Friday, February 24, 2012

Unapopata Mitihani Subiri Unapopata Mitihani Subiri


‘Abdun-Naaswir Hikmany

 Muombe Mola wako Akujaalie katika wale ambao wanapopewa mtihani wanasubiri, kwani wengi wanaporomokea kwenye maasi kwa sababu ya kushindwa kusubiri kwa mitihani waliyopewa.

Basi kwa hakika, kila Muislamu ni mwenye kukumbwa na mtihani. Bali sio hao tu, hata wanyama na mimea wanakumbana na matatizo. Isipokuwa wanaadamu wanalipwa kutokana na subira yao mbele ya Hisabu. Tumuombe sana Mola wetu kuwa miongoni mwa wenye kusubiri.

Mitihani yaweza kuja katika sura tofauti. Yawezekana ukazushiwa mambo kutoka kwa walimwengu ambayo hujayafanya. Pia mtihani upo katika mwili, huenda ukakumbwa na maradhi ikawa maji ya kunywa unapenyezewa kwa mirija, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Asitufikishe huko. Halikadhalika, mtihani mwengine ambao wengi wao unawakumba lakini hawauelewi kwamba ndio mkubwa ni mali. Nayo mali ipo kwa watoto, wake na fedha. Vyote hivyo ni fitnah na kila Muislamu ana wajibu wa kuvitumia namna Alivyoelekeza Mola Mlezi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

{{Na jueni ya kwamba mali zenu na watoto wenu ni mtihani (huo Aliokupeni Mwenyezi Mungu kutazama mtaendesha vipi) na jueni ya kwamba kwa Mwenyezi Mungu yako malipo makuu (kabisa).}} [Suratul-Anfaal: 28]

Subira ya mtihani wa mali sio tu wakati wa kuihodhi, bali hata pale inapopungua, kuondoka kabisa ama kutoipata basi Muislamu anastahiki kusubiri. Mola wetu Mlezi Hayupo pamoja na wanafiki, mafisadi, makafiri wala mabadhirifu. Bali Allaah Yupo pamoja na wenye kusubiri na kwa hakika hilo ndio kundi lililofuzu:

{{Hakika leo Nimewalipa (Pepo) kwa sababu ya kusubiri kwao, bila shaka hao ndio wenye kufuzu.}}[Suratul-Mu'minuun: 111]

Kufariki kwa mtu wa karibu pia ni mtihani, nao waweza kumfanya Muislamu kuingia katika shirki kwa kuomboleza hadi kwenda kwa waganga kupiga ramli. Kwa hapa omba uwe miongoni mwa wale ambao wanapofariki vipenzi vyao wanasema:

{{Ambao uwapatapo msiba husema: "Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye tutarejea (Atatupa jaza Yake)".}} [Suratul-Baqarah: 156]
Kwa hakika hakuna mtihani ambao unatukuta, isipokuwa umeandikwa katika Lawhul-Mahfuudh. Hivyo ni wajibu wetu kusubiri.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget