Friday, February 10, 2012

Uislamu na manufaa


MUISLAMU wa kawaida unamuliza, nini maana ya Uislamu? Bila shaka atajibu suala au swali hili kwa lugha fupi tu mfano wa maisha. Si busara kuridhika tu na lugha fupi kama hii kwani katika kulikubali hilo hali ya ujinga fulani inaweza kujengeka au kujitokeza katika wafuasi wa Uislamu.

Mwenyezi Mungu ameuweka wazi Uislamu katika mambo makuu mawili. Jambo la kwanza ni suala la maada na roho. Vyote hivi viwili vinategemeana. Kinyume chake Uislamu utakuwa umekosewa na hivyo ndiyo kusema kuwa Waislamu hawawezi kupata maisha bora hapa duniani na akhera kwa ujumla.
Mali ya asili ni muhimu sana katika shughuli za uchumi. Kwa mfano, ardhi, bahari, maziwa, mito, mabonde, wanyapori, miti, madini na kadhalika ni miongoni mwa maliasili tulizopewa na Muumba wetu. Shurti la matumizi ya vitu vyote hivi ni kwamba vitumike vizuri kwa faida ya kukidhi mahitaji ya binadamu na kuondoa kama siyo kupunguza umaskini uanomzunguka. Je, Mwenyezi Mungu anazungumzia nini katika kitabu chake juu ya maliasili? Mwenyeiz Mungu anasema: "Yeye ndiye aliyekuumbieni vyote vilivyomo ardhini" (2:29)

Tunalazimika kuishi kufuatana na aya hii maisha yetu yote ili tupate mafanikio ya kiuchumi. Lakini leo ni tofauti sana kiasi kwamba maisha ya kizazi chetu kipya tumeyaweka katika mashaka makubwa. Bado hatujajenga misingi mizuri ya kutumia maliasili kwa maendeleo yetu mbalimbali.

Pia tunayo dhana kuwa hili halituhusu, bali linawahusu watu nje ya Waislamu. Pia dhana hii ni potofu na inachangia kutuweka kwenye umaskini zaidi. Na ile dua tunayoomba katika sala au baada ya sala zetu za kila siku, yaani tupe dunia nzuri, na tupe akhera nzuri, bado haijafanyiwa kazi. Inatosha kusema tumeifanya dua hii ni wimbo tu. Kutokana na hali hii, hivi sasa tunaomba misaada kutoka kwa wafadhili mbalimbali kujenga na kuendesha asasi na taasisi zetu hapa nchini. Kuna haja kubwa mno kupiga vita hali hii ya omba omba ili tuweze kurejesha heshma yetu ambayo imepotea.

Wakati wa utawala wa Khalifa Umar (r.a.) jamii yote iliondokana na umaskini. Hii ndiyo heshima ya Uislamu na ndiyo marejeo yetu katika harakati zote za uchumi.
Uchumi wa Kiislamu unazingatia uhalali na uharamu wa miradi na programu zake. Unatofautiana sana na uchumi unaopangwa na makafiri, ambao wanaendesha mambo yao kwa fikra zao tu na wala hawazingatii uhalali na uharamu.

Huu ni uchafu ambao umeingia katika jamii, na kamwe tusitegemee jamii hii kuwa katika mstari uliyonyooka. Mamlaka pekee hapa ardhi yenye kuhalalisha na kuharamisha ni Mwenyezi Mungu pakee. Binadamu anapoingilia mamlaka haya basi fahamu fika kuwa anafanya shirki. Na shirki ni sawa kabisa na kuwa mbali na baraka za Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu huyafutilia baraka mali ya riba, na kuyatia baraka mali yanayotolewa sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila kafiri (na) afanyae dhambi.
Tanzania kama nchi nyingi changa duniani, inachukua mikopo yenye riba kutoka nchi za Marekani na Ulaya. Imejitahidi kuzunguka nchi mbalimbali zilizotoa mikopo kwa dhamira ya kuomba nchi hizo kufuta mikopo iliyotolewa. Tanzania imefanikiwa kufutiwa madeni hayo na haijapata 'afueni' kwa madeni yaliyobaki.

Sababu, madeni badala ya kupungua, yanazidi kutokana na riba. Pamoja na kufutiwa baadhi ya madeni hayo, imeshindwa kuboresha huduma za jamii na uchumi. Bado uchumi ni dhaifu, na bila shaka viongozi hawana majibu sahihi kujenga uchumi wenye nguvu. Hatuna viwanda ya chuma. Ni yapi manufaa ya chuma?
Mwenyezi Mungu, fundi wa maumbile, tunayoyaona na tusiyoyaona, anasema katika Qur'an: Na tumekiteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu ajulishe anayemnusuru na Mitume yake, na hali ya kuwa hawamuoni Mwenyezi Mungu, kwa yakini Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye kushinda. (57:25).

Bado zipo dalili za wazi kuwa hatujarejea kwa Mwenyezi Mungu na hatujawa wakweli katika mambo yetu. Kama tungalikua hivyo, basi hapana shaka tungeliwashinda makafiri katika suala la uchumi. Tayari wamekwisha ugeuza ulimwengu uende katika mifumo ya soko huria la uchumi. Soko huria lina faida kubwa kwa nchi tajiri za ulimwengu wa kwanza, na ni lenye hasara kubwa kwa nchi changa. Waislamu hatuna chochote tutakachoambulia!

Ni bayana kuwa mifumo ya riba ni mifumo ya dhulma. Hivyo Waislamu hatuna budi kuepuka dhulma hiyo, kwani Uislamu unaamrisha kuwa tusidhulumu wala kudhulumiwa katika jamii yoyote ile iwayo. Muislamu anayekubali kudhulumu au kudhulumiwa, Uislamu wake uko katika mashaka makubwa. Huu ni wakati muafaka kwetu kuacha kubweteka, n akuanza kujishughulisha na kuanzisha taasisi zetu za fedha na maendeleo. Zipo taasisi mfano wa hizo katika nchi za Ulaya, Uarabuni ambazo zimekwisha fanya maendeleo makubwa.

Jambo jingine muhimu ni kilimo na ufugaji. Uislamu umeeleza kilimo (na ufugaji) kuwa ni kemiya iliyo bora. Mitume walio wengi walikuwa ni wakulima na wafugaji. Hapakutokea hata siku moja jamii kukosa chakula wala nyama. Wakati wa Ukhalifa wa Sayedna Umar bin Khattab, aliwasaidia sana wakulima, Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Vile vile alianzisha kilimo cha umwagiliaji maji ambacho kilifaulu mno. Tazama uongozi wa Kiislamu ulivyokuwa unawajali watu wake bila ya ubaguzi na tofauti za kiimani.

Hebu tuangalie kilimo chetu hapa Tanzania, kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Pamoja na sifa hii, lakini kilimo kimeumia sana kuliko kitu chochote.
Vyama vya ushirika vya wakulima vimefilisika kiasi kwamba vilivyovingi haviwezi tena kununua mazao shambani. Hali ambayo imemuongezea mkulima umaskini mkubwa. Mamlaka za mazao hazipo kwani zilishindwa kabisa kutekeleza sera zake kwa faida ya wote waliohusika.
Pia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo iliyochangia kuanguka kwa ushirika na mamlaka za mazao.

Wakulima wa Afrika Kusini, wakulima wa Zimbabwe, wakulima wa Misri, na kwa ujumla wakulima wa Amerika na Ulaya ni matajiri kuliko wa Tanzania. Inavyonekana bado hatujakubali kujifunza kutoka kwa wenzetu waliondelea. Tatizo ni uongozi wa nchi kwa ile tabia yake ya kukataa fikra mpya za maendeleo. Rejea ripoti ya utafiti iliyoandika matatizo na maendeleo ya kilimo inayoitwa "East Africa Royal Commission Report". Mkoloni ndiyo mwandishi wa ripoti hii.

Pamoja na matatizo yote, bado ukulima ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Tanzania bado ina ardhi asilimia sabini inayofaaa kilimo, lakini bado haijatumika

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget