Wednesday, February 22, 2012

KITABU-ULIMWENGU WA KIISLAMU, FURSA NA CHANGAMOTO


ULIMWENGU WA KIISLAMU, FURSA NA CHANGAMOTO

Assalamu alaikum ndugu Waislamu
hichi ni kijitabu kilichokusanya idadi ya makala kutoka Radio ya kiswahili ya Iran (kiswahili.irib.ir), na mkusanyaji wa makala hizi ni ndugu yenu Salim Al-Rajihiy, kwa hiyo haki za kunukuu au kuchapisha zimehifadhiwa na (kiswahili.irib.ir) Iran, na hakukua na malengo yeyote katika kuzikusanya makala hizi, isipokua ni kueneza fikra na utamaduni wa Kiislamu. Ahsanteni sana tusiache kuombeana dua.

Ulimwengu wa Kiislamu Fursa na Changamoto
Kwa jina Allah Mwingi wa rehema Mwenye Kurehemu Assalaam Alaykum wasomaji na wapenzi wa Redio Tehran Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Huu ni mfululizo wa makala za Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa na Changamoto ambao utatupia jicho na kuchunguza fursa pamoja na changamoto zinazoukabili Ulimwengu wa Kiislamu. Ulimwengu wa Kiislamu si jina geni katika fasihi, maandiko, istilahi za kisiasa na kiutamaduni na hata katika masikio ya walimwengu pia.

Kabla ya neno Ulimwengu wa Kiislamu kubainisha hali ya eneo fulani kijiografia, linabeba maana na kuweka wazi utambulisho wa jamii fulani ya watu wapatao bilioni moja na nusu ambao wana mitazamo, dini, utamaduni,ustaarabu, mila na desturi zinazoshabihiana. Mbali na sifa maalumu ulionao ulimwengu wa Kiislamu kijiografia, ulimwengu huu una maliasili na utajiri mkubwa, utajiri ambao umeufanya kufahamika kuwa, eneo lenye utajiri mkubwa kabisa duniani. Sifa hiyo na suhula ulizonazo ndiyo zilizoufanya ulimwengu wa Kiislamu kwa karne kadhaa kuwa na nafasi muhimu katika uhusiano wa kimataifa. Hapana shaka kuwa, pana haja ya kuainishwa malengo na mipango madhubuti ambayo itasaidia kustafidi vizuri na suhula hizo na kwa njia sahihi na iliyo bora.

Katika mfululizo huu wa ''Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa na Changamoto'' tutazungumza na kujadili fursa na suhula zilizopo katika nchi za Kiislamu ambazo bila shaka kutumiwa kwake vyema kutaimarisha nafasi ya Waislamu katika nyanja mbali mbali ulimwenguni iwe ni kiuchumi au kisiasa na vile vile kuyaleta na kuyakurubisha pamoja mataifa ya Kiislamu na wafuasi wa dini hii tukufu. Aidha tutatupia jicho pia changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu zikiwemo za kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa, kielimu na kadhalika.

Matukio ya hivi sasa ulimwenguni yamebainisha kwamba, madola ya kibeberu hayataki kuona ulimwengu wa Kiislamu ukiwa na nafasi muhimu katika matukio mbalimbali duniani. Madola yanayopenda kujitanua daima yanatafakari na kutaamali ni namna gani yataweza kuudhibiti ulimwengu wa Kiislamu. Ndio maana madola hayo yakawa hayako tayari kuukubali utamaduni asili na tajiri wa Kiislamu, hasa kutokana na kuwa, utamaduni huo si tegemezi wala hauigi tamaduni za mataifa au watu wengine. Masuala hayo na mengineyo, ndiyo yaliyoufanya Ulimwengu wa Kiislamu leo hii ukabiliwe na vitisho na migogoro ya kupandikizwa kuliko karne za nyuma; na hapana shaka kuwa, yote hayo yanatokana na njama za maadui wa Uislamu.

Ili ulimwengu wa Kiislamu uinue nafasi na kiwango chake pamoja na kudiriki utambulisho wake halisi, pana haja ya kuweko mitazamo mipya, mwamko, kuwa macho pamoja na mipango imara na madhubuti. Ili tuwe na taswira ya mustakbali wa huko tuelekeako, kuna haja ya ulimwengu wa Kiislamu kufahamu nafasi yake halisi ya hivi sasa, suala ambalo litasaidia mno kufikiwa malengo muhimu na aali na yenye mafanikio makubwa. Kama tulivyoashiria mwanzoni mwa makala hii Ulimwengu wa Kiislamu ni jina ililopewa jamii ya Waislamu yenye idadi ya takribani watu bilioni moja na nusu ambao wanapatikana na kuishi katika nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu.

Kinachoifungamanisha pamoja jamii hiyo licha ya kuwa na makabila, lugha na rangi tofauti ni dini tukufu ya Kiislamu. Bara la Asia ndilo linaloongoza kwa kuwa na Waislamu wengi ambao idadi yao inakadiriwa kufikia bilioni moja. Barani Afrika kuna Waislamu wapatao milioni 391. Amma katika bara la Ulaya takwimu zinaonyesha kwamba, kuna Waislamu wapatao milioni 20 na wengine zaidi ya milioni 27 wanapatikana nchini Russia. Kadhalika kuna idadi nyingine ya Waislamu takribani milioni tisa huko Amerika ya Latini, Marekani na Canada.

Kuna baadhi ya mataifa na lugha ambazo zina nafasi muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa mfano lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki zinahesabiwa kuwa lugha muhimu mno katika ulimwengu wa Kiislamu. Waaidha Waislamu wengi wanaopatikana katika nchi za Pakistan na India wanazungumza lugha ya Ki-Urdu. Karibu asilimia 14 ya idadi ya Waislamu katika Ulimwengu wa Kislamu wanapatikana katika nchi za Indonesia na Malaysia na wanazungumza lugha ya Kimalayu au Kimalay.

Moja kati ya maeneo ya kiistratejia katika ulimwengu wa Kiislamu, ni eneo la Mashariki ya Kati ambayo ni njia fupi zaidi ambayo inayaunganisha mabara ya Asia na Ulaya. Lango bahari na vivuko muhimu vya kiistratejia kama vile Kanali ya Suez, Malango Bahari ya Jabal Twariq na Hormoz ni baadhi ya njia muhimu za mawasiliano ya baharini baina ya mabara mbalimbali, ambazo zinapatikana katika ulimwengu wa Kiislamu. Kuweko maliasili, nishati na utajiri wa madini na bidhaa mbalimbali za mazao ni baadhi tu ya mambo yanayouongezea umuhimu Ulimwengu wa Kiislamu na kuufanya uzingatiwe mno kimataifa.

Kama inavyofahamika, mataifa ya Kiislamu yanaundwa na lugha na makabila mbalimbali. Katika nchi 19 za Kiislamu, asilimia kubwa ya wakazi wake ni Waarabu na Wasemiti. Hata hivyo, kuna watu wengine wa makabila ya wachache kama vile Waturuki katika nchi za Kiarabu kama vile Iraq na Syria. Katika nchi za Kiafrika ambazo wakazi wake ni Waarabu wanapatikana pia watu wa jamii ya Wabarbari.

Ulimwengu wa Kiislamu una jumla ya nchi 57 na nchi yenye wakazi wengi zaidi ni Indonesia na ile yenye wakazi wachache ni Maldives. Mbali na Afghanistan, Iraq na Palestina nchi zote za Kiislamu zimejikomboa kutoka katika makucha ya wakoloni na wavamizi. Mpenzi msomaji sina shaka utakuwa umefahamu japo kwa mukhtasari, jiografia ya kimakazi na kisiasa ya ulimwengu wa Kiislamu. Makala zetu zitakazofuata zitazungumzia kwa urefu nafasi ya nchi za Kiislamu katika masuala mbalimbali ulimwenguni.

ULIMWENGU WA KIISLAMU, FURSA NA CHANGAMOTO (SEHEMU YA PILI)
Assalaam Alaykum wasomaji na wapenzi wa Redio Tehran Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Karibuni katika sehemu ya pili ya mfululizo huu wa makala za Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa na Changamoto. Tunaianza makala yetu ya juma hili kwa matamshi ya Ayatollah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambaye anazungumzia hatari zinazoikabili jamii ya mwanadamu kwa kusema: Jamii ya mwanadamu inakabiliwa na madhara ya aina mbili.

Madhara ya kwanza ni ya ndani ambayo yanatokana na udhaifu wa mwanadamu, shaka na kutokuwa na imani na Pili ni maadui wa nje ambao wamevuruga mfumo na mazingira ya maisha ya mwanadamu kutokana na ubeberu, kupenda kujitanua na kuvamia ardhi za wengine kwa mabavu na vita, na kusababisha kupotea ovyo na kiholela roho za watu wasio na hatia.'' Waislamu ni miongoni mwa jamii zinazokabiliwa na vitisho viwili hivyo. Leo hii mbali na maadui wa Uislamu kueneza ufisadi na tamaduni za Kimagharibi katika nchi za Kiislamu, wameshadidisha mashinikizo ya kijeshi, kisiasa na kiuchumi dhidi ya baadhi ya mataifa ya Kiislamu kama Lebanon, Palestina, Afghanistan na Iraq. Mibinyo na mashinikizo hayo yamekuwa na athari mbaya kutokana na kutokuweko radiamali sahihi na mwafaka za baadhi ya nchi za Kiislamu.

Ili leo Waislamu waweze kujua umuhimu wa zama zao hawana budi kuirejea na kuipitia historia ili wapate ibra na mazingatio na kwa njia hiyo waweze kuratibu na kuandaa mipango kwa ajili ya mustakabli mzuri na wenye mafanikio. Karne 14 zilizopita, kudhihiri Uislamu, kulipelekea kutokea mabadiliko makubwa katika historia ya mwanadamu na kwa kipindi kifupi tu, jamii ya mwanadamu ikafanikiwa kuvuka milima na mabonde na mipaka ya ubaguzi wa rangi, jiografia na ukabila na kwa kusimama misingi ya tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, jamii mbalimbali zikaweza kukaribiana na kuwa pamoja.

Uislamu ukiwa na uhai na ujumbe mpya, ulienea kwa kasi na kufanikiwa kudhibiti maeneo mengi ulimwenguni na kuyaweka chini ya mamlaka yake. Katika kipindi ambacho Uislamu ulipata umashuhuri na kuwa katika kilele cha kutambulika, jamii za Kimagharibi zilikuwa katika usingizi mzito. Kwa mujibu wa wasomi, Wamagharibi walikuwa wakipita katika kipindi kilichojulikana kama Zama za Giza. Ulimwengu wa Magharibi haukuwa na fikra mpya ya kuinufaisha jamii ya mwanadamu. Vita vya Msalaba vilianza baada ya madola yaliyokuwa na nguvu ya Magharibi kuushambulia kijeshi ulimwengu wa Kiislamu.

Hata kama katika kipindi cha karne mbili madola ya Magharibi hayakuweza kufikia malengo yao ya kijeshi, lakini kipindi hicho kiliwaandalia uwanja wa kufahamu taratibu utamaduni, mila, desturi na maendeleo ya kifikra yaliyoku katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa hakika hilo pekee lilitosha kuandaa uwanja wa kutokea mwamko wa kifikra katika ulimwengu wa Magharibi. Hata hivyo, ni katika kipindi hicho ndipo ulimwengu wa Kiislamu uliathiriwa na mambo mawili na kubaki nyuma kimaendeleo. Mosi, upenyaji ukoloni wa Magharibi katika eneo hili muhimu kijiorafia. Dhulma na mmomonyoko wa misingi ya kijamii au mfumo uliokuwa ukitawala wa baadhi ya watawala wa Kiislamu katika zama hizo ni sababu nyingine iliyopelekea Waislamu kuwa mbali na fikra na mitazamo ya Kiislamu.

Karne ya 20 Miladia ilishuhudia kuanza mashambulio makubwa ya kijeshi na kifikra ya Magharibi dhidi ya Ulimwengu wa Kiislamu, kiasi kwamba Waislamu wenyewe wakajiona kuwa ni wageni. Walijidanganya kwamba, kwa kufuata na kuiga tamaduni za Kimagharibi, wangeweza kufidia kubaki kwao nyuma. Natija ya Waislamu kuwa mbali na Uislamu na mafundisho yake, ndio hii tunayoiona leo ya kubaki kwao nyuma kiuchumi, kielimu na kisiasa. Hata hivyo, suali la kujiuliza hapa ni hili kwamba, je, Waislamu walijitenga vipi na Uislamu na fikra zake?

Jibu la swali hilo ni moja tu, nalo ni kwamba, kuibuka makundi na madhehebu mbalimbali, na kuenea kwa imani potofu, bidaa na uzushi ni moja ya mambo yaliyowafanya Waislamu kuacha matukufu yao ya kidini. Nchi za Kiislamu hazikuwa na tafsiri moja kuhusiana na Uislamu na hata wakati mwingine tafsiri na mitazamo ya nchi fulani ya Kiislamu ilitofautiana mno na ya nchi nyingine. Tofauti hizo kwa hakika ndizo zilizopelekea sheria moja mathalani itekelezwa mara kadhaa na wakati mwingine hata utekelezwaji wake kugongana na kukinzana. Namna ya kufahamu sheria hiyo na wakati mwingine kufurutu ada katika kuitekeleza leo hii ndiko kuliyapa fursa na kuyaandalia uwanja madola ya kibeberu kuingilia kati masuala ya nchi za Kiislamu.

Mfano hai kuhusiana na suala hilo ni mtazamo wa kupotoka kundi la wanamgambo wa Taliban waliokuwa wakitawala nchini Afghanistan, ambao miamala yao kwa hakika ilikuwa haioani na misingi pamoja na mafundisho ya dini ya Kiislamu. Miamala hiyo ya Taliban ilizipa fursa nchi na vyombo vya habari vya Magharibi kuushambulia Uislamu na kuupa majina ya kejeli chungu tele. Leo hii kwa kiwango fulani Waislamu wanatambua umuhimu wa kuunganisha siasa na dini.

Wanafikra wengi wa Kiislamu, wanaaamini kwamba, ni muhali kutenganisha dini na siasa na kwamba, viwili hivyo vimesisitizwa na dini ya Kiislamu. Imam Khomeini Muasisi wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran anaamini kwamba, dini si njia na mawasiliano baina ya mja na muumba wake pekee, bali dini inamfundisha pia mwanadamu namna ya kuendesha mambo yake ya kisiasa na kimaanawi. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akaona kuwepo umuhimu mkubwa wa kuundwa dola la Kiislamu na kwamba, hiyo ni haja kubwa ya kisiasa kwa Waislamu. Wapenzi wasomaji sehemu ya pili ya makala yetu ya Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa na Changamoto inaishia hapa; sina shaka mumenufaika vya kutosha. Wasalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

ULIMWENGU WA KIISLAMU, FURSA NA CHANGAMOTO (SEHEMU YA TATU)
Sehemu ya tatu ya makala ya Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa na Changamoto itaendelea kutupia jicho baadhi ya changamoto na sababu zilizozikwamisha nchi za Kiislamu na kuzifanya zisiwe na mitazamo na misimamo mimoja. Miongoni wa matatizo makubwa yanayoukabili ulimwengu wa Kiislamu hii leo, ni kutokuweko umoja, mshikamano na mitazamo ya pamoja ya kisiasa baina ya nchi za Kiislamu. Kwa hakika suala hilo huenda likawa limesababishwa na sababu mbalimbali.

Mosi ni kuwa, serikali nyingi zinazotawala katika nchi za Kiislamu zinaamini kwamba, kwa kuzingatia hali ya kiuchumi na kiteknolojia, na muhimu kuliko yote uwezo wa kijeshi wa Magharibi, maslahi na manufaa yao yanaweza tu kudhaminiwa kwa serikali zao kuwa na uhusiano na nchi za Magharibi. Katika upande mwingine, hali ya kulegalega kisiasa na matatizo ya vita vya ndani pamoja na vitisho vya kieneo katika baadhi ya nchi ni mambo yaliyoziongezea nchi hizo hasa watawala wake woga na kuhisi kutokuwa na amani.

Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana nchi hizo zikaamua kuwatumia Wamagharibi ili kulinda nafasi zao, kiasi kwamba, baadhi ya nchi hizo zinayategemea madola hayo katika kukidhi mahitaji ya chakula, silaha na hata usalama wao. Leo hii nchi zinazoendelea zimekuwa zikitenga bajeti kubwa ya kununulia silaha na zana za kivita kutoka kwa madola makubwa.

Na ndio maana nchi za Mashariki ya Kati leo hii zikahesabiwa kuwa wanunuzi wakubwa wa silaha duniani. Katika kipindi cha vita vya kichokozi vya Iraq dhidi Iran na Kuwait, takribani dola bilioni 200 za Kimarekani za akiba ya fedha za kigeni za nchi za eneo kama Iraq, Kuwait na Saudi Arabia zilitumika kununulia silaha na zana za kivita kutoka kwa madola ya Magharibi. Hofu ya mashinikizo ya nchi zenye nguvu na satua za madola ya Magharibi na vitisho vyao vya kuziwekea nchi nyingine vikwazo vya kiuchumi na kifedha ni mambo mengine yaliyozifanya nchi za Kiislamu kutokuwa na hamu ya kuanzisha uhusiano baina yao na kutiliana saini mikataba ya ushirikiano.

Hussein Abul Fadhli mwandishi wa kitabu cha Mitazamo ya Pamoja ya Ulimwengu wa Kiislamu anaamini kwamba, rasilimali ya kimaanawi huifanya nchi fulani kuwa na nguvu kazi yenye fikra madhubuti. Ikiwa wasomi na wanafikra watalelewa katika misingi ya kitamaduni na ustaarabu wao asilia na wakafanya shughuli zao katika fremu ya matukufu na itikadi zao, hapana shaka kuwa, watakuwa wenzo na nguzo muhimu ya desturi na utamaduni huo. Lakini kinyume na hivyo, endapo watajitenga na kuwa mbali na utamaduni, mila na desturi za taifa lao na wakawa na matatizo ya utambulisho wao ni wazi kuwa, watapelekea jamii yao nayo kukumbwa na matatizo hayo.

Tukichunguza nafasi na mchango wa wanafikra waliolelewa katika mifumo ya kisekula katika kufungamana nchi zinazoendelea na Magharibi, tunaupata kuwa nao si mdogo. Wasomi hao wa Magharibi bila kwanza ya kuwa na uelewa sahihi wa mapungufu na kasoro pamoja mazuri na mabaya ya ustaarabu wa Magharibi wamekuwa wakifuata kibubusa mifumo ya maisha ya Magharibi na kuifanya mifumo hiyo kuwa, kioo na kiigizo chao katika ufumbuzi wa matatizo yao.

Natija ya kuiga na kufuata mfumo huo ni kushindwa na kutokuwa na utambulisho huru. Mbali na matatizo ya ndani, tukitazama kwa makini tunaona kuwa, kuna matatizo na sababu za nje pia zilizopelekea nchi za Kiislamu kubaki nyuma katika masuala mbalimbali. Ukoloni wa moja kwa moja na usikokuwa wa moja kwa moja katika jamii za Kiislamu ulikuwa na nafasi muhimu katika kudhoofisha imani na tamaduni za Kiislamu.

Kuenea kwa mbegu za chuki baina ya kaumu na jamii mbalimbali za Kiislamu ni sababu nyingine iliyopelekea mori, moyo wa izzah na ile hali ya kupigania kujitawala na kujiamulia mambo ipungue katika nyoyo za jamii za wananchi hao. Waislamu ambao kwa makumi ya karne walikuwa waking'ara katika elimu mbalimbali, hivi sasa wanaonekana kubaki nyuma kutokana na njama za wakoloni na hali hiyo inazidi kushuhudiwa kila uchao kutokana na nchi za Kiislamu kuwa tegemezi kwa Wamagharibi. Leo hii kwa kuanzishwa hiki kinachoitwa utandawazi inaonekana kwamba, madola yenye nguvu duniani, yanataka kuutawala na kuudhibiti zaidi ulimwengu lakini kwa mbinu na mtindo mpya. Katika mazingira kama hayo, hapana shaka kuwa, nchi za ulimwengu wa tatu zikwemo nchi za Kiislamu zinakabiliwa na changamoto nyingi.

Kwa mfano, kuwepo kwa utandawazi wa kiutamaduni kutaishia kwa kutawaliwa nchi zote na utamaduni wa Magharibi ambao ni wa mambo na masuala ya kimaada na isirafu katika matumizi. Hasa kwa kuzingatia kwamba, utamaduni wa Magharibi ni wa kutangaza na kueneza vitu vya anasa na vinavyoonekana kuwa ni vya kisasa katika kila pembe ya dunia. Na hasa kwa kutilia maanani kuwa, nembo na vielelezo vya utamaduni wa Magharibi kama vile sinema, intaneti, video, matangazo ya mitindo ya mavazi ambazo vimetawala kwenye mtandao wa vyombo vya mawasiliano duniani, hazitoi fursa ya uwiano wa kubadilishana utamaduni baina ya ulimwengu wa Magharibi na nchi nyingine.

Katika uwanja huo, baadhi ya wakosoaji wa utandawazi wanasema kuwa, mwenendo huo ni mtindo mpya wa ubeberu wa kiutamaduni. Edward Said mhadhiri wa Vyuo Vikuu nchini Marekani mwenye asili ya Palestina anaamini kwamba, Wamagharibi kwa kutumia satua kwa mara nyingine tena wanafanya njama za kuukoloni kiutamaduni ulimwengu wakitumia utamaduni wao. Makala zetu zijazo zitaanza kuchunguza njia za kujiondoa na kujikwamua katika matatizo hayo. Kwa leo tunaishia hapa. Wasalaam Alaykum

ULIMWENGU WA KIISLAMU, FURSA NA CHANGAMOTO (SEHEMU YA NNE)
Miongoni mwa sifa za ubeberu wa kiutamaduni ni kueneza thamani za mfumo wa ubeberu kama vile namna ya matumizi, mavazi, uhusiano wa kijinsia, haki za binadamu na usekulari au mfumo wa kukana nafasi ya dini katika mfumo wa kisiasa. Kwa utaratibu huo, utandawazi unatoa utamabulisho mpya katika uwanja wa utamaduni, ambao kimsingi unaambatana na kupotea na kuangamia kwa utamaduni na ustaarabu asili wa nchi husika. Jamii za Kiislamu nazo zimekuwa wahanga wa kadhia hiyo. Katika uwanja wa kiuchumi, utandawazi pia unaweza kudhoofisha muundo wa ndani wa kiuchumi wa mataifa ya Kiislamu na kupelekea kuporwa maliasili na utajiri wa nchi hizo. Uchumi wa asili wa jamii hizo unaweza kukabiliwa na matatizo makubwa na ya kimsingi ya utandawazi kupitia mashirika ya kimataifa na taasisi kama Shirika la Biashara Duniani WTO na mengineyo.

Hasa kwa kuzingatia kwamba, nchi hizo hazina suhula za kutosha na muundo wao wa kiuchumi hauna uwezo wa kushindana na madola makubwa na yenye nguvu kiuchumi duniani. Ama kwa upande wa kisiasa, kutokea mihimili mipya yenye nguvu duniani kama vile mashirika na makundi ya kimataifa hasa vyombo vya mawasiliano kama vile Intaneti, satalaiti na mitandao mingi ya vyombo vya habari kumepelekea kulegalega kwa mipaka ya kitaifa. Cha kusikitisha zaidi ni kuwa, asasi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa wakati mwingine zimekuwa zikitumiwa kama wenzo wa madola makubwa kwa ajili ya kutekeleza matakwa ya madola hayo.

Ibn Khaldun alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, anazungumzia sababu muhimu za maendeleo katika jamii akisema, mambo mawili ni muhimu kwa ajili ya maendeleo. Mosi, kiongozi muadilifu na pili ni kuungana kwa jamii au kwa taifa na taifa jingine. Kuhusiana na suala hilo, leo hii baadhi ya wanafikra wamefikia natija hii kwamba, kutokuwepo tawala za kiadilifu na kukosekana moyo wa kuwaunganisha pamoja watu na kushirikiana pamoja ni miongoni mwa sababu zilizozifanya nchi nyingi kubaki nyuma kimaendeleo.

Mazingira yanayotawala leo hii ulimwenguni yanazilazimisha tawala kuliko kipindi kingine chochote kile kuwashirikisha wananchi katika nyanja mbalimbali ili ziweze kukabiliana au kutatua matatizo yanayozikabili. Kwa hakika suala hilo ni nguzo muhimu ya kuzihalalisha tawala zilizoko katika nchi mbalimbali ulimwenguni zikwemo nchi za Kiislamu. Katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, kumetokea matukio tofauti katika masuala mbalimbali ambayo yamepelekea mlingano wa dunia kukumbwa na mabadiliko makubwa. Kutokea mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kusambaratika Umoja wa Kisovieti, maendeleo makubwa yaliyopatikana katika uwanja wa teknolojia na mawasiliano, ni miongoni mwa matukio ambayo yaliibadilisha mno sura ya miaka ya mwishoni mwa karne ya 20.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran si tu kwamba, yalivuruga mahesabu ya madola ya Maghribi katika eneo muhimu na la kiistratejia la Mashariki ya Kati, bali mapinduzi hayo, adhimu yalikuwa na taathira kubwa kwa Waislamu ulimwenguni kote. Miongoni mwa mabadiliko makubwa yaliyotokea katika ulimwengu wa Kiislamu ni kutokea ufahamu na mwamko mkubwa wa wananchi.

Dr Hasan Rahimpour Azghadi, mtafiti wa Kiirani na mhadhiri wa chuo kikuu anasema hivi kuhusiana na suala hilo: "Ufahamu na mwamko huo ambao ni mwamko wa kidini, huenda karne moja iliyopita, ulikuwako katika kundi dogo la wanafikra waliobobea kwenye ulimwengu wa Kiislamu. Lakini leo hii mwamko huo unaonekana kuenea katika uma wote wa Kiislamu." Mtafiti huyo wa Kiirani anaendelea kusema, "mwamko huo hasa katika kipindi cha miaka 100 ya mwisho, umetokea baada ya karne kadhaa za kusalimu amri na kujilegeza mbele ya ukoloni. Leo hii Waislamu wanatambua vyema kwamba, sababu kuu ya kubaki kwao nyuma kiuchumi na kielimu na mifarakano na migawanyiko iliyopo katika ulimwengu wa Kiislamu imetokana na Waislamu kuwa mbali na mafunzo aali ya dini yao tukufu." Mwisho wa kunukuu.

Kutokana na Waislamu kubadilika kuhusiana na matukio mbalimbali yanayowazunguka, leo hii tunaona kuwa, katika ulimwengu wa Kiislamu kumekuwa kukipendekezwa masuala kama ya umoja wa uma wa Kiislamu, kuundwa asasi na jumuia za Kiislamu, ustawi wa kieilmu ambao kimsingi ni maendeleo na ustawi katika uga wa fikra za walimwengu kwenye ulimwengu wa Kiislamu. Suala hilo limeyafanya madola ya Kiislamu kufahamu kwamba, leo hii matakwa ya wananchi yana daraja ya juu zaidi kuliko mahitaji yao ya kila siku. Hata wito wa mabadiliko ya kisiasa wa Magharibi au mapendekezo yao ya demokrasia ulimwenguni hasa katika Mashariki ya Kati, ni masuala yanayotokana na kudhihiri mabadiliko ya kifikra katika ulimwengu wa Kiislamu.

Hapana shaka kuwa, madola ya Magharibi kamwe hayazingatii matakwa ya wananchi wa mataifa ya Kiislamu, bali yanajaribu kuzipotosha fikra za waliowengi kwa kutanguliza mbele matakwa ya wananchi hao, kumbe wanataka kufikia malengo yao haramu ili kwa njia hiyo waweze kudhibiti hali ya mambo katika eneo na matukio ya ulimwengu wa Kiislamu. Mashambulio ya Marekani na washirika wake dhidi ya Iraq yalifanywa kwa kisingizio cha kuwaletea demokrasia wananchi wa nchi hiyo, lakini wavamizi hao hawajawaletea chochote wananchi hao ghairi ya machafuko na mauaji. Hii ni katika hali ambayo, Marekani ilikuwa ikimuunga mkono kijeshi, kisiasa na kiuchumi dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein.

Mpenzi msomaji na mfuatiliaji wa makala hizi za Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa na Changamoto, sehemu ya nne ya makala yetu inaishia hapa. Sehemu ijayo ya makala hii mbali na kuzungumzia umuhimu wa kuweko kambi moja au mtazamo mmoja katika ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto unazozikabili, itatupia jicho pia uwezo na suhula zilizoko katika nchi za Kiislamu. Wassaalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget