Monday, February 20, 2012

MISINGI NA IMANI ZA UKRISTO

Tukizungumza kwa haraka haraka, msingi na imani ya Uungu inasema kwamba Yesu ni mwana Mungu - Neno la Mungu lililofanywa mwili.
Hata hivyo, kama tulivyoona hapo nyuma, Yesu mwenyewe hakuwahi kudai kuwa yeye ni Mungu, Paulo alimpa sifa hii kwa sababu moja kubwa: alitaka kupata wafuasi wengi miongoni mwa Warumi na Wagiriki (watu wa mataifa).

Wajentaili (Wagiriki na Warumi) walikuwa ni wapagani waliokuwa wakiabudu miungu wengi wenye historia ndefu iliyojaa imani za ajabu ajabu zisizokuwa na hoja wala dalili za kiakili. Miungu wengi wa kipagani wa wakati ule - Mithrus, Adonis, Attis na Osiris, hawa wakiwa ni baadhi tu - wote walikuwa ni watoto wa mungu mkuu anayetawala, na kila mmoja wa watoto hawa wa mungu (ambao nao ni miungu) alikufa kwa ajali mbaya katika utoto wake, kisha akaja muda mchache baadaye ili kuokoa maisha ya watu wake.

Paulo alilizingatia hili, akawapa wapagani jambo linalofanana na hilo katika Ukristo, akamfanya Yesu kuwa Mungu, kwa kudai kuwa alikuwa mtoto wa Mungu (Mkuu) na kwamba, yeye pia alikufa kwa ajili ya dhambi zao. Kwa kufanya hivyo Paulo aliyapatanisha (aliyafananisha) mafundisho ya Yesu na imani za kipagani ili kuufanya Ukristo ukubalike zaidi kwa watu wa mataifa (Warumi na Wagiriki).
Ilivyo hasa, Paulo hakutangaza wazi kwamba msingi na imani hii ya Mungu imetokana na upagani.
Ni yule tu anayejaribu kuichimba historia - watu na utamaduni wao - ndio ataweza kuuona ukweli huu. Paulo alithibitisha imani na msingi huu wa Uungu kwa namna nyingine. Paulo ilihisi kuna sababu kama tano zinazomfanya Yesu awe Mungu.
1) Yesu alizaliwa na mwanamke bikira bila ya "msaada" wa baba wa kibinadamu.
Kulijibu hili, tunaweza kuangalia mfano wa Adam, mwanadamu wa kwanza. Aliumbwa bila ya baba wala mama lakini hatumfikirii kuwa yeye ni Mungu.
2) Yesu alifanya miujiza.
Kuliangalia hili tunaweza kuangalia mfano wa Nabii Musa na Nabii Elisha, wote walifanya miujiza mikubwa mikubwa, lakini hakuna yeyote kati ya hawa anayefikiriwa kuwa ni Mungu. Ukweli kwamba Yesu alifanya miujiza sio ushahidi kwamba Yesu alikuwa Mungu, na wakati miujiza hii ilipotokea, ilitokea kwa uwezo na ridhaa ya Mwenyezi Mungu sio kwa uwezo wake Yesu mwenyewe.
Miujiza yake ilifanyika kwa kusudio lile lile kama la Mitume waliotangulia kabla yake nalo ni kuuthibitisha ukweli wa ujumbe na utume wake kwa watu waliokuwa wagumu kuamini.
3) Yesu alikuwa na tabia njema "isiyofikiwa na yeyote".Kujibu hili tunaweza kuonyesha baadhi ya mifano katika injili - kama vile kumwita Petro "Shetani" katika Mathayo 16:33, na kuwaita wengine "nyoka na kizazi cha nyoka wenye sumu" katika Mathayo 23:33, na katika Mathayo 5:22 tunaambiwa kuwa "anayemwita mwenzake pumbavu" anastahili kuingia moto wa Jahanam. Hivyo tukiangalia maneno aliyomwambia Petro kuwa ni shetani na kwamba wengine ni nyoka wenye sumu inaleta mashaka juu ya sifa hii kwamba Yesu alikuwa na tabia njema isiyoweza kufikiwa na yeyote.
4) Yesu alifufuka kutoka katika mauti.Ni kweli, "kuyashinda mauti" ni muujiza, lakini vipi kuhusu Nabii Eliya ambaye hakufa kabisa, lakini alichukuliwa kwenda mbinguni moja kwa moja kwa kutumia troli yenye matairi mawili iliyokuwa kama moto (Wafalme wa pili 2:11)? Ni muujiza mkubwa kabisa, lakini bado hatumchukulii yeye kuwa ni Mungu. Na mwisho, Wakristo wanasema kwamba:
5) Yesu alitabiriwa katika Agano la Kale.Wakristo hufanya haraka kusoma Isaya 53 kama utabiri wa kuja kwa Yesu na ujumbe wake kwa wanaadam. Tatizo hapa ni kwamba halikutajwa jina halisi katika sura hii. Bila kutaja jina kamili, nani anaweza kuelewa ni NANI hasa anayetabiriwa katika sura hii.
Neno "Mwana wa Mungu"
Neno "Mwana wa Mungu" hali kuwa neno jipya au geni, lilitumika katika Agano la Kale kumaanisha Daudi (Zaburi 2:7), pia lilitumika katika mambo ya Nyakati wa Kwanza 22:10 kuwa Nabii Suileman (Solomon) ni mwana wa mungu, na Nabii Adam ameitwa mwana wa Mungu katika Luka 3:38 katika agano jipya.
Katika hotuba yake maarufu kule Mlimani ambayo imeelezewa kwa urefu katika Mathayo 5, Yesu anawaambia wasikilizaji wake:
"Heri yao wapatanishi kwa maana wataitwa wana wa Mungu". (Mathayo 5:9)
Katika aya zote hizi neno "Mwana wa Mungu" halimaanishi maana ya kilugha - yaani baba kumzaa mtoto kabisa bali linamaanisha upendo na mapenzi ya Mungu kwa watu waongofu (wacha Mungu). "Mwana wa Mungu" ina maana ukaribu maalumu kwa Mwenyezi Mungu, na si kwamba Mwenyezi Mungu kamzaa huyo mwana. Juu ya yote kila mtu ni mwana wa Mungu kwa vile Mwenyezi Mungu ndiye Muumbaji wa uhai na kila kitu.
Neno "Masiya - Masihi"
Neno jingine linalotumika na Wakristo kuipa uzito nadharia kwamba Yesu ni Mungu ni neno Masihi (Angalia Yohana 1:41). Neno Masiya ni la kiebrania lenye maana "Mtu wa Mungu aliyepakwa mafuta " na neno "Kristo" ni tafsiri tu ya kigiriki ya neno la Kiebrania "Masiya." Masihi au kristo, Kiebrania au Kigiriki - yote yana maana moja "Mtu wa Mungu aliyepakwa mafuta".
Neno hili hata hivyo, halikutumika kwa Yesu peke yake, limetumika kwa watu wengine kabla yake pia. Katika Zaburi 2:2, limetumika kwa Nabii Daudi na katika (Isaya 45:1) neno Masihi pia limetumika kwa Koreshi.
Wayahudi waliwaita Wafalme wao "Masiya" kwa dhana kwamba Mungu aliwapaka mafuta na kuwatawaza kuwa Wafalme. Wazo zima la neno Masiya ni la kiyahudi, lililotumika kwa mkombozi wa taifa ambaye waliamini kwamba, kwa msaada wa Mungu angewaokoa kutokana na uonevu na ukandamizaji wa watu wa Mataifa. Hata hivyo neno Masihi ndani yake halikuwa na maana ya uungu.
Neno "Mwokozi"
Neno la mwisho linalotumiwa na Wakristo ni "mwokozi". Hata hivyo neno "mwokozi" halikuanza kutumika kwa Yesu. Shamu (Syria) ilipofanya vita dhidi ya ufalme wa Israel, Jehoahaz, mfalme wa wakati ule, aliomba kwa Mwenyezi Mungu kutaka msaada katika Wafalme wa pili 13:5, Mungu alimwambia:"Bwana akawapa Israel mwokozi". (2 Wafalme13:5)Pindi Jehoahaz mwana wa mfalme, alipochukua ufalme, alifanya kama Mungu alivyoahidi katika 2 Wafalme 13:25, Jehaohaz alikuwa mwokozi wa watu wake kwa sababu aliwashinda Wasyria (Washamu) na akairejesha miji ya kaskazini ya ufalme wa Israel. Neno "Mwokozi" halina kabisa maana ya Uungu ndani yake
Uungu wa Yesu:
Utumiaji wa Tafsiri Mbaya
Mbali na majina, njia nyingine inayotumiwa na wakristo wanapojaribu kuthibitisha uungu wa Yesu ni kutafasiri vibaya baadhi ya vifungu vya aya za Biblia. Kuna vifungu viwili wanavyopenda sana kuvinukuu kwa kusudio hili:
1) Aya ya kwanza ni Yohana 10:30 ambapo Yesu anasema:
"Mimi na Baba yangu ni kitu kimoja".
Uchambuzi wa kiakili na kimantiki wa aya hii unaonyesha kwamba, Yesu anazungumza kwa jina la Mungu na sio kwamba yeye ni Mungu. Yesu na Mungu ni kitu kimoja kimadhumuni - sio kwa asili yao. Mkristo anaweza kuangalia zaidi katika Yohana 17:1-26:"Baba saa imefika! Mtukuze mwanao ili naye akutukuze. Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uzima wa milele wote hao uliompa. Na uzima wa milele ndio huu, kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma--".
Katika dua hii ya Yesu inadhihirisha wazi kwamba yeye hakuwa Mungu bali alikuwa ni mja na Mtume wa Mungu.
Kuthibitisha wazo hili la kuwa kitu kimoja kimadhumuni (Yesu na Mungu) na si kwa asili yao. Hebu tuangalie aya kadhaa katika sura ya kumi na saba ya Yohana, aya ya kwanza ikiwa ni Yohana 17:8. Hapa Yesu anasema:
"Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa; nao wameupokea; wanajua kwamba kweli nimetoka kwako; na wanaamini kwamba wewe ulinituma".
Katika Yohana 17:11 kuna uthibitisho mwingine unaoonyesha kuwa Yesu na Mungu ni kitu kimoja kimadhumuni (Yaani kuwapa uongofu wanadamu). Yesu anasema:"Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja".
Nukta hii ya kuwa pamoja imeelezewa zaidi katika Yohana 17:21-23.
Kwa kifupi maelezo ya Yesu yaliyo katika Yohana 10:30, hayajaribu kuthibitisha kuwa yeye ni Mungu bali yeye na Mungu ni kitu kimoja kimadhumuni, kama inavyoonekana katika aya zilizotajwa hapo awali katika Yohana 17.
2) Aya nyingine ambayo Wakristo wanapenda kuitumia ni Yohana 14:9. Ndani yake Yesu anamwambia Filipo:
"Aliyeniona mimi amemuona Baba".Ni vizuri kwa Wakristo wanaotumia aya hii kuthibitisha uungu waYesu wakaangalia Yohana 5:37, ambapo Yesu anasema:"Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Nanyi hamjapata kamwe kusikia sauti Yake, wala kuuona uso wake".
Kama Mkristo atakuwa hakuridhika na aya hiyo juu basi anaweza kuangalia Agano la Kale katika kitabu cha kutoka 33:20, Mungu anamwambia Musa:"Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi".
Ili kuielewa vizuri aya hii ya Yohana 14:9, ni lazima tuiangalie kiusanifu: Kwa vile Yesu alikuwa ameleta ujumbe wa Mungu, kumuona na kumsikiliza yeye ilikuwa ni sawa na kuwepo Mwenyezi Mungu. Yesu alikuwa anafanya mambo kwa amri ya Mwenyezi Mungu - si kwamba yeye mwenyewe alikuwa Mungu. Hii inaonekana zaidi katika Yohana 8:19, ambapo Yesu anasema:"Kama mngenijua mimi, hata Baba pia mngemjua".Zipo aya nyingine zaidi ambazo mkristo anaweza kuzigeukia katika jitihada zake za kumpa Yesu Uungu, lakini zote si chochote ila ni kuzielewa vibaya au kuzitafsiri vibaya kwa ajili ya kutaka kusoma au kukiona kitu fulani ambacho kiuhalisia hakipo. Katika Yohana 17:3 tunaweza kuona kuwa Yesu hakuleta ujumbe mpya; hapa anasema:"Ili wakujue wewe Mungu wa kweli na wa pekee na wamjue Yesu Kristo uliyemtuma".Hapa anatuambia kwamba ni lazima tumuamini Mungu mmoja tu na ambaye ni wa kweli na kwamba yeye, Yesu ni mjumbe tu aliyetumwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Je Yesu Aliwahi Kujitangaza Kuwa
Yeye ni Mungu?
Wakristo wengi, mara nyingi huonyesha rejea nyingi katika injili ya Yohana ambapo Yesu anajiita "Mwana wa Mungu". Kwa upande mwingine wanapuuzia rejea nyingi katika injili hiyo hiyo ya Yohana ambapo Yesu anajiita "Mwana wa Binadamu". Hii inaonyesha wazi kuwa neno "Mwana wa Mungu" kama linavyotumika hapa halina maana ya kilugha. Yesu alikuwa na ukaribu maalum kwa Mwenyezi Mungu - alikuwa mwana wa Mungu kama ilivyo sisi wote ni wana wa Mungu.
Katika Mathayo 16:13, Yesu anawauliza wanafunzi wake kuwa wanafikiri yeye, Yesu, ni nani? Wakristo wanalipenda zaidi jibu la Petro ambalo lipo katika Mathayo 16:16 ambapo Petro anasema "Wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu aliyehai."
La kufurahisha zaidi, katika swali hilo hilo linalopatikana katika Marko 8:16, Petro anasema "Wewe ni Kristo". Ni maneno kidogo tu yameongezeka kwenye Mathayo ikilinganishwa na Marko, lakini yanabadilisha maana yote ya maneno. Zaidi ya hilo, kuna nukta moja ambayo wakristo wanaipuuza inayopatikana katika aya chache zinazofuatia chini ya Mathayo 16. Katika aya ya 20 - pia katika Marko 8:30 - Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa wasimwambie mtu yeyote zaidi kuwa yeye ni Kristo. Kwa nini hakutaka watu wengine walijue hili?
Je Paulo Alifanikiwa Kitu Gani?
Kwa kusema kwamba Yesu alikuwa Mungu, Paulo aliwaridhisha sana Watu wa Mataifa kwa sababu ni jambo walilokuwa wamelizoea (Katika imani yao ya kipagani kulikuwa imani kama hii) na mafanikio yake yakawa hayana kikwazo. Bidii na uwezo wake mkubwa wa kushawishi watu pamoja na kuwa kwake tayari kuchanganya ujumbe halisi wa Yesu na imani za kipagani zilimpelekea kumpachika Yesu uana wa Mungu - imani potofu kabisa, kwa sababu uana (wa Mungu) una maana (mwana) aliyeumbwa, wakati Uungu una maana "uwezo wa kuwepo milele na bila kuumbwa".
Baadaye viongozi wa kanisa waliamua kuondoa utata huu kiulaini kwa kusema kuwa Yesu alikuwa Mungu aliyevaa mwili wa kibinadamu - na ni wa milele "aliyeamua" kuwa mwanadamu katika tumbo la Bi Mariamu. Kwa maneno mengine, Yesu alikuwa na asili (maumbile) mbili - Umungu na ubinadamu ambavyo viliungana na kuwa mtu mmoja. Huenda hawa viongozi wa kanisa walikuwa na nia nzuri lakini katika maelezo haya wameleta utata na mkorogano zaidi.
Mtazamo wa Uislamu juu ya Yesu
Kama ilivyo katika Biblia, Quran pia inasema, Yesu alizaliwa bila ya baba (mwanadamu). Hii hata hivyo haina maana kwamba Yesu alikuwa Mungu, isipokuwa inaonyesha tu kwamba Mungu aliyeweka kanuni za maumbile (Laws of Nature), kama vile mtoto kuzaliwa na wazazi wawili, baba na mama, ana uwezo vilevile wa kuzisimamisha kanuni hizi na kufanya anavyotaka.
Kama Yesu angekuwa ni Mwana wa Mungu kiuhalisi kabisa - angekuwa ni mshirika katika uungu na yeye mwenyewe angekuwa ni Mungu, na kwa msingi huu Mungu angekuwa amezaa, amezaliwa, ameishi kama binadamu na kufa. Fikra hii ni mbovu mno na haikubaliki mbele ya watu wenye kufikiri na wenye akili.
Uislamu unashikilia kwa nguvu kuwa Yesu alikuwa ni Binadamu, aliyepewa ujumbe na Mwenyezi Mungu.
"Hakuwa Isa mwana wa Mariamu isipokuwa ni Mtume tu". (4:117)
Msimamo na imani kwamba Yesu alikuwa Mungu ni tofauti na kinyume kabisa na imani ya kuamini umoja wa Mwenyezi Mungu - kuwa Mungu ni mmoja tu."Kwa kuwa Allah ni Mungu Mmoja. Utakatifu na heshima vinamstahiki yeye. Ametukuka kwa utukufu mkubwa na ameepukana kuwa na Mtoto". (Quran 4:171)Nadharia, msingi au imani yenye mzizi yake kwenye ukafiri (upagani) na ambayo inakwenda kinyume na imani ya kuamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu mmoja tu asiyekuwa na mshirika, haina nafasi na haikubali kabisa katika Uislam.2) Tatu katika mmoja (Trinity)?Kwa haraka haraka imani ya Utatu Mtakatifu inasema kwamba Mungu mkuu ameundwa na vitu vitatu: Mungu Baba, Mungu Mwana - Yesu, na Mungu Roho Mtakatifu. Pamoja na kuamuamini Yesu, imani ya Utatu Mtakatifu ni moja ya misingi mikubwa kabisa ya Ukristo na ambayo juu yake imejengwa misingi na imani nyingine za Ukristo".[5]
Imani ya Kuamini Kuwepo Kwa Mwenyezi Mungu Mmoja Asiyekuwa na Mshirika (MONOTHEISM)
Kamusi iitwayo "Webster's New World Dictionary" imelitafsiri neno "MONOTHEISM" kuwa ni imani kuwa kuna Mungu Mmoja tu"[6]. Uyahudi, Ukristo na Uislamu zote zinadai kuwa zinaamini na kufuata imani hii. Imani hii ilihimizwa sana na Nabii Musa katika kifungu katika Biblia kinachoeleweka kama "Shema" au shema ya imani ya kiyahudi:"Sikieni, enyi Israel: Bwana Mungu wetu ni Mungu Mmoja tu" (Marko 12:29)
Alipokuja Nabii Muhammad (SAWW) takriban miaka 600 baada ya Yesu, alileta ujumbe huo huo:"Na Mola wenu ni Mungu mmoja tu: hakuna Mungu mwingine isipokuwa Yeye". (Quran 2:163)Ukristo umeondoka kwenye imani ya umoja (upweke) wa Mwenyezi Mungu na umepotea kwenye utata na mkorogano wa Utatu Mtakatifu: Vipi Mwenyezi Mungu anaweza kuwa mmoja wakati unamjumuisha Yesu na Roho mtakatifu?

Athari za Paulo na Walengwa (hadhira) Wake : Watu wa Mataifa (Gentiles)
Ingawa imani na msingi (doctrine) huu haukupendekezwa rasmi na Paulo, hapana shaka yoyote kwamba alikuwa na wazo hilo akilini. Na bado kama Yesu atachukuliwa kuwa ni mwana mwenye asili ya uungu basi itabidi tumtafute baba yake mwenye asili ya uungu pia. Kulikuwa pia mijadala juu ya Roho Mtakatifu, ambaye Paulo alidai kuwa ni chombo cha usafiri kilichotumika kuleta ufunuo kwa mwanaadam. Kimsingi, Paulo alitaja hivi vitu vitatu vinavyounda utatu mtakatifu yaani Mungu Baba, Yesu - Mungu mwana, na Mungu Roho Mtakatifu. Lakini kanisa halikuvitambua rasmi mpaka karne ya nne ambapo kanisa liliitangaza rasmi imani hii ya utatu mtakatifu na kwamba Mungu Mkuu ameundwa na Utatu Mtakatifu.
Kama ilivyo kwa imani nyingine zilizobuniwa na kuanzishwa na Paulo katika Ukristo, Utatu Mtakatifu pia, chanzo na asili yake ni imani za kipagani (kikafiri). Mfumo wa ibada wa watu wa Nimrod, ulianza Babylon lakini wakati wa zama za Paulo ulikuwa umeenea sana hadi maeneo ya miji alipokuwa akiishi Paulo na watu wengi walikuwa ni wafuasi wa imani hii. Nimrod, alikuwa ni kijana mdogo aliyekuwa amemuoa mama yake. Watu wake waliamini kuwa Nimrod alikuwa Mungu na kwamba Baal, Mungu wa jua, alikuwa ndiye baba yake. Baada ya kufa katika umri wake mdogo, mama yake Nimrod akawa mkuu wa ibada hizi za kipagani na akaanzisha imani kwamba mwanaye alikuwa anaendelea kuishi katika maumbile ya kiroho. Kwa hiyo kwa mara ya kwanza utatu mtakatifu ukawa umeibuka. Baal, Mungu Baba, Mama wa Nimrod, na Nimrod - Mungu Mwana. Ni kutokana na kisa hiki kwamba Paulo alianzisha Utatu Mtakatifu katika Ukristo.
Utatu Mtakatifu Katika Biblia
Kuna rejea mbili tu katika Biblia juu ya utatu mtakatifu, na zote zinatatanisha.1) Rejea ya kwanza inapatikana katika Mathayo 28:19. Hapa, Yesu anawaambia Wanafunzi wake"Nendeni, mkafundishe na kuhuburi mataifa yote, mkibawatatiza kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu".
Katika aya hii kuna utatanishi mkubwa:
a) Aya hii inataja nafsi tatu kila mmoja ikijitegemea ambazo baadaye ziliunganishwa na kuwa utatu mtakatifu wa Kikirsto na aya hii haizizungumzii nafsi hizi tatu kuwa ni sehemu tu ya Mungu Mkuu.
b) Tukichunguza zaidi juu ya mada hii hii - "Tume Kuu" katika Marko 16:15, Yesu anasema: "Nendeni ulimwenguni mkahubiri Injili kwa watu wote". Je maneno ya ziada (yaliyozidi) tunayoyaona katika rejea ya Mathayo yametoka wapi?
c) Ubatizo katika zama za mwanzo wa kanisa ulifanywa kwa jina la Yesu tu, kama ilivyoaminiwa na kuidhiniwa na Paulo katika nyaraka zake mbalimbali.

2) Rejea ya pili inapatikana katika 1Yohana 5:7 ambapo imeandikwa "Kwa kuwa wapo watatu wenye kumbukumbu za mbinguni, Baba, Neno, na Roho Mtakatifu: na watatu hawa ni "Mmoja".
Japo rejea hii ipo wazi zaidi juu ya utatu matakatifu, wasomi na wanazuoni wa Biblia katika karne ya 19 walikubali ukweli kwamba maneno "Baba, Neno na Roho Mtakatifu" ni maneno ya uzushi yaliyoongezwa - na maneno haya hayamo katika Biblia za zamani. Na pia maneno haya yameondolewa katika Biblia mpya za siku hizi.
Mbali na aya hizi mbili, kinachoshangaza zaidi ni kule kukubali ukweli kwamba maneno Baba, Neno, na Yesu kristo (bila shaka na maneno mengine mengi) hayakuwepo ila yamezusha na kuongezwa ndani ya Biblia. Zaidi ya hayo HAKUNA rejea nyingine YA AINA YOYOTE katika Biblia inayozungumzia Utatu Mtakatifu. Kwa kifupi dhana ya utatu katika ukristo - Mungu Baba, Yesu Mwana na Roho Mtakatifu kama Mungu Mkuu anayemuongoza mwanaadamu - haikuwahi kutolewa hata siku moja na Yesu au Mtume yeyote mwingine aliyetangulia kabla yake. Misingi na asili ya imani hii tayari ilikuwepo katika imani ya kipagani ingawa Paulo mwenyewe ilikuwa siri yake, hakutangaza waziwazi lakini alifanya hivi ili imani ya kikristo ifanane na ya kipagani katika mambo ya msingi ili apate wafuasi wengi wa kipagani. La kusikitisha ni kwamba licha ya ukweli imani hii kwamba imeundwa na mwanadamu, Paulo, lakini kanisa liliichukua imani hii na kuifanya kuwa ni msingi mkuu wa imani ya Ukristo.

Ukristo wa Mwanzo
Tertullian, mwanasheria na kiongozi wa kanisa katika mji wa Carthage, alikuwa ni wa kwanza kutumia neno "utatu mtakatifu" katika karne ya tatu alipotoa nadharia kwamba, Mwana na Roho Mtakatifu ni sehemu za Mungu Mkuu lakini wote ni kitu kimoja (Mungu mmoja).
Mabishano makali juu ya mada hii ya utatu mtakatifu yaliendelea kwa miaka mingi miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa kanisa. Baadhi waliafikiana na Tertullian kwamba Utatu Mtakatifu ndani yake ulikuwa na nafsi au asili tatu, lakini baadhi walidai kuwa utatu ulikuwa utatu wa ufunuo tu - kwamba Yesu alijazwa na Roho Mtakatifu wa Baba ambapo Roho huyo aliishi ndani yake (Yesu).
Mfalme Constantine alijikuta katika vita na mapigano mnamo mwaka 381 B.K, wakati mabishano juu ya utatu mtakatifu yalipokuwa makali sana baina ya viongozi wawili wakubwa wa kanisa kutoka Alexandria, Arius - afisa wa ngazi ya juu wa kanisa, anayemfuatia askofu, na Alexander, aliyekuwa askofu wake.
Mkutano wa Baraza la Nisea (NICEA)
Mfalme Constantine, japo alikuwa hajui la kufanya juu ya mambo na imani za kanisa za kibubusa lakini alikuwa na yakini kwamba umoja wa kanisa ulikuwa muhimu sana kwa ajili ya dola na ufalme wenye nguvu. Constantine alijaribu kuwapatanisha hawa viongozi wawili wa kanisa. Askofu aliposhindwa kumaliza tatizo hili, Constantine aliitisha mkutano wa baraza la Wasomi wakubwa katika masuala ya dini kwa mara ya kwanza katika historia ya kanisa lililokutana mwaka 325 B.K katika mji wa Nicea.
Maaskofu 300 walihudhuria mkutano huu; baada ya kufanya kazi kwa wiki sita, imani ya utatu mtakatifu iliundwa rasmi. Mungu wa Wakristo kuanzia siku hiyo alitambulika kuwa ana nafsi tatu - au asili tatu - katika muundo wa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Imani hii mpya iliyozinduliwa rasmi na Baraza la Nicea ilieleza hivi:
"....... tunamwabudu Mungu mmoja katika utatu mtakatifu, na utatu katika umoja --- kwa vile kuna nafsi moja ya baba, nyingine ya mwana na nyingine ya roho mtakatifu ---- sio miungu watatu, isipokuwa ni Mungu mmoja - nafsi zote tatu ni sawa milele hata milele --- kwa hiyo yeyote anayetaka kuokoka (kuokolewa) ni lazima aamini imani hii ya utatu mtakatifu".[7]Licha ya jitihada za Costantine, mabishano na mzozo juu ya utatu haukuisha na wala haukukaribia kuisha japo Costantine mwenyewe alikuwa na matumaini makubwa ya kumalizika kwa mgogoro huu. Arius na askofu mpya wa Alexanderia ayeitwa Athanasius walianza mabishano hata baada ya kutiwa saini Imani ya Nicea; "Arianism" - yaani imani ya Arius - iliyokuwa kinyume na utatu mtakatifu iliharamishwa na yeyote ambaye hakuamini imani ya utatu mtakatifu alikamatwa na kufungwa.
Hakuna Ustahimilivu Tena
Mnamo mwaka 451 B.K. katika mkutano wa Baraza la Chalcedon, imani ya Nicea, Constantinopole (inayoamini Utatu Mtakatifu) ilifanywa kuwa ndiyo imani rasmi inayotambulika na yenye mamlaka. Mabishano juu ya utatu hayakuendelea kuvumiliwa hata kidogo; kuzungumza dhidi ya utatu ilionekana ni kashfa dhidi ya dini na Mungu, na adhabu yake ilikuwa ni kipigo kikali na kuharibiwa au kuondolewa baadhi ya viungo na pengine kuuliwa kabisa. Sasa Wakristo wakawageukia Wakristo, wakiwaharibu au kuondoa baadhi ya viungo vya miili yao na kuwachinja maelfu kwa melfu kwa sababu ya tofauti ya maoni.
Ingawa adhabu za kikatili za wakati ule sasa hivi hazipo, utatanishi na mabishano juu ya utatu mtakatifu unaendelea mpaka leo. Wakiwa hawajakata tamaa, bado wakristo walio wengi bado wanashikilia kwa nguvu imani hii ambayo ni msingi wa imani yao.
Utatu Mtakatifu: Inakubalika Kimantiki?
Imani ya utatu mtakatifu inaweza kuwa msingi mkuu wa imani ya Ukristo lakini haina ukweli au msingi wowote kutoka kwenye Maandiko Matakatifu - imani yote imeundwa na mwanadamu kwa asili yake. Huu ni mfano - mwingine wa kwamba ni jinsi gani imani za kipagani zilivyoingizwa kwenye ububusa wa ukristo ili kuufanya ukristo ukubalike zaidi kwa wapagani.
Wakristo walio wengi, wanapoombwa kuielezea imani hii (ya utatu), hawawezi kutoa jibu lolote isipokuwa kusema: "Ninaamini hivyo kwa sababu niliambiwa niamini hivyo". Wanaliezea kwamba "Ni siri ya Mungu - hakuna mtu anayejua" ingawa Biblia inasema katika Wakorinto wa kwanza 14:33 kwamba:
"Mungu sio mwanzilishi wa utatanishi na migongano". (Mysteries).
Hata aliyeipa nguvu na kuihimiza imani hii ya utatu aliona ugumu mkubwa katika kuielewa imani hii. Inasemekana kwamba Athanasius, askofu aliyeitwa na kuitangaza rasmi imani hii ya utatu, alikiri kwamba alivyokuwa akizidi kuandika juu ya imani hii, ndivyo uwezo wake wa kuielezea imani hii ulivyokuwa ukizidi kupungua.
Mtazamo wa Uislamu juu ya
"Mungu Mmoja"
Wakati ukristo unababaika kueleza maana ya "Mungu mmoja" tatizo hilo halipo katika Uislamu:"Wamekufuru wale wasemao - Mwenyezi Mungu ni mmoja katika (wale waungu) watatu - (yeye ndiye wa tatu wao). Hali hakuna Mungu ila Mwenyezi Mungu mmoja (tu peke yake). (Quran 5:73)Mwandishi Mmarekani wa kiislamu Suzanne Hannef ameliweka jambo hili wazi kabisa pale aliposema: "-- Mungu sio kama nanasi au chungwa linaloweza kugawanywa katika sehemu tatu zinazounda kitu kimoja kizima. Kama Mungu ni nafsi tatu au ana sehemu tatu, basi kwa vyovyote vile hawezi kuwa Mmoja, wa pekee (kwa sababu tayari zipo nafsi nyingine mbili zenye sifa ya uungu). Wala hawezi kuwa ASIYEONEKANA, kwa sababu tayari Yesu ambaye ni moja ya nafsi ya Mungu ameshaonekana, jambo linaloharibu sifa muhimu za MUNGU HALISI NA WA KWELI.[8]
Tukiliangalia suala hili kwa upande mwingine: utatu una maana Mungu ana vijisehemu vitatu vilivyo tofauti tofauti (havikuungana) - Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Ikiwa Mungu ni mmoja tu (kwa mujibu wa wale wanaoamini utatu mtakatifu kuwa ni Mungu mmoja) itakuwaje huyo huyo mmoja awe Baba na awe Mwana? Ina maana kuwa yeye atakuwa ni mtoto (mwana) wa yeye mwenyewe. Matumizi ya akili na mantiki hayakubaliani na utatanishi na mkorogano wa mambo kama huu. Ukristo unadai kuwa unaamini kuwepo Mungu mmoja asiyekuwa na mshirika, lakini kwa kuwepo utatu mtakatifu unaodaiwa kuwa una nafsi tatu zote zikiwa na uwezo na sifa za uungu, hakuna shaka katika fikra za Waislamu kwamba ukristo umeshapoteza kabisa imani ya kumwabudu Mungu mmoja. Wakristo wameondoka kwenye ibada na imani ya Mwenyezi Mungu mmoja na badala yake wameingia kwenye ushirikina kwa sababu sasa hivi hawamwabudu Mwenyezi Mungu mmoja bali wana waabudu miungu watatu.
Wakristo hawazichukulii shutuma hizi kuwa ni nyepesi. Kwa upande wao wanawashutumu Waislamu kwamba hawaelewi hata maana ya utatu mtakatifu, wakidai kwamba Quran inauelewa utatu kuwa ni Allah. Mungu Baba, Yesu - Mungu Mwana na Bi Mariamu - mama yake Yesu - eti ndiyo maana Quran inaupinga utatu mtakatifu. Ambapo Kanisa katoliki lilibuni cheo cha "Mama wa Mungu" tangu mwaka 431 B.K., katika mkutano wa Baraza la Efesazi (Ephesus), uchunguzi makini wa aya za Quran ambazo hutumiwa zaidi na Wakristo kuthibitisha shutuma zao zinaonyesha madai kwamba Quran inamhesabu Bi Mariamu kuwa ni "Mmoja" wa nafsi tatu za Mungu katika utatu ni ya uongo.
Quran inaishutumu vikali imani ya utatu Mtakatifu (4:171), (5:73). Pia inaishutumu ibada ya kumwabudu Yesu na Mama yake Bi Mariamu (5:116). Hakuna sehemu yoyote katika Quran ambapo Quran inazikubali au kuzichambua nafsi tatu za utatu wa kikristo. Msimamo wa Quran ni kwamba NANI au NINI kinachounda imani hii si suala la msingi, bali imani yote ya utatu ni tusi dhidi ya upweke (umoja) wa Mwenyezi Mungu.
Hakuna sehemu yoyote katika dini inayompwekesha Mwenyezi Mungu (Uislamu) inapotajwa kumuabudu yeyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mmoja, na juu ya hili Quran ina msimamo thabiti:
"Na - - Mola wenu ni Mungu Mmoja: hakuna mungu mwingine isipokuwa yeye, Mwingi wa Rehema, Mwingi wa kurehemu". (Quran 2:163)
"- - Mimi ni Mola wenu na Mwenye kuwaruzukuni: kwa hiyo msimuabudi yeyote asiyekuwa Mimi". (Quran 21:92)
3) Kifo Kimoja Kufuta Dhambi za Wote?
Kwa haraka haraka, imani ya kafara inaeleza kwamba Yesu alipatwa na masaibu makubwa na kufa msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka kwenye minyororo ya dhambi.
Imani ya Kuwepo kwa Dhambi ya Asili
Lau Paulo angekuwa mfanyabiashara bila shaka angejenga nyumba iliyojaa fedha, lakini alikuwa mtu mbunifu hodari na mjanja sana, hii inaweza kuonekana kwa jinsi alivyounda mfumo wenye mzunguko mrefu usiokuwa na ulazima wa imani kwa ajili ya uokovu katika Ukristo. Hii inaweza kuonekana vizuri zaidi katika Imani ya Mateso na kifo cha Yesu - Imani ambayo imani nyingine zote - ile ya uungu wa Yesu, Utatu Mtakatifu na kuokoka kwa imani peke yake zimejengwa juu yake.
Mbele ya Paulo, wanadamu wote ni waovu na wadhambi, sifa ambayo wote wameirithi kutoka kwa Adam na dhambi lake la kula tunda la mti uliokatazwa katika Bustani ya Eden. Hii "dhambi ya asili" imewatambaa na kuwaambukiza wanadamu wote tokea wakati wa Adam. Kwa sababu ya maambukizi haya ya dhambi, mwanadamu hawezi kijinusuru kutoka kwenye minyororo ya dhambi hata afanye jitihada kubwa kiasi gani. Yesu ndiye angeweza kumkomboa na kumnusuru mwanadamu kutoka kwenye minyororo ya dhambi kwa kuwa yeye hakuzaliwa kutokana na mbegu ya mwanadamu.
Japokuwa kimantiki (kiakili) hii ni dhulma kwa Mwenyezi Mungu na Mwanadamu, ukristo kwa moyo mkunjufu umeichukua na kuihalalisha imani hii ya dhambi ya asili ili kuithibitisha dhana yao ya ujumbe na kazi ya Yesu, yaani kuteswa na kufa kwa ajili ya dhambi za mwanaadamu.
Alipokuwa akiunda imani hii ya dhambi ya asili yaelekea Paulo alisahau maneno ya Mungu katika Ezekiel 18:20 -22:
"- - Mtoto hatabeba dhambi za baba, wala baba hatabeba dhambi za mtoto."
Mwokozi Yesu: Muhanga wa Mwisho
Kwa mujibu wa Paulo, mwokozi alikuja katika sura ya Yesu: Mungu alimtuma mwanaye wa pekee duniani ili aje apate mateso na hatimaye afe msalabani ili damu itakayomwagika iwe kafara ya dhambi za wanaadamu, kwa hiyo Yesu ndiye aliyetolewa kafara (mhanga). Paulo alipata fikra hii kutokana na kafara zilizokuwa zikitolewa na Wayahudi kwa Mungu - ambapo maelezo yake yanapatikana katika agano la Kale na akahisi kwamba kafara hizi zilitolewa ili kupata msamaha wa Mungu kutokana na madhambi ya watu.
Wakati baadhi ya kafara hizi zilizotolewa na Wayahudi zilifanywa kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, Mitume waliokuja baadaye walikataza jambo hili. Katika Hosea 6:6, kwa mfano, tunasoma:
"Kwa kuwa Ninataka upendo thabiti na sio kafara".Mungu alitaka upendo - ambao husababisha kumwamini Yeye na utii wa sheria yake - kwani hii ni bora kuliko damu ya kafara. Hata Yesu mwenyewe aliusisitiza ujumbe huu tena, katika Mathayo 9:13, ambapo anasema:"Nendeni na mkajifunze maana ya maneno haya: Ninataka rehema sio kafara."Paulo aliyaweka yote haya pembeni akasema kwamba Yesu, kiumbe mkamilifu, alikuwa "Kafara (muhanga) wa mwisho" alipoyatoa maisha yake msalabani.
Nadharia ya Paulo ni kwamba Mungu hawezi kuchukuliwa kuwa ni Muadilifu mpaka amuadhibu mwenye dhambi. Toba peke yake haiwezi au haitoshi kuwa sababu "muhimu" kwa ajili ya kusamehewa madhambi yaliyofanywa. Anasema kuwa kuteswa na kufa msalabani kwa Yesu, ni muhimu sana kwa sababu heshima, haki, utukufu na uongofu wa Mungu haviwezi kukamilika kwa toba "tupu". Mkristo anaamini kwamba Yesu alisuluhisha na kupatanisha baina ya wanadamu na Mwenyezi Mungu kupitia kifo chake.
Mwandishi wa Kikristo Anis Shorrosh alilichunguza jambo hili kwa umakini sana miaka mingi iliyopita, na akahitimisha kwamba hakuna ukweli juu ya kuteswa na kufa katika kukiri imani na toba; nani atakayechukua mzigo wa dhambi zetu?[9]
Kutokana na suala zima kwamba Mwenyezi Mungu alimtaka Yesu ayatoe maisha yake kwa ajili ya dhambi za wanadamu, Paulo alimchukua Mwenyezi Mungu anayewapenda na kuwajali viumbe wake akamfanya kuwa ni katili na aliye mbali sana ambapo kitu kingine chochote kisichokuwa damu ya Yesu hakiwezi kumfikia wala kumridhisha.
Mungu wa Upendo
Fikra ya kwanza kubuniwa na Paulo na ambayo hutumika mara nyingi katika Ukristo kuhusiana naYesu ni Upendo na Mungu.
Kwa mujibu wa wakristo, upendo wa Mungu umekuwepo tu kwa sababu ya kusulubishwa na kufa kwa Yesu - alama ya upendo wa Mungu ni msalaba, kwa mujibu wa Wakristo. Kwa mujibu wa namna yao ya kufikiri, Mungu alitupenda mno hata akamtuma mwanae wa pekee ili apate mateso na hatimaye afe ili amwokoe mwanadamu kutoka kwenye minyororo ya dhambi.
Je Mungu Aweza Kufa?
Tukiendelea na dhana yenye kutatanisha kwamba Mungu wa Wakristo anaweza tu kusamehe dhambi ndogo kwa kusababisha dhambi kubwa - dhambi ya kumtoa Yesu ili auliwe - dhambi ya kuua, tunalazimika kujadili mada ya uungu ili tuweze kuijadili mada hii. Mungu ni wa milele, alikuwepo tangu na tangu na atakuwepo milele na milele: Hakuumbwa; Hawezikufa; n.k.
Kama Yesu ni mtoto wa Mungu, kama wakristo wanavyodai, hii ingemfanya na yeye kuwa Mungu pia, ingewezekanaje yeye, kama Mungu, afe msalabani kama wanavyodai?
Ikiwa "mwili wake wa ubinadamu" ndio ulikufa, hii italeta maana kwamba alikufa kama mtu mwingine yeyote. Na kama ni hivi - imani yote ya kuwa Yesu aliteswa na kufa msalabani kwa ajili ya dhambi za wanaadamu, itakuwa haina msingi wowote - kwani damu ya mtu wa kawaida haiwezi kuwa fidia ya dhambi za mtu mwingine.
Athari za Upagani Katika Imani Ambazo
Paulo Aliziingiza Katika Ukristo
Paulo hakuielewa maana halisi ya kafara zilizokuwa zikitekelezwa na Wayahudi katika Agano la Kale; waliteketeza kafara hizi kama shukrani kwa Mwenyezi Mungu kutokana na rehema nyingi ambazo Mwenyezi Mungu aliwajaalia - na sio kwa ajili ya kuhakikishiwa msamaha wa Mwenyezi Mungu kutokana na madhambi yao.
Karibu dini zote za kipagani zinaamini kwamba kafara wanazozitoa kwa miungu yao ni kwa ajili ya kutaka msamaha wa madhambi yao. Mimea, wanyama na hata watu waliuawa ili kuwa na uhakika ya "rehema ya Mwenyezi Mungu".
Sio hivyo tu bali karibu wafuasi wa dini zote za kipagani huchukua vyakula hasa mikate na pombe, vinavyokuwa vimetengwa kwa ajili ya sadaka kwa miungu. Wapagani waliamini kwamba kwa kula vyakula hivi vilivyotengwa kwa ajili ya miungu, wao pia (wapagani) walikuwa wanapata baadhi ya sifa na nguvu za kimungu - roho za miungu hao ziliingia na kuishi ndani yao (hao wapagani).
Paulo alichukua imani hii akaiingiza katika Ukristo, akaiita kuwa ni "Sakramenti ya chakula cha Bwana au Ekaristi". Kwa sababu inachukuliwa kuwa ni sehemu kubwa ya imani ya kuteswa na kufa kwa Yesu. Mfumo na tendo hili la Ekaristi umekuwa ni moja wa Sakramenti muhimu kabisa katika Ukristo kwa sababu ni alama na ukumbusho wa tendo la Yesu kutoa mwili na damu yake kama kafara na fidia ya dhambi za mwanadamu.
Imani hii ambayo Paulo aliingiza katika Ukristo kutoka kwenye upagani ilimrahisishia sana kazi. Kwa hadhira yake - watu wa mataifa hawakuona taabu yeyote kuingia katika ukristo kwani imani ya Mungu kufa akiwa kijana na baadaye kuwa hai kuwaokoa watu wake ili kuwepo katika imani zao za kipagani. Ikiwa miungu wao akina Adonis au Mithran waliwahi kufanya kitu cha aina hii kwa ajili yao kwanini Yesu ashindwe kulifanya hilo sasa hivi?
Paulo Alifanikiwa Kitu Gani?
Watu wa mataifa kwa mara nyingine tena walifarijiwa: walikuwa na waokozi katika dini zao za zamani za kipagani, na mara hii tena, Paulo aliwapa mwokozi mmoja katika imani yao mpya ya Ukristo. Aliwaambia kwamba walichokuwa wanatakiwa kukifanya ili kuwa na yakini kwamba Mwenyezi Mungu atawasamehe madhambi yao ni kuamini kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zao, hilo tu ndilo walilotakiwa kulifanya.
Katika sheria ya Kiyahudi, mambo muhimu katika kafara au fidia kwa ajili ya madhambi ni Rehema ya Mwenyezi Mungu, toba na jitihada za dhati katika kufanya mambo ya kheri; kafara ya damu haikuhitajika. Katika jitihada zake za kuwapata watu wa mataifa, Paulo alilitafsiri upya Agano la kale na akawapa Wakristo wapya mwokozi wao - mtu ambaye huyatoa maisha yake kwa ajili ya wengine.
Wakristo wa leo hawana ukaribu na upagani kama ilivyokuwa katika wakati wa Paulo. Imani yake ya kuteswa na kufa kwa Yesu kwa ajili ya dhambi za wanadamu - aliyoiingiza katika ukristo, imekuwa ni tatizo kubwa kwa Wakristo kuilezea ikaeleweka, baada ya kuona jambo zima linatatanisha wakati nguvu za hoja na akili zinapojaribu kufurukuta na kutaka kutumika.

Mtazamo wa Uislamu Juu ya
Dhambi Ya Asili
Uislamu inaichukulia imani ya dhambi ya asili na kifo cha Yesu kama inavyoaminiwa na Wakristo kama ifuatavyo:1) Dhana ya Dhambi ya AsiliImani ya ukristo juu ya dhambi ya asili haina nafasi yoyote katika Uislamu, kwani Waislamu wanaamini kwamba mwanadamu huzaliwa akiwa hana dhambi yoyote. Ndani ya Quran, Mwenyezi Mungu anasema:"Uelekeze uso wako katika dini iliyokuwa sawa ambayo Allah amemuumbia mwanadamu, ambayo inawiana na maumbile ya mwanaadamu". (Quran 30.30)Aya hii inatueleza kwamba Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu katika umbile zuri kabisa, na akiwa ni twahiir, asiyekuwa na dhambi lolote; na kwamba umbile lake lilikuwa linamwongoza kutii na kuinyenyekea sheria ya Mwenyezi Mungu.[10]Dhambi hairithiwi: ni kitu ambacho mwanaadamu hujiletea mwenyewe anapofanya jambo ambalo hakutakiwa kulifanya au anapoacha kufanya jambo ambalo alitakiwa kulifanya. Kusema kwamba kila mmoja wetu huja duniani anapozaliwa akiwa na mzigo wa dhambi iliyofanywa na babu yake wa nyuma kabisa huko itakuwa si chochote isipokuwa ni kukana sifa ya Mwenyezi Mungu ya uadilifu na rehema yake.
Ingawa Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu uhuru wa kuchagua na kufanya mambo anayoyapata hapa duniani, mwanaadamu ni kiumbe mwenye mfumo maalumu na mwenye asili na uwezo maalum. Mwanadamu atalipwa au kuadhibiwa kwa lile alilofanya yeye mwenyewe, si kwa lile lililofanywa na ndugu yake wa zamani huko. Matendo yetu wenyewe ndiyo yatakayoangaliwa siku ya hukumu na katika muda wa uhai wetu, Mwenyezi Mungu hutupatia kila nafasi inayowezekana ili tuweze kufanikiwa na Mwenyezi Mungu si mwenye kutudhulumu, mwenye kututwisha mzigo wa dhambi ambazo hatukuzifanya. Kwa hiyo ni sisi wenyewe ndio tutakaoitengeneza au kuiharibu hatima yetu hapa duniani na kesho huko akhera.
Hii ni kwa sababu Waislamu wanaamini kuwa Mwenyezi Mungu alimsamehe Adam, kosa lake la kutotii amri ya Mwenyezi Mungu.
"Kisha Iblis aliwatekelezesha (wakala tunda katika ule mti) katika Bustani, na akawatoa katika ile hali waliyokuwa nayo -- kisha Adam akafunuliwa kuwa anatakiwa atubu, alipotubu Mwenyezi Mungu alimsamehe, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi kusamehe, Mwingi wa Rehema". (Quran 2:36-37)
Mwenyezi Mungu alimsamehe Adam, na vilevile alimuondolea aibu na alamu ya kutorehemewa ambayo wakristo wanadai kuwa inarithiwa na wanadamu wote tokea wakati huo wa Adamu mpaka leo na watakaondelea kuzaliwa.2) Kifo Cha YesuKuhusiana na suala la kifo cha Yesu msalabani - ingawa ni wazi kwamba Yesu, kama alivyokuwa kwa mitume wengine kabla yake, walipatwa na masaibu makubwa kwa sababu ya kujaribu kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watu ambao hawakuonyesha nia na ari ya kuupokea. Na alikuwa anajua vizuri kwamba hili lingemtokea, hata hivyo hakufikia kiwango cha kuuliwa na hususan kuuliwa kulikopangwa na Mungu - kama ilivyodai Paulo baadaye, yaani kuuliwa ili kumwokoa mwanadamu kutoka kwenye minyororo ya dhambi.
Katika Bustani ya Gethsemane, Yesu aliomba kwa unyenyekevu na shauku kwa Mwenyezi Mungu kuwa "kikombe kinipite" (Mathayo 26:39), ambapo kikombe hiki kinamaanisha kukamatwa na kufa kwake. Hivi kweli tunaamini kwamba mja mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu anaweza kuomba rehema akanyimwa?
Wazo zima la kuteswa na kufa kwa Yesu msalabani ili awe kafara ya dhambi za wanadamu halikubaliani na hoja za kiakili na mantiki linapohusishwa na Mwenyezi Mungu ambaye ni muadilifu. Je inawezekana kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwadilifu kwa kiwango cha juu kabisa akakataa kumsamehe Adam - na kizazi chake baada yake kwa ajili ya dhambi lake tu (Adam) - mpaka Yesu aje? Je inawezekana kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni muadilifu amlazimishe mmoja wa waja wake akataka na kuruhusu kudhalilishwa na kuuwawa kwa mmoja wa mitume wake aliyekuwa mnyenyekevu na mtii sana kwake? Je inawezekana kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni muadilifu amlazimishe mmoja wa waja wake afe kwa ajili ya dhambi za watu wengine? Katika Uislam, hatudhani kuwa hili linawezekana.
Tukiliangalia hili kutokana na mtazamo wa upendo Mwenyezi Mungu, hoja zile zile zinatajitokeza kuhusiana na uadilifuwa Mwenyezi Mungu: Je Mungu mwenye upendo mkubwa kwa waja wake angewaadhibu wanaadam wote bila kuja Yesu? Je Mwenyezi Mungu mwendo upendo mkubwa kwa waja wake angehitaji kuwa ni lazima mmoja wa waja wake wema na waaminifu (Yesu) adhalilishwe na kuuawa ili awasamehe wanadamu madhambi yao? Yeyote na kila mtu anaweza kushangaa na kujiuliza hii ni AINA gani ya upendo wa Mungu unaoweza kudai kiasi cha gharama kikubwa kiasi hicho na cha kutisha namna hii.
Uislam unashikilia kwa nguvu msimamo kwamba kila mtu anawajibika kwa vitendo vyake: kila mtu ataadhibiwa kwa maovu yake. Haiingii akilini kwamba Mwenyezi Mungu ambaye ni muadilifu anaweza kumuadhibu mtu kwa dhambi alizofanya mtu mwingine.
"Kila nafsi italipwa kutokana na matendo yake na nafsi haitaulizwa juu ya matendo ya nafsi nyingine". (Quran 6:164)Hakuna mtu anayeweza au atakaye adhibiwa kwa dhambi za mtu mwingine. Mwenyezi Mungu anatuambia kwamba kila mmoja wetu atalipwa au kuadhibiwa kutokana na aliyoyafanya yeye mwenyewe katika maisha yake."Na Mwenyezi Mungu hamtwishi yeyote mzigo mkubwa kuliko ule anaoweza kuubeba. Kila jema nafsi inalolifanya ni kwa faida yake, kila uovu inaoufanya ni kwa hasara yake." (Quran 2:286)3) Kuhusiana na Kafara"Na katika kila ummah tuliwafundisha namna ya kufanya kafara ili wapate kulikumbuka na kulitukuza jina la Mwenyezi Mungu kwa riziki alizowaruzuku - - - nyama na damu havimfikii Mwenyezi Mungu, ni uchaji Mungu wenu ndio humfikia". (Quran 22:34,37)Kwa hiyo, Uislamu haumini kwamba Yesu aliuliwa. Quran inasema:"Walisema kwa jeuri, tulimuua Yesu kristo, mwana wa Mariamu, mjumbe wa Mwenyezi Mungu --- lakini hawakumuua wala hawakumsulubisha - bali Mwenyezi Mungu alimpaisha juu kwenda kwake (Mwenyezi Mungu)." (Quran 4:157-158)Kwa kifupi, imani ya ukristo kuwa Yesu aliteswa na kuuliwa ili awe kafara ya dhambi za wanadamu haina nafasi yeyote katika Uislam. Waislamu wanaamini kwamba Mwenyezi Mungu anachotaka ni toba ya kweli:"Ombeni msamaha kwa Mwenyezi Mungu na tubuni toba ya kweli. Kwani Mola wangu bila shaka ni mwingi rehema na Mwenye kuwapenda waja wake." (Quran 11:90)
Uokovu Unatoka kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake
"Lakini kwa yeyote atakayetubia, akaamini, na kufanya vitendo vizuri, atakuwa ni miongoni mwa wale watakaookoka (na adhabu ya moto). (Quran 28:67)Tukimwamini Mwenyezi Mungu, na tukijinyenyekesha kwake na kuufuata Mwongozo wake, tutakuwa na yakini (uhakika) wa Huruma na Rehema yake. Kama aya hapo juu inavyoonyesha, ikiwa toba yetu ni ya kweli, Mwenyezi Mungu anaweza na hutusamehe madhambi yetu. Hakuna haja ya mwombezi kwani kila mmoja wetu anaweza kumweleza Mwenyezi Mungu shida zake zote moja kwa moja na wakati wowote. Kwa kifupi hakuna haja ya mwokozi: Mwenyezi Mungu peke yake anaweza kulifanya hili.[11]4) Kuokoka kwa Imani Peke YakeKwa haraka haraka, imani ya wokovu katika Ukristo inasema kwamba mwanadamu anaweza kuokoka kwa kuamini tu kuwa Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi za wanadamu.
Kuwaridhisha Watu wa Mataifa (Gentiles)
Kulikuwa bado kuna suala juu ya nini kitakachotokea baada ya kifo. Mitume wote walifundisha juu ya raha za peponi na shida za motoni, Yesu pia alilifundisha hili. Waumini wapya wa Paulo walihofishwa sana juu ya hili. Walitaka kujua ni namna gani wangeweza kuwa na uhakika wa kuingia peponi pindi mwisho wa dunia utakapofika.
Sheria ya Kiyahudi ilifundisha kwamba mtu angeweza kuokoka kwa kutii sheria za Mwenyezi Mungu, watu wa mataifa, hawakulifurahia wazo hili. Walikwenda kulalamika kwa Paulo kwamba kutii sheria za Mwenyezi Mungu lilikuwa ni jambo gumu sana kwao. Katika kulitatua tatizo hili, Paulo alisema utii wa sheria halikuwa jambo la lazima:
"- - Ni dhahiri kwamba sheria haiwezi kumfanya mtu akubalike mbele ya Mungu- - - hakuna uhusiano kati ya sheria na imani --- kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria- - -". (Wagalatia 3: 11-13)Japokuwa sheria ilikuwa inamweleza mwanadamu yepi ni mazuri na yepi ni maovu na kuwahimiza kufanya mema na kuepuka maovu Paulo alisema kwamba kuja kwa Yesu kulibatilisha msingi kwamba utii wa sheria ni muhimu kwa ajili ya wokovu:"Maana mtu hufanywa akubalike mbele ya Mungu kwa imani si kwa kutimiza matakwa ya sheria." (Waroma 3:28)Licha ya ukweli kwamba Yesu mwenyewe alisema kuwa hakuja kuivunja sheria bali kuikamilisha (Mathayo 5:17), Paulo alilidharau kabisa wazo hili, akasema kwamba kumuamini Yesu peke yake kunatosha kumfanya mtu aokoke. Kwa mujibu wa Paulo, kuja kwa Yesu na kuyatoa maisha yake kama kafara ya dhambi za wanadamu, kulikuwa ndio mwisho wa haja ya kufuata sheria ya Mungu ili kupata wokovu. Sasa hivi imani peke inatosha. Uokovu sasa hivi haukutegemea ubora wa maisha ya mtu kimaadili au vitendo vizuri alivyovifanya, bali unategemea imani mtu aliyokuwa nayo.
Laana ya Sheria
Paulo alikuwa na sababu nyingine kuhusiana na msimamo wake juu ya sheria ya Mwenyezi Mungu. Katika kumbukumbu la Torati 21:23, Mungu anamwambia Musa kwamba mtu "aliyetundikwa katika mti"--- kwa maneno mengine aliyesulubiwa "amelaaniwa na Mungu".
Ili kulinda hoja yake kuwa Yesu alisulubiwa kwa ajili ya dhambi zetu, na kwa sababu sheria inasema aliyesulubiwa amelaaniwa, Paulo aliamua kuiponda sheria kwa kusema:
"Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na sheria, wako chini ya laana. --- Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajiliyetu; maana maandiko yasema "Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa". (Wagalatia 3:10:13)Kwa sababu Paulo aliiona sheria ya Mungu kuwa ni laana, hivyo maneno ya Mungu katika kumbukumbu la Torati 21:23 hayakuwa na maana yoyote. Alipotosha maneno ya aya hii kwa kusema kuwa kwa sababu Yesu alipatwa na laana kwa kuwa aliuliwa kwa kusulubiwa msalabani, na kwa vile yeye hakuwa na hatia, aliibeba laana hii kwa sababu ya dhambi za wengine. Na kwa sababu hii (Yesu) hakuwa na chembe chembe zozote za aibu au udhahili unaotokana na laana. Alilofanya Paulo hasa ni kulipa utukufu jambo ambalo awali lilikuwa linaonekana ni la aibu sana (kutundikwa msalabani) ili aweze (Paulo) kutetea imani aliyoanzisha kwamba uokovu umepatikana kwa sababu ya kusulubiwa na kufa kwa Yesu kwa kudai kuwa kutundikwa kwake msalabani (Yesu) hakukumletea aibu yoyote japo sheria haikubaliani na wazo hili.Anis Shorrosh anasema: "Msalaba, alama ya aibu, kupitia kwa Yesu ulibadilika na kuwa changamoto. Msalaba, uliokuwa alama ya kifo, kupitia kwa Yesu, ulibadilika na kuwa alama ya uhai".[12]
Kwa sababu ya upinzani mkali kutoka kwa wanafunzi wa Yesu, Paulo alilazimika kwenda pole pole katika utekelezaji wa jambo hili. Alianza na kitu kimoja ambacho watu wa mataifa walikipinga sana, yaani kutahiri (tohara). Kwa mujibu wa Paulo, Ibrahimu alikuwa mwongofu hata kabla ya kutahiriwa, sasa kwa nini watu waendelee kusumbuliwa kwa kuwataka watahiriwe? Paulo aliuupuza ukweli kwamba Mungu alikuwa ameweka agano hili mamia ya miaka kabla ya kuja Ibrahim. Kwa upande wake Nabii Ibrahim alipewa amri hii kutoka kwa Mungu juu ya kuwatahiri watoto wa kiume wote kuanzia wa zama zile na wote ambao watafuatia baadaye katika kitabu cha Mwanzo 17:14, Mungu aliliweka wazi jambo hili:"Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu".Mtu anaweza kushangaa vipi Paulo aamue kuyafuta maneno haya ya Mungu bila uoga wowote. Ubatizo ulichukua nafasi ya tohara (kutahiri), kumwagiwa maji sasa kumefanywa kuwa ndio alama ya agano baina ya Mungu na Mkristo. Watu wa mataifa walifurahia sana mabadiliko haya yaliyofanywa na Paulo.
Baada ya hili alianza kufanya mabadiliko katika uhalali na uharamu wa vyakula, na masuala mengine yalifuatia moja baada ya jingine. Ndani ya muda mfupi, sheria ya Mwenyezi Mungu haikuonekana tena kuwa ni mwongozo, unaostahiki kufuatwa katika maisha ya kila siku bali lililokuwa muhimu ni tu kuwa na imani kuwa Yesu aliteswa na hatimaye kufa msalabani kwa ajili ya dhambi za wanadamu. Hii ilikuwa inatosha kabisa kwa uokovu na sio kufuata sheria ya Mungu.
Kwa mujibu wa Paulo, suala la kufanya matendo mazuri kwa Mkristo linaweza tu "kuja lenyewe". Na muhimu zaidi kwa mkristo ni kuelewa kwamba vitendo vizuri peke yake haviwezi kumfanya mtu aokoke hata kidogo. Jambo pekee linaloweza kumfanya mtu aokoke ni imani juu ya uwezo wa Yesu wa kuokoa na kwamba alikufa kwa ajili ya dhambi zetu ili tupate kuokoka - imani hii peke yake inatosha kumfanya mtu aokoke na adhabu ya moto wa jahanamu.

Paulo Alifanikiwa kwa
Kukamilisha Jambo Gani ?
Paulo iliwapatia wakristo wapya imani ya wokovu kwa imani peke yake kwa sababu kubwa moja: Kupata wafuasi miongoni mwa watu wa mataifa. Watu wa mataifa walikuwa wamechunguza matendo mbali mbali ya kidini yaliyokuwa yanafanywa na Wayahudi lakini walikuwa wanasita kuukubali ukristo kwa sababu ya kuepuka miongozo na kanuni katika sheria ya Musa.
Imani na msingi huu wa mwisho yaani kuokoka kwa imani peke yake, imani ya kumwamini Yesu, ilikuwa ni imani kubwa na muhimu sana kuliko zote iliyobuniwa na Paulo. Na japokuwa ilikuwa ni dhambi kubwa sana kufanya mabadiliko katika imani kubwa na muhimu kama hii, lakini mabadiliko haya ndiyo yaliyopelekea mafanikio makubwa aliyoyapata Paulo katika kazi yake, kwa sababu aliwapa mambo yote muhimu waliyoyataka. Na kwa sababu hii watu wengi walimiminika makundi kwa makundi kuingia katika hii dini mpya ya Paulo yaani "Ukristo wa Paulo" sio "Ukristo wa Yesu". Yesu hakuwa amekusudia kufundisha mafundisho tofauti na yale waliyokuwa nayo Wayahudi kutoka kwa Nabii Musa wala hakukusudia kuanzisha dini mpya, lakini kwa sababu ya Paulo, Ukristo ulizaliwa na kuenea duniani kote, shukrani ziyaendee mafundisho ya Paulo.
Mtazamo wa Uislamu
Mungu alimtuma Yesu kwa Wayahudi kwa sababu waliiacha ibada ya Mwenyezi Mungu kwa madai na visingizio kwamba wanafuata sherehe na uchambuzi wa kina wa sheria. Vitabu 63 vya Talmud - ambavyo ni tafsiri na uchambuzi wa sheria ya kiyahudi - ni uthibitisho juu ya jambo hili. Wayahudi waliamini kwamba wokovu unapatikana kwa kutii sheria ya Mungu.
Yesu alitumwa katika jitihada za kuwaelewesha kwamba vitendo vizuri peke yake sio mwisho wa mambo yote bali walitakiwa pia kumuamini Mwenyezi Mungu. Yesu alihimiza tena na tena kwamba "ibada tupu bila imani thabiti", si jambo lililotakiwa na Mungu kutoka kwao bali lililokuwa likitakiwa ilikuwa ni kufuata sheria zilizomo katika maandiko matakatifu "kwa dhati, uchaji Mungu na kumhofu Mwenyezi Mungu kwa dhati".[13] Hili ndilo jambo ambalo Yesu alilifundisha bila kuchoka lakini kwa bahati mbaya, leo hii haya sio mafundisho ambayo Ukristo unasimamia utekelezaji wake ule ujumbe wa Yesu:
"Amri kuu kuliko zote ni, sikieni, Enyi Israel; Bwana Mungu wetu ni Mungu mmoja".Unaopatikana katika Marko 12:29, si chochote ila ni maandishi tu katika karatasi Paulo alimpachika Yesu uungu, kisha akaandaa masharti ya uokovu kwamba kilichotakiwa ni imani peke yake juu ya Yesu kwamba alikufa kwa ajili ya dhambi za wanadamu. Utii wa sheria ya Mwenyezi Mungu ulitupiliwa mbali na ukaitwa kuwa ni "Laana". Quran imeliweka jambo hili wazi kabisa. Imetaja masharti ya uokovu kuwa ni mawili, kumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja na kutii sheria zake."Kwa wale ambao wameamini na wakafanya vitendo vizuri Mwenyezi Mungu amewaahidi msamaha na malipo makubwa". (Quran 5:9)[5] This Is The Catholic Church, p. 4. (Hili ni Kanisa Katoliki, uk. 4).[6] Webster's New World Dictionary, p. 879. (Kamusi mpya ya ulimwengu ya Webster, uk. 879.)
[7] Excerpts from the Athanasian Creed.. (Nukuu kadhaa kutoka katika dhehebu la Athanasi).
[8] What Everyone should Know About Islam and Muslims, pp. 183-4. (Mambo yampasayo kila mmoja kuyajua juu ya Uislamu na Waislamu, uk. 183- 4).
[9] Ibid, p. 135. (Kitabu hicho hapo juu).
[10] Islam In Focus, p. 137 (Uchunguzi juu ya Uislamu, uk. 137).
[11] What Everyone Should Know About Islam and Muslims, p. 183. (Mambo yampasayo kila mmoja kuyajua juu ya uislamu na Waislamu, uk. 183).
[12] Islam Revealed, p. 137. (Uislamu wawekwa wazi, uk. 137).
[13] What Everyone Should Know About Islam and Muslims, p. 180. (Mambo yapasayo kila mmoja kuyajua juu ya Uislamu na Waislamu, uk. 180.)

Imechukuliwa kutoka Al-Islam.org

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget