Thursday, February 23, 2012

Mtazamo Wa Uislamu Juu Ya Sayansi


Katika Hadith mashuhuri ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tunasoma hivi:“kutafuta elimu ni wajibu kwa kila Muislamu”. Ni aina gani ya elimu ambayo Hadith hii inaizungumzia?
tunasema ‘fani yoyote ya elimu ambayo ina manufaa kwa jamii ya Kiislamu lazima ikubalike kuwa ni sehemu ya elimu ya Kiislamu’.
Mfumo wa elimu uliopendekezwa na Uislamu ni mpana sana kwa mnasaba wa aya ya 5 ya sura ya 96 ya Qur’an. (MwenyeziMungu) kamfundisha mwanadamu yale yote ambayo alikuwa hayajuwi.
Hii inatukumbusha ukweli kuwa chanzo cha elimu zote ni Allaah. Katika Qur’an nabii Suleiman anazungumzia ukweli kuwa yeye amefundishwa lugha za ndege na anaiona hii ni fadhila kutoka kwa MwenyeziMungu:
“Enyi watu! Sisi tumefundishwa (hata kutambua) usemi wa ndege na tumepewa kila kitu, hakika hii ni fadhila iliyo dhahiri (27:16).
MwenyeziMungu anazungumzia alivyomfundisha nabii Daud kutengeneza nguo za chuma kuwakinga watu wake vitani:
“Na Tukamfundisha (Daudi) matengenezo ya mavazi ya vita kwa ajili yenu ili kukuhifadhini katika mapigano yenu. Je! Mtakuwa wanaoshukuru?” (21:78-80).
Halafu ipo Hadith ndefu inayoelezea kigezo cha elimu halali ambayo ni aina yoyote ya elimu  inayokidhi mahitaji halali ya waja wa MwenyeziMungu ili kuendeleza maisha yao.
“Aina yoyote ya elimu ambayo inamuondolea shida mwanadamu au ina manufaa kwa waja wa Mwenyezi Mungu na inawasaidia kuendeleza maisha yao na kujikidhia mahitaji yao ya kila siku ni halali katika dini kuifundisha au kujifunza.
Kwa mfano Uandishi, Hisabati, Biashara, utengenezaji wa vito, ufyatuwaji matofali, ususi, ushoni, uchoraji na uchongaji picha (isipokuwa za watu na wanyama) na kutengeneza vyombo au vifaa vinavyohitajiwa na watu.
Hata kama elimu au ujuzi huo unaweza kutumika kwa malengo mabaya na mema kwa wakati mmoja mathalani uandishi unaoweza kutumika kuimarisha tawala za madhalimu bado si haramu kuusomea na kuufundisha.
Hivyo, uhunzi wa kutengeneza visu, mapanga, mikuki, pinde, bunduki ambavyo vinaweza kutumiwa vizuri au vibaya si haramu.
Kufundisha, kujifunza mambo hayo au kupokea ada kwa ajili ya kuyafundisha maadamu ni kwa ajili ya kunufaisha waja wa  MwenyeziMungu, ni halali.
Vyovyote iwavyo, si dhambi kwa mtu kufundisha au kujifunza fani hizo kwani manufaa yake ni makubwa zaidi kuliko madhara yanayosababishwa na matumizi mabaya ya fani hizo. Maisha ya jamii ya wanadamu huvitegemea mno vitu hivyo.
Hata hivyo, matumizi mabaya ya vitu hivyo ndiyo yaliyoharamishwa. Hii ni kwa sababu MwenyeziMungu Ametukataza kukiendea kitu chochote kibaya kisicho na matokeo mazuri. 
Aya za Qur’an  na Hadith za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilizonukuliwa hapo juu zinabainisha kuwa, katika Uislamu, kusoma au kutafuta elimu hakukomei tu katika fani za elimu ya dini tu..
Uhalali huu haukomei katika maana ya kusafiri kwenda mbali bali hata kama mahali alipo Muislamu pana taasisi ya elimu inayomilikiwa na watu wasiofuwata dini ya Uislamu na hata kama mtalaa wa taasisi hiyo haujumuishi elimu ya dini ya Kiislamu bado ni muhimu kujiunga nayo kwa ajili ya kupata elimu na ujuzi wenye manufaa kwa jamii nzima 
Hoja ya kupanuwa zaidi wigo wa fani za elimu  kwa mtazamo wa Uislamu inatiwa nguvu hata na sherehe za wanachuoni kuhusiana na fani za elimu. Wanazuoni hao waliukubali urathi wa elimu kutoka jamii nyingine.
Wanazuoni hao waliziona fani hizo za elimu kuwa ndiyo njia muhimu za kumjua MwenyeziMungu kwa dalili za kimaumbile. Waliongozwa na Qur’an na Sunna katika jitihada zao za kushughulika na elimu katika eneo hili.
Sasa tuligeukie swali je ni aina gani ya elimu ipewe umuhimu wa kwanza? Hapa tunakuta Hadith za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa upendeleo utolewe kwa ile yenye manufaa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema, “elimu bora kabisa ni ile inayoleta manufaa”.
Bado swali jingine linazuka, ni kipi hasa kigezo cha manufaa ya fani ya elimu? Kutokana na Qur’an na Hadith, tunaweza kusema kuwa elimu yenye manufaa ni ile yenye sifa moja au zaidi miongoni mwa sifa hizi:
1.     Ile inayomfanya mtu amjuwe zaidi MwenyeziMungu
2.     Ile yenye kuipatia jamii ya wanadamu ustawi bora
3.    Ile inayojenga maadili bora na kuupa nafasi ya juu utamaduni wa Muumba. “Na neno la Allaah ndio liwe juu zaidi” (9:40)
Nafasi ya Fani za Elimu katika kumjuwa MwenyeziMungu
Kuna aya nyingi za Qur’an ambazo zinaelezea maumbile ya ulimwengu na kumtaka mwanadamu ayatazame na kuyatafakari.
“Sema: ‘Tazameni nini yanayotokea katika mbingu na ardhi! (10:101)’”
“Sema: ‘Tembeeni katika ardhi na tazameni Alivyoanzisha kuumba, kisha MwenyerziMungu ndiye Atakayeumba umbo la baadae. Bila shaka MwenyeziMungu ni Mwenye Uweza juu ya kila kitu. (29:20).
Hali kadhalika tunahimizwa kusoma historia ya jamii zilizopita ili kujuwa kanuni za MwenyeziMungu katika maumbile.
“Zimepita adabu namna kwa namna walizotiwa waliokuwa kabla yenu. Basi safirini katika nchi na muwone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.” (3:137)
 1-    Nafasi ya Fani za Elimu katika maendeleo ya jamii
Ilikuwa ni programu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuanzisha jamii ya wacha Mungu ambamo maneno ya MwenyeziMungu ndiyo yatawale na ambapo makafiri wasiwe na cha kuwashindia waumini.
“Na MwenyeziMungu Hatawajaalia makafiri njiya ya kuwashinda Waumini.” (4:141)
Na tunayo Hadith ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa: “Uislamu ndio bora kuliko vingine vyote na hakuna cha kuushinda.”
Qur’a inawataka walioamini kujiandaa kukabiliana na nguvu za makafiri.
“Basi waandalieni nguvu mziwezazo ili kwazo muwaogopeshe maaduwi wa MwenyeziMungu na maaduwi zenu” (8:20).
 “Iwapo hatari ya utawala wa kisiasa na kiuchumi wa aduwi inazidi kuwa kubwa kiasi kwamba inaweza kuiweka jamii ya Kiislamu chini ya mamlaka yake (na kusababisha udhalili na idhilali kwa Uislamu na Waislamu, na kuwatia unyonge), itawapasa Waislamu wote kuilinda dini yao kwa njia na kwa zana zile zile za aduwi yao.”
Hapana shaka kuwa katika zama zetu hizi sayansi na tekinolojia ndizo zinazochukuwa nafasi muhimu katika kulinda uhuru na hadhi ya jamii yoyote ile.
Hivyobasi, sisi Waislamu tunatakiwa kuwa mstari wa mbele katika fani hizi, ili kuweza kuiongoza dunia kama wenzetu waliopita walivyofanya katika zile enzi bora za utawala wa Kiislamu.
2. Nafasi ya Sayansi katika Qur’an na Sunna
Nini tunachotakiwa kujifunza katika zile zinazoitwa aya za kisayansi ndani ya Qu’an, aya zinazozungumia maumbile? Ujumbe wa aya hizo zinazoitwa za “kisayansi  ni kuwa tuzione dalili za MwenyeziMungu katika maumbile.
Hiyo itatupelekea kuutambuwa uweza wa MwenyeziMungu. Zaidi ya hivyo, kwa kuzitambuwa kanuni za maumbile, twaweza kuzitumia vema kwa ajili ya ustawi wa wanadamu.
Lakini katika Qur’an tunajifunza mambo ambayo masomo ya sayansi na sayansi za maumbile haziwezi kutupatia mtazamo wa jumla juu ya ulimwengu.
Kwa mujibu wa  Qur’an milango yetu ya nje ya fahamu ina umuhimu wa kufahamia maumbile
“Na MwenyeziMungu amekutoeni matumboni mwa mama zenu hali ya kuwa hamjuwi chochote na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo..” (16:78)
Hivyo, kwa mtazamo wa Qur’an milango ya fahamu ni nyenzo muhimu za kupatia elimu kuhusu ulimwengu wa nje, lakini  milango hiyo pekee haitoshi kutupatia elimu juu ya maumbile kwa sababu njiya hii ya utambuzi hutupatia tu mtiririko wa ishara na dalili za hapa na pale.
Ni akili yetu inayokamilisha utendaji kazi wa milango ya fahamu. Kuthibitisha dai hili, tunatazama ndani ya Qur’an na katika Hadith za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Inaelezwa mara kwa mara ndani ya Qur’an kuwa uwezo wetu wa kutambua mambo uzidishwe kwa kutumia akili. Vinginevyo hautatupelekea kufanya uamuzi sahihi.
 “Na amekutiishieni usiku na mchana na juwa na mwezi. Na nyota pia zimetiishwa kwa amri yake. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wenye akili.” (16:12)
Kuna watu wenye macho, masikio na kadhalika lakini milango hii ya fahamu haina manufaa halisi kwao kwani hawayatafakari yale yanayoonwa au kusikiwa na milango hiyo ya fahamu.
 “Nyoyo wanazo lakini hawafahamu kwazo, na macho wanayo lakini hawaoni kwayo, na masikio wanayo lakini hawasikii kwayo” (7:179)
Kuna msemo wa mwanachuoni mmoja ambao unabainisha kazi ambayo akili inafanya baada ya milango ya fahamu kutimiza kazi yao ya kuona au kusikia. Mwanachuoni huyu anasema hivi:
“unapoona jiwe likiruka juu hewani, papo hapo unaelewa kuwa kuna mtu tu aliyerusha jiwe hilo. Uelewa huu hautokani na macho yako. Bali unatokea akilini kwani, akili ndiyo inayojenga hoja kuwa jiwe haliwezi kujirusha lenyewe hewani.”
Katika Qur’an Allaah analikanusha dai la wale wanaodhani kuwa milango ya fahamu ndiyo chanzo pekee cha elimu. “Na mliposema: ‘Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumuone MwenyeziMungu waziwazi.” Yakakunyakueni mauti ya ghafla na hali mnaona. (2:55).
Aidha inaelezwa katika Qur’an kuwa hatuwezi kutambua mambo mengi ya dunia kwa milango tu ya fahamu.
“Basi naapa kwa mnavyoviona na msivyoviona.” (69:38-39)
“Ametukuka MwenyeziMungu aliyeumba dume na jike katika vitu vyote, katika vile ivioteshavyo ardhi, na katika nafsi zao (wanadamu) na katika vile wasivyovijuwa”. (36:36)
“Na ni vya MwenyeziMungu tu vyote vilivyofichikana katika ardhi na mbingu...” (11:123)
Kwa kifupi uchunguzi na majaribio yetu hayawezi kuwa chanzo cha elimu yoyote isipokuwa mpaka vipitie katika mchakato wa kiakili. Juu ya hivyo, si taarifa zote kuhusu ulimwengu ambazo hutokana na milango ya fahamu.
Kuna mambo mengi ulimwenguni ambayo hatuwezi kuyafahamu na hatuna namna ya kuyajuwa.
Hakika ya mambo tunayoipata kupitia Qur’an hutupatia mtazamo mpana zaidi juu ya ulimwengu (broader worldview) kuliko ule unaotolewa na sayansi ya kisekula.
Mtazamo wa Qur’an juu ya sayansi ndio unaotupatia “Sayansi ya Kiislamu” na mtazamo wa Qur’an juu ya elimu ndio unaotupatia “Elimu ya Kiislamu”. Inapozungumziwa elimu ya Kiislamu, watu wengi kwa mtazamo wa harakaharaka, hudhani ni Fiqhi, Sira, Hadith, Hukumu za usomaji wa Qur’an tu.
La hasha huo si mtazamo wa jumla juu ya elimu ya Kiislamu bali huo tunaweza kuuita “nusu-mtazamo” ambao hatari yake ya kuigawanya elimu katika mapande mawili imekwishauletea dhahama kubwa ulimwengu wa Kiislamu. Hii ikiwa na maana kuwa mtazamo huu ndio unaotenganisha ile inayoitwa “Elimu ya dini” na “elimu dunia!”
Mtazamo sahihi na wa jumla ni kuwa fani zote za elimu zikisomwa kwa lengo na tafakari ya kumjuwa Muumba na kuitumia kila elimu kwa manufaa kama anavyotaka Muumba basi hapo ndipo tunapopata ainisho la “Elimu ya Kiislamu”
Kwa mantiki hiyo, Sayansi ya Kiislamu na teknolojia ya Kiislamu ni ile inayoendana na maelekezo ya Muumba. Fizikia ya Kiislamu ni ile inayoleta manufaa ya kifizikia na si madhara ya kifizikia, Kemia ya Kiislamu ni ile inayoleta manufaa ya kikemia na si madhara ya kikemia na Baiolojia ya Kiislamu ni ile inayoleta manufaa ya kibailojia na si madhara ya kibaiolojia. 
Kwa maana hiyo, mwalimu wa Fiqhi au Sira asiwe na ukiritimba wa hisia kuwa yeye ndiye anayefundisha elimu ya Kiislamu. Bali hata mwalimu wa Baiolojia anayewatanabahisha wanafunzi juu ya kuwepo kwa ufalme wa Allaah ambao ndio unaoendesha ‘”zoolojia” (maisha ya wanyama) na “botania” (maisha ya mimea) naye pia ni mwalimu anayefundisha elimu ya Kiislamu. Huu, bila shaka, ni mfano mwepesi wa kumsaidia mtu kuepuka kabisa ile dhana potofu kuwa “kuna elimu ya dini na dunia”
Kwa mtazamo wa Uislamu juu ya ulimwengu, kupata maendeleo ya vitu si lengo pekee la maisha bali maendeleo hayo yawe nyenzo ya kuzidishia mahusiano bora kati ya roho ya mja na Dhati ya MwenyeziMungu.
 Kwa mtazamo wa Qur’an, kufanikiwa maana yake  ni kuitakasa nafsi kwa mnasaba wa mahusiano yake na Muumba na kufeli ni kuvuruga mahusiano baina ya nafsi ya mja na Dhati ya Allaah.
Mtu au jamii hata ikipata maendeleo makubwa kiasi gani kwa mizani ya sayansi na teknolojia bado haitakuwa imefanikiwa kama itakuwa inafanya mambo yanayovuruga mahusiano bora na Muumba.
Maisha ya dunia si maisha halisi, kwa hiyo, mafanikio kwa mtazamo wa Uislamu, sio hayo ya kupata kila kitu cha dunia.
“Kwa hakika tumevifanya vilivyoko juu ya ardhi viwe pambo lake, ili tuwatazame ni nani katika wao wenye vitendo vizuri.” (18:7)
Kuhitimisha makala haya, hizi ni nukta za mapendekezo:
1. Katika kipindi hiki ambacho ulimwengu wa Kiislamu hauko katika hali nzuri kimtazamo na kielimu ambapo unautegemea ulimwengu wa magharibi katika kila jambo, ipo haja ya kuirekebisha hali hii ya kubaki nyuma. Kwa kweli, kwa maslahi ya Umma wa Kiislamu na kwa maslahi ya dunia, tunahitajika kuchuana na ulimwengu wa magharibi au hata kuushinda katika nyanja za sayansi. Lakini hii inahitaji dhamira na istiqama ya kweli (serious commitment) kwa upande wa serikali za nchi za Waislamu na kwa upande wa wanazuoni. Hili lisipofanyika basi maadili na utamaduni wa Kiislamu utazidi kuwa hatarini.
2. Kwa kuangalia uelekeo wa nchi za magharibi, lazima tutanabahi kuwa ili tuweze kusalimika na maangamizi ya sayansi ya Magharibi, lazima na sisi tuunde sayansi yetu kwa mtazamo wa Kiislamu. Hili ndilo litakalotuhakikishia furaha katika dunia hii na mafanikio Akhera na ndilo litakalotuwezesha kuitimiza aya hii kwa vitendo 
“Nyinyi ndio umma bora kuliko umma zote ulimwenguni, mnaamrisha mema na mnakataza yaliyo maovu na mnamwamini MwenyeziMungu.” (3:110)
Imeandikwa na Ummu Ashraf katika Al Hidaya

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget