Monday, February 20, 2012

Kusoma dua pamoja baada ya swala


Mwanzo tunatakiwa tufahamu kuwa du’aa ni jambo ambalo linahitajika kwa Muislamu. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatufahamisha kuwa du’aa ni silaha ya Muumini. Kwa hiyo, baada ya kila ‘Ibaadah, Allaah Aliyetukuka Akatuwekea du’aa. Na ‘Ibaadah ya Swalah si tofauti, kwani Aliyetukuka Ametuambia:

Mkisha swali basi mkumbukeni Allaah mkisimama, na mkikaa, na mnapo jinyoosha kwa kulala. Na mtapotulia basi simamisheni Swalah kama dasturi. Kwani hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu” (4: 103).
Na Akasema: “Na itakapokwisha Swalah, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Allaah, na mkumbukeni Allaah kwa wingi ili mpate kufanikiwa” (62: 10).

Hata hivyo, inatakiwa tuilete hiyo du’aa kwa njia ambayo tumefundishwa na sheria sio tunavyotaka sisi.

Tukianza na Hadiyth ya Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu). Nadhani itakuwa bora mwanzo tuanze na kuifasiri kwa ukamilifu wake ili ifahamike vizuri. Imepokewa kwa Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

Aliulizwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni du’aa gani yenye kusikilizwa zaidi (inayokubaliwa)?” Akasema: “Sehemu ya mwisho ya usiku na baada ya kila Swalah ya faradhi” (at-Tirmidhiy ambaye amesema ni Hasan).


Hivyo ndivyo ilivyonukuliwa na Imaam an-Nawawiy. Labda tuitazame msimamo wa wanachuoni kuhusu Hadiyth hiyo. Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn al-Albaaniy ameiweka Hadiyth kuwa ni ya 1508, naye amesema Hadiyth hii ni Sahihi. Hata hivyo, Shaykh Shu‘ayb al-Arna’ut amesema Hadiyth hii ni dhaifu kwa sababu ya Isnadi yake lakini inatiliwa nguvu na Hadiyth nyingine, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mja anakuwa karibu zaidi katika du’aa zake wakati wa usiku wa mwisho” (at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy, na Isnadi yake ni Sahihi).



Hata hivyo, tukichukulia kuwa Hadith hii ni sahihi kabisa kama alivyosema Sh. Muhammad Naaswir ad-Diyn al-Albaaniy haimaanishi kuwa adhkaar na du’aa zinazoletwa baada ya Swalah ni kwa pamoja. Zipo Hadiyth nyingi Sahihi zinazotufundisha adhkaar na du’aa kwa mpangilo maalumu baada ya Swalah ya Faradhi. Na kufanya hivyo kunampatia mwenye kutekeleza ujira na thawabu nyingi. Kwa hiyo, ni muhimu kuhifadhi du’aa hizo na kuzileta kwa njia inayotakiwa na sheria. Pia tunatakiwa tulete baada ya Swalah tu na kabla ya kuinuka latika sehemu aliyoswali Muislamu. Utaratibu wenyewe ni kamaufuatao:

1.    Kusema AstaghfiruLlaah mara tatu baada ya salamu na kisha kusema: Allaahumma Antas Salaam wa Minkas Salaam tabaarakta yaa dhal Jalaal wal Ikraam (Muslim).


2.    Kisha ni kusema: Laa ilaaha illaa Allaahu wahdahu laa shariyka lahu, lahul Mulku wa lahul Hamdu wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr. Allaahumma laa maani’a limaa A‘twayta walaa Mu‘twiya limaa mana‘ta walaa yanfa‘u dhal jaddi Minkal Jadd. (al-Bukhaariy na Muslim).


3.    Baada ya hapo, Laa Hawla walaa Quwwata illaa Billaahi. Laa ilaaha illaa Allaahu walaa na‘budu illa Iyyaahu lahun Ni‘matu wa lahul Fadhwlu wa lahuth Thanaaul Hasan. Laa ilaaha illa Allaahu mukhliswiyna lahud Diyna walaw Karihal kaafiruun (Muslim).


4.    Kisha utaleta: Tasbiyh mara 33, Takbiyr 33, Tahmiyd 33 na kukamilisha mia utasema: Laa ilaaha illaa Allaahu wahdahu laa shariyka lahu lahul Mulk wa lahul Hamd wa Huwa ‘alaa kulli shay’in Qadiyr. (Muslim).


5.    Na baada ya Swalah ya Maghrib na Alfajiri utaleta Tahliyl mara kumi (Ahmad) na Rabbi ajirniy minan Naar mara saba (Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).


6.    Kusoma Ayaatul Kursiy (2: 255) {an-Nasaa’iy, atw-Twabaraaniy na Ibn Sunniy}

7.    Kusoma Suratul Ikhlasw, al-Falaq na an-Naas (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy).



Shaykh Dkt. Swaalih Fawzaan bin ‘Abdallaah al-Fawzaan katika kitabu chake al-Mulakhkhaswu al-Fiqhiyy amesema: “Na inapendeza kujihirisha Tahliyl, Tasbiyh, Tahmiyd na Takbiyr baada ya kila Swalah lakini isiwe kwa sauti ya pamoja. Kila mmoja ananyanyua sauti peke yake. Baada ya kumaliza adhkaar hizi, kila mmoja anaomba kwa siri kwa anachotaka. Hakika ni kuwa du’aa baada ya ‘Ibaadah na hizi adhkaar tukufu inaleta uwezekano mkubwa zaidi wa kujibiwa. Haifai kujihirisha du’aa bali anaifanya kwa sauti ndogo, kwani kufanya hivyo ni karibu zaidi na Ikhlaswi, unyenyekevu na mbali zaidi na riyaa. Na ama kwa yale yanayofanywa na baadhi ya watu katika baadhi ya nchi kwa kuleta du’aa ya pamoja baada ya Swalah kwa sauti kubwa au Imaam aombe na maamuma waseme Aamiyn. Hii ni bid‘ah inayochukiza kwani haijapokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa anaposwalisha watu na baada ya kumaliza Swalah akiomba kwa njia hii. Hakufanya hivyo katika Swalah ya Alfajiri, wala Alasiri, wala Swalah nyinginezo, wala hakupendeza hilo yeyote miongoni mwa maimamu” (Mj. 1, uk. 154 – 160).

Ama tukija katika Fat-hul Baariy nimeipitia Hadiythi hizo ulizozitaja katika Mj. 11, uk. 159, chapa ya Daar as-Salaam, chapa ya tatu ya mwaka 1421 H/ 2001 M. Imaam al-Bukhaariy ana mlango wa 18:Baab ad-Du’aa’i ba‘da asw-Swalaah (Mlango wa Du’aa baada ya Swalah). Imaam al-Bukhaariy ameweka Hadiyth mbili zilizoshereheshwa na Ibn Hajar, nazo ni kama zifuatazo:


1-    Imepokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu): Wakasema: Ewe Mtume wa Allaah! Hakika wametangulia wenye mali kwa daraja na neema za kuendelea. Akasema: Itakuwaje hivyo? Akasema: Wanaswali kama tunavyoswali, wanapigana Jihaad kama tunavyopigana, na wanatoa katika fadhila za mali zao, nasi hatuna cha kutoa. Akasema: Je, niwajulishe jambo ambalo mkifanya mtawafikia waliokuwa kabla yenu na kuwashinda wanaokuja baada yenu, wala hatofikia yeyote kwa mlioleta ila atakayeleta mfano wake? Leteni Tasbiyh baada ya kila Swalah mara kumi, Tahmiyd kumi na Takbiyr kumi.


2-   Mughiyrah bin Shu‘bah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuandikia Mu‘awiyah bin Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema baada ya kila Swalah baada ya salaam: Laa ilaaha illa Allaahu wahdahu laa shariyka lahu, lahul Mulku wa lahul Hamdu wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr. Allaahumma laa maani’a limaa A‘twayta walaa Mu‘twiya limaa mana‘ta walaa yanfa‘u dhal jaddi Minkal Jadd



Kauli yake: “Mlango wa Du’aa baada ya Swalah”, yaani baada ya Swalah za faradhi. Hadiyth hizo mbili zilizo hapo juu zinatufahamisha kuwa ipo du’aa baada ya Swalah, du’aa ambazo ni makhsusi kamaalizotufundisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata hivyo, hizo Hadiyth hazionyeshi kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakiitikia Amiyn.


Ama tukija katika Hadiyth ulizozitaja kwa muhtasari ambazo amezitaja Ibn Hajr al-Asqalaaniy, na pia kuna nyingine umeziacha zote hazina dalili ya kuomba du’aa kwa pamoja baada ya Swalah. Na hivyo akamuusia Mu‘aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ‘anhu) asiache kuomba du’aa baada ya Swalah, du’aa maalumu ((Abu Daawuud, an-Nasaa’iy, al-Haakim na Ibn Hibbaan). Pia Hadiyth ya Abu Bakrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kauli:

Ewe Allaah! Najilinda Kwako kutokana na ukafiri, ufakiri na adhabu ya kaburi”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba kwayo baada ya kila Swalah (Ahmad, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, na kusahihishwa na al-Haakim).


Na pia Hadiyth ya Sa‘d, Zayd bin al-Arqam, Swuhayb na Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ‘anhum) zatuonyesha du’aa za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya Swalah kwa njia ya siri ila kwa wakati mwengine alikuwa akinyanyua sauti ili wafuasi wake wapate kujifunza kwa njia sahali na rahisi.

Na maelezo yote hayo yanaweza kufupishwa kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka Aliyesema:


Na mkumbuke Mola Mlezi wako nafsini kwako kwa unyenyekevu na khofu, na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni. Wala usiwe miongoni wa walioghafilika” (al-A‘raaf [7]: 205).


Imaam ash-Shawkaaniy amesema kuieleza Aayah hii katika tafsiri yake Fat-hul Qadiyr kuwa, “Hiyo ni kuisikilizisha nafsi yake bila kutoa sauti, yaani kwa unyenyekevu na kwa khofu na kuzungumza kwa mazungumzo chini ya kujihirisha”. Na Ibn Kathiyr naye amesema katika tafsiri yake, Tafsiyr Qur-aanil ‘Adhwiym: “Mtaje Mola wako Mlezi kwa matumaini na hofu na kwa kimoyomoyo, si kwa jahara. Na hivi ndivyo Dhikr inavyopendekezwa iwe, si kwa sauti ya juu wala kwa jahara”.


Na Aayah hii inafafanuliwa na Hadiyth iliyowazi kabisa kutoka kwa Abu Muusa al-Ash‘ariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:


Watu walinyanyua sauti zao katika du’aa wakati wa baadhi ya safari, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: ‘Enyi watu! Jifanyieni wepesi katika nafsi zenu, kwani mnayemwomba si kiziwi wala si wa kughibu. Kwa hakika mnayemwomba ni Mwenye kusikia, wa karibu, yu karibu zaidi ya mmoja wenu kuliko shingo ya mnyama wake” (al-Bukhaariy na Muslim).

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget