Monday, February 20, 2012

Kuvaa kanzu ni sunnah?


Inafahamika vyema kwa kila mmoja wetu Muislamu na asiyekuwa Muislamu kuwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asili yake alikuwa Mwarabu. Katika maisha yake aliishi (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mazingira ya Kiarabu na vazi lake lilikuwahilo.

Kwa kulichukua kubaki vazi la kanzu kuwa ni vazi lake baada ya kupatiwa utume ni dalili tosha kuwa kuvaa vazi hilo ni kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hivyo kuingia katika Sunnah. Kwa muhtasari ni kuwa Sunnah ni kauli, vitendo na iqrari ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa kuwa alivaa na hakukanya wafuasi wake kuvaa ikaingia hiyo katika Sunnah zake. Kwani ni wazi kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa haachi jambo ambalo si zuri kuendelea katika wafuasi wake.

Mbali na kusema hayo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuusahilishia Ummah wake katika mambo mengi na mavazi vile vile alikuwa na mavazi tofauti kama zinavyotueleza Hadiyth zake nyingi. Wakati mwengine alikuwa anavaa ‘Imaamah (kilemba), ‘Izaar (nguo ya chini kama kikoi), kofia, aina nyengine za nguo za kutoka Shaam, Yemen, na hata Misri na kadhalika. Na katika mavazi alikuwa anapenda sana kuvaa vazi la rangi nyeupe.

Baadhi ya Hadiyth zinazoelezea hayo ni:

§         Imepokewa kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Vaeni katika nguo zenu nyeupe, kwani hizo ni katika nguo zenu zilizo bora kabisa na pia muwakafini nazo maiti zenu” (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy, na akasema ni Hadith Hasan Swahiuh. Isnadi yake ni Sahihi na ameisahihisha Ibn Hibbaan).

§        Na amesema Abu Ramthah Rifaa‘ah at-Taymiy (Radhiya Allaahu ‘anhu): Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na nguo mbili za kijani (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy kwa Isnadi iliyo Sahihi. Pia imenukuliwa na an-Nasaa’iy, na Isnadi yake ni Sahihi).

§        Na imepokewa kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia siku ya kufunguliwa Makkah akiwa na kilemba cheusi(Muslim).

§        Na amesema mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amevishwa sanda ya nguo tatu nyeupe zilizotengenezwa Sahuuliyyah (aina ya nguo kutoka kijiji hicho cha Yemen) kwa pamba, katika hizo hamna kanzu wala kilemba (Ahmad, al-Bukhaariy na Muslim).

§        Na amesema Mughiyrah bin Shu‘bah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba: Usiku mmoja tulikuwa katika safari pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) …Wakati huo alikuwa amevaa juba la sufi na hivyo hakuweza kutoa mikono yake mpaka alipoitoa kutoka katika sehemu ya chini ya hilo juba. Aliosha mikono yake na kupangusa kichwa chake. Kisha nilitaka kumsaidia ili atoe soksi zake, akaniambia: “Ziache kama zilivyo kwani nilizivaa nikiwa katika hali ya twahara na usafi”. Hivyo akapangusa juu yake (al-Bukhaariy na Muslim). Na katika riwaya: Alikuwa amevaa juba la Shaam lililokuwa na mikono membamba.

§        Amesema Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha): Ilikuwa nguo bora kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kanzu (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy, na akasema hii ni Hadyith Hasan).

§        Na imepokewa kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Hatawaangalia wale watu walioburuza (zikavuka mafundo ya miguu) nguo zao kama kikoi na kanzu na kilemba kwa kiburi” (Abu Daawuud na an-Nasaa’y kwa Isnadi Sahihi).

§        Na imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Hamuangalii mwenye kuburuza (kuvaa nguo yenye kuvuka mafundo ya miguu [Isbaal]) nguo yake kwa kiburi” (al-Bukhaariy, Muslim na Maalik).

Kwa mujibu wa Hadiyth hizi tunapata kuwa vazi bora lake ni kanzu mbali na kuwa alikuwa akivaa mavazi mengine. Kulingana na Hadiyth wanazuoni wamekuja na masharti kwa vazi kukubalika Kiislamu. Miongoni mwa masharti hayo ni:

i.                    Vazi lisiwe ni lenye kubana.
ii.                   Vazi lisiwe ni la kuonyesha ndani.
iii.                 Kutoburuza nguo aina yoyote kwa mwanamme [Isbaal - kuvuka mafundo ya miguu].
iv.                Kutosifu umbile lake (lisimbane).
v.                 Lisifanane na vazi la kike.
vi.                Lisifanane na vazi la makafiri.
vii.              Lisiwe vazi la kifakhari, umaarufu, na mitindo [fashion].

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget