Saturday, February 11, 2012

Uislamu na Haki za Kibinaadamu na Uadilifu


Uislamu unatoa fursa ya haki nyingi za kibinaadamu kwa ajili ya mtu binafsi. Zifuatazo ni baadhi ya haki hizo za kibinaadamu ambazo Uislamu huzilinda.
Maisha na mali za wananchi wote katika taifa la Kiislamu huchukuliwa kuwa ni vitukufu, iwe mtu huyo ni Muislamu ama la, Uislamu unalinda heshima pia. Hivyo, katika Uislamu, jambo la kuwatukana wengine na kuwakejeli haliruhusiwi. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika damu zenu, mali zenu na hadhi zenu ni tukufu.)) (Imeandikwa ndani ya Swahiyh Al-Bukhaariy, Na. 1739 na Musnad Ahmad,Na. 2037)
Ubaguzi wa rangi hauruhusiwi katika Uislamu, kwani Qur-aan inazungumzia usawa wa binaadamu kwa maneno yafuatayo: “Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na Tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mcha Mungu (Mchamungu ni Muumini anayejiepusha dhidi ya kila namna ya madhambi, anatenda amali zote njema ambazo Mwenyezi Mungu anamwamuru azifanye, na anamwogopa na kumpenda Mwenyezi Mungu)zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.” (Qur-aan, 49:13)
Uislamu nakataa suala la baadhi ya watu au mataifa kupewa upendeleo kwa sababu ya mali zao, nguvu au rangi. Mwenyezi Mungu Aliwaumba wanaadamu kwa usawa ambao wanaweza kutofautiana baina yao kwa imani na ucha Mungu wao. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Enyi watu! Mola wenu ni Mmoja na baba yenu (Adam) ni mmoja. Mwarabu si mbora zaidi ya asiye Mwarabu, na asiye Mwarabu si mbora zaidi ya Mwarabu, na mwekundu (mweupe aliyechanyika na wekundu) si mbora zaidi ya mweusi na mweusi si mbora zaidi ya mwekundu, (Rangi zilizotajwa katika Hadiyth hii ya Mtume ni katika mfano tu. Maana yake ni kwamba, katika Uislamu, hakuna yeyote aliye mbora zaidi ya mwingine kwa sababu ya rangi yake, ikiwa ni nyeupe, nyeusi, nyekundu, au nyingine yoyote.isipokuwa katika ucha Mungu.))(Imesimuliwa katika Musnad Ahmad, Na. 22978)
Moja kati ya matatizo makubwa yanayowakumba wanaadamu katika zama hizi ni ubaguzi wa rangi. Ulimwengu uliosonga mbele kimaendeleo unaweza kumpeleka mtu mwezini lakini hauwezi kumzuia mtu dhidi kumchukia au kumpiga mwanaadamu mwenzake. Tangu katika zama za uhai wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Uislamu umeonesha mfano dhahiri wa namna ubaguzi wa rangi unaweza kukomeshwa. Hija ya kila mwaka inaonesha undugu khasa wa Kiislamu kwa rangi na mataifa yote, katika wakati ambapo kadiri ya Waislamu milioni mbili kutoka ulimwenguni kote wanakuja Makkah kutekeleza ibada ya Hija.
Uislamu ni Dini ya uadilifu. Mwenyezi Mungu Amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu Anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu." (Qur-aan, 4:58)
Amesema tena: “...Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wanaohukumu kwa haki.” (Qur-aan, 49:9)
Tunapaswa tuwe waadilifu hata kwa tunaowachukia, kama Mwenyezi Mungu Alivyosema: “...Wala kuchukiana na watu kusikupelekeenikutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na ucha Mungu...” (Qur-aan, 5:8)
Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Enyi watu! Nakutahadharisheni dhidi ya dhuluma,(Yaani, kuwakandamiza wengine, kunyima haki, au kuwafanyia wengine isivyotakiwa)kwani dhuluma itakuwa kiza katika Siku ya Hukumu,))(Imesimuliwa katima Musnad Ahmad, Na. 5798, na Swahiyh Al-Bukhaariy, Na. 2447)
Na wale ambao hawakuzipata haki zao (yaani, ambazo walikuwa na madai ya haki) humu duniani, watazipata katika Siku ya Hukumu, sawa na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Katika Siku ya Hukumu, haki watapatiwa wale waliostahiki (na makosa yatalipiwa fidia)...))(Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim, Na. 2582, na Musnad Ahmad, Na. 7163)

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget