Monday, February 20, 2012

Ubora wa kupiga mswaki


Mswaki ni miongoni mwa Sunnah nzuri ambazo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ametuachia na kusema: “Lau si ugumu ambao Ummah wangu ungepata ningeweka ulazima wa kupiga msuwaki kabla ya kila wudhuu” (Maalik, Abu Daawuud, ash-Shaafi’iy, al-Bayhaqiy na al-Haakim).

Msuwaki unaweza piga katika sehemu nyingi kwa mfano chooni, Msikitini wakati unatawadha, unapoingia nyumbani, pia chumbani. Hata hivyo, ukipiga chumbani mtu ahakikishe kuwa hajachafua kwa kutema mate au vinavyotoka mdomoni ovyo ovyo. ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema:Kitu cha kwanza ambacho Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya anapoingia nyumbani ilikuwa ni kupiga msuwaki (Muslim).

Kwa kawaida, msuwaki wenyewe huwa na dawa lakini ukitaka kutia dawa kwa juu hakuna shida yoyote ile. Utumiaji huwa ni kwa utumiaji wa kijiti au kitu chengine chochote kusafisha meno yake. Kitu bora cha kusafishia meno ya mmoja wetu ni kijiti cha mti wa arak ambao unapatikana Hijaaz. Ada hii ya utumiaji wa msuwaki huimarisha ufizi, hulinda meno kuoza na magonjwa ya meno, inasaidia usagaji wa chakula na kusahilisha utokaji wa mkojo. ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Msuwaki unasafisha mdomo na unampendeza Mola” (Ahmad, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy).

Utumiaji wa msuwaki unapendeza kila wakati, lakini zipo nyakati nyingine ambazo inapendeza zaidi haswa nyakati zifuatazo:

  1. Wudhuu,
  2. Swalaah,
  3. Usomaji wa Qur-aan,
  4. Unapoamka, na
  5. Pindi ladha yam domo inapobadilika. Wasiofunga au waliofunga wanaweza kutumia bila ya tatizo lolote. Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatumia msuwaki na huku amefunga (Ahmad, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).

Ni Sunnah kuuosha msuwaki baada ya kupiga, amesema hilo ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu ‘anha), “Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam)
Alipomaliza kutumia msuwaki, alikuwa ananipatia mimi. Nilikuwa nauosha, nautumia, nauosha tena, kisha namrudishia” (Abu Daawuud na al-Baihaqiy).

Na pia Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kutuonyesha umuhimu wa msuwaki amesema: “Mambo kumi ni katika fitrah: … kupiga msuwaki, …” (Muslim na Abu Daawuud).

Ni muhimu umfundishe mtoto wako kuwa mtu anaweza kupiga msuwaki mahali popote bora tu achunge usafi la sivyo, basi mtoto atakuwa anapiga chooni peke yake na akifika Msikiti hatakuwa na hamu wala motisha ya kupiga.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget