Monday, February 13, 2012

Kumpenda Kikweli Mtume


Kumpenda Kikweli Mtume (صلي الله عليه وسلم)

بسم الله الرحمن الرحيم
Leo In shaa Allaah tutaangalia mada ya kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) kutokana na umuhimu wake katika kukamilisha imani ya mja, na kutokana na kutofahamika vyema maana halisi ya kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) kwa Waislamu walio wengi.


Neno محبة  ni neno la Kiarabu kilugha lina maana ya; Hisia za kumili kwa moyo. Na katika Sheria, ni kumili kwa moyo kunako ambatana na kiwiliwili, hisia, akili, matakwa, na matendo ya moyo yanayothibitishwa na matendo ya viungo. Na hiyo ndio Imani.

Imani kwa mtazamo wa Ahlus Sunnah wal Jama’ah ni kauli na matendo, yaani kauli ya moyo na ulimi, na matendo ya moyo na viungo. Kwa maana hii ya kisheria, mapenzi huwa na uhusiano moja kwa moja na Imani ya mtu.

Lakini kama mtu atatafsiri mapenzi kwa maana ile ya kilugha, yaani kumili kwa hisia za moyo tu, mapenzi ya mtu huyu yatakuwa na dosari kubwa, na yatakuwa yanahukumiwa na matamanio zaidi kuliko Imani, na huu ndio mtihani uliowasibu wengi katika Ummah wetu, wa kutotofautisha baina ya mapenzi ya kiimani, na mapenzi ya kumili kwa hisia za nyoyo.

Mtu anaweza kumpenda mtu mwengine kwa hisia hizo za kumili kutokana na vigezo vyake, lakini akawa bado anatofautiana naye katika mambo mengi, na wakati mwingine hakubaliani nae katika mitazamo yake na kauli zake, lakini bado moyo wake ukawa unamili kwa mtu huyo, tafsiri kama hii ya mapenzi ndio iliyowapotosha wengi miongoni mwa Waislamu kwa kudhani kuwa mapenzi ya aina hii, ni mapenzi yenye uhusiano na Imani.

Moja miongoni mwa misingi mikuu ya Imani ya Dini yetu ni kumpenda mtume wetu Muhammad (صلي الله عليه وسلم) kuliko tunavyozipenda nafsi zetu na ukimuuliza Muislamu yeyote duniani atakuthibitishia mapenzi makubwa aliyonayo kwa kipenzi chetu Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم), lakini tunatofautiana katika uelewa wa jinsi ya kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) kwa mujibu wa tafsiri tulizozitaja hapo juu.

Wapo miongoni mwetu ambao ukimtaja tu Mtume (صلي الله عليه وسلم) anaweza kububujikwa na machozi kwa hisia kali alizonazo juu ya Mtume wetu (صلي الله عليه وسلم), mwengine atatoa sauti kali ya kumtakia rehma na amani Mtume (صلي الله عليه وسلم) kwa kusema kwa vishindo ‘Allaahumma salim alee’, au wengineo waliozuka siku hizi na kuleta itikadi yao ya kutukana Maswahaba, utawakuta anapotajwa Mtume, huitikia kwa vishindo ‘Allaaaahumma Swaliii ‘alaa Muhammad wa aaaali Muhammad’ lakini ndio hao hao wanautukana wake zake na Maswahaba zake!! Na si ajabu ukawakuta watu hao pamoja na mapenzi makubwa wanayoyaonyesha kwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) hawatimizi Swalah tano kwa siku, wake zao na mabinti zao hawajisitiri, wana vimada nje, nyumba zao zimejaa taarabu za rusha roho, zimepambwa na vinyago na mapicha, wavuta sigara, wala mirungi, wakaa mabarazani kusengenya, panapoaziniwa na kukimiwa hawasimami kwenda kuswali na Waislam,  achilia mbali kupuuza kwao baadhi ya Sunnah muhimu kama vile kufuga ndevu n.k. Watu hawa wana mapenzi makubwa kwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) lakini ni mapenzi ya aina gani ? je, haya ndio mapenzi ya kiimani?

Neno mapenzi katika Uislamu lina maana nzito sana, haifai kulichukulia kwa maana nyepesi nyepesi kwani lina uhusiano mkubwa na ‘Aqiydah ya Dini yetu; Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema katika Qur-aan:

(ومن الناس من يتخذ من دون اللــه أندادا يحبونهم كحب اللــه والذين آمنوا أشد حبا للــه) البقرة 165

“Na katika watu kuna wanaofanya waungu wasiyekuwa Mwenyezi Mungu, wanawapenda kama kumpenda, lakini walioamini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana.” 2:165

Kumpenda Allaah (سبحانه وتعالى) ni katika alama za Tawhiyd, kamailivyobainisha Aayah, na kumpenda Allaah (سبحانه وتعالى) ndio msingi wa kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم), huwezi kumpenda Mtume kabla hujatimiza mapenzi ya Allaah (سبحانه وتعالى) na huwezi kumpenda Allaah kwa kumkwepa Mtume (صلي الله عليه وسلم).



VIGEZO VYA KUMPENDA MTUME (صلي الله عليه وسلم)


1.  KUTHIBITISHA SHAHADA YA UTUME WAKE 

Ni kuthibitisha utume wa Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم) kuwa ni mjumbe aliyetumwa kwa waja wote, kuthibisha kivitendo yote aliyoyaamrisha, na kujiepusha na yote aliyoyakataza na kuyakemea, kwa maana nyingine ni kumuabudu Allaah (سبحانه وتعالى) kama Alivyofundisha na kuelekeza Mtume, na Allaah Anathibitisha hayo kwa kusema:

(قل إن كنتم تحبون اللــه فاتبعوني يحببكم اللــه ويغفر لكم ذنوبكم واللـه غفور رحيم) العمران 31

“Sema, ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni, Mwenyezi Mungu Atakupendeni na Atakughufirieni madhambi yenu”3:31

Allaah Anathibitisha kuwa, ili mja awe na Tawhiyd iliyokamilika ya kumpenda Allaah, basi ni lazima amfuate Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم) na ndio kisha Allaah Atampenda mja huyo na kumsamehe. Hivyo basi, mapenzi ya kweli yanakuwa kwa kumfuata Mtume (صلي الله عليه وسلم) katika yote aliyokuja nayo na kumtii na ndipo Allaah Atampenda mja huyo, na atakayebahatika kupendwa na Allaah (سبحانه وتعالى) hakika huyo amefaulu kufaulu kulikokuwa kukubwa.

  
2.    KUMUIGA MTUME (صلي الله عليه وسلم)
Mapenzi ya kweli ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) yanakuwa ni kwa kumuiga kwa yote aliyokuja nayo, kumuiga katika tabia zake, katika maisha yake, katika nyumba yake, katika ibada zake, katika mahusiano yake na majirani, na katika maisha yake kwa ujumla, kama alivyotuambia Allaah (سبحانه وتعالى)

لقد كان لكم في رسول اللــه أسوة حسنة لمن كان يرجو اللــه واليوم الآخر وذكر اللــه كثيرا) الأحزاب 21

“Bila shaka mnao mfano mwema kwa mtume wa Mwenyezi Mungu kwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na kumtaja Mwenyezi Mungu sana.” 33:21

Kumuiga Mtume na kumfanya kuwa ruwaza njema ndio mapenzi ya dhati ya kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم), lakini kumpenda mtume kwa kumsifu tu, na akawa hana nafasi katika maisha yako na maisha ya familia yako, basi huko si kumpenda bali ni kujifanya kumpenda na inawezekana ikawa ni kumcheza shere.

Katika Hadiyth iliyopokelewa na ‘Abdu-Rahmaan bin Quraad (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa “Mtume (صلي الله عليه وسلم) alikuwa anatawadha, na Maswahaba wakaanza kukinga maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka katika wudhuu wa Mtume (صلي الله عليه وسلم) na wakijifutia katika miili yaokutafuta baraka za wudhuu ule kutoka kwa Mtume, Mtume (صلي الله عليه وسلم) akawauliza; “kwa nini mnafanya hivi? Wakasema; ni kwa ajili ya kumpenda Allaah na Mtume Wake, Mtume (صلي الله عليه وسلم) akawaambia, anayetaka kumpenda Allaah na Mtume Wake, au kupendwa na Allaah na Mtume Wake, basi aseme ukweli anapozungumza, na atekeleze amana yake anapoaminiwa, na awe jirani mwema kwa jirani yake” Al –Albaaniy ‘Mishkaatul Maswaabiyh

Mtume (صلي الله عليه وسلم) anawaelekeza Maswahaba zake, na ndio anatuelekeza sisi jinsi ya kumpenda mapenzi ya kweli, mapenzi yenye tija na yenye kuleta mabadiliko katika tabia za mja, Mtume alikuwa anawaelekeza Maswahaba kuwa kumpenda kwa kugombea maji yake ya wudhuu peke yake ili kupata baraka, hakutoshi, na kutakuwa hamna maana kama watu hao watakuwa waongo katika mazungumzo yao, hawatekelezi amana zao, wanaudhi majirani zao, mapenzi hayo ya kutafuta baraka tu na kuacha kumfuata Mtume (صلي الله عليه وسلم) yatakuwa ni mapenzi ya kumcheza shere Mtume (صلي الله عليه وسلم).


3.    KUMFANYA HAKIMU KATIKA MIZOZO YOTE

Na katika dalili za kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) ni kumfanya hakimu katika mizozo yetu yote, na kuridhika na hukmu yake, na katika zama tulizonazo ambazo Mtume (صلي الله عليه وسلم) hayupo nasi, basi Qur-aan na Sunnah zake ndizo zitakazotumika katika kutatua mizozo yetu, na Allaah (سبحانه وتعالى) anatuambia katika Qur-aan:

(فلا وربك لا يؤمنون حتى يحكموك فيما شجر بينهم ثم لا يجدوا في أنفسهم حرجا مما قضيت ويسلموا تسليم)النساء 65
“Naapa kwa (haki ya) Mola wako. Wao hawawi wenye kuamini (kweli kweli) mpaka wakufanye hakimu katika yale wanayokhitalifiana, kisha wasione uzito nyoyoni mwao juu ya hukumu uliyotoa, na wanyenyekee kabisa” 4:65

Katika kutafsiri Aayah hii, Imam Ibnul Qayyim katika kitabu chake cha Sharhu Al-Manaazil anasema kuwa Aayah ii imekusanya ngazi tatu za Dini, amabzo ni: UISLAM, IYMAAN, NA IHSAAN, na atakayeikanusha na kuacha kuitekeleza basi atakuwa amekanusha ngazi zote za Dini.

Jambo la kuhuzunisha ni kuwa, Waislamu tulio wengi ambao tunasema tunampenda Mtume (صلي الله عليه وسلم), haturudi kwa Mtume katika kutatua mizozo yetu, bali kila mtu, kila kundi linarudi kwa sheikh wake, kwa madh-hab yake au kwa kutumia ra’aiy zao, na unapotoa ushahidi wa kauli ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) kuhusu suala lenye mzozo basi unaweza kuambiwa mbona Imaam ash-Shaafi’iy, au Maalik kasema hivi, na mtu huyu huyu anapotajwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) humtakia rehma kwa kishindo kudhihirisha mapenzi yake kwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) na unapochelewa wewe kumtakia rehma Mtume basi hudiriki kukutuhumu kuwa humpendi Mtume (صلي الله عليه وسلم).

Katika Aayah nyingine Allaah Anasema:

( فإن تنازعتم في شيء فردوه الى اللــه والرسول إن كنتم تؤمنون بالله واليوم الآخر) النساء 59

“Na kama mkikhitalifiana katika juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho” 4:59

Aidha Allaah Anatuamrisha katika Aayah nyingine kurejesha mizozo yetu Kwake na kwa Mtume, lakini asilimia kubwa ya Waislamu hawaitekelezi Aayah hii, na kwa bahati mbaya hata wale wanaojinasibisha kutetea Sunnah za Mtume (صلي الله عليه وسلم) na mwenendo wa As-Salaf As-Swaalih baadhi yao wameshindwa kuitekeleza Aayah hii, na wanaona bora kuhukumiwa na mahakama za kitwaaghuut kuliko kukaa na kuyamaliza matatizo yao kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah.

Hali ya Ummah inahuzunisha, wako wanaotosheka kumsifu tu Mtume (صلي الله عليه وسلم) na kuridhika kuwa wameonyesha mapenzi yao kwa Mtume (صلي الله عليه وسلم), huku wakipinga Sunnah zake zizlizo dhaahir kwa utashi tu wa nafsi zao, na kuwatanguliza masheikh wao, na wakati mwingine kwa ajili tu ya kuwaonyesha Waislamu wenzao ukaidi wao na ubishi wao wa ushindani.


Bado hatumtendei haki Mtume wetu (صلي الله عليه وسلم), bado hatujafikia daraja ya kumpenda kwa dhati kuliko nafsi zetu, kuliko maslahi yetu, kuliko masheikh zetu, kuliko wafuasi wetu, na kuliko majina ya Taasisi na makundi yetu.

Allaah (سبحانه وتعالى) Anawasifu waumini wa kweli kwa kusema:

(إنما كان قول المؤمنين إذا دعوا الى اللــه ورسوله ليحكم بينهم أن يقولوا سمعنا وأطعنا  وأولئك هم المفلحون)  النور 51

“Haiwi kauli ya Waislamu wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila kusema “Tunasikia na tunakubali, na hao ndio watakaofuzu” 24:51
  
 4.    KUTOTANGULIZA JAMBO MBELE YAKE, NA KUINAMISHA SAUTI

Katika kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) ni kutotanguliza jambo lako, au rai yako, au kauli ya sheikh wako, au madh-hab yako, mbele ya kauli ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) na kutonyanyua sauti yako, na fikra zako mbele ya mafundisho ya Mtume (صلي الله عليه وسلم), katika uhai wake na hata baada ya kifo chake (صلي الله عليه وسلم), kwa kuheshimu mafundisho yake na kuyaweka mbele na juu ya mafundisho yote, na kutonyanyua sauti yako juu ya kauli na hukmu ya Mtume (صلي الله عليه وسلم).

Siku moja Imaam Ash-Shaafi’iy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alijiwa na mtu na akamuuliza mas-ala katika mas-ala ya Dini, Imaam akamwambia kuwa Mtume (صلي الله عليه وسلم). Amesema kadha, na akamsomea kipengele cha Hadiyth ya Mtume (صلي الله عليه وسلم). Yule muulizaji akamuuliza tena Imaam Ash-Shaafi’iy; na wewe Imaam unaonaje? Imaam Ash-Shaafi’iy akakasirishwa sana na yule mtu, na akamwambia, je unaniona mimi nipo kanisani hapa? Nakwambia amesema Mtume (صلي الله عليه وسلم) kadha unaniuliza rai yangu? Huku ndio kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) ukweli wa kumpenda.

  
5.    KUWAPENDA NA KUWAHESHIMU WATU WA FAMILIA YAKE

Kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) ni kuipenda familia yake, wakiwemo wake zake na kuwapenda Maswahaba zake, huwezi kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) na ukawa unawachukia wakeze na Maswahaba zake, bali kwa kuwachukia wake za Mtume na Maswahaba zake utakuwa unamchukia Mtume mwenyewe, na ukiwatukana utakuwa umemetukana Mtume mwenyewe

 6.    KUTOMSIFIA KWA SIFA ASIZOSTAHIKI
 Kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) hakuwi kwa kumsifia kwa sifa ambazo hastahiki, au ambazo zimepetuka mipaka ya utume wake. Wapo Waislamu ambao wanadai kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) na wanampachikia sifa ambazo zinakaribia kufikia sifa za Allaah (سبحانه وتعالى), na unapohoji juu ya uzushi huo na shirki hizo, basi utatuhumiwa kuwa wewe ni adui wa Mtume na humpendi.

Mtume (صلي الله عليه وسلم) alitabiri hali hii na akautahadharisha Ummah wake usije ukawa kama Manaswara waliomsifu ‘Iysaa bin Maryam mpaka wakamgeuza Mungu, Mtume (صلي الله عليه وسلم) Alisema:

(لا تطروني كما أطرت النصارى ابن مريم وإنما أنا عبد فقولوا : عبدالله ورسوله )

“Msinisifie kama walivyomsifu Manaswara ‘Iysaa bin Maryam hakika mimi ni mja, niiteni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.”

Lakini pamoja na tahadhari hizo za Mtume (صلي الله عليه وسلم) bado baadhi ya Waislamu hawaoni kuwa wamempenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) mpaka wamsingizie sifa ambazo hana, na baadhi yao wamefikia hata kubadilisha Aayah ya Qur-aan ili ikubaliane na upotofu wao, Allaah (سبحانه وتعالى) aliposema kupitia ulimi wa Mtume (صلي الله عليه وسلم) katika kuthibitisha kuwa Mtume ni binadamu kama binadamu wengine isipokuwa yeye huteremshiwa wahyi, alisema:

(قل إنما أنا بشر مثلكم يوحي  إلي أنما إلهكم إله واحد ) الكهف 110

“Waambie, Bila shaka mimi ni binadamu kama nyinyi (isipokuwa nimeletewa wahyi tu ndio tofauti yangu). Ninaletewa wahyi ya kwamba Mungu wenu ni mungu mmoja tu.” 18:110

Wapotoshaji hao waliona wamkosoe Allaah kwa kumshusha cheo Mtume, wao wakaona waiandike upya Aayah ili isomeke...

قل إن ما أنا بشر مثلكم يوحي إلي ...
Kwa maana, sema hakika mimi si binadamu mfano wenu…

Hii ni kufru ya wazi kabisa ambayo inafanywa kwa jina la kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم).

Na wengine wanadai kuwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) anajua elimu ya ghayb na anajua lini itakuwa Qiyaamah, na kuwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) ameumbwa kutokana na nuru ya Allaah, kama isemavyo kauli inayonasibishwa na ‘Abdul-Qaadir Al-Jaylaaniy katika kitabu cha ‘Sirru Al Asraar’ anasema: “Elewa Allaah Akuwafikishe kwa Anachokipenda na kuridhia, Allaah Aliumba roho ya Muhammad kwanza kutokana na nuru yake na uzuri wake, kama alivyosema Allaah: Nimeumba roho ya Muhammad kutokana na nuru ya uso wangu…”
na huo ni uongo dhaahir na kumsingizian Allaah ambacho Hajakisema.

Aidha wanadai kuwa siku ya kuzaliwa kwake Mtume (صلي الله عليه وسلم) ni siku bora kuliko hata usiku wa Laylatul Qadr, na wanadai kuwa roho ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) huhudhuria katika maulidi na huwa anazungumza na mawaliiy.

Kwa ujumla, mambo mengi yamezushwa katika Dini hii kwa kumzushia Mtume (صلي الله عليه وسلم) mambo ambayo mengine tumeshindwa kuyaandika katika safu hii kutokana na kutunza heshima ya kipenzi chetu Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم)

Ndugu zangu Waislamu, tumpende Mtume (صلي الله عليه وسلم) ukweli wa kumpenda, tumuingize katika maisha yetu, awe ni kiongozi wetu, ruwaza yetu, mshauri wetu, hakimu wetu, mwalimu wetu, tuyafundishe mafundisho yake kwa walimwengu wote, na tuuthibitishie ulimwengu kuwa, Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم) ni Mtume aliyetumwa kwa watu wote na ni rehma kwa walimwengu wote.

Tunayo Dhimma kubwa ya kuhakikisha kuwa mafunzo ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) yanafahamika vyema kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu, na njia nyepesi ya kufanikisha hilo ni sisi wafuasi wa Mtume (صلي الله عليه وسلم) kumpenda Mtume wetu ukweli wa kumpenda, na kuyaingiza mafundisho yake katika maisha yetu ya kila siku.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget