Monday, February 20, 2012

Kunywa maji wima


Hakika zipo Hadiyth zinazokataza kunywa maji kwa kusimama na zipo nyingine zinazoruhusu.

Hadiyth zenyewe ni kama zifuatazo:

1.     Imepokewa kwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza kunywa kwa kusimama. Amesema Qataadah: Tukamuuliza Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Je, kula?” Akasema: “Hiyo ni mbaya zaidi au ni chafu zaidi” (Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy). Na katika riwaya yake nyengine: “Hakika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekemea kunywa kwa kusimama”.

2.     Na imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asinywe mmoja wenu kwa kusimama, na anayesahau basi ajitapishe” (Muslim).

3.     Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Nilimpa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) maji ya Zamzam akanywa huku amesimama (Al-Bukhaariy, Muslim, at-Tirmidhiy na an-Nasaaiy).

4.     An-Nazzaal bin Sabrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Alikuja ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwenye mlango wa Rahbah (sehemu pana iliyopo Kufah) na akanywa akiwa amesimama, na akasema: “Hakika mimi nimemuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifanya kamamunavyoniona nikifanya” (Al-Bukhaariy, Abu Daawuud na an-Nasaaiy).

5.     Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: Tulikuwa tukila katika zama za Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nasi twatembea na tukinywa nasi tumesimama (At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh. Pia imenukuliwa na Ahmad, Ibn Maajah na ad-Daarimiy. Isnadi yake ni Hasan).
6.     Na imepokewa kwa ‘Amru bin Shu‘ayb kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake (Radhiya Allaahu ‘anhum) ambaye amesema: “Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akinywa kwa kusimama na kwa kukaa” (At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh. Na imenukuliwa na Ibn Maajah na Isnadi yake ni Hasan. Pia ipo kwa Ahmad kwa njia nyengine kutoka kwa Ibn ‘Umar. Hivyo Hadiyth ni Sahihi).

Kulingana na Hadiyth tulizozitaja hapo juu ni wazi kabisa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekataza baadaye akaruhusu watu kufanya hivyo kwa matendo yake ya kunywa akiwa amesimama. Imaam an-Nawawiy amejaribu kuoanisha baina ya Hadiyth hizi katika kitabu chake “Riyaadhw asw-Swaalihiyn” kwa kuweka mlango alioupatia jina “Kubainisha kujuzu kunywa kwa kusimama lakini ubora ni kunywa kwa kuketi”
Na hiyo ndio rai ya Maulamaa wengi kuwa kunywa kwa kukaa ni bora zaidi kuliko kunywa kwa kusimama, ingawa hakuna uharamu wa kunywa kwa kusimama. Na ndiyo huenda Shaykh uliyemtaja amelisisitiza hilo la kunywa kwa kusimama kwa kumweka mtu katika usalama na ubora zaidi.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget