Tuesday, February 28, 2012

Tahadhari ya Tanzania na Al Shabbab

Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu nchini, imeihadharisha Serikali kutojihusisha na mambo ya kidini hasa yanayohusu kundi la Al-shaabab kwa shinikizo la mataifa makubwa.

Katibu wa kamati hiyo, Shekhe Ponda Issa Ponda, aliyasema hayo Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari.

Alisema kamati hiyo imemwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, kupinga kauli yake aliyowataka Watanzania kuwa makini na wahamiaji haramu ili kudhibiti kundi hilo lisiingie nchini.

Shekhe Ponda alisema ni vyema Serikali ikawa makini na sera za mataifa makubwa ambayo yameingia katika migogoro na baadhi ya nchi za Afrika kwa maslahi binafsi, “Serikali iache kujiingiza katika migogoro na kundi hili, jambo la msingi ni kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu si vinginevyo,” alisema Shekhe Ponda na kuongeza kuwa, si kweli kwamba kundi hilo ni la kigaidi kama alivyosema Nahodha bali kinachofanywa na kundi hilo ni kulinda mipaka ya nchi yao.

Alisema Nahodha hapaswi kuwaweka Watanzania katika hofu ya kuvamiwa na kushindwa kusafiri kwa shughuli mbalimbali ambazo ndioz huwapatia kipato na kukuza uchumi wao kutokana na taarifa za upotoshwaji dhidi ya kundi hilo, “Waziri anapozungumzia kundi hili ni sawa na kudhalilisha Uislamu, mbona hivi karibuni wameingia Wakongo wakiwa na silaha nzito lakini Serikali haikufanya kitu, kwanini Al-Shaabab,” alihoji Shekhe Ponda.

Ponda alisema kauli iliyotoa Nahodha, imelenga kuwagawa Watanzania ili waichukie nchi ya Somalia kitu ambacho si sahihi.

Hivi karibuni, Waziri Nahodha alisema kutokana na nchi jirani ya Kenya kukumbwa na vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na kundi hilo, umefika wakati wa Watanzania kuwa makini na watu ambao wanaingia nchini kinyemela bila kufuata utaratibu.

taarifa via Majira
UPDATE ya tamko rasmi:
Bismillahir Rahmanir Rahiim
KUMB: KKHWT/WMN/1/011
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
S.L.B 2217 Dar es Salaam Tanzania.

YAH: TAHADHARI KWA TANZANIA KUTUMIWA NA MAREKANI DHIDI YA UISLAMU KATIKA SUALA AL-SHABAB
Ndugu Waziri Tarehe 16.11.2011 ulikutana na vyombo vya habari. Lengo ilikuwa ni serikali kutoa tahadhari ya uwezekano wa nchi kushambuliwa na wapiganaji wa Al-Shabab wa Somalia. Wiki tatu kabla, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania naye alitoa tahadhari kama hizo. Katika suala la majeshi ya Kenya kuivamia Somalia Serikali ya Tanzania ilipongeza hatua hiyo.

Sababu zilizo tolewa na serikali katika tahadhari hiyo ni 5:
1. Al-Shabab ni magaidi.
2. Al-Shabab wameshambulia Kenya mara 3.
3. Watanzania wanadhaniwa kujiunga na Al-Shabab
4. Tanzania imekamata ‘wahamiaji haramu’ kutoka Somalia.
5. Al-Shabab wamesababisha ukosefu wa ajira Somalia na hatimaye vijana
wamechagua ugaidi kama ajira

UKWELI KUHUSU AL-SHABAB NA SOMALIA. Ndugu Waziri, Somalia ni nchi huru katika nchi za bara la Afrika.
Somalia ni nchi ya Waislamu kwa asilimi 99.
Kama zilivyo nchi nyingi duniani, imepita katika kipindi cha amani na vita.
Tafauti zinazoendelea Somalia ni tafauti za ndani na za kiutawala.

Somalia imekuwa na mpishano mkubwa wa utawala kama zilivyo nchi nyingine.Utawala ulio muhimu kwa muktadha wa sasa wa Somalia ni ule wa Rais Mohammed Siad Barre. Yeye aliongoza kwa kufuata siasa za mrengo wa magharibi mpaka alipoangushwa mwaka 1991. Utawala uliofuatia zilikua tawala za Koo. Tawala hizi ziliondolewa na Utawala wa Mahakama za Kiislamu. Utawala huu wa Kiislamu ambao uliripotiwa na mashirika ya kimataifa kurejesha amani kwa kiasi kikubwa katika maeneo kadhaa ya Somalia, ulidhoofishwa na mashambulizi ya majeshi ya uvamizi ya Marekani na Ethiopia. Ni kwa muktadha huo wapiganaji wa Somalia walijipanga upya kwa anuani ya Al-Shabab kulinda nchi yao dhidi ya uvamizi na kuendeleza utawala wa Kiislamu ulio asisiwa na Mahakama za Kiislamu.

UREJESHWAJI WA AMANI SOMALIAKatika hali inayoendelea Somalia, baadhi ya mataifa ya nje yalijipa jukumu la kuunda serikali mezani kwa kushirikiana na baadhi ya wasomali. Hatimaye serikali hiyo iliyoundwa nchini Kenya imepelekwa Somalia kwa msaada wa majeshi ya nchi hizo na kutangaza kuwa ndio serikali halali kwa wananchi. Matarajio yenye dhamira njema,yalikuwa ni kuona Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na wengineo wakiunga mkono amani iliyoanza kujitokeza Somalia chini ya Utawala wa Mahakama za Kiislamu.

Vilevile kupinga uvamizi wa Marekani na Ethiopia dhidi ya taifa huru. Matarajio mengine makubwa ilikuwa ni kuona mataifa na makundi yenye sifa ya uadilifu,yakielekea Somalia kutafuta amani kwa njia ya mazungumzo. Kigezo kikubwa kikiwa ni ridhaa ya wananchi walio wengi kwa mfumo wa utawala wanaoutaka wenyewe.

SIO HALALI KUIVAMIA SOMALIA. Somalia ni nchi huru ni dola ya wasomali wenyewe. Marekani bila ya ushahidi wa kisheria ndio walioanzisha propaganda za kuwahusisha mahasimu wao wakubwa Al-Qaida na Mahakama za Kiislamu na Al-Shabab nchini Somalia. Hatimaye Marekani ikaivamia kijeshi Somalia mpaka leo.

Katika hali ya kushangaza na inayo thibitisha ile dhana ya mataifa makubwa kufikiri kwa niaba ya mataifa ya Afrika, nchi za Burundi, Uganda, Ethiopia na hivi karibuni Kenya, nazo zimepeleka majeshi Somalia kwa tuhuma zile zile za Marekani. Mataifa hayo pia yanalazimisha kukubalika serikali iliyoundwa Kenya. Tanzania kwa upande wake ikijihusisha na mafunzo ya kijeshi kwa serikali iliyoundwa Kenya.

Ndugu Waziri jambo lingine la kuzingatia hapa ni kwamba, takriban nchi zote zilizo peleka majeshi Somalia, hazina amani katika nchi zao kutokana mashambulizi ya vikundi vinavyopinga serikali zao. Ajabu ya Mungu majeshi hayapelekwi katika nchi hizo kupambana na wapinzani wa serikali kama inavyofanywa kwa Somalia.
Ndugu Waziri, hatua hizi za Marekani na wapambe wake sio halali kwa kipimo chochote cha ukweli, utu, sheria, au hatua za kutafuta amani. Kwa muktadha huo utaona wasomali chini ya Al-Shabab wana kila sababu za kupambana na majeshi haya ya kigeni ima iwe ndani au nje ya Somalia na kufanya hivyo sio ugaidi bali ni hatua muhimu katika kulinda sio tu uhuru wa nchi yao bali uhuru wa Afrika nzima.

TANZANIA ISIJIINGIZE KIJESHI SOMALIA Pia isiwadhuru raia wake kwa propaganda za ugaidi.

Katika magereza yetu Tanzania wafungwa wana ‘vyeo’ visivyokuwa rasmi. Moja ya vyeo hivyo kinaitwa ‘kiherehere”. Huyu ni mfungwa ambaye ana tabia ya jambo lisilo muhusu kabisa lakini atajitahidi mpaka na yeye ahusike. Katika suala la Al-Shabab Tanzania inajitokeza kama ‘Kiherehere’.

Viongozi wa serikali ya Tanzania wanawashambulia Al-shabab bila hoja za msingi. Hoja za viongozi ni hizi zifuatazo: Al-Shababu ni magaidi, Al-Shabab wameshambulia Kenya,Watanzania wanadhaniwa kujiunga na Al-Shabab, Tanzania imekamata wahamiaji haramu kutoka Somalia, Al-Shabab wamesababisha ukosefu wa ajira Somalia na hatimae vijana wa wamechagua ugaidi kama ajira. Hoja hizi hazina mashiko.

Kwanini tupewe taarifa za wale tu wanaokwenda Somalia na sio kwengineko?. Na kama mtanzania shida yake imempeleka Somalia kujiunga na Al-Shabab iweje kosa liwe la Al-Shabab?.

Suala la nchi jirani kushambuliwa ni suala la ndani la nchi husika na aghlabu nchi zote tunazo pakana nazo zina matukio kama hayo. Mbona serikali ya Tanzania haijajitokeza kuvalia njuga mashambulizi ya kikundi cha Lord Resistance Arm kinacho uwa maelfu ya raia Uganda?. Mbona hatuja laani harakati za Mungiki wa Kenya?. Maimai wanapambana na serikali Kongo na huko Burundi na Rwanda nako kuna matukio kama hayo kila siku. Tanzania kama nchi inatakiwa kuimarisha ulinzi wa mipaka yake na matukio katika nchi jirani hayapaswi kubadilisha sera za ndani na nje ya nchi.

Hili la Tanzania kupokea wahamiaji wa kivita ni utaratibu wa kimataifa. Mwaka 2001, serikali ya Tanzania, ilipofanya mauwaji makubwa dhidi ya raia kule Pemba,Somalia kama nchi iliwapokea wakimbizi wa Tanzania. Wakimbizi hao mpaka leo wako Somalia wanatunzwa. Vipi wakimbizi wa Somalia wawe tishio kwa Tanzania na wakimbizi wa Tanzania wasiwe tishio kwa Somalia?. Katika kuthibitisha kuwa wakimbizi ni utaratibu wa kawaida, mwezi huu, Wakongo wakiwa na silaha za kivita wameingia na kupokelewa nchini mwetu. Ndio maana wananchi hawaja tahadharishwa wasiwasi wa nchi kuvamiwa na magaidi kutoka Kongo.

Ndugu Waziri, historia sahihi ya kuzaliwa Al-Shabab tumegusia huko nyuma. Suala la kukosekana kwa ajira kwa vijana wa Somalia hayo ni mambo ya kawaida kwa nchi maskini. Na kama ni kweli ulichosema, zingatia miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ukosefu wa ajira kwa vijana ni Tanzania. Je ni sahihi kusema moja ya viashiria vya kutokea ugaidi Tanzania ni serikali kushindwa kukidhi ajira kwa vijana?.

Hoja nzito mnayoitoa katika kuwashambulia Al-Shabab ni ugaidi. Hivi kweli Tanzania mnao ushahidi wa kisheria unao thibitisha kuwa Al-Shabab ni magaidi?. Au bwana mkubwa Marekani akisema Al-shabab au kikundi fulani ni magaidi basi huo ni ushahidi tosha kwa Tanzania?. Hivi siku moja Marekani akiwageukia wakatangaza kuwa Chama kinachounda serikali CCM ni magaidi, mtakua na uso gani wa kuwaambia raia kuwa walichosema Marekani ni uongo?.

Ndugu Waziri kwa jinsi mlivyojitokeza katika suala hili wasiwasi wetu mkubw na huenda tayari Tanzania imeburuzwa na Marekani na sasa mnatafuta uhalali wa kupeleka rasmi majeshi Somalia. Tunatumia fursa hii kuwatahadharisha na kuwashauri muachane kabisa na agenda zinazoweza kuitumbukiza nchi katika
madhara makubwa yasiyokuwa ya lazima. Kama mmepeleka majeshi Somalia yarudisheni na kama hamjapeleka msipeleke. Aidha raia wasitiwe misukosuko kwa sababu tu ya kuwaridhisha wakubwa.

MSIMAMO WA WAISLAMU KUHUSU AL-SHABABHawa ni walinzi na wapiganaji wa Kiislamu walio tangaza wazi dhamira yao ya kulinda uhuru wao na kusimamisha mfumo wa utawala wa Kiislamu nchini mwao. Msimamo huu ni agizo la Qur’an Tukufu na historia inathibitisha Mtume wetu Muhammad (SAW) alitekeleza agizo hili kwa ufanisi mkubwa. Hatua yoyote ya kuwashambulia Waislamu wenye msimamo kama huu, hayo ni mashambulizi ya kiitikadi dhidi ya Uislamu na Waislamu wote duniani.

Serikali inapaswa kufahamu kuwa sehemu kubwa ya raia wa Tanzania ni Waislamu,tena wanao fahamu na kufuatilia kwa makini sera na siasa za ndani na nje za Tanzania.

Ndio maana tunawapa nasaha kwamba, kama ambavyo serikali ya Tanzania haikutangaza uadui na Rais Frederick Chiluba alipotangaza Zambia kuwa dola ya kikristo, na kama ambavyo haikutangaza uadui na kikundi cha Lord Resistance Arm kinachodai kutaka kusimamisha utawala wa Kikristo Uganda, na kama ambavyo haikutangaza uadui na Tume ya majeshi ya Kanisa nchini Tanzania, basi vile vile hapashwi kutangaza uadui na Waislamu wanaojitetea na kulinda utawala wa Kiislamu tena nchini Somalia.

SHERIA YA UGAIDI TANZANIA Ndugu Waziri utakumbuka mwaka 2002 Tanzania ilijadili muswada wa sheria iliyodaiwa ya kupambana na ugaidi. Bila shaka ulishuhudia upinzani mkali kutoka kwa makundi muhimu yakiwemo ya Waislamu, wanasiasa na wanasheria bobezi. Moja ya sababu zilizopelekea kupingwa kwa muswada huo ni kufanana kwa 99% na ule uliounda sheria ya ugaidi ya Marekani. Sheria ya ugaidi ya Marekani haina uhuru kwa watuhumiwa wala ukomo kwa watendaji wanapo shughulikia kinachoitwa ugaidi.

Muswada huo pia ulikuwa unashughulikia makosa na adhabu ambavyo tayari vina shughulikiwa na sheria zilizopo. Kilicho watisha walio wengi ni kuwagawa watanzania kwani muswada ulikuwa unatazama hisia za Kiislamu kama ushahidi tosha wa makosa ya ugaidi kwa mtu, taasisi au jamii fulani. Na mwisho wa yote ilibainishwa jinsi sheria hiyo itakavyo pingana na Katiba ya nchi na vilevile kujenga fursa kwa mataifa makubwa kuingilia mambo ya ndani na kuvifanya vyombo vya usalama kuwajibika katika kulinda usalama wa mataifa hayo dhidi ya mahasimu wao. Pamoja na yote hayo,hatmae Desemba 14, 2002, Rais aliekuwepo madarakani alisaini muswada huo na kuwa sheria ya nchi. Toka kupitishwa kwa sheria hiyo Waislamu hapa nchini wamekuwa wakihujumiwa na kupata madhara makubwa.

RAIA NA PROPAGANDA ZA AL-SHABAB Tayari serikali ya Tanzania imeanza kuwakamata Waislamu kwa tuhuma za kujihusisha na Al-Shabab. Kabla ya hapo imekuwa ikizuwia shughuli mbalimbali za Kiislamu kwa tuhuma hizo. Watanzania wenye asili ya kisomali wanapekuli na kudhalilishwa na vyombo vya dola sehemu mbalimbali nchini. Serikali pia imekuwa ikizuia shughuli za vyama vya kijamii kwa madai ya uwezekano wa shughuli hizo kutumiwa na Al-Shabab.

Pamoja na muelekeo tuliouona huko nyuma lakini yaelekea kuna hujuma kubwa iliyoandaliwa nyuma ya pazia hili la ugaidi wa Al-Shabab dhidi ya baadhi ya raia wa Tanzania. Tunatahadharisha serikali isijiingize kabisa katika agenda za kidini za kitaifa au kimataifa. Ichukue tahadhari kubwa kwa mashinikizo na masharti ya mataifa makubwa ikiwemo Marekani.

Imetolewa na:
Sheikh
Ponda Issa Ponda
KATIBU

Nakala:
1. Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisia za Kiislamu (T)
2. Shura ya Maimamu Tanzania
3. Wanazuoni wa Kiislamu (HAY-YATUL-ULAMAA)
4. Jumuiya ya Maimamu Zanzibar
5. Jumuiya ya Uamsho (JUMIKI) Zanzibar
6. Wanataaluma wa Kiislamu (TAMPRO)
7. Idara ya Usalama wa Taifa
8. Mabalozi
9. Vyombo vya Habari


Source: http://www.wavuti.com/4/post/2011/11/kamati-ya-kutetea-waislamu-tanzania-yaihadharisha-serikali-kuhusu-wito-wake-dhidi-ya-al-shaabab.html#ixzz1ngLWIQiR

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget