Thursday, February 23, 2012

Mahakama ya Kadhi na Hoja ya Msingi


Ni dhahiri kuwa mjadala wa kurejeshwa Mahakama ya Qaadhi kwa Waislamu nchini unaendelea kuchukua sura mpya kutokana na hoja zinazoibuliwa na wadau tofauti kuhusiana na ajenda hiyo muhimu.
 Hoja kuu za msingi ni zile zinazotolewa na Waislamu kupitia baadhi ya masheikh na viongozi wa juu wa baadhi ya Taasisi za Kiislamu nchini, na zile zinazotolewa na wakristo kupitia viongozi wao wa dini wa ngazi ya juu kabisa.
 Waislam, wao wanadai kuwa Mahakama ya Qaadhi ni haki yako ya msingi waliyopewa na dini yao, kisha nchi yao na hatimae kuporwa haki hiyo katika mazingira ya kutatanisha mnamo mwaka 1963, hivyo kwa mujibu wa msingi huo, na hasa ikizingatiwa kuwa Chama Tawala cha CCM kiliona hoja hiyo na kuiweka katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2005-2010, Waislamu wanadai serikali ya CCM iliyopo madarakani hivi sasa itekeleze ahadi hiyo iliyoitoa kwa wananchi na hatimae Waislamu nchini kukipigia kura chama hicho na kushinda ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2005.
 Lakini kwa upande mwingine, viongozi wa juu wa madhehebu ya kikristo hawakusita kutoa maoni yao bayana kuwa suala hili kama litapitishwa na Bunge basi litakuwa limekiuka Katiba ya nchi hii, ambayo maongozi yake si ya dini, na aidha itakuwa ni upendeleo kwa kuwapa baadhi ya raia haki hiyo na kuwanyima wengine, hasa ikizingatiwa kuwa Mahakama hiyo itaingizwa katika bajeti za serikali ambazo chanzo chake ni kodi za wananchi wa Tanzania wakiwemo wakristo.
 Hizo ni hoja za msingi ambazo ni vema zikajadiliwa kwa utulivu na mantiki bila kuchukua mwelekeo wa ushabiki na kubezana ambako kunaweza kubadilisha sura nzima ya hoja iliyopo.
Sheria za Kiislamu ni moja miongoni mwa vyanzo vya sheria nchini Tanzania, mwaka 1964, Bunge la Tanganyika kwa wakati huo lilipitisha “Sharia ya Kiislamu (Sheria ndogo)” iliyompa madaraka Waziri aliyehusika na mambo ya Sheria kuandaa na kuchapisha kipengele cha Sharia ya Kiislamu baada ya kushauriana na wanachuoni wa Sharia za Madh-hebu za Kiislamu. Na hatimae Katibu Mkuu wa Bunge wakati huo, alikamilisha kuandika Mswada wa ndoa wenye sehemu 4 (kwa msaada wa masheikh wa madh-hebu za Kiislamu).
Mswada huu uliotolewa kama Sharia ndogo chini ya kifungu kidogo cha Sharia ya Kiislamu (Na: 56 ya mwaka 1964) ikiwa ni sehemu ndogo ya Gazeti la Serikali na Na: 34 la tarehe 27, Juni, 1967.
Ilifahamika kuwa sehemu zilizosalia, kuhusiana na kuwalea watoto na talaka n.k. zingechapishwa mapema. Lakini zoezi hili lilisitishwa na badala yake serikali ilitunga sheria ya ‘Ndoa’ kupitia Mswada wa Ndoa wa mwaka 1971.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kumbukumbu zangu, kanuni ya Sheria ya Kiislamu 1964 bado haijafutwa na bado ni sehemu ya Kitabu cha Bunge.
 Hoja ya msingi hapa ni kuwa sheria hizo zilikuwepo, pamoja na kutokuwepo kwa Mahakama ya Qaadhi, aidha sheria husika katika mswada jadiliwa zinahusiana tu na yale mambo ya Ndoa, Talaka, Mirathi, na malezi ya watoto kwa Waislamu na hazigusi kabisa uhuru wa raia wengine katika kuabudu dini zao.
 Hoja nyingine ya kuwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Qaadhi kutawabagua raia wengine wasio Waislamu, pamoja na kuwa raia wote wa Tanzania wataichangia Mahakama hiyo kupitia kodi zao, ni hoja ya msingi, lakini ni vema ikaeleweka kuwa, katika mfumo wa Demokrasia, kodi za wananchi baada ya kukusanywa na serikali, matumizi yake huidhinishwa na Bunge ambalo ndilo linalowakilisha wananchi kupitia wawakilishi wao, aidha ilani ya Chama cha Mapinduzi ilikuwa wazi kabla ya uchaguzi, na inaeleweka kuwa chama hujinadi kwa wapiga kura kupitia ilani yake ya uchaguzi, hivyo ilikuwa ni vema hoja hizi zikaibuka wakati huo, na labda kukishinikiza Chama Cha Mapinduzi wakati huo kuondoa kipengele hicho katika ilani  ambayo ni ahadi kwa wapiga kura wake kwamba kama watawaingiza madarakani basi watatekeleza waliyowaahidi.
 Kwa mtazamo wangu, kuitaka serikali ya CCM kuiangalia upya ahadi hiyo ambayo ni itikio la ombi la wananchi ni kutoitakia wema Serikali, na madhara yake yatakuwa ni makubwa kwa taifa letu kuliko haya yanayodhaniwa kuletwa na Mahakama ya Qaadhi, kwani yataibua hisia za chuki na kutotakiana mema baina ya waumini wa Dini mbili kuu nchini, na zitahatarisha kuondoa usamehevu (Tolerance) na kuzidisha ufa wa kitaifa.
 Hoja yangu ya msingi katika mjadala huu itawahusu walengwa wa mswada huo ambao ni Waislamu, ambao dhahiri wanaonekana wamoja katika kutetea haki hii ya msingi ya kuwa na Mahakama ya Qaadhi, lakini ndani yao kuna hofu,woga na minun’guniko ya jinsi Qaadhi huyo atakavyopatikana na mipaka ya majukumu yake kwa Waislamu.
 Hofu hizo za baadhi ya Waislamu, zinatokana na ukweli kuwa mara nyingi kama sio zote, serikali ya Chama Chama cha Mapinduzi imekuwa ikiangalia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kama msemaji rasmi wa Waislamu Tanzania,na msimamizi mkuu wa maendeleo ya Waislamu nchini, jambo ambalo si sahihi.  
 Dhana hiyo ambayo ina ukweli mkubwa ndani yake, kama itatumika katika suala zima la kuanzishwa Mahakama ya Qaadhi,basi mahakama hiyo huenda ikakosa ridhaa za Waislamu wengi nchini, na ikalisababishia taifa hasara kubwa ya fedha na muda. Hii inatokana na ukweli usiopingika kwa mtafiti yeyote, na mfuatiliaji wa mambo ya Waislamu kuwa Bakwata kama chombo hakikubaliki kwa Waislamu wengi wa Tanzania, na wengi hawasiti kusema bayana kuwa Bakwata haipo pale kwa ajili ya maslahi ya Waislamu.
 Hofu nyingine ya msingi ni jinsi Qaadhi Mkuu atakavyopatikana, zile hatua zitakazowezesha (mechanism) kupatikana kwa Qaadhi, kama atateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au atateuliwa na jopo la wanazuoni wa Kiislamu ikiwa atateuliwa na Rais, ni dhaahir kuwa atakapokuwa Rais si Muislamu uteuzi huo utapingana na aya za Qur-aan zinazozuia asie Muislamu kuwachaguliwa Waislamu kiongozi wao pamoja na kuwa baadhi ya masheikh wanaweza kuzitafsiri aya hizo ili zihalalishe uteuzi huo. Ukweli utabaki palepale, na kundi kubwa la Waislamu wanaweza kujitenga na mahakama hiyo kutokana na misingi ya itikadi zao.
 Kwa upande mwingine ikiwa Qaadhi Mkuu atateuliwa na Jopo la Wanazuoni wa Kiislamu, ni taratibu gani zitakozotumika kulipata jopo hilo na kwa vigezo gani? Hasa ikizingatiwa kuwa Taasisi za Kiislamu Tanzania ni nyingi na zinatofautiana katika mielekeo na maono. Kwa mfano tu, Taasisi za Answaar Sunnah ambazo zina mtandao Tanzania nzima na zina wafuasi wengi na nguvu za kiuchumi na miundo mbinu, zitashirikishwaje katika jopo hilo na kwa kiwango gani?
 Hofu yangu ya msingi ni kuwa, Waislamu wengi hawaelewi kinachoendelea na wale wanaoelewa wanaogopa kutoa dukuduku zao kwa kuogopa kuonekana wanapinga jambo la msingi katika Uislamu, au wanashirikiana na wapinzani wa mswada huu jambo ambalo si sahihi kwa dharura.
 Kwa kuhitimisha makala hii ningependa kuwarejesha wasomaji katika hoja ya msingi; Mahakama ya Qaadhi haipo dhidi ya waumini wa dini nyingine, bali ni haki ya msingi ya Waislamu ambao ni sehemu ya taifa hili.
 Lakini je, Waislamu wako tayari kuyapokea mabadiliko haya ya kihistoria yanayokuja katika zama za utandawazi na mabadiliko makubwa ya mifumo ya jamii? Wakati wakiwa hawana chombo kinachowaunganisha na kulinda maslahi yao? Je viongozi wa Kiislamu ambao wengi wao bado wanaongoza kwa kutumia mifumo ya karne iliyopita, wanaweza kukabiliana na changa moto ya utandawazi, soko huria, na uhuru wa kufikiri miongoni mwa wanajamii?
 Kama hatutayaangalia vizuri hayo, nina wasiwasi kuwa Mahakama ya Qaadhi itakuwa ni mtihani mkubwa kwa Waislamu wa Tanzania, na historia na vizazi vijavyo havitatusamehe.
Imekopiwa kutoka Al-Hidaya

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget