Wednesday, February 22, 2012

Njama za Israel dhidi ya maridhiano ya Wapalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema kuwa, mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Ukanda wa Gaza ni njama za kukwamisha utekelezwaji wa makubaliano ya maridhiano ya kitaifa yaliyotiwa saini baina ya Hamas na Fat'h. Fauzi Barhoum, Msemaji wa Chama cha Hamas sanjari na kulaani mashambulio yasiyokoma ya Israel huko Gaza amesema, kila mara inapotokea kwamba, Wapalestina wamo katika harakati za kutaka kutekeleza maridhiano ya kitaifa, viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel hukesha wakipanga njama za kuzusha mgogoro baina ya Wapalestina. Daima utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa umo mbioni kupeleka mbele siasa zake za kujitanua katika ardhi za Palestina na kufanya njama zao mbalimbali kwa minajili ya kuwadhoofisha Wapalestina lengo hasa likiwa ni kutaka kuwatwisha Wapalestina siasa zake za kujitanua.
Moja ya hatua za Wazayuni za kuvuruga mwenendo wa umoja na mshikamano wa Wapalestina ni kutaka kuuarifisha muqawama wa Palestina kwamba, ndio chanzo cha kuzorota zaidi hali ya Wapalestina.
Kwa muktadha huo, kila mara kunapopigwa hatua katika njia ya maridhiano ya kitaifa ya Wapalestina, utawala wa Kizayuni wa Israel hukithirisha mashambulio yake ya kijeshi katika maeneo ya Wapalestina sambamba na kushadidisha mzingiro dhidi ya Gaza ambapo sanjari na kusukuma mbele gurudumu la siasa zake za kujitanua huko Palestina, hukusudia pia kukwamisha maridhiano ya kitaifa ya Wapalestina. 
Katika upande mwingine utawala wa Kizayuni hufanya njama za kuivuta Mamlaka ya Ndani ya Palestina upande wa mazungumzo ya mapatano na ushirikiano wa kijeshi na utawala huo hususan katika kuwatia mbaroni wanaharakati wa Kipalestina ili kwa njia hiyo uweze kuleta mgawanyiko baina ya Wapalestina. Hivi sasa Israel ikitumia siasa za kuwagawa Wapalestina inafanya juhudi kubwa za kuzuia kutekelezwa maafikiano ya Wapalestina katika fremu ya mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa. Kasi hiyo ya utawala wa Kizayuni inatokana na kuwa, licha ya kuweko vitisho, kamatakamata, kuizingira Gaza zaidi ya miaka mitano na kushadidisha siasa zake za ukandamizaji, umeshindwa kuwafanya Wapalestina wasalimu amri na kuzikubalia siasa zake za kupenda kujitanua. Katika hali ya sasa, njia pekee ambayo imebakia ni kutumia vita kama karata yake ya mwisho; hata hivyo katika uga huu pia, viongozi wa Tel Aviv wanachanga karata zao kwa hadhari kubwa kutokana na kipigo walichokipata kutoka kwa wana muqawama wa HAMAS katika vita vya siku 22 huko Gaza. 
Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kwa sasa Israel imejikita zaidi katika propaganda na kujaribu kuwahadaa walimwengu kuwa, Wapalestina wametumbukia katika mifarakano mikubwa na kwamba, hakuna sauti moja baina yao ili kutumia vibaya hali hiyo.
Katika mazingira kama haya jukumu na masuuliya muhimu ya makundi ya Kipalestina ni kusimama kidete katika mwenendo wa maridhiano ya kitaifa na kuwaonyesha walimwengu kwamba, propaganda za Wazayuni na madola ya Magharibi ni urongo mtupu na ni dua la kuku lisilompata mwewe.
Na Salum Bendera

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget