Saturday, February 11, 2012

UISLAMU NA HIJABU


TUJIULIZE:
1·NINI MTIZAMO  WA UISLAMU KATIKA SUALA LA HIJABU KWA  MWANAMKE NA HAKI YAKE YA KUSOMA NA KUFANYA KAZI.
2·JE NI KWELI KUWA HIJABU HAIENDI SAMBAMBA NA MAISHA YA LEO? (IMEPITWA NA WAKATI).
Kwanzakabisa ni vema tukaelewa  tunapozungumzia Hijabu tunazungumzia nini. Tunapoizungumzia Hijabu tunaikusuduia Hijabu kama ilivyo ndani ya Qur - ani Tukufu. Neno Hijabu limetumika ndani ya Qur - ani zaidi ya mara nane. Miongoni mwa aya zilizoitaja Hijabu ndani ya Qur - ani ni hizi zifuatazo:-
".. NANYI MNAPOWAULIZA (wakeze Mtume) WAULIZENI NYUMA YA PAZIA (Hijabu) ..." (33:53)

Hii ndio Hijaabu kwa lugha ya Qur - ani:-
"(NA WAKASEMA: "NYOYO ZETU ZI KATIKA VIFUNIKO KWA YALE UNAYOTUITIA; NA  KATIKA MASIKIO YETU MUNA UZITO; NA BAINA YETU NA BAINA YAKO KUNA PAZIA. (Hijaabu) ???" (41:5)
Ione Hijaabu kupitia Qur - ani:-
"BASI AKASEMA ; NAVIPENDA VITU VIZURI KWA KUMKUMBUKA MOLA WANGU. KISHA  (mafarasi) WAKAFICHIKANA NYUMA YA KIZIUIZI (Hijaabu, kwa kutiwa zizini mwao)" (38:32)

Ijue Hijaabu kupitia Qur-ani-
"NA AKAWEKA PAZIA (Hijaabu) KUJIJINGA NAO??.." 19:170.
Ielewe Hijaabu kupitia Qur-ani- "NA UNAPOSOMA QUR-ANI (inakuwa kama kwamba) TUMETIA BAINA YAKO NA BAINA YA WALE WASIOAMINI AKHERA PAZIA LILILOFUNIKWA (sana hata hawafahamu kinachosemwa)" (17:45)

Hizi ndizo baadhi ya aya za Qur-ani Tukufu ambazo ndani yake limetajwa na kutumika neno "Hijaabu". Kupitia aya hizi tunaweza kusema kuwa Hijaabu ya Kiislamu ni:-
a)Sitara ya kutokuchangayika pamoja wanume na wanawake.
b)Sitara ya kutokusikia sauti ya mwanamke kwa mwanamume.
c) Sitara ya mwili (mavazi) yaani kutoonekana mwili wa mwanamke ila na maharimu zake tu.
Hii ndio eleweko la Hijaabu kwa mtazamo wa kiislamu, kama tutakavyolithibitisha hilo na kulijengea hoja kupitia Qur-ani yenyewe. Hijaabu hailengi ila kuwa ni chombo cha kujenga na kuratibisha uhusiano mwema uliopo baina ya jinsia mbili zihitajianazo na kutegemeana, mwanamume na mwanamke. Huu ni utaratibu na nidhamu ya lazima inayozisaidia jinsia mbili hizi kuistawisha dunia na kuyafurahia maisha katika misingi waliyowekewa na Mola Muumba wao. Kila mmoja, mwanamume na mwanamke ameamrishwa na kukalifishwa kuishi kwa kuufuata utaratibu na nidhamu hii. 

Hii ni kwa ajili ya kuidhibiti na kuitawala nguvu ya kimaumbile iliyopo baina ya jinsia mbili hizi. Nguvu ambayo ina athari kubwa katika kuvuruga na kuharibu mwenendo na  silka nzima ya mwanadamu. Mvuto na matamanio ya kijinsia alio nayo mwanamume, yanapatikana pia kwa mwanamke. Kila mmoja kwa mwenzie ni mfano wa sumaku inayokivuta chuma na hatimaye kukinasa na kushikamana nacho. Haya ndio maumbile yaliyokamilika na chanzo/sababu yake ya msingi ni "Homonsi" alizoumbiwa kila mmoja wao. Ni kwa kulijua na kuzingatia tabia hii ya maumbile ya mwanadamu ndio tunaikuta Hijaabu hata katika vilabu vya Mwenyezi Mungu Mtukufu vilivyoitangulia Qur-ani.

Hijaabu ya Kiislamu haikomelei tu katika kusitiri na kuhifadhi mapambo (sehemu zenye kuamsha na kuchochea fitna kati ya mwanamume na mwanamke), na kuinamisha macho tu bali Hijaabu ni pamoja na:-
1·Kutokukaa faraghani mwanamume na mwanamke. Haya ndiyo maelekezo na mafundisho ya Bwana Mtume- Rehema na Amani zimshukie - kupitia kauli yake:-"Asikae, asikae, rafaghani mmoja wenu na mwanamke ila (awe pamoja na mwanamke huyo) maharimu (yake, baba, kaka, babu n.k). Bukhariy na Muslim.
2·Kutogusana mwili na mwanamume na mwanamke. Haya ndio mafundisho ya Uislamu kupitia kauli ya Mtume wa Uislamu- Rehema na Amani zimshukie:- "Mmoja wenu kuchomwa kichwani kwake na sindano ya chuma na bora kwake kuliko kumgusa mwanamke asiye halali yake" Twabaraany. Amesema mkewe Bwana Mtume , Bi Aysha- Allah amuwiye radhi: "Wallah! Mkono wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Haukupata kabisa kumgusa mwanamke (asiye halali yake), ila alikuwa akipeana nao ahadi kwa maneno (kwa kuzungumza) tu"
3·Mwanamke kutokulegeza sauti yake mbele ya mwanamume. Tusome: ENYI WAKE WA MTUME, NINYI SI KAMA YOYOTE TU KATIKA WANAWAKE WENGINE (ninyi wakeze Mtume). KAMA MNATAKA (kufanya jambo la) KUMCHA ALLAH, BASI MSILEGEZE SAUTI (zenu mnaposema na wanaume) ILI ASITAMANI MTU MWENYE UGONJWA MOYONI MWAKE (kufanya mabaya na nyie) NA SEMENI MANENO MAZURI " (33:32). Semezo (kihitwaabu) la aya hii linaelekezwa moja kwa moja kwa wakeze Bwana Mtume lakini amri hii inawahusu na kuwaenea wanawake wote wa Kiislamu.
4·Kuzuia picha, magazeti, majarida, vipeperushi, nakala na matangazo ambayo kwa namna moja au nyingine huchochea na kuamsha tmaa na matamanio ya kimwili.
5·Mwanamke kujitia manukato na kupita mbele ya wanaume . Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie - anatahadharisha juu ya hili kwa kutuambia "Mwanamke yeyote atakayejitia manukato na kupita mbele ya wanamume ili waipate harufu ya (manukato) yake, basi mwanamke huyo ni mzinifu (anapata dhambi za kuzini kwa sababu ya kushawishi kwake zinaa) na kila jicho (limtazamalo) pia ni zinifu" Abuu Daawoud, Tirmidhiy, Nasaai, Ibn Khuzaymah na Ibn Hibban.
Haya ni baadhi tu ya maeneo yanayoguswa moja kwa moja na Hijaabu ya Kiislamu. Msingi na asili ya suala la Hijaabu ni kauli tukufu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya Qur-ani Tukufu isemayo "NA WAAMBIE WAISLAMU WANAWAKE WAINAMISHE MACHO YAO, NA WAZILINDE TUPU ZAO WALA WASIDHIHIRISHE VIUNGO VYAO ISIPOKUWA VINAVYODHIHIRIKA (nao ni uso na vitanga vya mikono). NA WAANGUSHE SHUNGI ZAO MPAKA VIFUANI MWAO, NA WASIONYESHE MAPAMBO YAO ILA KWA WAUME ZAO, AU BABA ZAO, AU BABA ZA WAUME ZAO (wakwe zao) AU WATOTO WAO, AU WATOTO WA WAUME ZAO, AU KAKA ZAO, AU WANA WA KAKA ZAO, AU WANA WA DADA ZAO, AU WANAWAKE WENZIWAO, AU WALE ILIYOWAMILIKI MIKONO YAO YA KIUME (watumwa wao) AU WAFUASI WANAUME WASIO NA MATAMANIO ( kwa wanawake) AU WATOTO AMBAO HAWAJAJUA MAMBO YANAYOHUSU UKE, WALA WASIPIGE MIGUU YAO ILA YAJULIKANE WANAYOYAFISHIA KATIKA MAPAMBO YAO NA TUBIENI NYOTE KWA ALLAH ENYI WAISLAMU ILI MPATA KUFAULU" (24:31).
Alisema Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie - wakati Asmaa Bint Abuu Bakri - Allah awawiye radhi wote - alipoingia kwa Mtume akiwa amevaa nguo nyepesi: "Ewe Asmaa, hakika mwanamke anapofikilia umri wa kupata hedhi (anapovunja ungo) haifai kuonekanwa (mwili) wake ila hiki na hiki. Na (Mtume) akaashiria uso na vitanga vyake" Abuu Daawoud.
Miongoni mwa sharti za Hijaabu ya vazi la mwanamke wa Kiislamu ni kwamba:-
a)Isiwe nguo yenyewe ni pambo linaloweza kumvutia mtazamaji. Hilo ndilo eleweko na fahamisho la kauli ya Allah isemayo" "WALA WASIDHIHIRISHE MAPAMBO YAO??." (24:31) Na kauli isemayo, "NA KAENI MAJUMBANI MWENU, WALA MSIONYESHE MAPAMBO YENU KAMA WALIVYOKUWA WAKIONYESHA MAPAMBO YAO WANAWAKE WA ZAMA ZA UJAHILI (Ujinga ukafri)??.' (33:33).
b)Iwe  nzito isiwe nyepesi ionyeshayo rangi ya mwili. Hii ni kutokana na kauli ya Mtume isemayo:" Watakuwepo mwisho wa umati wangu wanawake watakaovaa (lakini) wako uchi. Vichwani mwao kuna nundu (kutokana na mitindo ya nywele) kama nundu  za ngamia. Walaanini kwa kuwa wao wamelaaniwa??" Ahmad.
c)Isiwe yenye kubana sana kiasi cha kuonyesha ramani/finyango la mwili.
d)Isiwe imetiwa manukato au kufukizwa kwa udi, Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie aliposema" Mwanamke yeyote atakayejitia manukato, kisha akapita mbele ya wanaume ili waipate harufu yake, basi yeye ni mzinifu",
e)Isifanane na nguo za wanaume, hivyo ndivyo tunavyofahamu kutokana na kauli ya Bwana Mtume - Rehama na Amani zimshukie - isemayo: "Si katika sisi mwanamke mwenye kujishabihisha na wanaume wala mwanaume mwenye kujishabihisha na wanawake. Twabaraaniy na Ahmad.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget