Thursday, February 16, 2012

Lowassa asipokua rais 2015,Mniue–Askofu


Kiongozi mkuu wa kanisa la Last Glory Church la hapa nchini Basileus Ezekiel Mabumba, amesema amepokea ujumbe kutoka kwa Mungu unaoeleza kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzuru, Edward Ngoyay Lowassa, atakua rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Katika mahojiano na gazeti hili (Nyakati), Mabumba alieleza kuwa atawajibika iwapo unabii wake hautatimia. Kwa mujibu wa Torati kile ambacho kilikuja kubainika baadaye kuwa unabii wa uongo, adhabu kwa mtoaji unabii ilikua ni kupigwa mawe hadi afe.

Jumatano iliyopita, Mabumba alitinga katika ofisi za gazeti hili na kueleza kuwa, kwa muda mrefu sasa amekua akipokea ujumbe kutoka kwa Mungu ukieleza kuwa Lowassa ndiye atakuwa rais wa nchi hii ya awamu ya tano.

Sehemu ya mahojiano ya gazeti hili na Askofu Mabumba, ambaye hujulikana pia kama Mtume, ilikua kama ifuatavyo:

Mwandishi: Umesema kwa muda mrefu umekuwa ukiletewa huo ujumbe. Tuambie ni tangu lini? Tuambie pia mtu wa kawaida kabisa anaelewa nini kuhusu unabii?

Mabumba: Tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Kwa uhakika unabii huu nimepata kuwaeleza waumini pale kanisani. Sasa nimeona niufikishe kwa watu wengi zaidi.

Unabii ni tofauti na kutabiri. Kuna unabii wa aina mbili. Kwanza, ni ule unabii ambao Mungu anakuruhusu kuona mambo yajayo. Ni pale Mungu anapokuonyesha kutakua na nini siku zijazo. Ni karama za ufunuo. Aina ya pili ya unabii ni pale mtu aliyekusudiwa kufikisha unabii huo anaweza kutamka jambo kwa msukumo wa Roho Mtakatifu. Sasa hapo ndio ujue kwamba kuna msukumo wa kibinadamu, wazo la mwanadamu mwenyewe, msukumo wa shetani na msukumo wa Mungu.

Mwandishi: Sasa Mtu anaweza kutofautisha vipi kama jambo fulani lina msukumo wa mwanadamu, kwa Shetani au wa Mungu?

Mabumba: Unajua kama ni la Mungu kuna msukumo unaolazimisha kulitafakari kila mara kabla hujalikubali. Unakua kama una mzigo fulani ukikubaliana na Mungu ndipo utapata amani ya kulisema.

Mwandishi: Lakini kuna nabii nyingi zimetolewa na watumishi hazikutimia. Kuna mtumishi aliwahi kusema angesigina Biblia iwapo unabii wake usingetimia. Haukutimia na hakusigina, leo yuko kimya. Mwingine akasema kutakua na vita…ziko nabii nyingi tu.

Mabumba: Unabii wangu lazima utimie nimekua nikioneshwa mambo mengi lakini siyatamki. Kuna vitu vidogo  vidogo nimeoneshwa na ikawa kweli. Yako na mambo makubwa labda kwa sababu sikuwa ninayasema kama ninavyofanya leo kwa hili. Hili ninasukumwa sana kulitamka.

Mwandishi: Usipotimia?

Mabumba: Niko tayari kuwajibika. Manabii waliwajibika kwa unabii wao. Hata nisipopondwa mawe, watu hawataniamini tena, hayo tayari ni ‘mawe’

Mwandishi: Kwa mazingira ya sasa ambayo watu wamepunguza imani wapo ambao wanaweza kufikiri kuwa umetumwa na unatumia nafasi yako ya utumishi wa Mungu kutumikia wanasiasa? Wengine wanaweza kufikiria kuwa unatafuta umaarufu.

Mabumba: Kwanza kabisa sitaki kuwa karibu na wanasiasa, hata chama sina, sijishughulishi kabisa na wanasiasa. Sifahamiani na Lowassa. Na ninafikiri kama ni hivyo Lowassa mwenyewe angeenda kwa wahubiri wakubwa. Mimi ninasema nilicholetewa.

Kama kuna watakaofikiria ninatafuta umaarufu, watakuwa wamekosea. Sihitaji umaarufu zaidi ya hapa. Naandika vitabu watu wengi wananifahamu kupitia huduma hiyo. Ninaandika vitabu na vinapendwa, inatosha. Siwezi kutumia unabii feki kujijenga.

Mwandishi: Unaweza kuzungumza chochote kuhusu dhana ya kujivua gamba ndani ya CCM ambacho Lowassa ni mwanachama na kiongozi?

Mabumba: Sifuatilii mambo ya vyama. Kwa habari ya unabii Mungu anakuonesha kidogo tu. Hayo mengine siyajui bwana. Kama kuna kuna kuvuana gamba mi sijui.

Lowassa Waziri Mkuu aliyejiuzuru kutokana na kashfa ya Kampuni ya umeme ya Richmond hajapata kutangaza hadharani kuwa ana nia ya kugombea urais mwaka 2015, lakini harakati za kisiasa ndani na nje ya chama chake cha CCM zinaashiria kuwa ni mmoja wa wanasiasa walioko katika ‘vita’ ya urais.

Hivi karibuni Lowassa alionekana katika televisheni akishiriki kwenye ibada katika kanisa linaloongozwa na mhubiri maarufu wa nchini Nigeria, TB Joshua.

Kushiriki kwa Lowassa katika ibada hiyo kulizua minong’ono, wengine wakihusisha na harakati za urais 2015 na kwamba alienda kuombewa ili ‘nyota yake ing’ae’.

Hata hivyo baadhi ya watumishi wa Mungu walikerwa na kitendo cha baadhi ya watu kushangazwa na uwepo wa Lowassa katika Ibada hiyo, wakisema ni kuingilia uamuzi binafsi wa mtu anayemtafuta Mungu wake.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget