Friday, February 24, 2012

Hakuna Kulazimishana Katika Dini


Hakuna Kulazimishana Katika Dini

Imefasiriwa na Muhammad Faraj Saalim Al-Saiy
 Ni wajibu wa kila Muislamu kufahamu kuwa miongoni mwa mafundisho muhimu na ya msingi yasiyopingika katika dini yaliyomo ndani ya Qurani na ndani ya mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) ni kuwa hapana kulazimisha katika dini.
 Lazima afahamu haya kwa sababu kutokana na kuzidi kuenea, kukubalika na kufuatwa dini hii na watu wengi sana huko Ulaya na Marekani, maadui wa Islam wanajaribu kuwadanganya watu kuwa eti dini hii imeenezwa kwa ncha ya upanga.
 Kila Muislamu anawajibika kuufahamu na kuufikisha ujumbe huu pamoja na dalili zake kwa kila mtu ili ukweli udhihiri na uongo ujitenge, kisha baada ya hapo anayetaka kufuata afuate na anayetaka kuendelea kupinga na aendelee. Hairuhusiwi kwa vyovyote vile kuwatisha watu wala kuwadhuru ikiwa hawataki kuukubali Uislamu.
 Zifuatazo ni baadhi ya dalili zisizopingika kuhusu maudhui haya:
 Mwenyezi Mungu anasema:
"Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua."
Al Baqarah – 256
 Na akasema:
"Angeli taka Mola wako Mlezi wangeli amini wote waliomo katika ardhi. Je, wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe Waumini?."
Yunus – 99
Na akasema:
"Na pindi wakikuhoji, basi sema: Mimi nimeusalimisha uso wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu, na kadhaalika walio nifuata. Na waambie walio pewa Kitabu na wasio na kisomo: Je! Mmesilimu? Wakisilimu basi wameongoka. Na wakikengeuka basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake."
Al Imran -20
 Na akasema:
"Haimlazimu Mtume ila kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnacho kidhihirisha na mnacho kificha."
Al Maidah – 99
 Ni muhimu kufahamu pia kuwa aya mbili za mwisho zimeteremshwa Madina, wakati Waislamu wakiwa na nguvu. Hili lina umuhimu wake ili mtu asiseme kuwa huenda amri hizo ziliteremka Makkah wakati Waislamu walipokuwa wachache na dhaifu.
 Mtu anaweza kushangazwa akajiuliza: 'Ikiwa dini ya Kiislamu inafundisha mafundisho haya, nini basi hizi habari tunazozisikia juu ya Jihadi? Tutawafahamisha vipi watu juu ya vita alivyopigana Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) pamoja na Sahaba zake (Radhiya Llahu anhum) dhidi ya washirikina?'
 Jawabu ni kuwa; Jihadi 'Vita vitakatifu' vinapiganwa kwa sababu nyingi, lakini kuwalazimisha watu kuingia katika dini si mojawapo ya sababu hizo. Sababu asili ya kufaridhishwa Jihadi ni kuwaruhusu Waislamu kujitetea nafsi zao kutokana na mateso na mauaji na kufukuzwa majumbani mwao.
 Mwenyezi Mungu anasema:
 "Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.
Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nyumba za wat'awa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu."
Al Hajj – 39-40

 Wengi miongoni mwa maulamaa waliotangulia wamesema kuwa hizi ni aya za mwanzo zilizoteremshwa kuhusu Jihadi, kisha zikateremshwa aya zifuatazo:
 "Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanao kupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao uadui. Na wauweni popote mwakutapo, na muwatoe popote walipo kutoeni; kwani fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala msipigane nao kwenye Msikiti Mtakatifu mpaka wakupigeni huko. Wakikupigeni huko basi nanyi pia wapigeni. Na hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri.
 Lakini wakiacha basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha basi usiweko uadui ila kwa madhalimu."
Al Baqarah – 190-193

Kutokana na aya zilizotangulia tunaona kuwa maana ya Jihadi ikaongezeka kutoka katika hali ya kujitetea tu na uadui, Waislamu wakaruhusiwa kupambana na wanaowafanyia uadui na pia wenye kuwanyima uhuru wa kuabudu na kuchagua dini wanayoitaka wenye na kuwazuwia kuilingania dini yao.

Lakini katika kuieneza dini, Waislamu wanatakiwa kutumia njia za kielimu usalama na amani pekee kwa kutumia ndimi na kalamu zao. Silaha hairuhusiwi kutumika isipokuwa dhidi ya wenye kuwazuwia kufanya ibada zao na dhidi ya wenye kuwazuwia Waislamu kuilingania dini yao. Waislamu hawawezi kukaa kimya na kutizama kwa macho tu huku watu wakinyimwa haki yao ya kuamini na sauti zao zikinyamazishwa. Na hii ndiyo maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:

 "Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha basi usiweko uadui ila kwa madhalimu."
Al Baqarah –193


Katika barua aliyomuandikia Heracles mfalme wa Warumi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) alimuambia:
"Nakuita katika Uislamu. Ukiukubali utapata amani. Ukiukubali Uislamu Mwenyezi Mungu atakulipa mema mara mbili. Na kama utaukataa basi utabeba dhambi za watu wako."
Sahih Muslim

 Muislamu akiweza kuufikisha ujumbe kwa watu bila ya pingamizi, anakuwa keshatimiza jukumu lake. Anayetaka kuamini anakuwa huru kufanya hivyo, na asiyetaka pia yuko huru.


Hata pale Waislamu wanapolazimika kupigana vita wakafanikiwa kuteka nchi, basi jukumu lao linakuwa kuiweka sheria ya Mwenyezi Mungu katika nchi hiyo na kuweka haki sawa baina ya watu wote. Waislamu na wasiokuwa waislamu. Hawana haki ya kuwalazimisha raia kuukubali Uislamu dhidi ya matakwa yao. Wasiokuwa waislamu lazima wapewe haki ya kufanya ibada zao, isipokuwa watalazimika kuiheshimu sheria ya nchi.
  
Ingelikuwa sababu ya kupigana jihadi ni kuwalazimisha watu kufuata dini ya Kiislamu basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) asingewaamrisha Waislamu kutowashambulia maadui pale wanapoacha kupigana wakarudi nyuma, na asingekataza kuua wanawake na watoto, na hivi ndivyo alivyofanya.


Siku moja katika vita, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) aliona kundi la watu limejikusanya. Akatuma mtu kutaka kujuwa kuna nini. Akaambiwa kuwa watu wameizunguka maiti ya mwanamke aliyeuliwa. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) akasema:  "Asingeshambuliwa!"
Khalid bin Al Waliyd (Radhiya Llahu anhu) ndiye aliyekuwa kiongozi wa majeshi hayo, kwa hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) alimtuma mtu kwa Khalid akamuambia:
"Muambie Khalid asiue wanawake wala wafanya kazi."
Sunan Abi Daud
   
 Hata katika vita vikali dhidi ya adui, wanaoruhusiwa kushambuliwa na kuuliwa ni wapiganaji tu.

Ingelikuwa sababu ya kupigana jihadi ni kuwalazimisha wasioamini kufuata dini ya Kiislamu basi Makhalifa walioongoka (Radhiya Llahu anhum) wasingekataza watu kuwaua makasisi na wacha Mungu wasioshiriki katika kuwapiga vita Waislamu.


Khalifa wa Waislamu Umar bin Khattab (Radhiya Llahu anhu) akilihutubia jeshi lake lililokuwalikijitayarisha kwenda Syria kupambana na Warumi waliokuwa wakiwashambulia Waislamu aliwaambia:
  
"Mtawakuta watu waliojitenga kwa ajili ya shughuli za ibada tu (makasisi). Hao waacheni waendelee na wanayofanya na wala msiwadhuru."
  
Tumekwisha onyesha hoja mbali mbali kuthibitisha kuwa katika misingi ya mafundisho ya dini ya Kiislamu ni kuwa hapana kulazimisha katika dini, na tukaelezea juu ya malengo na sababu za kupigana jihadi, na hivi sasa tutaelezea juu ya baadhi ya mafundisho yaliyowakanganya baadhi ya watu wakayatafsiri vibaya.

 Moja katika mafundisho hayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
"Na ikisha miezi mitukufu basi wauweni washirikina popote mwakutapo, na washikeni na wazungukeni, na wavizieni katika kila njia."
Al Tawbah -5

 Baadhi ya watu, hasa wale waliojiunga hivi karibuni katika kuandika dhidi ya dini ya Kiislamu wanadai kuwa eti aya hi inaifuta ile aya isemayo:
"Hapana kulazimisha katika Dini."


Wanadai kuwa eti aya hii "Na ikisha miezi mitukufu basi wauweni washirikina popote mwakutapo…", kwa ujumla inataka kila asiyekuwa muislamu apigwe vita. Wanasema kuwa dalili ni kuwa aya hii ni katika aya za mwisho kuteremshwa juu ya vita.

 Ukweli ni kuwa aya hii haikuletwa kwa ajili ya kufuta msingi wa mafundisho ya Kiislamu kuwa hapana kulazimishana katika dini. Inaweza kuwa inaonyesha hivyo katika maneno yake, lakini tafsiri yake inafahamika vizuri kwa kuzisoma aya zilizokamatana na aya hii pamoja na hadithi zinazoelezea sababu za kuteremshwa kwa aya hii ambazo tutazungumza juu yake kila tukiendelea mbele na darsa hii.

 Waliokusudiwa katika aya hii ni washirikina wa Kiarabu peke yao waliojishughulisha na kuwapiga vita Waislamu wakati ule. Kwani wao waliivunja mikataba yote iliyokuwepo baina yao na Waislamu.
Aya hii haizungumzi juu ya washirikina wengine wa Kiarabu wasiovunja mikataba na wale wasiochukuwa silaha kuwapiga vita Waislamu, na bila shaka haizungumzi juu ya Mayahudi na Manasara na haizungumzi pia juu ya washirikina walio nje ya bara ya Arabu.

 Tutaweza kuifahamu vizuri tafsiri ya aya hii tunayoizungumzia ikiwa tutautizama vizuri mfumo wote wa aya hizi - zile aya zilizo kabla na baada ya aya hii zilizomo katika Surat al Tawbah.

Aya ya mwanzo na ya pili katika sura ya Al Tawbah zinasema:

"Huku ni kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwenye jukumu la maagano na mlio ahidiana nao katika washirikina.
Basi tembeeni katika nchi miezi mine, na jueni kwamba nyinyi hamwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anaye wahizi makafiri."
Al Tawbah -1-2



Katika aya hizi tunaona kuwa washirikina walipewa miezi mine ya amani huku wakijulishwa kuwa baada ya kumalizika miezi mine hiyo mapambano yataanza tena.dhidi yao. Lakini katika aya ya nne ya sura hiyo hiyo Mwenyezi Mungu amewatenga mbali washirikina wengine katika kuanzisha tena mapambano nao.
Mwenyezi Mungu anasema:


"Isipo kuwa washirikina ambao mliahidiana nao kisha wasikupunguzieni chochote, wala hawakumsaidia yeyote dhidi yenu, basi hao watimizieni ahadi yao mpaka muda wao. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wacha-Mungu."
Al Tawbah -4


Kwa hivyo katika aya ya tano Mwenyezi Mungu anaposema:


"Na ikisha miezi mitukufu basi wauweni washirikina popote mwakutapo, na washikeni na wazungukeni, na wavizieni katika kila njia."
Al Tawbah -5

Lazima tuelewe kuwa kuwa aya hii haijumuishi wote wasiokuwa Waislamu na kwamba aya inazungumza juu ya kundi maalum la washirikina wa Kiarabu waliokuwa vitani dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) na ni wale tu waliovunja ahadi.



Haya yanafahamika vizuri zaidi kama tutaendelea kusoma hadi kuifikia aya ya 13 ya sura hii ya Al Tawbah, Mwenyezi Mungu aliposema:


"Je, hamtapigana na watu walio vunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumfukuza Mtume, nao ndio walio kuanzeni mara ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumwogope, ikiwa nyinyi ni Waumini."

 Katika kuifasiri aya hii amesema Ibn Al Arabi:
  
"Ni wazi kabisa kuwa maana ya aya hii ni kuwaua washirikina waliokuwa wakiwapiga vita Waislamu."
Ahkam al Quran (2/456)

 Katika aya iliyokuja baada ya aya tunayoizungumzia Mwenyezi Mungu anasema:

"Itakuwaje iwepo ahadi na washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake, ila wale mlio ahidiana nao kwenye Msikiti Mtakatifu? Basi maadamu wanakwenda nanyi sawa, nanyi pia nendeni sawa nao. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wachamungu." 
Al Tawbah – 7



Fundisho lingine waliloshindwa kufahamu maana yake ni hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) aliposema:
"Nimeamrishwa kupambana na watu mpaka wakubali kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah, na kwamba mimi ni mjumbe wa Allah. Wakinitii katika hilo basi damu zao na mali zao zitakuwa haramu isipokuwa katika haki zake.[1]"
Bukhari na Muslim

 Hapana wasiwasi wowote juu ya usahihi wa hadithi hii, kwa vile imo ndani ya Sahih al Bukhari na Sahih Muslim. Hata hivyo, hadithi hii haijuzu kufasiriwa kwa ujumla nje ya mfumo wake bila kujali ushahidi mwingine ulioambatana nayo.

Neno 'Watu' katika hadithi hii haina maana ya watu wote.
Anasema Ibn Taymiyah:


"Linakusudiwa tu wale wanaopigana vita dhidi ya Waislamu, wale ambao Mwenyezi Mungu ameturuhusu kupambana nao. Halikusudiwi wale tulioahidiana nao ambao Mwenyezi Mungu anatuamrisha kutimiza ahadi zetu.
(Majmû` al-Fatâwâ (19/20))

  Mwenyezi Mungu anawaamrisha Waislamu wawe waadilifu kwa wenye itikadi nyingine, wawe Mayahudi au Manasara au washirikina. Uislamu unatufundisha kuwa wapole nao na kujaribu kufanya urafiki nao ikiwa hawajachukuwa silaha na kutupiga vita.
Mwenyezi Mungu anasema:

 "Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu.
Hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni kufanya urafiki na wale walio kupigeni vita, na wakakutoeni makwenu, na wakasaidia katika kufukuzwa kwenu. Na wanao wafanya hao marafiki basi hao ndio madhaalimu."
Al-Mumtahanah: 8-9
 Mwenyezi Mungu anawaamrisha Waislamu kuwaheshimu wazazi wao wasiokuwa Waislamu na kuishi nao kwa kwema.
Qurani inatufundisha kujadiliana nao kwa njia nzuri.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake."
Al-`Ankabût: 46
Tunaamrishwa pia kutimiza ahadi zilizo baina yetu na wasiokuwa Waislamu na kwamba tusiwaendee kinyume wala kuvuka mipaka dhidi yao.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam) alitupa onyo kali sana na kutukataza kuua wasiokuwa waislamu tulio na mikataba ya amani baina yao. Alisema:
"Yeyote atakayemuua katika wale tulio na mikataba ya amani nao hatoionja harufu ya Peponi."  Sahih Muslim
 Mtu haukubaliwi uislamu wake ikiwa hajaiamini Mitume yote walioletwa kabla yake (Swallah Llahu alayhi wa Ssallam).
Mwenyezi Mungu anasema:
"Enyi mlio amini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha kabla yake. Na anaye mkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Akhera, basi huyo amekwisha potelea mbali."
Al Nisaa -136

[1] (Kwa sababu ni haramu kumwaga damu ya Muislamu na hata asiyekuwa Muislamu anayeishi kwa amani chini ya himaya ya dola ya Kiislamu.
Na pia ni haramu kuchukua mali zao (isipokuwa kwa haki yake) yaani aliyeua anauawa na mwenye kudhulumu au kukataa kulipa Zaka  analazimishwa kulipa haki za watu.).

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget