Monday, February 20, 2012

Isbaal – Vazi La Mwanamme Lenye Kuvuka Mafundo Ya Miguu (Uburuzaji Au Kuburura)


Isbaal ni urefushaji wa kitu na makusudio hapa katika makala hii ambayo itazungumzia vazi la mwanamme, makusudio yake kishari’ah ni kuvaa kivazi chochote chenye kuvuka chini ya mafundo ya miguu kwa mwanamme; iwe ni kikoi, shuka, kanzu, joho au suruali.  Nalo ni jambo lenye kukatazwa na limeharamishwa kwa nuswuus (maandiko) mbalimbali ya kishari’ah kutoka katika Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Lengo la makala haya, ni kuwatanabahisha Waislam wanaume kuhusiana na ubaya na madhara ya jambo hilo na pia kuweka sawa ufahamu wa makatazo hayo kuwa hayawahusu tu wenyye kuvaa kwa kiburi au kwa fakhari, bali ni kwa wanaume wote wa hali zote.

Kwa kumkumbusha aliyesahau, kumjuza asiyejua, na kumweka sawa mwenye ufahamu wa kinyume wa Hadiyth hizo za Mtume wetu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tutakuwa tumesaidiana katika kuyaepuka makatazo ambayo yanaweza yakawa sababu ya kutupwa motoni kwa jambo ambalo si zito kabisa kuliepuka. Na pia kwa kukumbushana huku, kutatusaidia kufuata mafunzo ya kipenzi chetu na kufanana naye pamoja na Maswahaba zake wema kama tutakavyoona katika makala haya inshaAllaah.

Na kwa kuwa wengi wetu wanaliona jambo hili la Isbaal ni jambo dogo sana na halina maana hata ya kulizungumzia au kukumbushana, tunapenda kumkumbusha mwenye fikra finyu kama hiyo kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitujulisha kuhusu watu wa makaburi mawili ambayo alipita katikati yake, akasema:
“Hakika hawa wanaadhibiwa na hawaadhibiwi kwa mambo makubwa; ama mmoja wao alikuwa hajilindi na chembe chembe za mkojo, na mwengine alikuwa akipita na kuhamisha maneno (umbea)”Al-Bukhaariy na Muslim.

Makusudio hapo ya kuwa walikuwa hawaadhibiwi kwa mambo makubwa, ni kuwa kwa mtazamo wao au dhana zao, hayo waliyokuwa wakiyafanya yalikuwa si makubwa kwao. Lakini kiuhakika hayo ni makubwa na ndio maana wakawa wanaadhibiwa.

Hivyo, ndugu Waislam, wale wenye mawazo ya kuwa suruali yake ikiwa ndefu na kuvuka mafundo yake ya miguu, kuwa  ni jambo dogo sana, basi ni bora ajihadhari tena ajihadhari na amche Mola wake mapema. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) singeweza kutoa makemeo makali kama tutakyosoma huko chini ikiwa jambo hilo si zito na kubwa. Suruali zetu, kanzu zetu, majoho tunayovaa ya kuolea au kutolea khutbah za Ijumaa na siku ya ‘Iyd au suti za ofisini na za harusini, zisije kuwa ni sababu ya kututumbukiza kwenye moto na kufanya tusitazamwe na Allaah, au kusemeshwa Naye au kutakaswa Naye na mwisho kupata adhabu iumizayo.
Hadiyth zifuatazo zinatoa kwa uwazi makatazo ya mtu kufanya Isbaal (kuburuza/kuburuta nguo yake):

1- Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Chenye kuvuka chini ya mafundo ya miguu katika vazi hupelekea motoni” Al-Bukhaariy

2- Kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Watu watatu Hatowasemesha Mwenyeezi Mungu siku ya Qiyaamah, na  Hatowatazama, na Hatowatakasa, na watakuwa na adhabu iumizayo. Akarudia mara tatu. Abu Dharr akasema: Wameangamia na wamekhasirika hao ni nani ee Mjumbe wa Allaah? Akasema (Mtume): (Hao ni) Al-Musbil – Mwenye kuburuza nguo yake, Mwenye kutoa na kukizungumzia (kusimbulia) alichokitoa, Na mwenye kuuza bidhaa zake kwa kutumia kiapo cha uongo” Muslim

3- Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) anasema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
Mtu mmoja alipokuwa anatembea, huku anaburuza nguo yake kwa kibri, alifanywa amezwe na ardhi na ataendelea kudidimia ndani yake mpaka siku ya Qiyaamah” Al-Bukhaariy

Pamoja na makatazo yote hayo yaliyotangulia yaliyoambatana na makemeo, makaripio, na maonyo ya mwisho mbaya wa jambo hilo,  na pamoja na kuwa Isbaal – kuburuza nguo ni katika madhambi makubwa, lakini utakuta watu wengi wanatumbukia katika madhambi hayo ima kwa wengi kutokujua ubaya wake, wengine kwa kughafilika, na wengine wanaojua hayo bado wanaendelea kubaki katika hali hiyo wakidai kuwa makatazo hayo yanahusu wenye kuvaa nguo ndefu (wanaoburuza au kuburuta) kwa kiburi wakitegemea baadhi ya Hadiyth zinazoonyesha hivyo.

Hata hivyo, mtu huyo huyo anayetoa hoja hiyo; awe ni Mwanachuoni, mtafutaji elimu au mtu wa kawaida, anajua wazi kabisa kuwa, ikiwa mwenyewe ameamua kuvaa kwa kuburuza vazi lake hilo pamoja na kufahamu maelezo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au utamkuta amekwenda mwenyewe dukani na kuchagua vazi refu lenye kuburuza, au aende kwa fundi na kumtaka amshonee suruali au kanzu yenye urefu huo unaovuka mafundoni na labda wakati fundi akiteremsha utepe wake wa kupimia kwenye mafundo yake, atamwambia teremsha kidogo chini ya mafundo…je, hapo ataweza kudai kuwa hicho si kiburi na hali ameshasikia au kuziona au kujulishwa Ahaadiyth zote za Mtume zenye kukemea, kukaripia, na kukataza jambo hilo? Na kama hicho si kiburi basi kiburi kitakuwa kipi?


Kuwa Isbaal Inawahusu Wenye Kuvaa Kwa Kiburi Au Kwa Fakhari Tu

Baadhi ya watu wanarukhusu Isbaal kwa kudai kuwa makatazo yaliyokuja katika Hadiyth mbalimbali ni kwa wale tu wanaovaa kwa kiburi au kujifakharisha. Ima kwa wale wanaovaa tu bila kukusudia kiburi basi inafaa na hakuna ubaya wowote. Wakitoa hoja kwa kutumia baadhi ya Hadiyth, mojawapo ya Hadiyth hizo ni Hadiyth maarufu ya kumhusu Abu Bakr (Radhiya Allaahu kuwa nguo yake ilikuwa ikiburuza, ambayo Mtume ‘anhu) anasema:
“Mwenye kuburuza nguo yake kwa kiburi, Allaah Hatomtazama siku ya Qiyaamah” Abu Bakr akasema: Ee Mjumbe wa Allaah! Upande mmoja wa kikoi changu unashuka hadi niuvute na kuuzuia, Mtume akamjibu: Wewe si mwenye kufanya kwa kiburi”Imesimuliwa na al-Bukhaariy


Majibu Ya Hoja Hiyo:

Kwa kujibu hoja yao ya kutegemea Hadiyth hiyo kuonyesha kuwa Abu Bakr alikuwa akiburuza nguo yake, tunajibu kwa maneno ya Wanachuoni ambao wameunganisha Hadiyth za pande zote kuhusiana na suala hilo na kuweka ufahamu ulio sahihi:

1- Ametaja Mwanachuoni Ibn Hajar kuwa, katika masimulizi ya Imaam At-Tirmidhiy kuna ziada baada ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Atakayeburuza nguo yake kwa fakhari (kiburi), Hatomtazama Allaah mtu huyo siku ya Qiyaamah), akasema Ummu Salamah: Je, watafanyaje wanawake na mikia yao (nguo zao zenye kuburuza)? Akasema (Mtume): Waongeze shibri (kiasi cha kiganja kimoja), Akasema (Ummu Salamah): Hata hivyo bado miguu yao itakuwa wazi. Akajibu (Mtume): Basi wazidishe dhiraa na si zaidi ya hapo.”

Ibn Hajar akasema: Alivyofahamu – yaani Ummu Salamah – ni kuwa makatazo ya kuburuzwa kwa nguo makusudio yake ni kwa hali zote; iwe kwa kiburi au bila kiburi. Ndipo alipomuuliza Mtume hukumu ya wanawake kuhusiana na hilo kwa kuhitajia kwao kuburuza ili waweze kujistiri vizuri miguu yao ili isiwe uchi… kisha akaendelea kusema Ibn Hajar katika uchambuzi wake: Na Qaadhi ‘Iyaadhw amenukuu ‘Ijmaa’ (makubaliano) ya kuwa makatazo ya Isbaal ni kwa wanaume na si wanawake, na makusudio yake ni kuwa kukatazwa kwa Isbaal ni kwa kukariri kwake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Ummu Salamah ili kumfahamisha. Fat-hul Baariy Mj. 10, uk. 259.


2- Na akasema Ibn Hajar (Allaah Amrehemu): Ama Isbaal bila ya kiburi, ni wazi kutokana na Hadiyth mbalimbali kuwa ni Haraam. Kisha akasema: Na ikiwa nguo ni ndefu kuliko urefu wa mtu mwenyewe basi hiyo huenda ikapelekea kwenye makatazo kwa ajili ya israfu na kufikia kwenye uharamu. Na vilevile inapelekea makatazo kwa kufanana nako na mavazi ya wanawake, na hii inawezekana zaidi kuliko sababu ya mwanzo. Na kadhalika ameeleza Al-Haakim usahihi wa Hadiyth iliyopokelewa na Abu Hurayrah kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwanamme anayevaa mavazi ya mwanamke. Vilevile yanapelekea makatazo ya Isbaal kwa mwenye kuvaa kutosalimika na kupatwa vazi lake na najisi kwa upande mwengine. Fat-hul Baariy Mj. 10, uk. 263.


3- Ibn Al-‘Arabiy (Abu Bakr) naye kasema: Haijuzu kwa mwanamme kuachia nguo yake kuvuka mafundo ya miguu, na akasema: Siburuzi kwa kiburi, kwa kuwa makatazo yanaweza kuhusu hali hiyo kimatamshi, na wala haijuzu kwa mwenye kuchukulia matamshi hayo ya makatazo kwa kiburi kuwa ndio hukumu akasema: Mimi hukumu hiyo hainihusu kwa kuwa ‘ilah(sababu) yake hainihusu. Hakika anayesema hivyo, ajue kuwa madai hayo hayajasalimika, bali ni kuwa kurefusha nguo na kuvuka mafundo kunaonyesha kiburi chake (huyo mwenye kurefusha). Fat-hul Baariy Mj.10, uk. 264.


4- Isbaal ni mwelekeo wa kiburi. Anasema Ibn Hajar (Allaah Amrehemu): Isbaal inalazimu kuburuzika kwa nguo, na kuburuzika kwa nguo kunalazimu kiburi japo ikiwa mwenye kuvaa hajakusudia kiburi. Na yanaungwa mkono maneno yake hayo na aliyosimulia Ahmad bin Muniy’i kwa upande mwengine kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kutoka katika Hadiyth ambayo inasema,
“Ole wako na kuburuza nguo (kuvuka mafundo ya miguu), kwani kuburuza nguo ni alama ya kiburi”. Fat-hul Baariy Mj.10, uk. 264.


5- Amesema Mwanachuoni Shaykh Muhammad bin Swaalih bin Al-‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) kuhusu Hadiyth hii,
“Mwenye kuburuza nguo yake kwa kiburi, Allaah Hatomtazama siku ya Qiyaamah” na Hadiyth hii, “Chenye kuwa chini ya mafundo ya miguu katika mavazi, basi ni motoni”: Kwa kuwa kumekhitilafiana adhabu hizo mbili, basi kunakatazika kuifanya hukumu hiyo (ya Isbaal) kuwa ‘Mutwlaq’ (iliyo wazi ya moja kwa moja) ni yenye kuwa juu ya ‘Muqayyad’ (iliyofungamanishwa na kitu), kwani kanuni ya kubeba ‘Mutwlaq’ juu ya ‘Muqayyad’ ni sharti kukubaliana ‘Nasw’ (maandiko) mbili katika hukumu. Ama ikitofautiana hukumu (kama ilivyo kwenye hizo Hadiyth mbili juu) basi haibebeshwi mojawapo juu ya mwenzake. Na hivyo ndivyo hata Aayah ya kutayamamu ambayo Amesema Allah:
Na mpanguse nyuso zenu na mikono yenu kwayo” haikufunganishwa na Aayah ya Wudhuu ambayo Allaah Amesema:
“Na muoshe nyuso zenu na mikono yenu hadi kwenye viwiko” maana haiwi Tayammum hadi kwenye viwiko.


6- Naye Mwanachuoni mwengine, Shaykh Mash-huur Aal-Salmaan (Allaah Amhifadhi) anasema: Na ametupa faida Shaykh wetu Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) katika baadhi ya vikao vyake kwamba haijuzu Muislam kukusudia kurefusha vazi lake miguuni kwa madai kuwa hafanyi hivyo kwa kiburi, na anaunganisha hayo kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyomwambia Abu Bakr, “Wewe si mwenye kufanya kwa kiburi”, kwa sababu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuwa akivaa nguo ndefu, na Mtume akamwambia, “Wewe si mwenye kufanya kwa kiburi”, ila hayo majibu ya Mtume kwa Abu Bakr yalikuwa ni kwa sababu Abu Bakr vazi lake lilikuwa lamshuka lenyewe, na akawa akionekana ni kama mwenye kurefusha nguo. Na Mtume akamjibu kumwambia kuwa hilo ni jambo ambalo huchukuliwi kwalo, kwani hujakusudia na wala hukulifanya kwa kiburi. Hivyo, ni makosa kabisa watu kuuunganisha tukio la Abu Bakr na kuburuza kwao nguo kwa makusudi kisha wakadai kuwa: ‘Sisi hatufanyi kwa kiburi’! Tukio la Abu Bakr haliwezi katu kuwa hoja ya wanayoyafanya.


7- Amesema Mwanachuoni Faqiyh Shaykh Muhammad bin Swaalih bin Al-‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu): “Hakika Abu Bakr katakaswa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatoa Mtume ushahidi kuwa Abu Bakr si katika wale wanaofanya hivyo (kuvaa nguo ikaburuza) kwa fakhari. Sasa je, hao wanaovaa nguo zikavuka mafundo (zikaburuza) wamepata utakaso au ushuhuda kama huo wa Abu Bakr?!

Lakini Shaytwaan anawafungulia baadhi ya watu milango ya kufuata yale maandiko yenye utata kwenye Qur-aan na Sunnah ili yaendane na matashi yao na yale wayafanyayo, na Allaah Ndiye Humuongoza Amtakaye katika njia nyoofu, tunamuomba Allaah Atupe sisi na wao hidaaya”

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget