Friday, February 10, 2012

Hekima ya ruhusa ya ukewenza


KUNA sababu nyingi za kibinafsi, kimaadili, kiuchumi na kijamii zinazoonyesha kuwa wakati mwingine, kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo lilisilobudi. 

Hebu tujrejee mifano ya hali kadhaa zifuatazo:

Kama Mke ni Tasa
Mfikirie mwanamume ambaye amehakikisha kuwa mkewe ni tasa na bado anahamu ya kupata mtoto atakayekuwa mrithi wake. Katika hali hii mwanamume huyu atafanya mojawapo katika haya yafuatayo:
Atakaa na kusononeka kwa kukosa mtoto katika maisha yake yote au atamuacha huyu mke asiye zaa ili aoe mwingine anayezaa au
Atatembea na wanawake wengine nje ya ndoa ili wampatie watoto, japo kisheria si watoto wake au ataendelea kukaa na mkewe kwa mapenzi na furaha, kisha aoe mke mwingine atakaye mzalia watoto ambao watakuwa wake kisheria.
Utakuta, uchaguzi wa kuoa mke wa pili, ndio ulio bora kabisa. Wengi katika jamii ya Kiislamu, wameoa mke wa pili kwa sababu hii

Kama Mke ana maradhi ya kudumu
Mfikirie tena mwanaume ambaye mkewe ana ugonjwa wa kudumu kwa kiasi kwamba hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake kama mke. Bila shaka mwanamume huyu atafanya mojawapo katika haya yafuatayo:
Atajizuia na matamanio yake ya kimwili kwa muda wote wa maisha yake uliobakia.
Anaweza kumtaliki mkewe mgonjwa wakati ambapo anahitajia uangalizi, huruma na mapenzi ya hali ya juu kutoka kwake, ili aoe mke mwingine atakaye tosheleza mahiataji yake, au
Anaweza kubakia na mkewe mgonjwa na kufanya uzinifu kwa siri na wake wengi nje, au
Ataoa mke wa pili atakayemsaidia kumuhudumia mkewe mgonjwa.
Hebu tuzijadili hizi hatua tatu kwa mtazamo wa mafundisho ya Uislamu. Hatua ya kwanza inakwenda kinyume na umbile la mwanaadamu. Mwenyezi Mungu (s.w.) analifahamu fika umbile la mwanaadamu na haja yake ya kutosheleza matamanio ya jimai na ameweka utaratibu mzuri wa sheria ya ndoa wa kutosheleza mahitajio haya ya kimaumbile.
Hatua ya pili ni kinyume kabisa na ubinadamu. Kumwacha mke kwa sababu amekuwa mgonjwa, badala ya kumuhudumia kwa upendo na huruma, ni kinyume kabisa na utu.
Utaona kuwa hatua ambayo itamuwezesha mume huyu aendelee kutunza mkewe kwa huruma na wakati huo huo aweze kutosheleza mahitajio yake ya kimaumbile kwa utaratibu mzuri wa heshima ni kuoa mke wa pili.

Wanawake Wajane
Wajane ni wanawake waliofiwa na waume zao. Hakuna jamii isiyo na wajane, na idadi yao kuongezeka zaidi nyakati za vita ambapo wanaume wengi huuliwa vitani. Je, wanawake hawa warudishwe kwa wazazi au walezi wao na kukaa hivyo hivyo bila ya kukidhi matashi yao ya kimaumbile mpaka wazeeke? Au waachwe wawe malaya na kuitokomeza jamii kutokana na matatizo mbali yanayosababishwa na zinaa? Kwa vyovyote vile utaona kuwa njia pekee ya kuwahifadhi wanawake wajane na watoto wao ni hii ruhusa ya kuoa mke zaidi ya mmoja hadi wanne - kwa kufuata masharti yaliyowekwa.

Wanawake ni wengi katika jamii
Katika jamii nyingi wanawake huwa wengii zaidi kuliko wanaume. Katika jamii hizi, kama tutaweka sheria ya mume mmoja - mke mmoja, kama wanavyodai watetezi wa usawa wa mwanamke, wanawake watakao kosa wanaume wa kuwaoa watakwenda wapi? Watafanyaje ili kukidhi matashi yao ya kimaumbile? Je, kama watajizuilia mpaka wazeeke huoni hii itawaathiri kimwili, na kifikra na kuwafanya wasiwe watu wenye manufaakatika jamii? Nani atakayetoa hifadhi kwa wanawake hawa kiuchumi na kimaadili? Ilivyo katika maumbile ya mwanaadamu, kila mwanamke wa kawaida anahitajia kuwa na mwanamume anayempenda na kumhurumia. Hivyo, wanawake hawa watakapowakosa wanaume wa ndoa, watafanya kila hila ya kuwashawishi wanaume kwa kuwawekea mitego mbali mbali kama vile kujipitisha mbele yao wakiwa wamejipodoa na kujiremba, kutembea mbele yao uchi, kuzurura kwenye majumba ya sinema, n.k., ambayo itawanasa na kuwatumbukiza katika zinaa.

Mfikirie mwanamke anayeishi kwa kuvizia wanaume. Je, atakuwa na utulivu na usalama katika maisha yake? Je, jamii yenye wanawake wa namna hii wa kuwavizia na kuwadanganya waume za watu, inaweza kuwa jamii yenye amani na furaha? Wanawake wa namna hii mara nyingi wamekuwa ndio chanzo cha vurugu katika unyumba wa watu, kuwafitinisha watu na kusababisha vifo. Ikitokea mwanamke wa namna hii kupata mimba, jukumu la kumlea mtoto ni lake mwenyewe. 
Hivyo, watoto wanaozaliwa nje ya ndoa mara nyingi hukosa malezi mazuri na wengi wao huishia kuwa wezi wavuta bangi, na wahuni wa kupindukia katika jamii. Matatizo ya zinaa katika jamii tutayaona kwa upana katika kurasa za mbele.
Kwa vyovyote vile iko haja kwa kila mwanamke kupata mume wa kukidhi haja zake na kuhifadhi maisha yake na utu wake. Uislamu umetoa ruhusa ya kuoa wake zaidi ya mmoja hadi wanne ili kumfanya kila mwanamke anayetaka kuolewa, aolewe na kupata hifadhi na haki zake zote zinazomstahiki.
Kwa nini mwanamke asiruhusiwe kuolewa na Mume zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja?
Wapinzani wa ukewenza, wanadai kuwa ili pawe na usawa, wanawake waruhusiwe kuolewa na mume zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja endapo wanaume wataruhusiwa kuoa mke zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.

Kimaumbile na kisaikolojia, mwanamke ni wa mwanamume mmoja. Kwanza, ilivyo, takriban katika jamii zote za ulimwenguni, mwanamume ndiye kiongozi wa familia. Fikiria ingalikuwaje kama familia moja ingalikuwa na viongozi wawili au zaidi. 

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget