali, na mizaituni, na mikoma-manga inayofanana na isiyofanana, na kuleni matunda yake inapozaa; na toeni haki yake siku ya mavuno yake, wala msifanye ubaadhirifu, hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafanyao ubadhilifu.”(6:141).

Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu ni Mkarimu sana kwa watu wake kwa kuwaumbia ng’ombe na wanyama ili kutumia manyoya na kula nyama zao kwa ajili ya kuhifadhi maisha yao. Inakisiwa kwamba ni kwa sababu hii ndipo Mwenyezi Mungu akamwamuru Mariam baada ya kumzaa Isa (a.s.) kula tende mbivu ili kufidia kiasi cha damu alichokipoteza. Mwenyezi Mungu amesema katika Qur’ani: “Na amewaumba wanyama katika hao mnapata (vitiavyo) joto, na manufaa mengine, na wengine mnawala.” (16:5). Amesema tena pia katika Aya nyingine: “Mna (katika hiyo bustani) matunda na hasa mitende na mikomamanga.”( 55:68). 

Mwenyezi Mungu (hapa) amezihusisha tende na mikoma-manga (mikudhumani) kwa ajili ya ubora wa matunda hayo kushinda mengine. Miongoni mwa faida (za kiafya) zipatikanazo kwenye matunda hayo mawili: Ni kiasi kikubwa cha sukari (Glucose) kilichomo ndani yake ambayo huyeyushwa na kutumiwa na mwili kwa haraka ili kuweza kuzalisha nguvu (Calorie) na joto mwilini. Mwenyezi Mungu amesema: “Na litikise kwako shina la mtende litakuangushia tende nzuri zilizoiva na unywe na utulize jicho lako (upumzike)…”(19, 25-26). Ama kuhusu koma-manga, imegunduliwa kuwa ina kiasi kikubwa cha ‘Limonic acid’ ambayo inasaidia kupunguza ukali wa tindikali (acid) katika mkojo na damu pindi inapoyeyuka mwilini. Kwa kuongezea ni kwamba tunda hilo pia lina kiasi kikubwa cha joto ambacho huyeyushwa na mwili kwa urahisi zaidi na hutumika kwa kuupa mwili. Kuhusu asali ya nyuki, imeainishwa kwa kutajwa ndani ya Qur’ani: “…..kinatoka katika matumbo yao (nyuki) kinywaji (asali) chenye rangi mbalimbali, ndani yake kina tiba kwa wanaadamu…..”(16:69). Amesema tena Mwenyezi Mungu: 

“Na alama (ya rehma za Mwenyezi Mungu) juu yao, ni ardhi iliyokufa (isiyo na rutuba) tunaifufua na tukatoa ndani yake nafaka ambazo wanazila, na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu na kupitisha chemchem ndani yake ili wale matunda yake….”(36:33- 35). Amesema tena Mwenyezi Mungu: “Na katika wanyama kuna wale wabebao mizigo na wanaopandwa. Kuleni katika alivyokuruzukuni Mwenyezi Mungu.” (6:142). Amesema tena Mwenyezi Mungu kuhusu maji: “Yeye ndiye anayekuteremshieni maji kutoka mawinguni, kwa hayo mnapata ya kunywa na (yanatoa) miti ya kulishia (wanyama).” (16:10). Amesema tena Mwenyezi Mungu kuhusu maziwa kwa ajili yenu. “Tunakunywesheni katika vile vilivyomo matumbo mwao (vikitoka) baina ya kinyesi na damu, (nayo ni) maziwa safi mazuri kwa wanywao.” (16:66). 

Amesema tena Mwenyezi Mungu: “Na kuleni katika vile alivyowaruzukuni Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri.” (5:88).


SEHEMU YA NNE
i. Maoni ya Uislamu juu ya malezi ya mtoto Watoto ni maua yenye kuchanua katika maisha yetu, ni ahadi ing’aayo katika mustakbali wetu, na ni kiburudisho cha macho yetu. Wao ndiyo wanaodumisha historia adhimu ya mataifa yao. Watoto na vijana wana jukumu kubwa tena la maana la kufanya wakati wa maisha yao. Kwanza, wamekadhibiwa ulinzi wa kuhakikisha kuwa kazi kubwa inafanyika kwa ajili ya nchi zao. Pili, wanatarajiwa kutumia uwezo na ujasiri walionao ili nguvu zao ziweze kufaidisha kuinua hali ya maisha ya mataifa yao.

Na kwa sababu hiyo, ndipo Uislamu ukahimiza sana umuhimu wa malezi ya mtoto. Qur’ani ina maagizo na masharti kwa ajili ya kulinda maisha ya mtoto. Pia kumwongoza na kumpangia utaratibu katika maisha yake. Wakati Uislamu unapopanga utaratibu wa maisha ya mtoto, familia na jamii zinazingatia kwamba pana uhusiano wa ndani baina yao unaoonyesha kwamba mabadiliko au uharibifu wowote ukitokea upande mmoja basi utawadhuru wote.

Kwa hivyo fikra za Uislamu zimempangia Mwislamu njia nzuri ya maisha ambayo msingi wake ni ushirikiano, huruma na imani, ili kutoa mchango wake katika kuwatengezea maisha jamii ya kiislamu. Na ili kufanya hivyo, Uislamu unaanza kwa kumpangia mtu mmoja, kwani yeye ndicho kiungo cha mwanzo katika kuunda maisha ya familia na ya jamii ya watu, na mwishowe taifa zima.

Mtu mmoja ndiye msingi wa kitu cha kwanza, na ndipo asili ya maisha ya taifa zima yanapoanzia. Mtu mmoja ndiye chanzo, naye si mwengine bali ni mtoto ambaye huongozwa na maumbile yake ya kiasili na tabia zake alizojifunza kutoka kwa jamii yake kupitia njia ya kuishi pamoja. Kutangamana na watu wengine ndiko kunakotengeneza tabia ya mtu na kumpangia utaratibu wa heshima za kiutu (zinazothaminiwa katika jamii hiyo). Iwapo atakuzwa katika njia bora na yenye nidhamu, basi atakuwa ni nguzo ya mafanikio katika maisha ya familia ambayo ni sehemu ndogo tu ya jamii ya watu.

Kwa hivyo mafanikio katika familia (ambazo zikiungana pamoja zinaunda jamii), mwishowe yataunda taifa imara na lenye nguvu. ii. Mtoto baina ya silika na athari na mazoea ya mazingira, na jukumu la wazazi Maendeleo makubwa sana yamepatikana katika elimu ya saikolojia (nafsi) ambayo kwayo wataalamu wa elimu hiyo huweza kumiliki kutengeneza tabia ya mwanaadamu na kuilezea nguvu ya maumbile ya kudumu ambayo inafanya mtu kutenda jambo kwa njia maalum. Tena, wataalam hao katika utafiti wao, wanachimbua kwa undani zaidi kuhusu nafsi ya mwanaadamu na wamegundua vipengele mbali mbali vya makuzi ya maumbile ya mtoto na tabia zake kiasili.

Tena wakazifafanua silika mbali mbali zinazoongoza mwenendo wa mtoto katika kila hatua ya kukua kwake. Pia wameeleza kwa urefu zaidi kuhusu mahitaji ya watoto na jinsi ya kuwatosheleza. Uislamu umetangulia elimu hiyo katika kupambanua hatua mbali mbali za makamuzi ya mtoto, haki zake, na mahitaji yake. Kazi hii iliyotangulia iliyofanywa na Uislamu inatoa mchango mkubwa katika kuleta ustaarabu wa binaadamu. Kabla hatujaenda mbali zaidi katika kueleza jinsi Uislamu unavyotoa maoni yake kuhusu malezi ya mtoto, hatuna budi kwanza kufafanua mambo muhimu yafuatayo: Kuna baadhi ya watu wanaounga mkono fikra kwamba mtoto huzaliwa mwema kimaumbile. Hii ina maana kwamba mtoto, kiasili, huzaliwa katika hali ya kuwa mwema ila tu ni ulazimishaji wa mazingira ndio unaogeuza na kuathiri mwenendo wake, na ndio unaoamua iwapo atadumisha mwenendo wake mzuri ama la. Kwa upande mwingine kuna wengine wanaoshikilia mawazo yanayosisitiza kwamba, mtoto huzaliwa akiwa ni karatasi nyeupe (yaani si mwema wala si mwovu) ila ni kutokana na mazingira (anamoishi) ndipo huanza pole pole kujizoesha kushika mwenendo na tabia za mazaingira hayo. Mtoto huyo hushika tabia tofauti zinazomfanya kuwa ni sehemu ya mazingira yale anayoishi, mwishowe huunda tabia yake.

Basi kwa vyovyote, aidha iwe maoni ya kwanza ama ya pili ndiyo yenye nguvu zaidi, hapana shaka yoyote kwenye njia zote mbili kwamba, yale mazingira anayoishi mtoto yana mchango mkubwa na wa muhimu katika kuunda tabia, mwenendo, na maisha yote. Miongoni mwa watu wa kwanza katika mvuto wa kitabia wa mtoto, ni wazazi wake. Mtoto huwachukulia wazazi wake kuwa ndiyo kielelezo katika maisha, na ni kwa sababu hii muhimu ndipo wazazi siku zote wanatakiwa wawe mfano bora wa kufuatwa na watoto wao katika jambo walisemalo ama walifanyalo.

Ikiwa ni hivyo, ni dhahiri kwamba maumbile ya kiasili anayozaliwa nayo mtoto na mazingira anayoishi yana athari kubwa katika kumjenga na kumwendeleza awe raia mwema. Kwa sababu hii, ndipo Uislamu kama tulivyoelezwa hapo mwanzo, unamlinda mtoto hata kabla hajazaliwa. Mwenyezi Mungu amewataka watu kuwaangalia vizuri sana watoto wao. Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: “Wapendeni watoto wenu na muwahurumie, na mtakapowaahidi (kitu) basi watimizieni, kwani wao hawaoni anayewapatia mahitaji yao ila nyinyi.” Hadithi hiyo iliyotangulia inafafanua mambo matatu yaliyo adhimu kabisa: 

1. Upendo: Huu ni dhamana inayokusanya watu pamoja kwenye huruma na ihsani, na hasa kwa wale waliofungamana nasi zaidi kushinda jamaa zetu wote, nao ni kiwiliwili chetu na damu yetu, yaani watoto.
2. Huruma: Hili ni kimbilio kubwa la binaadamu ambalo hukusanya mapenzi na uaminifu katika ukumbi wake. Mambo mawili haya husaidia kuleta yaliyo bora kwa watu.
3. Kutelekeza ahadi: Kufanya hivyo kwa baba juu ya watoto wake kunaonyesha namna upendo wa ndani ulio imara na huruma vinavyounganisha uhusiano wao, na hivyo ndivyo tulivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Fikra za mzazi anayemtimizia ahadi mtoto wake baadaye huwa maishani mwake ni moja kati ya kukuza tabia ya kutangamana. Kutangamana kwa wazazi na watoto wao, humpatia mtoto sifa na tabia njema na hutengeneza mwenendo wake. Amesema Mtume (s.a.w.): “Kueni dhamana (mtangamane) na watoto wenu.”

Hapa Mtume (s.a.w.) anakusaidia kwamba watoto wasiachiwe bila ya kupatiwa chakula, wasitupwe, au kuachiwa watu wengine (wasiohusika) kuwaangalia, kwani kufanya hivyo kutawafadhaisha na kuwatia hatarini. iii. Mwalimu aliye mfano bora, na kumfundisha mtoto nidhamu Amesema Utba bin Sufyani wakati alipokuwa akimweleza mwalimu wa mtoto wake: “Mfano kwa mtoto wangu uwe ni mfano wako (vile ufanyavyo), kwani macho yao (watoto) siku zote huwa yanaangalia machoni kwako. Chochote kizuri watakachokiona machoni kwao kitakuwa ndicho kile kizuri ulichokiona wewe, na chochote kiovu watakachokiiga kitakuwa ni kile ulichokionelea.”

Amesema Ibn Khaldun akieleza kuhusu Rashid alipokuwa akimwambia mwalimu wa mtoto wake Al-Amin kwamba: “Kiongozi amekuamrisha kwa furaha ya moyo wake uwe dhamana kwake (mtoto), na umfanye aku- tii, uwe kama anavyokutaka uwe: Msomeshe Qur’ani, mfundishe elimu na bayana, mfundishe namna ya kuhifadhi na kusoma mashairi, mfafanulie kuhusu elimu ya Hadith za Mtume, muonyeshe namna ya kuanza na kumaliza hotuba, asicheke ila kwa sababu. Tena usiache hata saa moja ipite bila kutumia nafasi hiyo kwa kumfundisha jambo lenye faida, na usiache kujihusisha na hivyo kumsumbua na kuichosha akili yake. Usimwache awe goigoi, mfundishe adabu kadri ya uwezo wako lakini kwa uaminifu na huruma.”

Wanavyuoni mabingwa wa fikra za kiislamu kama al-Ghazaali, Ibn Khaldun na Ibn Muskawieh, wamesisitiza umuhimu wa malezi mazuri ya mtoto, adabu na mwenendo mzuri. Mtume (s.a.w.) amesema: “Kila mtoto huzaliwa katika maumbile ya kihulka.” Amesema Mwenyezi Mungu: “....ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumba watu…..” (30:30). Kufunza adabu ni jambo la kwanza linalotakiwa apatiwe mtoto wakati wa utoto ili ajizoeshe kuwa na mwenendo mwema na tabia nzuri. Amesema Mtume (s.a.w.): “Kumfunza adabu mmoja wenu mtoto wake ni bora kwake kuliko kutoa sadaka ya nusu pishi kila siku.”

Tunapowafunza adabu watoto wetu, huwa tunasaidia kuweka msingi imara kwa taifa letu na hivyo ndivyo mafunzo ya Kiislamu yanavyotutaka tutekeleze. Uislamu kwa kufuatilia unatutaka tufanye hivyo na kwa njia kama hiyo na ndio maana ukayapita majaribio yote ya kumfunza adabu mtoto. Uilsamu umeunganisha malezi mazuri na zawadi ambayo inatunzwa na kupewa wenye kufunza adabu. Kwa maana hiyo, Uislamu umewapa moyo wazazi kuwalea vizuri watoto wao. Mtume (s.a.w.) amesema: “Wakirimuni watoto wenu na muwape adabu.” iv. Uislamu na malezi ya kujitegemea kwa mtoto Wakati Uislamu ulipowapa wazazi jukumu la kuwalisha watoto wao na kuwaongoza, haukudharau kwa vyovyote vile uwezo alionao mtoto mwenyewe, kwa kufanya hivyo, Uislamu haukusudii kuwafanya wazazi wa mtoto kuyafikiria na kuyapanga maisha yake yote kabisa na wakati huo huo awe akiwategemea wao kabisa. Hata hivyo, Uislamu umekusudia kuwafanya wazazi wawalinde na kuwaongoza watoto wao wadogo, wasiwapotee njia kwa kuingia mashakani na kwenye dhana.

Uislamu umewaamuru wazazi kuwaongoza na kuwalisha watoto wao tu, bila kujiingiza sana katika shughuli zao. Maoni ya Uislamu kuhusiana na malezi ya mtoto yamefafanuliwa zaidi na Muhammad Rashid Ridha kwa mifano mingi katika tafsir ya Al Manar. Imethibithishwa katika matukio mbali mbali kwamba kujitegemea kwa mtoto ndiyo mwanzo wa kuunda vizazi vyema na watu barabara wa kutegemewa watakaoweza kuchukua jukumu la kujenga taifa.


Imetajwa katika ushauri kwa mzazi ya kwamba: “Cheza na mtoto wako mpaka atakapofikia umri wa miaka saba, kisha mfundishe adabu kwa miaka mingine saba ijayo, kisha uwe suhuba naye kwa miaka mingine saba ijayo, kisha baadaye mwache ajitegemee.” Ni jambo la muhimu sana kumruhusu mtoto ahudhurie katika majadiliano na kutoa maoni yake, japo maoni yake yatakuwa ni ya kijuujuu tu, na ya kuchekesha, au yasiyohusiana na suala linalozungumziwa hapo, inaweza kuwa pia kumdhihaki si jambo la busara, bali ni vizuri wazazi wawe na bidii ya kumfahamisha pale anapokosea wakati wa kutafakari au kuamua. Anapaswa kutiwa moyo kusema kwa kile hasa anachokifikiria kuwa ni sawa. Kwa kufanya hivyo, bila shaka kutanufaisha mambo yafuatayo:
1. Siku zote hataogopa kutoa maoni yake.
2. Ataweza kujisahihisha na kila alilokosea ama kwa kutofahamu vizuri upande wake, na hilo litamfanya kurekebisha maoni yake na kuchukua uamuzi ufaao.
3. Wakati watu wazima watakapopata shauri (juu ya jambo fulani) atajifunza kutoka kwao uamuzi wa sawa, na jinsi ya kukata shauri katika mambo mbali mbali.
4. Atakuwa anafahamu jinsi ya kujadiliana katika mambo na kuweza kupata suluhisho la matatizo, ili asiachwe hivi hivi tu bila ya kuweza kutatua matatizo.
5. Atakuwa ameandaliwa katika kupambana na mikasa ya kimaisha.
6. Hii pia itamsaidia kutojiamulia tu bila ya kufikiri, na itamfanya atambue matatizo, kwa hivyo, atajua jinsi ya kuyaelezea na kuyatatua yatakapomkabili wakati wa maisha yake na hatofadhaika. Mfano ni ule uliotokea kwa Abdalla bin Abbas, wakati Mtume (s.a.w.) alipowaambia maswahaba zake: “Mwenyezi Mungu amemfananisha Mwislamu mwenye imani na mti ambao hautupi ovyo majani yake. “Kisha akawauliza: “Je mwajua ni mti gani huo?” Wote wakanyamaa, kisha Mtume (s.a.w.) mwenyewe akajibu: “Huo ni mtende.”

Walipokuwa wakienda nyumbani, Abdallah bin Abbas huku akifuatana na baba yake alimwambia baba yake kuwa alijua jibu la swali alilouliza Mtume (s.a.w.) lakini aliogopa kusema mbele za kadamnasi ya watu, kwani huenda ikawa ni makosa kufanya hivyo. Baba yake akamwambia: “Lau kama ungelijibu, basi ingekuwa jambo kubwa kwangu kuliko kupata mifugo iliyo bora.” 

Uislamu na kumuelimisha mtoto
Uislamu unawataka waislamu kutafuta elimu. Kutafuta elimu ni wajibu kwa kila Mwislamu awe ni mwanamume au mwanamke. Haikuamrishwa kwa jinsia moja ya watu au nyingine tu, au kikundi fulani cha watu au kingine, kwani (elimu) inaongoza maisha ya watu. Jamii ya watu iliyoundwa kwa elimu na yenye watu walioelimika, ndiyo jamii iliyo bora kushinda zote, kwa kuwa watu wamepata umashuhuri na ufanisi kwa ajili ya elimu. Kwa sababu kama hizo, kanuni za Kiislamu zinapigania sana elimu ambayo itaongoza watu (ya mwenye kuelimika), na itastawisha 

jamii ya watu wote. Ili kufikia lengo hili, inasemekana kwamba katika vile vita mashuhuri vya Badr, Mtume (s.a.w.) aliamuru kila mateka anayejua kusoma na kuandika, aliyeshikwa katika vita hivi, aachiliwe huru iwapo atawafundisha watoto kumi wa kiislamu jinsi ya kusoma na kuandika. Vile vile Mtume (s.a.w.) amesema: “Wafundisheni watoto wenu kwani, wao wamezaliwa katika zama tofauti na zama zenu.” Amesema tena: “Tafuteni elimu hata kama ni (kwenda) China.” Uislamu unaagiza kwamba, waislamu wafanye kila wawezalo kutafuta elimu hata kama itawabidi kusafiri mbali kama China kwa ajili ya kutafuta elimu. Ni dhahiri Uislamu jinsi unavyotetea elimu, hasa tukizingatia kwamba aya yake ya kwanza tu kushuka inazungumzia elimu kama alama ya uongofu. Imetajwa katika Qur’ani: “Soma! Kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu. Soma! Na Mola wako ni Mkarimu sana, ambaye amemuelimisha mwanaadamu kwa njia ya kalamu. Amefundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui.” (96:1-5).

Kisha amesema tena: “(Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehma; amefundisha Qur’ani, amemuumba mwanadamu, akamfundisha kusema (kwa ufasaha).” (55:1-4). Elimu katika Uislamu haikuwekewa mipaka ya kusoma kitabu maalum au mtunzi maalum tu, bali inahusisha chochote kile ambacho akili inahitajia kusoma na kuongeza mbinu mbalimbali za maarifa. Amirul-Mu’minin, aliwataka Waislamu kuwafunza watoto wao hata kuogelea, kutupa mishale na kutoa shoti farasi. Kutupa mishale na kupanda farasi ilikuwa ndiyo burudani (kubwa) ya maisha yote ya Waarabu zama hizo, na lau Amirul- Mu’minina angeishi hivi leo, basi angeongezea mengine mengi katika hayo aliyoyasema, (kama kompyuta n.k) ili yaende sambamba na wakati na hali ya mabadiliko ya jamii katika maisha ya kisasa.

v. Umuhimu wa vidude vya kuchezea watoto (toys) katika Uislamu Vijidude vya kuchezea na michezo mbali mbali (toys), vinaleta furaha na burudani katika maisha ya mtoto. Vijidude hivyo pia hupanua akili ya mtoto ya kielimu. Mtume (s.a.w.) amesema: “Mwenye kwenda sokoni, na akanunua kitu cha kuchezea (watoto) akakichukua mpaka kwa watoto wake, huwa ni kama aliyechukua sadaka na kuwapelekea watu wahitaji, basi na aanze kuwapatia watoto wa kike kwanza kabla ya watoto wa kiume.” Umuhimu huu alioupa Mtume (s.a.w.) kuhusiana na vitu vya kuchezea sijambo la kupuuzwa, kwani kufanya hivyo ni muhimu kama kutoa sadaka kwa wahitaji.

Imeelezwa kwamba watoto wa kike wapatiwe kwanza, ili kuwaridhisha na kuwafurahisha. Haya ndiyo mambo ambayo Uislamu unayapigania ambayo lau tutayatafuta, maisha yetu na ya watoto wetu yatajawa na furaha na Baraka. Nguvu na uzuri wa misingi hii inatoa mfano mzuri kwa jinsi ilivyoamuru kuhusiana na watoto wetu - kiburudisho cha macho yetu.

Mtoto mwema huwa ni mwenye kuendeleza ufanisi wa baba yake, na ni hazina nzuri kwa taifa lake. Mtume (s.a.w.) amesema: “Mtoto mwema ni mrihani (mti wenye harufu nzuri) miongoni mwa mirihani ya Peponi.” Mwenyezi Mungu atuangazie na atuongoze katika kuwalea vizuri watoto wetu ambao ni furaha ya maisha yetu, Amin



SEHEMU YA TANO
Elimu ya afya, kimwili na kimazingira Imetajwa katika Qur’ani ya kwamba: “…..Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wenye kutubia na wenye kujitakasa…..” (2:222). Tirmidhy amepokea Hadith sahihi kutoka kwa Sa’ad ya kwamba Mtume amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwema, Mkarimu anapenda ukarimu, mpaji anapenda upaji, basi safisheni nyua (boma) zenu.” Imepokewa Hadith kutoka kwa Tabraniy ya kwamba Mtume (s.a.w.) amesema: “Usafi unalingania kwenye imani, na mwenye imani hufuatana na Muumini hadi Peponi.”


1. Umuhimu wa Usafi
Unadhifu katika Uislamu unalingana na utakaso, na kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu unahusiana na usafi wa mwili, mavazi na makao. Usafi daima umekuwa ukitajwa katika Qur’ani kwa zaidi ya mara thelathini. Mwenyezi Mungu amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wenye kutubia na wenye kujitakasa.” (2:222). Amesema tena: “Ewe uliyejifunika nguo, simama na uonye. Na Mola wako umtukuze, na nguo zako uzisafishe.” (74:1-4). Amesema tena: “…..Mwenyezi Mungu hapendi kukutieni kwenye uzito; bali anataka kukutakaseni.….”(5:6). Habari ya usafi pia imekuja katika Hadith nyingi, k.v. Mtume (s.a.w.) amesema: “Haikubaliwi Swala yoyote pasi na tohara.” Amesema tena: “Tohara ndiyo ufunguo wa Swala.” Hadith zote hizi zinaonyesha kwa kiasi gani Uislamu unavyothamini na kuhimiza usafi, na kuuchukulia kuwa ndiyo chimbuko la uzuri na wema. Afya, usafi, na umaridadi wa binaadamu ni miongoni mwa mambo ambayo Uislamu unayatilia mkazo sana na kuyachukulia kuwa ni mambo makuu katika ujumbe wake Mtukufu.

Mtu hahesabiwi kuwa ni Mwislamu wa kweli iwapo hatasafisha mwili wake, ama hatajiepusha na uchafu na nongo, iwe ni katika chakula, kinywaji, mavazi ama katika mazingira yake yote kwa jumla. Afya na unadhifu si kwa ajili ya faida za kimwili tu, bali pia una manufaa makubwa kwa kutakasa nafsi na kumwezesha mtu kufanya kazi barabara maishani.

2. Usafi na Swala
Uislamu umeheshimu mwili wa mwanaadamu kwa kulazimisha usafi wa mwili uwe mwanzo wa kila swala. Na inajulikana kwamba tabia yoyote kwa kawaida huzoeleka kutokana na kuifanya mara kwa mara. Uislamu umefanya ‘wudhu’2 kuwa ndiyo nguzo ya muhimu sana na ya wajibu kwa Swala. ‘Udhu’ ni neno la Kiarabu lenye maana ya ‘usafi’ na halikuja kwa maana ya kujisafisha kwa maji tu, bali pia kwa kujitakasa kimwili kutokana na maovu. Tumuombapo Mungu wakati wa Swala, basi ni wajibu tuwe wasafi na tohara.

Kuweza kuhifadhi wudhu si jambo rahisi, kwa hivyo, wale wanaoweza kufanya hivyo wanahesabiwa kuwa ni waumini hasa. Mtume (s.a.w.) amesema: “Hakuna awezaye kuhifadhi wudhu ila Muumin.” Hii si ajabu tukizingatia kwamba Uislamu umeufanya ‘wudhu’ kuwa ndiyo ufunguo katika ibada yake kubwa ambayo ni Swala. Na hakuna Swala yoyote itakayokubaliwa kwa Mwislamu mpaka mwili wake, nguo, na mahali anaposalia pawe safi. “Yeyote miongoni mwenu atayetawadha, kisha asome dua: ‘Nashuhudia ya kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa ila Mwenyezi Mungu, nijaalie niwe miongoni mwa wenye kutubia na wenye kujitakasa’, basi mtu huyo hufunguliwa milango minane ya Pepo, ili aingie mlango wowote autakao.”

3. Usafi wa mikono
Kutokana na ukweli kwamba mikono yetu ndiyo mara kwa mara twaitumia kugusia vitu mbali mbali, ndipo Uislamu ukatutaka tuioshe kabla na baada ya chakula na pia wakati wa kutawadha. Kuhusiana na suala la kuweka mikono katika hali ya usafi, Mtume (s.a.w.) amesema: “Atakapolala mmoja wenu na katika mikono yake pana harufu ya nyama na kikimpata cha kumpata, basi na asilaumu ila nafsi yake.” Amesema tena: “Atakapoamka mmoja kutoka usingizini, na aoshe mikono yake.” Ni lazima ikumbukwe kwamba kula kabla ya kuosha mikono yetu, ni njia rahisi ya kueneza maradhi. Ni lazima tuwalazimishe watoto wetu 2 Wudhu: kujisafisha uso, mikono, kichwa na miguu kabla ya kuswali – maarufu kwa jina la ‘kutawadha’. 
kufuata kile kilichoamrishwa katika Uislamu kuhusiana na ulazima wa kuosha mikono vizuri kabla na baada ya kula. Mtume (s.a.w.) hakutuhimiza tuoshe mikono tu, bali ametuhimiza kukata kucha pia. Kupunguza kucha ni lazima kwa sababu ya kukusanyika uchafu na vumbi ndani yake ambavyo vinaweza kuleta madhara makubwa. Mtume (s.a.w.) amesema: “Punguzeni kucha zenu.”

4. Usafi wa kichwa
Mtume (s.a.w.) amesema: “Yeyote yule mwenye nywele na azitunze vizuri.” Kwa hivyo, wazazi wanapaswa kuwafunza na kuwaongoza watoto wao mara kwa mara waviweke vichwa vyao katika hali ya usafi na kuzitengeza nywele zao vizuri kwa kuziangalia kila mara. Wazazi ni lazima wawafafanulie watoto wao ukweli kwamba usafi ni sehemu ya dini. 

5. Usafi wa macho
Kwa kuwa macho ni kiungo nyeti, yamekuwa ndiyo mepesi sana kudhurika miongoni mwa viungo vyote vya mwili, hivyo basi yanastahili kutunzwa kwa uangalifu mno, na kusafishwa barabara. Kuyasafisha kwenyewe kusifanywe moja kwa moja kwa kutumia vidole, kwani vinaweza kuwa si visafi, na hivyo kuyaletea madhara. Iwapo inzi watalivamia jicho, basi ni lazima watimuliwe haraka. Mtume (s.a.w.) siku zote alikuwa mwangalifu sana kwa macho yake, na daima alikuwa akiwahimiza watu kufanya hivyo. Imepokewa Hadith kutoka kwa Aisha (mkewe), amesema: “Mtume (s.a.w.) alikuwa na wanja-manga aliokuwa akijipaka kila jicho mara tatu kabla ya kulala.”

6. Usafi wa pua
Uislamu umetilia mkazo hasa usafi wa pua mpaka ukafanya kuisafisha ni moja katika shuruti za wudhu. Inatakiwa kwa Muislamu atakapotawadha, kuingiza maji puani kisha kuyapenga, kwani hiyo ndiyo njia bora ya kusafisha pua, na afanye hivyo mara tatu.

7. Usafi wa mdomo (kinywa)
Uislamu umetuagiza tusukutue kwa maji wakati wa kutawadha na kupiga mswaki (kabla ya wudhu) na hivyo kutuwekea msingi wa kuyahifadhi meno yetu yawe na afya nzuri. Mtume (s.a.w.) mara kwa mara aliwahimiza waislamu kusafisha meno wakati wa kutawadha, na nyakati zingine pia. Mtume (s.a.w.) amesema: “Lau si kuwaonea uzito umma wangu, ningewaamrisha kupiga mswaki katika kila Swala.” Amesema tena: “Kupiga mswaki kunatakasa mdomo.”

8. Usafi wa nguo
Imetajwa katika Qur’ani: “Na nguo zako uzisafishe.” (74:4). Pia imetajwa: “Chukueni mapambo yenu wakati wa kila Swala.” (7:31). Mtume (s.a.w.) amesema pia: “Vaeni nguo nyeupe miongoni mwa nguo zenu, kwani hizo ndizo bora ya nguo zenu.” Kutokana na Hadith iliyopokewa na Jabir bin Abdallah, inasemekana siku moja Mtume (s.a.w.) alimuona mtu mmoja akiwa amevaa nguo chafu, akasema (s.a.w.): “Hivi (mtu huyo) hakupata maji ya kufua nguo zake?” 
Uislamu pia umeshauri mtu kuonekana msafi na maridadi awapo katika mkusanyiko wa watu kama vile katika Swala ya Ijumaa na wakati wa sikukuu. Imepokewa Hadith kutoka kwa Abu Dawud, Mtume (s.a.w.) amesema: “Yeyote kati yenu akiwa na uwezo, aweke nguo mbili maalum kwa ajili ya siku ya Ijumaa, zisizokuwa zile afanyiazo kazi.”

9. Usafi wa nyumba
Uislamu umetuhimiza kuziweka nyumba zetu katika hali ya usafi, kwa kufanya hivyo, waislamu watakuwa kielelezo cha kuonyesha kuwa usafi ni jambo la kuzingatiwa sana katika Uislamu, na ndilo lenye kuwapambanua kati yao na wengineo. Imepokewa Hadith kutoka kwa Tirmidhiy, Mtume (s.a.w.) amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwema, anapenda mambo mema, Mzuri anapenda mazuri, Mkarimu anapenda ukarimu, Mpaji anapenda upaji basi zisafisheni nyua (boma) zenu.”

10. Kufanya iktisadi katika matumizi ya maji
Imepokewa Hadith kutoka kwa Ibn Sa’ad: “Siku moja Mtume (s.a.w.) alipita nyumbani kwa Saad naye alikuwa akitawadha (huku akimwaga mwaga maji) akamwambia: “Ewe Saad! Israfu iliyoje hiyo uifanyayo?” Akasema Saad: “Je katika maji pia pana israfu?” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Ndio hata ukiwa katika mto upitao.” Umuhimu hasa wa maji na haja ya kuyatumia kwa iktisadi (kubana matumizi yake) uko dhahiri, kwa kuelewa kwamba Mwenyezi Mungu ameyajaalia maji kuwa ni asili ya maisha na kuwako kwa mwanaadamu. Mwenyezi Mungu amesema katika Qur’ani: “…..Na tukajaalia, kutokana na maji, kila kitu kilicho hai…..” (21:30). 

11. Usafi wa chakula na maji
Imepokewa Hadith kutoka kwa Abu Qataada isemayo kwamba, Mtume (s.a.w.) amekataza watu kupumua ndani ya mabakuli ama vikombe vyao wakati walapo au wanywapo, kukataza huko ni kwa ajili ya kuepukana na uchafuzi wa maji au chakula unaoweza kusababisha maradhi chungu nzima.

12. Makatazo ya kwenda haja ndogo kwenye maji yaliyotulia au kutuwama
Uislamu umelinda haki za kila mmoja kwa kutoruhusu mtu yeyote kutia uchafu wake wa mwili (kinyesi, mkojo n.k.) kwenye vyanzo (chemchem) vya maji. Imepokewa Hadith kutoka kwa Jabir ya kwamba Mtume (s.a.w.) amekataza kwenda haja ndogo kwenye maji yaliyotuama. Na katika Hadith nyingine amesema: “Asikojoe kabisa mmoja wenu katika maji yaliyosimama, kisha akaoga humo.”

Kanuni za iktisadi za Uislamu hazikuishia hapo tu, bali zimetukataza pia kukojoa katika kibwabwa cha kuogea. Imepokewa kutoka kwa Abdullah Ibn Mughaffal, Mtume (s.a.w.) amesema: “Asikojoe, tena asikojoe kabisa mmoja wenu ndani ya kibwawa cha kuogea kisha akaoga humo.” Kwa hivyo tunapaswa kuwakanya watoto wetu wasiyachafue maji ili kuzihifadhi afya zetu ziwe katika hali njema. Pia ni lazima tutambue ukweli kwamba, kukojoa ndani ya maji ni kuyachafua, kuyafanya yasifae kwa matumizi, na kuyafanya kuwa chanzo cha maambukizo na maradhi.

13. Makatazo ya kukojoa majabalini na maweni
Uislamu umeheshimu na kulinda haki za mwili wa binaadamu kwa kuzuia uchafu utokanao naye ili usilete uchafuzi na madhara. Imepokewa Hadith kutoka kwa Abdallah bin Sargas kwamba, Mtume (s.a.w.) alimkataza mtu kukojoa juu ya mawe ili mkojo usije ukamrukia. Mtume (s.a.w.) amekataza pia kukojoa juu ya ardhi ngumu.

14. Mambo matatu yaliyolaaniwa
Imepokewa Hadith kutoka kwa Muadh bin Jabal, Mtume (s.a.w.) amesema: “Ogopeni mambo matatu yaliyolaaniwa; kuenda haja mahali papitapo maji (au chemchem), mahali papitapo watu, na mahali penye kivuli.” Hadithi hiyo iliyotangulia pia ameithibitisha Ibn Abbas aliposema: “Nimemsikia Mtume (s.a.w.) akisema: “Ogopeni mambo matatu yaliyolaaniwa.” Akaulizwa: “Ni mambo gani hayo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akajibu: “Ni mtu kwenda haja kubwa mahali penye kivuli panapopumzika watu, au njiani (papitapo watu), au penye chemchem ya maji.” Tuliweka pamoja pia jambo hilo hilo, kuna Hadith ambayo Mtume (s.a.w.) amesema: “Ogopeni mambo matatu yaliyolaaniwa.” Maswahaba wakamuuliza: “Je ni mambo gani hayo?” Akawajibu: “Wakati mtu anapokwenda haja (ndogo au kubwa) penye njia ipitayo watu, au kivulini.”

Kutokana na maelezo yaliyotangulia, ni wazi kwamba kwenda haja kubwa ama ndogo kumekatazwa iwe ni katikati ya barabara au pembeni, kwa kuongezea ni kwamba, makatazo hayo yanahusu kila mahali patumiwapo na watu kwa ajili ya kujistiri (na mvua, jua, n.k.) au mahali papitapo watu (barabarani), pia yanahusu kwenye chemchem za maji na mikondo yake. Makatazo yote hayo ni kuwaepusha watu na kuwalinda kutokana na madhara makubwa yanayoweza kuwapata.

Kwa hivyo ni wazi kwamba, yeyote atakayefanya mojawapo kati ya mambo hayo ya laana, basi amelaaniwa na Mwenyezi Mungu. Laana hizo mbili mwanzoni zinarejea katika kufuatia vitendo hivyo vilivyobainishwa ambavyo hulaaniwa watendaji wake duniani na akhera.

15. Usafi wa barabara
Jukumu la Uislamu ni kuwalinda waislamu katika vitendo vyao vyote. Kwa hivyo unazingatia kwamba miongoni mwa haki zao ni kutopatwa na madhara yoyote wanapokuwa wakipita njiani. Ametaja Imam Muslim katika Sahih yake, kutokana na Hadith iliyopokelewa na Abi Said al-Khidr; Mtume (s.a.w.) amesema: “Tahadharini na kuketi mabarazani.”

Maswahaba wakasema: “Lakini sisi twalazimika kuketi kuzungumza mambo yetu.” Mtume (s.a.w.) akawaambia: “Ikiwa hapana budi mketi, basi ipeni hiyo njia haki yake.” Wakamuuliza: “Ni zipi hizo haki za njia?” Akawajibu: “Haki za njia ni kufumba macho (kutoangalia yasiyofaa), kutowaudhi wapita njia, kuitikia salaam, kuamrishana mema na kukatazana maovu.”

Tukizingatia Hadith hii inatudhihirikia kwamba, Mtume (s.a.w.) anatuongoza ili tushikamane na mojawapo ya amri zake kuu ambazo ni za wajibu wakati wowote na mahali popote. Amri hii kuu, inayotawala na kusimamia hali za kukaa njiani, inategemea ukweli kwamba, barabara ni mali ya watu wote na kila mtu hufaidika kutokana na matumizi yake. Mtume (s.a.w.) ametuamuru kujiepusha na kuwabughudhi wapita njia, iwe ni kwa mkono, ulimi, jicho ama kwa njia yeyote nyingine ijulikanayo, na kwamba Muislamu hasa ni yule ambaye Waislamu wenzake watasalimika kutokana na (shari ya) ulimi wake na mikono yake.

Iwapo mtu ataketi barazani, basi hafai kukaa hapo kwa ajili ya kusema uongo, udaku, kula njama au kuwadhihaki wapita njia. Jambo hili pia limeelezwa kwenye Hadith ifuatayo ilivyotajwa na Bukhari, Mtume (s.a.w.) amesema: “Bwana mmoja alipokuwa akitembea njiani, aliona tawi la miba njiani, akaliondoa, Mwenyezi Mungu akafurahikia kitendo hicho na akamsamehe.”

Vile vile, mtu yeyote atakayezingatia usafi wa barabara na akajiepusha na kuwabughudhi wapita njia, basi hupewa ahsante kwa juhudi yake na Mwenyezi Mungu humlipa kwayo. Kwa kuongezea, mtu huyu pia hupata shukrani za watu kwa vitendo vyake hivyo. Amesema Mtume (s.a.w.): “Huwa kila jema alifanyalo binaadamu ni sadaka. Kumsalimia anayeku- tana naye ni sadaka. Kuamrisha mambo mema ni sadaka, kukataza maovu ni sadaka, kuondoa uchafu njiani ni sadaka na kuwanunulia vitu familia yake pia ni sadaka.” Mtume (s.a.w.) amesema: “Imani ni kiasi cha vifungu sitini au sabini, kifungu cha chini ni kuondoa uchafu njiani, na cha juu kabisa ni kusema ‘Laa ilaaha illa llah’ (Hapana mola apasaye kuabudiwa ila Allah).”

Amesema Mtume (s.a.w.): “Nilidhihirishiwa amali za umma wangu zilizo nzuri na zilizo mbaya, miongoni mwa amali nzuri ni kuondoa uchafu njiani, na amali mbaya ni kuacha uchafu wa makohozi msikitini.” Amesema Mtume (s.a.w.): “Atakayeondosha uchafu kutoka katika njia ya Waislamu, huandikiwa jema, na yeyote atakayekubaliwa jema lake huingia Peponi.”

Imetajwa na Abu Shibu al-Harawi, Hadith inayofanana na hiyo kwamba, siku moja Mu’adh alikuwa akifuatana na mwenzake, mara akarejea nyuma ili kuondoa jiwe lililokuwa njiani, yule mwenzake akamuuliza: “Kwa nini kufanya hivyo?” Muadh akajibu, “Nilimsikia Mtume (s.a.w.) akisema: “Atakayeondoa jiwe njiani huandikiwa jema, na atakayekuwa na jema, huingia Peponi.” Anas bin Malik amesema pia: “Palikuwa na mti uliokuwa umezuia njia ya watu wapitao, kisha alikuja bwana mmoja na kuuondosha njiani hapo. Basi Mtume (s.a.w.) siku moja alisema kuhusu habari ya bwana huyo kwamba “Nimemuona Peponi akicheza kivulini.”

Kuna misemo na Hadith zingine mbali mbali zinazoonyesha umuhimu wa kuziweka barabara katika hali ya usafi na kufuata haki za njia ili kuepukana na matatizo yake.

Ingelikuwa ni vizuri kuwapa mafunzo haya watoto wetu ili waweze kuendeleza heshima kwa ajili ya haki za barabara. Kwa njia kama hiyo, tunaweza tukasema kwamba, Uislamu tayari umeshaweka kanuni zinazohusiana na haki za usalama barabarani ili zihifadhike kutokana na machafuko ya ghasia. 

ORODHAYA VITABU VILIVYO CHAPISHWA NA AL-ITRAH FOUNDATION:
1. Qur'an Al-Kariim - Tafsir Al-Kashif Juzuu ya kwanza mpaka
kumi na Tisa
2. Uharamisho wa Riba
3. Uharamisho wa uwongo Juzuu ya kwanza
4. Uharamisho wa uwongo Juzuu ya pili
5. Hekaya za Bahlul
6. Muhanga wa Imamu Husein (A.S.)
7. Mikingamo iliyomzunguka Imamu Ali (A.S.)
8. Hijab vazi Bora
9. Ukweli wa Shia Ithnaashari
10. Madhambi Makuu
11. Mbingu imenikirimu
12. Abdallah Ibn Saba
13. Khadijatul Kubra
14. Utumwa
15. Umakini katika Swala
16. Misingi ya Maarifa
17. Kanuni za Ndoa na maadili ya Familia
18. Bilal wa Afrika
19. Abudharr
20. Usahihi wa Historia ya Uislamu na Waislamu
21. Salman Farsi
22. Ammar Yasir
23. Qur'an na Hadithi
24. Elimu ya Nafsi
25. Yajue Madhehebu ya Shia
26. Ukusanyaji na Uhifadhi wa Qur'an Tukufu
27. Al-Wahda
28. Ponyo kutoka katika Qur'an
29. Uislamu mfumo kamili wa maisha ya kijamii
30. Mashukio ya Akhera
31. Al Amali
58
Malezi ya Watoto katika Uislamu
32. Dua Indal Ahlul Bayt
33. Udhuu kwa mujibu wa Kitabu na Sunna
34. Haki za wanawake katika Uislamu
35. Mwenyeezi Mungu na sifa zake
36. Amateka
37. Nafasi za Ahlul Bayt (a.s)
38. Adhana.
39 Upendo katika Ukristo na Uislamu
40. Nyuma yaho naje kuyoboka
41. Amavu n’amavuko by’ubushiya
42. Kupaka juu ya khofu
43. Kukusanya swala mbili
44. Bismillah ni sehemu ya Qur’ani na husomwa kwa Jahara
45. Kuwaongoza vijana wa kizazi kipya
46. Kusujudu juu ya udongo
47. Maulidi
48. Tarawehe
49. Malumbano baina ya Sunni na Shia
50. Kupunguza swala safarini
51. Kufungua safarini
52. Kuzuru makaburi
53. Umaasumu wa Manabii
54. Qur’an inatoa changamoto
55. Tujifunze misingi ya dini
56. Nahjul Balagha Sehemu ya Kwanza
57. Nahjul Balagha Sehemu ya Pili
58. Dua Kumayl
59. Uadilifu wa masahaba
60. Asalaatu Khayrunminaumi
61. Sauti ya uadilifu wa binadamu
62. Umaasumu wa Mitume Sehemu ya kwanza
63 Maswali na Mishkili Elfu Sehemu ya kwanza
64. Umaasumu wa Mitume Sehemu ya tatu
65. Umaasumu wa Mitume Sehemu ya pili
66. Maswali na Mishkili Elfu Sehemu ya pili
67. Maswali na Mishkili Elfu Sehemu ya tatu
68. Sala ni nguzo ya dini

BACK COVER
Ni jamii ile tu inayoweza kufikiriwa yenye bahati ambayo ina watu wachamungu, wenye tabia nzuri, wawajibikaji na waaminifu. Ili kuunda jamii kama hiyo na kupata watu kama hao, ni muhimu kutegemea kwenye malezi sahihi na mafunzo ya watoto kwa ajili ya mustakabali wao. Kwa kawaida, watu huangalia na kuwachukulia watoto kijuujuu tu.

Hawazingatii kwenye mafunzo yao sahihi, ingawa ukweli ni kwamba watu wa leo ni watoto wa jana na watoto wa leo ni watu wa kesho.

Mtoto ambaye hapati mafunzo sahihi wakati wa utoto na ujana wake hawezi kutegemewa kukua kama mtu mchamungu kiasi cha kuweza kuwa mwenye manufaa katika jamii yake.

Katika kitabu hiki, malezi ya watoto yameelezewa vizuri kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu - Uislamu ambao ni dini na mfumo wa maisha. Kimetolewa na kuchapishwa na: Al-Itrah Foundation

1 comment:

  1. Nao ni upande unaolenga kutia nguvu Imani ya mja kwa Mola wake, kupitia kujua majina ya Mwenyezi Mungu na sifa Zake, na kuwatanabahisha watu watazame alama za Mwenyezi Mungu katika ulimwngu Wake, jambo ambalo litapelekea kuzifungamanisha nyoyo za waja na Mola wao kwa kumtegemea Yeye na kuogopa mateso Yake na kutaraji malipo mazuri kutoka Kwake, ili mja aishi maisha ya utulivu yaliyojaa Imani na kuridhika

    ReplyDelete

Twitter Bird Gadget