Friday, February 24, 2012

Adhabu Ya Kifo


Imeandikwa na ‘Abdun-Naaswir Hikmany
 UTANGULIZI
 Dunia sasa imekuwa ni kijiji kidogo sana, ni mengi yanafanyika na kuweza kutufikia kwetu kwa muda mchache au ndani ya sekunde tu. Mfano ni mechi za mpira. Sisi tukiwa mwisho wa dunia ilhali goli linafungwa Ulaya twaliona sasa LIVE. Yote naweza kusema ni kutokana na utandawazi inayofanya dunia kuwa ni kama kijiji. Mfano mwengine mzuri tu ni namna Tsunami ilivyotikisha dunia. Makubwa yametokea Indonesia lakini yale mawimbi madogo madogo na ya mwisho yalitosha kuitikisha Tanzaniavizuri. Natoa mifano hii kuonesha ule uwiano uliokuwepo baina ya Kaskazi na Kusi, Magharibi na Mashariki. Ikiwa ni wa kiasili au wa kutengenezwa.
  MFUMO WA SHERIA ZA NCHI
 Tukumbuke vyema namna Tanzania ilivorithi sheria kutoka Ukoloni. Hata baada ya Uhuru, ziliendelea kutumika na kufanyiwa kazi. Ijapokuwa kulikuwepo na mabadiliko madogo lakini ziliendelea kutumika. Mfano mdogo ni kuhusu masuala ya ardhi, ambapo ile dhana ya ‘public land’ ilirithiwa kutoka Ukoloni hadi Uhuru. Hivi miaka ya karibuni, Tanzania imeibuka na kuona namna sheria zake zisivoendana kwenye hali halisi na kuanzisha Shivji Commission, pamoja na mambo mengine ilikuwa na kazi ya kupitia sheria za ardhi.
 Imekuwa ni ada tu, kufuata yale mabadiliko ya Magharibi. Sheria ya kupinga sigara ilianzishwa nchi zaMagharibi, Tanzania ikafuatia kuiweka ndani ya daftari lake za sheria za Tanzania. Rudia kifungu 12 cha Sheria ya Tumbaku – Tobacco Products (Regulation) Act no. 2 of 2003. Hali ya kuwa haikuwa na msingi wowote wa kuitunga kwani haina meno wala mapembe. Labda ni ulimbwembe wa kuzikumbatia sheria za nje.
 Sheria za Jinai zilizotungwa na Mataifa yasiyo na dini kawaida huwa zinatoa adhabu bila ya kueleza utaratibu wa kuisafisha hiyo jamii. Kwa mfano, Sheria ya Kuwalinda Wari na Wajane ya 1985 yaZanzibar inadai kuwalinda wajane na wari kutokana na mimba zisizo halali. Lakini Sheria ya Makosa ya Jinai nambari 6 ya mwaka 2004 haiweki bayana kuwazuia kufanya tendo la ndoa kwa wari na wajane, isipokuwa tu inaeleza uzinzi wa waliomo ndani ya ndoa (adultery). Kama kweli tunataka wari na wajane wasipate mimba, ilikuwa pamoja na vizuizi vyengine ni kuwazuia wasitembee utupu, kuondosha michanganyiko isiyo na maana na pia kuweka kosa la uzinifu. Katika Uislamu neno “uzinifu” tafsiri yake ni tendo la kukutana mwanamme na mwanamke nje ya ndoa. Iwe hao wanaofanya hilotendo ni wasaliti wa ndoa zao au wale wenye wazinzi (boy friend au girl friend).
Hali kadhalika, ule msemo wa tarumbeta la Zanzibar likipigwa…… kinadharia umefikia wakati wa kubadilishwa. Kwani tuufanyie mabadiliko na kusema tarumbeta la Magharibi likipigwa…… sote twaitika. Mfano mwengine ni kupitishwa kwa Sheria ya Ugaidi nambari 21 ya mwaka 2002. Inafaa watu wajiulize kwanini Sheria hiyo isipitishwe baada ya Tanzania na Kenya kuathirika vibaya na ugaidi mwaka 1998. Badala yake imepitishwa baada ya ugaidi uliofanywa Marekani? Jee ni kweli sheria hii imewekwa kwa maslahi ya Watanzania?
 Tukiingia kwenye mjadala wetu wa adhabu ya kifo, tunaona kwamba uhai wa mwanaadamu unathaminiwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar chini ya Kifungu 13. Hata hivyo, katiba zote mbili zimeweka nafasi ya raia kuchukuliwa uhai wake kwa mujibu wa sheria (angalia kifungu 25 cha Katiba ya Zanzibar). Kwa mfano, sheria zetu za Tanzania zinaruhusu adhabu ya kifo chini ya Kifungu cha 197 cha Makosa ya Jinai, sura ya 16 – Tanzania Bara.  Rudia pia kifungu cha 197 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya Zanzibar nambari 6 ya mwaka 2004.
 Sasa ghafla tumeanza kusikia sauti ya kupinga adhabu hii iliyoanza kupigiwa kelele huko juu. Nchi za Ulimwengu wa Tatu wakafuatia kuitikia: “HewAllaah Bwana” na wala haikuanzia Tanzania. Lakini kwa vile tumerithi hizi sheria, inapotokea mabadiliko pia huathiri ule urithi wetu. Sheria ya Makosa ya Jinai ni miongoni mwa mirathi za Ukoloni. Adhabu ya kuondoshwa viboko ilianza namna hii na hatimaye tumejikuta tunaiondosha kwa kuitikia huo wito. Hivi sasa, sheria za Zanzibar haziruhusu adhabu ya kiboko. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Jinai nambari 6 ya mwaka 2004 chini ya ya kifungu 26. Kwa hivyo, tusishangae pia Bunge kupelekewa na kuukubali mswada wa kuifuta adhabu ya kifo.
Kama kweli hili ni taifa linalojitegemea na lipo huru, kwanini isiwe ya mwanzo na kufuatwa kwa kuanzisha sheria ya kuzuia Pombe?! Athari ya pombe ni kubwa zaidi na hata hayo mauaji kwa kiasi fulani yanasababishwa na hiyo pombe.
 UISLAMU NA ADHABU YA KIFO
 Kama tutasoma sera zinazotumiwa na Uislamu kwenye kutoa adhabu, tutatambua kwamba Uislamu umeanza awali kuisafisha jamii kutokana na mazingira yatakayopelekea kwenye kosa la jinai. Jamii ya leo haina vizingiti hivi, na ndio maana kuna wauaji kila sehemu na makosa yaliyoenea kwa wengi. Katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka pale jamii inaposhindwa kuzuia mazingira yenye kupelekea jinai kutendeka au pale panapoonekana kuwepo utata wa kosa la jinai, adhabu haitatolewa. Huyo anayetuhumiwa ataachiwa huru. Uislamu umeweka masharti ya ushahidi. Yasipotimia, basi adhabu za jinai hazitolewi kwa mtuhumiwa.
 Zile dhana za kusema adhabu ya kifo iondoshwe, au mwizi asikatwe mkono n.k haziwezi kukubalika ndani ya Uislamu na Waislamu wanatakiwa kuzipinga dhana hizi. Adhabu za makosa ya jinai zimetoka kwa Muumbaji pekee. Mtuhumiwa huenda akapewa msamaha au akaachiwa huru kulingana na hoja zilizotolewa hapo juu, lakini sio kuzifuta sheria hizi.
 Nchi za Magharibi na wale wenye fikra finyu, wanadhani kwamba Uislamu unapozungumza adhabu kama hizo, ni kama vile zitahukumiwa kila siku. Sheria ya Kiislamu sio kama sheria nyengine. Wanachora akilini mwao kwamba kila siku kutakuwa na ukataji mikono, kukatwa vichwa na adhabu za bakora. Lakini ukweli ni kwamba; adhabu hizo zimehukumiwa mara chache mno. Ukweli ni kuwa adhabu ya mwizi kukatwa mkono imehukumiwa mara sita tu, kipindi chote cha miaka mia nne. Huu ni ushahidi tosha kwamba adhabu kama hizo zililenga zaidi kutoa funzo na kuzuia makosa kutendeka.
 Kwa upande mwengine, watu wengine wanafikiriwa kwamba adhabu kama hizo hazina mnasaba wowote. Hili si kweli. Kwani adhabu hizi zilitolewa kwa lengo la kuwatia khofu wale wasio na ushawishi wa kutenda kosa lakini bado tu wana msukumo wa hali ya juu katika kulitenda kosa.
 Hali hiyo ndio inayoizunguka kwa Sheria za Kiislamu. Kwani Uislamu, unathamini sana haki ya maishakama ni msingi mkuu wa Haki za Binaadamu. Haki hii inalindwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) ndani ya Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Sura An-Nisaa, aya ya 93:
 {{Na mwenye kumuua Muislamu kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu, humo atakaa milele; na Mwenyezi Mungu Amemghadhibikia na Amemlaani na Amemwandalia adhabu kubwa.}}
 Pia Surat al-Furqaan, aya ya 68. Allaah Anazungumza:
 {{…wala hawaui nafsi Aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa haki, wala hawazini; na atakayefanya hayo atapata madhara…}}
 Ni uwazi kwamba Uislamu unathamini sana haki ya kuishi, na wala hairuhusu kuuana kama wanyama. Nafsi ya mwanaadamu ni thamani Anayoijua Mwenyezi Mungu tu pekee na wala hakuna mwengine anayeweza kuileta thamani hii. Ndivyo kwa utoaji wake uhai, yabidi kanuni thaabit zifuatwe. Hivyo, Uislamu unatoa adhabu ya kifo kama vile ilivyo kwa Katiba na Sheria ya Jinai. Haki ya kuishi yaweza kutenguliwa kwa kuuliwa ikiwa atapatikana na hatia ya kuua.
 Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Si halali (kumwaga) damu ya Muislamu isipokuwa kwa matatu; Nafsi kwa nafsi (Aliyeua auwawe), na mzinzi 'thayyib' (aliyekwishaoa au kuolewa) na aliyeacha dini akafarikiana na kundi." [al-Bukhaariy na Muslim]
 Kuna hekima kubwa sana ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndani ya Hadiyth hiyo hapo juu. Ameanza kwa kusema kwamba si halali kuuwa na wala hakuanza kuzungumzia adhabu ya kifo kama zilivyo sheria zetu za nchi zinazotoa adhabu bila ya msingi wala mantiki yoyote. Qur-aan, Sunnah na Waislamu wote thaabit watakuwa hawaelewi pale dhana ya adhabu ya kifo inapotaka kuondolewa. Ni hakika kabisa kwamba Uislamu hauruhusu mabadiliko yasiyo na msingi, na moja wapo ni suala hili. Kwani, limeshazungumzwa ndani ya Qur-aan iliyoshushwa miaka 1400 iliyopita. Tena ikiwa bado hai haina kasoro wala mkono wa mwanaadamu.
 MAGHARIBI NA UISLAMU
 Tuelewe kwamba huko Magharibi wanajidai mno kutetea kuondoshwa adhabu ya kifo kwa sababu hao wauaji ni waathirika wa jamii iliyojaa rushwa, matatizo ya saikolojia na maradhi ya maadili mabovu ambayo wameshindwa kuyaondosha. Hii yote imesababishwa na kuondosha mzizi mkuu wa sheria, nayo ni maadili! Uislamu unakwenda sawa sawa na maadili. Hivyo, mataifa kama hayo wanajilazimisha kupunguza adhabu hadi kufikia uamuzi wa kwamba kuua sio tena adhabu halisi ya kosa la jinai.
 Inakuwaje karne hii ya ishirini na moja inatoa ruhusa ya kuuliwa wanyonge na wasio na hatia hata kidogo huko Palestina, Iraq, Afghanistan, Chechnya na nchi nyenginezo? Lakini karne hii hii inajadili na kuruhusu kuondoshwa adhabu ya kifo kwa yule mtu aliyetiwa hatiani.
 Uislamu unaweka usawa wa haki kwenye nafasi sahihi na kuhimiza kwenye kuchunguza masharti na mazingira yaliyoegemezwa na kosa hilo la jinai. Katika kusoma huko, Uislamu unachukulia kosa la jinai katika dhana mbili wakati wa hilo kosa lilipotendwa; uoni wa mtendaji na wa jamii. Kwa muangaza huo, Uislamu unatoa adhabu iliyo sawia ambayo inaendana na haja iliyo makini na yenye maana. Ambayo pia (adhabu itakayotolewa) haiathiriki kutokana na dhana za wale wazoefu wa makosa (delinquents) wala msamaha wa taifa au wa mtu mmoja.
 Uislamu unatoa adhabu kali ambazo kwa juu zinaweza kuonekana kuwa ni katili au za kutumia nguvu zaidi, kama tu zitaangaliwa kwa juu juu au bila ya kuangalia malengo yaliyo sahihi. Lakini Uislamu, hautoi adhabu hadi ithibitike kwamba hilo kosa la jinai limefanyika bila ya haki au kwamba mtendaji kosa hakutenda katika mazingira ya kulazimishwa.
 Uislamu unaeleza kwamba mkono wa mwizi ukatwe, lakini adhabu hii haiwezi kutolewa ikiwa kuna shaka nduchu kwamba mwizi huyo alilazimika kuiba kutokana na njaa kali mno iliyosababishwa na Viongozi wake.
 Halikadhalika, Uislamu unatoa adhabu ya mzinifu wa kike na kiume wauawe kwa kupigwa mawe, lakini haitosimamishwa adhabu hii hadi ithibitike kwamba hao wanaopigwa mawe ni wanandoa. Aidha mashahidi wakikhitalifiana, ushahidi wao huwa dhoofu na adhabu haitekelezwi hadi ushahidi ukamilike kwa kuonekana kwa uhakika katika tendo la uzinifu na mashahidi wanne.
 Anayekula pilipili ndiye aijuae ukali wake na utamu wake. Sasa yawezekana wazi yule muuaji au mbakaji na mzinzi ndio wanaoijua dhambi waliyoitenda hata wakafikia kujitetea kwamba hilo kosa sio tena kosa la jinai wala isitolewe adhabu ya kuuawa. Na kama inahitaji kuadhibiwa basi adhabu yake iwe ni ndogo na ya chini. Hakika zile sheria za kuhalalisha maingiliano ya jinsia moja yametokana na hao wenyewe watendaji hiyo dhambi, mfano huo huo kwa watoaji mimba na kadhalika. Hao wanaosema kuiondosha adhabu ya kifo bila ya shaka nao ni wauaji. Ni kusema wanaijua fika thamani ya roho kwani wameshaionja pilipili.
 Tukae tufikirie, wapi tunakwenda? Mabadiliko mangapi tunayahitaji kuyafanya? Tuzunguke na kuweka makini akilini mwetu. Kuna sheria zinaruhusu utoaji mimba, kioja zaidi kuna sheria nyengine za kuruhusu maingiliano ya jinsia moja. Tupo tayari pia kuzifuata hizi? Kama ni hivyo, tujitayarishie kufikiwa na makubwa zaidi kuliko yale tuliyoyaona kutokana na Tsunami.
 HITIMISHO
 Ni kweli kwamba Zanzibar wala Tanzania sio taifa linalofungamana na dini yo yote. Lakini tukae chini na kujiuliza. Jee tumefika wakati na sisi kuburuzwa na kufuata sheria zisizo na msingi kwa Tanzania? Adhabu ya viboko imefutwa, sasa tunataka kuifuta adhabu ya kifo. Tunaelekea wapi? Vijana wamejazana vibarazani kuvuta unga, wengine wakiingiliana kama wanyama au kuliko wanyama, wapo majambazi, wala rushwa, wauaji, wabakaji, wahaini, matapeli, msururu unaoendelea mbele. Makosa yote haya yanatarajiwa kuadhibiwa kwa kifungo cha jela, kifungo cha nje, kwa kazi za kuitumikia jamii na nyenginezo zisizokuwa muafaka. Hizi adhabu zitatosha kumhukumu yule ambaye amembaka mtoto wa miaka mitatu au yule aliyemuua mtu kwa makusudi?
 Mifano iko mingi (suala la idadi ya watu; masuala ya jenda; masuala ya mazingira; masuala ya haki za binadamu; masuala ya… ya… ya…)
Bila ya shaka yapo mazuri katika haya lakini mengine ni kinyume na maadili yetu na kwa kuwa yamejengeka juu ya mhimili wa akili ya mwanadamu, hubadilika kila baada ya muda. Leo tunaona Tory (UK) inataka mfumo wa elimu urudie uasili baada ya kubadilishwa 'kileo'.
Mengi ya maamuzi yetu kufuata kila linalokuja kutoka Magharibi yanatokana na  sababu zifuatazo kuu:
a) Kukosa misingi imara ya kutojua pande zote za shilingi, hivyo kushindwa kutetea yale ambayo ni sahihi kwetu lakini kwa kutotambua kwetu tunajikuta tunashindwa kuyatetea;
 b) Ufukara wetu unaotufanya tukubali nadharia ngeni kwa kubembeleza 'tonge ya rizki' toka kwa waitwao washirika wa maendeleo na nchi zinazochangia mashirika hayo.
Kwa kweli mifano ni mingi na inatosha tuishie hapa.

Nini cha kufanya?
1. Tujue kuwa hakuna anayejua zaidi kuliko Aliyetuumba; hivyo wajibu wetu ni kuwa sote kufuata maelekezo Yake Muumba.
2. Tusome dini na kuzijua sheria zake na maadili yaliyomo ndani yake ili tuwe na hoja madhubuti za kutetea mambo yetu.
3. Wasomi wetu wasione hayaa wala vibaya kutetea chao kilicho kizuri; wajiamini kwa kilicho chao.
Kutoka Al Hidaya

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget